Tafuta

Ujumbe huu umefumbatwa na maneno ya Yesu: “Mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na Kaisari yaliyo yake Kaisari.” Ujumbe huu umefumbatwa na maneno ya Yesu: “Mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na Kaisari yaliyo yake Kaisari.”  

Tafakari Dominika 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Dini na Serikali Halali: Utii Mkamilifu

Licha ya kuwa kwa ubatizo tumekuwa raia wa ufalme wa Mungu mbinguni, maadamu bado tuko duniani tunawajibu wa kuujenga ufalme wa Mungu huku tukizitii mamlaka za falme za kidunia zilizo halali. Ujumbe huu umefumbatwa na maneno ya Yesu: “Mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na Kaisari yaliyo yake Kaisari.” Na pale inapotokea Kaisari anakuwa tishio katika kutimiza mapenzi ya Mungu tusiogope maana Mungu daima atatupigania tutakapomuita kwa matumaini

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 29 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika ya 28 mwaka A yalitukumbusha kuwa kwa ubatizo tumestahilishwa kuingia katika karamu ya ufalme wa Mungu mbinguni. Masomo ya dominika hii yanatueleza kwamba licha ya kuwa kwa ubatizo tumekuwa raia wa ufalme wa Mungu mbinguni, maadamu bado tuko duniani tunawajibu wa kuujenga ufalme wa Mungu huku tukizitii mamlaka za falme za kidunia zilizo halali. Ujumbe huu umefumbatwa na maneno ya Yesu: “Mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na Kaisari yaliyo yake Kaisari.” Na pale inapotokea Kaisari anakuwa tishio katika kutimiza mapenzi ya Mungu tusiogope maana Mungu daima atatupigania tutakapomuita kwa matumaini kama wimbo wa mwanzo unavyohimiza tukisema; “Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, utege sikio lako ulisikie neno langu. Ee Bwana, unilinde kama mboni ya jicho, unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako” (Zab. 17:6, 8). Nasi daima tuombe neema zake tuweze kuyatimiza mapenzi yake kama sala ya mwanzo inavyohimiza kusema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuwezeshe kufuata daima mapenzi yako matakatifu na kuitumikia fahari yako kwa moyo mnyofu”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 45:1, 4-6). Katika somo hili tunasikia ahadi za Mwenyezi Mungu kwa Koreshi mfalme mpagani, alipomchagua na kumwita awe chombo chake cha kuwatoa Wayahudi toka utumwa wa Babeli. Kwanza kabisa kuitwa na kutumwa kwake ni fundisho kuwa Mungu wa Israeli ni Mungu wa mataifa yote na ni mkuu juu ya miungu yote. Pili ahadi alizompa Koreshi za ulinzi na ushindi dhidi ya mataifa mengine – adui zake – Mungu alizitimiza na hivyo kudhibitisha ukuu wake. Ndiyo maana zaburi ya wimbo wa katikati inaimba hivi; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, mwimbieni Bwana nchi yote, wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake.  Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana, na wa kuhofiwa kuliko miungu yote. Maana miungu yote ya watu si kitu, lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu” (Zab. 96: 1, 3-5, 7-10).

Tunapaswa kumtii Mungu kuliko mwanadamu.
Tunapaswa kumtii Mungu kuliko mwanadamu.

Koreshi mfalme akiongozwa na Mungu aliweza kuwarudisha Waisraeli katika nchi yao wakalijenge upya Hekalu na mji wao wa Yerusalemu. Tukio hili lilikuwa kinyume kabisa na matarajio ya waisraeli kwani wao waliotegemea kwamba siku moja wangekombolewa na kuwekwa huru na mfalme kutoka katika nyumba ya Daudi. Hii inatuonyesha kuwa mpango wa Mungu kwa mwanadamu ni fumbo ambalo mwanadamu kwa akili zake hawezi kulielewa bila Mungu mwenyewe kumfunulia. Na Mungu katika kutimiza mipango yake anaweza kuwatumia viongozi wa kisiasa kwa kuwapa mamlaka, nguvu na uweza. Hivyo mamlaka halali ya kidunia yanatoka kwa Mungu na zinapaswa kuheshimiwa. Lakini zikikengeuka na kuwa ovu, zinapaswa kukemewa, kuonywa na kurekebishwa na wale ambao Mungu anawachagua na kuwaangazia mwenyewe kwa kazi hiyo. Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike, (1Thes. 1:1-5). Katika somo hili Mtume Paulo kwa niaba ya Silwano na Timotheo anawapongeza Wathesalonike kwa kuipokea Injili na kuishi katika imani, matumaini na mapendo. Zaidi sana Mtume Paulo anaeleza furaha yake kwa kazi ya uinjilishaji ilivyofanikiwa kwa nguvu, uweza na maongozi ya Roho Mtakatifu. Kwetu sisi anatukumbusha kusali na kumshukuru Mungu daima kwa neema anazotujalia na pia tukumbuke daima kuwa kazi yeyote ya Mungu inayofanyika kwa maongozi ya Roho Mtakatifu huzaa matunda mema.

