Tafuta

Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 30 ya Mwaka A wa Kanisa: Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 30 ya Mwaka A wa Kanisa: Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 30 Mwaka A wa Kanisa: Amri Kuu Ni Upendo

Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha upendo usio na kikomo: Upendo kwa Mungu Baba na upendo kwa Jirani. Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu. Sheria, amri na kanuni zote vinapaswa kutuelekeza kwenye upendo. Anayempenda Mungu anammiliki Mungu ndani yake, alisema Mt. Tomaso wa Akwino. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Upendo!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Jimbo Kuu Katoliki Mwanza.

Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha upendo usio na kikomo: Upendo kwa Mungu Baba na upendo kwa Jirani. Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu. Sheria, amri na kanuni zote vinapaswa kutuelekeza kwenye upendo. Anayempenda Mungu anammiliki Mungu ndani yake, alisema Mt. Tomaso wa Akwino. Somo la kwanza (Kut. 22:21-27) linatuonesha namna gani ya kuishi upendo kwa jirani. Upendo kwa jirani unapaswa kudhihirishwa hasa kwa wanaoonewa na kwa wahitaji: kuwajali, kuwasaidia, kuwafariji na kuwaombea wajane, yatima na maskini. Tukiwapenda hawa tutampenda na Mungu. Hata hivyo, wengi wetu tunajifanya kumpenda Mungu na kujionesha kwa watu kuwa tunashika dini lakini wakati huo huo tunadhulumu mali za wajane na kuwazushia uongo kwamba wameua waume zao ili warithi mali, na tunadhulumu mali za yatima na kuwafanya wawe mitaani wakitaabika. Ni akina mama wangapi wanawalea kwa upendo watoto yatima? Ni ndugu wangapi wanamkumbuka mjane au yatima katika ukoo wao? Mbona tunawatesa kwa vipigo, masengenyo na ukatili? Ni watu wangapi wanajinufaisha na pesa za kuwasaidia wajane na yatima huku wahusika wakiambulia patupu. Ni mara ngapi haki ya maskini inadhulumiwa kwa sababu ya nguvu ya pesa? Hata hivyo, somo letu la kwanza lina maneno ya faraja kwa wajane, yatima na maskini. Mungu anasema, “Ukiwatesa watu hao [wajane, yatima na maskini] katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao…” Hakika maneno haya ni faraja kubwa. Wajane, yatima na maskini wanapaswa kumlilia Mungu katika mateso na mahangaiko yao, haidhuru ni makubwa kiasi gani kwa maana Yeye ni Baba wa yatima, Mume wa wajane na ni Mungu wa maskini. Hata kama walimwengu hawatawasaidia, Mungu atawasaidia; hata kama wataonekana wapweke lakini Mungu yupo nao na ni faraja yao; hata kama hawapendwi wakumbuke yupo Mungu anayewapenda. Mungu hawaachi kamwe maana anasema, “Je, mama aweza kumsahau mwanawe anayenyonya, asimwonee huruma mtoto wa tumbo lake? Hata kama mama aweza kumsahau mwanawe, mimi kamwe sitakusahau. Nimekuchora katika viganja vyangu…” (Isaya 49:15-16).

Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu.
Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu.

Katika Somo la Pili (1 Thes. 1:5-10) Paulo anaendelea kuwashukuru na kuwasifia Wakristo wa Thessalonike kwa namna walivyopokea Injili na kwa jinsi walivyobaki waaminifu kwa yale waliyohubiriwa. Wameendelea kuwa kielelezo kwa watu wote waaminio. Zaidi ya yote wameongoka na kuziacha sanamu na kuamini katika Mungu mmoja. Sisi nasi kwa ubatizo wetu tumeipokea Injili ya Kristo. Licha ya kuwa Wakristo tumeshindwa kuwa kielelezo kwa Wakristo na wasio-Wakristo kwa matendo yetu, maneno yetu, mawazo yetu, nia zetu na kwa kushindwa kuishi imani, matumaini na mapendo. Mara nyingi tunayumba kiimani na kutangatanga kwenye madhehebu mengine, kwa waganga, mara Freemasons. Wengi wetu tumepoteza matumaini na hata kunuia kujiua. Tunashindwa kuwa kielelezo cha upendo kwa kutojali mahitaji ya watu wengine, kwa kukosa uaminifu kwenye ndoa zetu na kwa viapo vya wito wetu, kwa kushindwa kuonesha upendo kwa familia zetu- mke, watoto, ndugu. Wakristo wa Thessalonike waliacha sanamu. Je, sisi tumeziacha “sanamu” (miungu ya uongo) na kumtumikia Mungu mmoja, aliye hai na wa kweli? Wengi wetu hatujaziacha “sanamu” (miungu ya uongo) tunaabudu ngono, biashara zetu, waganga, anasa, mali, teknolojia, hirizi, ndumba na mengineyo. Tubadilike. Mabadiliko yanawezekana kwa neema ya Mungu Roho Mtakatifu.

