Tafuta

Mababa wa Sinodi wametumia fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wa vita, kinzani na migogoro, bila kuwasahau wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Mababa wa Sinodi wametumia fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wa vita, kinzani na migogoro, bila kuwasahau wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa.   (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 30 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Upendo

Mababa wa Sinodi katika Waraka wao kwa watu wa Mungu mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wamejikita katika ushirika, Utamaduni wa ujenzi wa ukimya ili kusikilizana na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na ushirika; wongofu wa wa kichungaji na kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayosimikwa katika huduma; Upendo wa Kanisa unabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Upendo ni utimilifu wa sheria zote!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Utangulizi: Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Awamu ya Kwanza Ngazi ya Kiulimwengu yalizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023 kwa Sala na Mkesha wa Kiekumene, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Makanisa. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, alikazia umuhimu wa kujenga utamaduni wa ukimya, ili kumsikiliza Roho Mtakatifu na kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni fursa muhimu ya ujenzi wa umoja na udugu ndani ya Kanisa. Watu wa Mungu walisali pamoja na kusikiliza shuhuda za watu mbalimbali. Maadhimisho ya Sinodi yamekuwa ni muda muafaka wa baraka katika ujenzi wa ushirika wa kina kati ya watu wote wa Mungu; kwa kujikita katika mageuzi yatakayosaidia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unatoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kulitakasa Kanisa kutokana na mapungufu yake. Ukimya ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa na katika mchakato wa ujenzi wa umoja miongoni mwa Wakristo, kwani sala ni chemchemi ya majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamenogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Huu ulikuwa ni mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili watu wote wa Mungu waweze kuketi pamoja, ili kushiriki katika mkutano na hatimaye kupiga kura, mintarafu utimilifu wa miito, karama na huduma; kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu pamoja na uzoefu kutoka wa Mababa wa Sinodi.

Waraka wa Mababa wa Sinodi ya XVI: Utamaduni wa kusikiliza
Waraka wa Mababa wa Sinodi ya XVI: Utamaduni wa kusikiliza

Mababa wa Sinodi katika Waraka wao kwa watu wa Mungu mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wamejikita katika ushirika, Utamaduni wa ujenzi wa ukimya ili kusikilizana na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na ushirika; wongofu wa wa kichungaji na kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayosimikwa katika huduma; Upendo wa Kanisa unabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kanisa linahitaji ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote hasa wale wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni mwaliko wa kuwasikiliza waamini walei na familia na kuendelea kujikita katika utambuzi wake wa kisinodi; kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuimarisha mahusiano na mafungamano. Hii ndiyo njia hasa ya Sinodi ambayo Mwenyezi Mungu anaitarajia kutoka kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Kristo Yesu ndiye tumaini la pekee kwa waja wake. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023 anahitimisha rasmi maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu.

Tarehe 29 Oktoba 2023 Papa Francisko anafunga Maadhimisho ya Sinodi
Tarehe 29 Oktoba 2023 Papa Francisko anafunga Maadhimisho ya Sinodi

Katika dominika ya thelathini ya mwaka A wa Kanisa, wazo kuu la masomo yetu tutakayosikia ni upendo usi ona masharti, ni wazi kabisa ila mmoja wetu anapenda kupendwa na kuambiwa neno nakupenda, kwani mfano wetu ni Mungu mwenyewe aliye upendo nasi tu zao la upendo huo, Neno hili linatumika katika maana mbalimbali. Laweza kumaanisha mapendo ya kweli au mapendo ya uwongo. Mapendo ya kweli ni yale yaletayo faida kwa maisha ya mwanadamu katika Nyanja ya kiroho na kimwili. Mapendo ya uwongo ni yale yasiyoleta faida kwa binadamu. Somo la kwanza leo kutoka katika Kitabu cha Kutoka linaelezea amri ya Mungu kwa wana wa Israeli: upendo kwa jirani. Ni wakati gani upendo wangu kwa jirani utakuwa mkamilifu? Tunapo wapenda majirani zetu tunatamani na wao wapate nafasi katika ufalme wa Mungu. Tunakuwa tunatamani kama wataishi katika neema ya Mungu siku zote za maisha yao. Na hivyo waweze kuishi milele kwa sababu ya neema tuliopokea kutoka kwa Kristo. Tukiwapenda wenzetu namna hii hatuwezi kuwanyima chochote au mahitaji yeyote wanayo taka kwetu. Tunakumbuka alichosema Yesu, kwamba mlicho watendea wadogo hawa mlinitendea mimi. Tunaenda kuwatembelea watu walio katika mahitaji mbali mbali kwa njia ambazo zipo katika uwezo wetu. Na huu ndio upendo kwa jirani.