Utii kwa Mungu kwanza na pili ni kwa binadamu
Utii kwa Mungu kwanza na pili ni kwa binadamu

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 22:15-21). Sehemu hii ya Injili inaweka wazi wajibu wa kuzitii mamlaka ya kidunia na kutimiza mapenzi ya Mungu. Mafarisayo walipomwuliza Yesu kuhusu uhalali wa kulipa kodi, Yeye aliwajibu akionyesha mambo haya mawili. Kwanza, kwa vile wanayo sarafu ya Kaisari ni wazi kuwa wamekubali mamlaka yake, hivyo watimize wajibu wao kwake, walipe kodi. Pili, wajibu wao kwa Mungu isiwe sababu ya kutotimiza wajibu wao kwa serikali. Lakini kiundani zaidi swali la Mafarisyo liliongozwa na chuki, hiyana na unafiki kwani lilikuwa ni swali la mtego kutafuta namna ya kumshitaki Yesu ili ahukumiwe na kuuawa kwa kupanga kumuingiza katika malumbano kuhusu ulipaji wa kodi. Historia inasimulia kuwa Wisraeli walipokuwa uhamishoni Babeli walilipa kodi kwa mfalme wa Babeli. Baada ya kurudi kutoka uhamishoni Babeli waliendelea kulipa kodi kwa mfalme Koreshi wa Uajemi. Nyakati za Yesu walilipa kodi kwa Kaisari mfalme wa Kirumi na pesa iliyotumika kulipa kodi ilikuwa ni pesa ya Kirumi ambayo ilikuwa na sanamu ya Kaisari aliyeheshimiwa kama mungu wao. Hali hii kwa Myahudi ilikuwa ni kufuru na kuvunja amri ya kwanza ya kutokuabudu miungu mingine.  Hivyo majadiliano mazito yaliibuka kati ya viongozi wa kisiasa na viongozi wa kidini kuhusu uhalali wa Myahudi kulipa kodi kwa Serikali ya kikoloni. Kikundi cha Wazeloti walipinga ulipaji kodi kwa Warumi kwa kuwa kufanya hivyo ni dhambi ya kuabudu miungu mingine. Kikundi cha Waherodi walisema ni halali kwa Myahudi kulipa kodi kwa Warumi na wao ndio walikuwa wakusanya kodi na watoza ushuru. Kumbe swali hili: “Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi ama sivyo?” (Mt. 22:17) ni swali la mtego na uchonganishi. Maana Yesu angesema si halali, angefanya kosa la uhaini na kustahili adhabu ya kifo, na kama angesema ni halali angepingana na amri ya kwanza ya Mungu ya kutokuabudu miungu mingine maana kulipa kodi ilifananishwa na kumuabudu Kaisari aliheshimiwa kama mungu ndiyo maana sarafu ya kulipia kodi ilikuwa na chapa na anwani yake, ishara ya kumuabudu yeye.

Tujaliwe riziki hapa duniani na hekima na mambo ya mbinguni.
Tujaliwe riziki hapa duniani na hekima na mambo ya mbinguni.

Jibu la Yesu; “Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu” (Mt. 22, 21), ni la nyakati zote nalo linatukumbusha wajibu wetu wa kutii mamlaka halali ya kiserikali inayofanya yaliyo halali kwa maendeleo ya watu wake. Mitume Petro na Paulo, walishatoa maelekezo makini ya kutuongoza jinsi tunavyopaswa kujihusisha na mamlaka za kiraia: wakristo tunapaswa kuheshimu na kutii mamlaka halali (Rum. 13:1; 1Pet. 2:13-14); kuziombea katika utendaji wake (1Tim. 2: 1-2), na kulipa kodi halali (Rm.13:7). Ni pale tu, mamlaka ya kisiasa inapotoa amri ambayo ni kinyume na amri na mpango wa Mungu, wakristo tunalazimika kutoitii tukiongozwa na kauli hii ya mtume Petro; “Tunapaswa kumtii Mungu kuliko mwanadamu” (Mdo 5:29). Kumbe dini na Serikali havipaswi kupingana kwani ni taasisi mbili ambazo zinamshughulikia mtu yuleyule katika kumletea maendeleo ya kimwili na kiroho ili aweze kuishi maisha mema na ya kumpendeza Mungu. Lakini daima tunapaswa kukumbuka kwamba licha ya kuwa tuko raia wa falme hizi mbili: ufalme wa Mungu mbinguni unachukua nafasi ya kwanza na maandalizi yake yanaanza na ufalme wa dunia tunakoishi kwa mda tu. Basi kuwa falme za kidunia zina sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya kiutendaji. Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atuangazie tuweze kuzitambua mamlaka zilizo halali na kuzitii huku tukitimiza wajibu wetu kwa Mungu na kwa Kanisa kama sala ya kuombea dhabihu inavyoomba na kusema; “Ee Bwana, tunakuomba utuwezeshe kukutumikia kwa uhuru kwa vipaji vyako. Ututakase kwa neema yako na kwa sadaka hii tunayokutolea”. Nayo sala baada ya komunyo inahitimisha kusema; “Ee Bwana, utuwezeshe kupata maendeleo ya roho tunaposhiriki mara nyingi mambo haya matakatifu. Tujaliwe riziki za hapa duniani na hekima katika mambo ya mbinguni”. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari Dominika 29
20 October 2023, 15:13