Ushuhuda wa furaha ya Injili
Ushuhuda wa furaha ya Injili

Katika Injili ya leo (Mt. 22:34-40) tunaona Yesu akijaribiwa na mwanasheria ambaye ni Mfarisayo pia juu ya amri ipi iliyo kuu katika torati. Wayahudi walisoma kwa makini vitabu vitano vya mwanzo katika Biblia (ambavyo huitwa Torati au vitabu vya Musa) na kugundua kuwa kuna jumla ya amri 613 ambapo kati ya hizo amri 365 zinakataza kufanya tendo fulani (negative commandments), wakati amri 248 zinahimiza kufanya jambo fulani (positive commandments). Hivyo Wayahudi walihimiza watu wote washike amri/sheria zote 613. Jambo hili lilifanya sheria kugeuka kuwa mzigo mkubwa maana siyo rahisi mtu kushika amri zote 613 kwa ukamilifu (na kwa kweli nyingi kati ya hizo amri zilihusu mambo ya nje tu- external rituals: kunawa mikono mpaka kwenye viwiko, kuepuka aina fulani za vyakula na mengineyo). Hivyo badala ya amri kumsaidia mtu kuwa karibu na Mungu na kuonja upendo wake ziligeuka kuwa mzigo. Kutokana na wingi wa amri Wayahudi wengi walitaka kujua ni amri ipi ambayo inapaswa kushikwa zaidi ya nyingine- yaani ni amri ipi ni bora kuliko nyingine ili mtu aishike kwa ukamilifu ili kuepuka rundo la amri. Mawazo ya amri ipi ni bora kuliko nyingine yalitofautiana miongoni mwa walimu wa Kiyahudi wa sheria: wengine walifundisha kuwa amri iliyo kuu ni amri juu ya kutahiri; wengine walifundisha kuwa amri iliyo kuu ni kushika sabato na wengine walifundisha kuwa amri iliyo kuu ni ya utoaji wa sadaka. Hivyo Yesu aliulizwa ili kuona ataegemea upande gani. Lilikuwa ni swali la mtego. Kwa kuegemea upande wowote wa walimu wa sheria angeweza kuchukiwa na upande mwingine kwa kuona kuwa anapingana na mafundisho yao. Yesu anatoa jibu tofauti na mategemeo yao: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote… Mpende jirani yako kama nafsi yako” ndiyo amri kuu, anasema Yesu.

Amri kuu: Upendo kwa Mungu na jirani.
Amri kuu: Upendo kwa Mungu na jirani.

Jibu la Yesu ni muunganiko wa amri mbili: ya kwanza yatoka Kumb. 6:5 na ya pili yatoka Walawi 19:18. Kwa kadiri ya jibu la Yesu Amri kuu kuliko zote ni UPENDO: Upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani. Kushika amri ya kutahiriwa, au kushika Sabato au kutoa sadaka hekaluni hakutakuwa na maana yoyote kama hazituongozi kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Sehemu hizi mbili za amri iliyo kuu zinategemeana: Ukimpenda Mungu utampenda jirani yako na ukimpenda jirani yako utampenda Mungu: “Mtu akisema ‘Nampenda Mungu,’ naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” (1 Yoh. 4:20). Tutampenda Mungu kwa kushika amri zake, kwa kutumia nguvu na rasilimali zetu kumtumikia Yeye pekee, kwa kumtumainia Yeye tu, kwa kuwa na imani kwake, kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya Kanisa lake na kwa kusikitikia dhambi. Tumpende mazima mazima (totally): kwa moyo wetu wote, kwa roho yetu yote na kwa akili zetu zote. Yesu anasisitiza pia upendo kwa jirani. Jirani yangu ni nani? Jirani yangu ni binadamu mwenzangu ambaye naye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kigezo cha mtu kuwa jirani yangu hakipaswi kuwa utaifa (kama ilivyokuwa kwa Wayahudi), ukabila, vigezo vya kiuchumi, kigezo cha dini au hadhi yake katika jamii. Yesu ametupa kipimo cha upendo kwa jirani. Yesu hakusema “mpende jirani yako” bali mpende jirani yako “kama nafsi yako.” Inawezekana baadhi yetu tunawapenda jirani zetu, lakini Je, tunawapenda kama nafsi zetu? Je, tunawahangaikia kama tunavyojihangaikia wenyewe? Je, tunawathamini na kuwajali kama tunavyojithamini na kujijali wenyewe? Tunaguswa na matatizo yao kama tunavyoguswa na matatizo yetu? Sifa ya upendo wa kweli ni kujitoa sadaka na kuumia. Mt. Mama Theresa wa Calcutta anasema “Penda Mpaka Uumie” (Love until it hurts). Tena anasema “Ukipenda mpaka kuumia hutahisi maumivu bali furaha.” Yesu alitupenda sana hata akajitoa sadaka na akaumizwa msalabani. Upendo wa kweli hutafuta mafaa ya wote, hutazama mahitaji ya wengine na hasa wanyonge; upendo wa kweli unajitoa sadaka kwa ajili ya Mungu na watu; upendo wa kweli hautafuti sifa; upendo wa kweli hauna mipaka na wala haufi. Dominika Njema

27 October 2023, 07:40