Amri kuu: Upendo kwa Mungu na jirani.
Amri kuu: Upendo kwa Mungu na jirani.

Katika Injili agizo na himizo ni kumpenda jirani ili kuufikia ukamilifu, kumbe leo mwaliko wa ukamilifu tutaupata katika kupendana yaani Agape; Upendo unaongozwa na kanuni na unatia ndani mambo mengi; unahusisha fikra na unakusudi fulani na hauna ubinafsi. Upendo huu siyo hisia tunayokuwanayo bila kufikiri. Mara nyingi huhusisha uhusiano wa karibu wenye upendo. Agape ndio neon linaloelezea upendo kwa njia nzuri zaidi. Aidha kati ya maneno hayo yote kuhusu upendo; Agape limetumika mara nyingi zaidi katika Agano jipya. Mapendo yanawaka na kuangaza, upendo unatosha! Upendo huleta nuru pakiwapo giza… na kicheko penye huzuni, mateso na kukwazika… upendo unaponya, unaleta kuaminiana, kupokeana, kukua na kuheshimiana… tunavumilia, tunasamehe, tunajitahidi, tunakumbatia, tunasaidia na tunaweza kunyenyekea sababu tu ya upendo... Upendo ni Mungu mwenyewe! Mungu ameagiza, mimi ni nani nisitekeleze? Katika hali zote, na nyakati zote, popote… sina budi NIMPENDE MWENZANGU!! Ni amri kuu, nayo ni kanuni ya dhahabu…Nimpende mwenzangu ameumbwa kwa mfano wa Mungu kama mimi… Nimpende mwenzangu ni mtoto wa Kanisa kama mimi, Ee Bwana unisaidie nimpende mwenzangu kama Wewe unavyonipenda mimi…Hakuna aliye masikini kushindwa kutoa chochote wala tajiri asiyehitaji chochote, sote tunahitaji na kutamani kupendwa… tutoe mapendo yetu na tupokee ya wenzetu! Tusiwapende ndugu zetu tu, au tunaowafahamu tu, au tunaosali nao tu, wa chama chetu tu cha siasa, wa kabila letu tu, wakuu na wenye mamlaka, wanaotusaidia tu… tuwapende watu wote.

Upendo wa Kristo Yesu unatubidiisha kushiriki matendo ya huruma
Upendo wa Kristo Yesu unatubidiisha kushiriki matendo ya huruma

Katika jina la upendo migogoro inasinyaa, vita vinakoma, kauli zinanyooka, ukarimu unatawala, kilichopo chagawanwa kwa haki na usawa, fursa zinatolewa, mkono wa msaada unanyooshwa, mapungufu yanarekebishwa, makosa yanasamehewa, ndoa zinaimarika, wachumba wanafunga ndoa, furaha na amani vinatamalaki… Haitoshi kusali kila siku hadi kuchubua magoti, kufanya hija, njia ya msalaba na kutoa sadaka wakati huohuo kuwapigia kelele na kuwanyanyasa wenzetu hasa walio chini yetu au wanaotutegemea kwa vile tu hawafanyi vile sisi tunataka. Kusema tunampenda Mungu na kuwasahau, kuwashusha na kunyanyasa wengine ni unafiki… Mtakatifu Augustine anauliza “upendo unafafanaje? Una mikono ya kusaidia wengine, miguu ya kuwakimbilia masikini na wahitaji,waliopembezoni mwa jamii au kutengwa, je? una macho ya kuona shida za wengine na masikio ya kusikia vilio na uchungu wa watu” ndivyo upendo unavyofanania… tusitamani kufanya mambo makubwa kupita uwezo wetu, bali madogomadogo katika jina la upendo!  Upendo kwa wote ni ufunguo wa mlango wa mbinguni, upendo ndio kifungo na kilele cha ukamilifu na furaha timilifu Mkristo unadaiwa neno hili, moja tu lakutosha, lishike na ulifanye… PENDA, PENDA, PENDA!

Liturujia D30 Mwaka A
27 October 2023, 08:17