Shirika la Kaburi Takatifu linalaani vurugu na mvutano katika Nchi Takatifu!
Na Angella Rwezaula -Vatican.
Shirika la Kaburi Takatifu la Yerusalemu linaungana na Upatriaki wa Kilatini wa Yerusalemu katika mateso ya wakazi wa Nchi Takatifu kwa wakati huu wa vurugu na mvutano mkubwa, ulioibuka Jumamosi tarehe 7 Oktoba 2023 na kusababisha maafa makali kwa watu wasio na hatia. Hayo ni kutoka katika taarifa iliyotolewa na shirika hilo kuwa siku zote limekuwa na msaada kwa Nchi Takatifu, mazungumzo na amani moyoni, na kwa hiyo Shirika hilo linalaani mashambulizi hayo na kuwaombea waathirika na familia zao. Katika taarifa yao inabainisha kwamba: Tunasimama karibu na wanaume, wanawake, watoto na wazee wote ambao, wameathirika bila kuwa na hatia, wanateseka na matokeo ya unyanyasaji huu mbaya. Katika siku hizi ambazo Kanisa linajiandaa kusherehekea sikukuu ya Mama Yetu wa Palestina, msimamizi na mlinzi wa Shirika, Wajumbe wa Shirika hili wanapaswa kujikita katika sala kwa ajili ya amani katika Nchi hii inayoteswa katikati ya nia zao.
Ukaribu wa Baraza la Maaskofu Italia CEI
Na kutoka kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Italia CEI linasema kuwa Mashambulizi dhidi ya Israeli na majibu ambayo yanafuata, na kuongezeka isivyofikirika, yanasababisha maumivu na wasiwasi mkubwa. Kwa njia hiyo wanaelezea ukaribu na mshikamano na wale wote ambao, kwa mara nyingine tena, wanakabiliwa na vurugu na kuishi ndani ya hofu na uchungu. Wanaomba kuachiliwa kwa mateka haraka. Kama anavyotaka Papa Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 8 Oktoba 2023 ambapo alisema: "Mashambulizi na silaha vikomea, hata hivyo tafadhali, na ieleweke kwamba ugaidi na vita havileti suluhisho lolote, bali vifo tu na mateso ya watu wengi wasio na hatia. Vita ni kushindwa: kila vita ni kushindwa!”
Kwa njia hiyo Baraza la Maaskofu Italia wanabainisha kuwa - Tunatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kila juhudi ili kutuliza mambo na hatimaye kuanza njia ya utulivu kwa eneo zima, kuheshimu haki msingi za binadamu. Hiyo Nchi tunayoitambua kuwa Takatifu inastahili amani na haki kudumu, kuwa hatua ya kumbukumbu ya "imani, matumaini na upendo". Damu nyingi tayari imelipwa na mara nyingi sana na watu wasio na hatia. Tunaombea familia za waathirika na majeruhi zipokee faraja zetu. Katika mwezi huu, uliowekwa wakfu kwa sala ya Rozari, tunawaalika wote Jumuiya zetu kuombea amani: "Silaha zinyamaze na mioyo iongoke!" Wamehitimisha taarifa yao kutoka CEI.