Tafuta

2022.11.13 Pranzo con i Poveri

Tafakari Dominika 28 ya Mwaka A wa Kanisa: Vazi la Arusi: Upendo

Liturujia ya Neno la Mungu imesheheni ujumbe wa matumaini na furaha kwa watu wa Mungu; ujumbe wa imani na faraja ambako Mwenyezi Mungu atawafanyia watu wake karamu ya vinono, karamu ya divai, atafutilia mbali mauti hata milele na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zao zote na hivyo kuwawezesha kushangilia na kufurahia wokovu wake. Kwa hakika leo hii kuna vilio na machozi mengi sehemu mbalimbali za dunia. Vazi la arusi ni upendo na fadhila.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 28 ya Mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu imesheheni ujumbe wa matumaini na furaha kwa watu wa Mungu; ujumbe wa imani na faraja ambako Mwenyezi Mungu atawafanyia watu wake karamu ya vinono, karamu ya divai, atafutilia mbali mauti hata milele na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zao zote na hivyo kuwawezesha kushangilia na kufurahia wokovu wake. Kwa hakika leo hii kuna vilio na machozi mengi sehemu mbalimbali za dunia. Kuna watu wanalia huko Ukanda wa Gaza, watu wanaendelea kulia kutokana na vita, majanga asili ana hali ngumu ya maisha. Kila upande mwanadamu anaandamwa na hofu ya kifo. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuimarisha imani na matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu, tayari kujiachilia mikononi mwake atakayewakirimia furaha na maisha ya uzima wa milele.  Kwa maana mkono wa Bwana utatulia katika mlima huu. Itakumbukwa kwamba, Mlima ni ishara ya utukufu wa Mungu. Mama Kanisa leo hii anatuhimiza kushiriki katika Karamu ya uzima wa milele, lakini jambo la msingi ni kuwa na vazi la arusi. Ufalme wa Mungu unafananishwa na Karamu kubwa na heri yao wanaoalikwa, wakaitikia na hatimaye kushiriki kikamilifu katika karamu hii. Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa sura na mafano wake, akamkirimia uhuru wa kuchagua mema na mabaya. Leo katika karamu ya uzima wa milele, mwanadamu anaonesha jeuri kwa kutumia vibaya uhuru wake, kwa kutokujali mwaliko, kwa kuwatenda vibaya manabii na hata wamisionari katika ulimwengu mamboleo. Lakini pamoja na matumizi mabaya ya uhuru, Mwenyezi Mungu katika historia ya ukombozi ameendelea kuonesha na kufunua huruma na upendo wake wa daima. Lakini wale waliokataa mwaliko, watawajibika kwa kutumia vibaya uhuru wao.

Vazi la arusi ni upendo na tunu msingi za Kiinjili
Vazi la arusi ni upendo na tunu msingi za Kiinjili

Sharti muhimu la uwepo na ushiriki katika karamu ya maisha ya uzima wa milele ni vazi la arusi. Karamu ni alama ya fadhila, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mungu anaheshimu na kujali uhuru na ushiriki wa watoto wake, kwa sababu huruma na upendo wa Mungu ni dira na mwongozo wa maisha ya mwanadamu na kwamba, imani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Mababa wa Kanisa wanasema, vazi la arusi ni upendo; imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani. “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.” Gal 3:27-29. Hii ndiyo siri ya maisha yenye heri katika Kristo Yesu na mwaliko katika kuambata tunu msingi za Injili na Heri za Mlimani na kielelezo makini cha ushiriki na umoja katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko unaotolewa katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayoendelea mjini Vatican. Leo hii, Mama Kanisa anatuuliza Je, tunalo vazi la arusi, yaani neema ya utakaso tuliyokirimiwa na Mama Kanisa siku ile ya Ubatizo wetu, tayari kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu? Au tunaiadhimisha Ekaristi Takatifu kwa mazoea na kwa kufuata mkumbo? Je, tuna mwabudi Kristo Yesu katika roho na kweli Rej. Yn 4:23.

Ufalme wa Mungu unafananishwa na karamu ya arusi
Ufalme wa Mungu unafananishwa na karamu ya arusi

Mtume Paulo katika Somo la Pili Flp 4:12-14; 19-20 anawaandikia Wafilipi kwamba anajua kudhiliwa, kufanikiwa, kushiba na kuona njaa, lakini anayaweza mambo yote katika yeye amtiaye nguvu, yaani Kristo Yesu. Anawashukuru na kuwapongeza kwa wema na ukarimu waliomtendea katika maisha na utume wake na anakiri kwamba, uweza na nguvu zote zinatoka kwa Kristo Yesu. Paulo Mtume, katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu anaendelea kuwahimiza waamini kujikita katika ukarimu, majitoleo na moyo wa sadaka kwa ajili ya jirani zao. Waendelee kudumisha imani kwa Mungu kwani ndiye Muweza wa yote. Wawe na upendo katika kutangaza na kushuhudia Injili ya faraja na matumaini! Ninawatakieni ushiriki mwema na mkamilifu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili hatimaye, kila mmoja wetu aweze kustahilishwa kuingia katika karamu ya uzima wa milele. “Ee Bwana, tunakuomba neema yako itutangulie daima na kutusindikiza, nayo itubidiishe kutenda mema. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.”

Liturujia D28
13 October 2023, 15:17