Tafuta

Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.  (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Parokia Ni Kitovu cha Uinjilishaji na Sehemu ya Mchakato wa Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara yaani wa kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya: Sala, Sakramenti, Tafakari na Matendo ya huruma, wanapewa malezi na makuzi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Na Ndahani Lugunya, -Dodoma & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Vatican.

Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania pamoja na mambo mengine, kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, sehemu muhimu ya uinjilishaji wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa linaloinjilisha. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni msanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia.”

Parokia ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Parokia ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Parokia ni mahali muafaka pa waamini kujisikia kupenda na kupendwa; mahali pa kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara yaani wa kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, wanapewa malezi na makuzi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha na utume wake. Watu wote wa Mungu wanaitwa, wanatumwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko mpya wa kimisionari.

Parokia ni kitovu cha uinjilishaji wa kina: kiroho na kimwili
Parokia ni kitovu cha uinjilishaji wa kina: kiroho na kimwili

Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, amezindua rasmi Parokia ya Mtakatifu Cecilia Muungano-Ndachi inayohudumiwa na Mapadre wa Shirika la Madonda Matano ya Yesu na kwamba Padre Devid Thawapo wa Shirika la Madonda Matano ya Yesu ametangazwa na kusimikwa rasmi kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia hiyo. Askofu mkuu Kinyaiya ameisimika pia Kamati Tendaji ya Halmashauri ya Parokia teule kuwa sasa Kamati Tendaji ya Parokia ya Mtakatifu Cecilia Muungano-Ndachi, Jimbo kuu la Dodoma. Katika wosia wake, Askofu mkuu Kinyaiya amekazia sana umuhimu wa maisha ya sala kuanzia ngazi ya mtu binafsi hadi jumuiya ya Parokia, Maisha ya Kisakramenti hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho tayari kufisha mizizi ya dhambi au vilema saba vya dhambi. Mababa wa Kanisa wanavitaja vilema saba vya dhambi kuwa ni: majivuno, uroho, uzinifu, hasira, ulafi, kijicho na uzembe. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kutunza ile neema ya utakaso waliyoipokea wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo.

Parokia ni mahali pa: Neno, Sakramenti na Ushuhuda wa imani.
Parokia ni mahali pa: Neno, Sakramenti na Ushuhuda wa imani.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa imara na thabiti katika imani ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwa tayari kuishuhudia katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo thabiti cha imani tendaji, yenye mvuto na mashiko kwa maisha ya watu! Wakristo wajitahidi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake, ili watu wengine waweze kuyaona na hatimaye, kuyaiga matendo yao, tayari kumtukuza Mwenyezi Mungu na kumfuasa Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Kuna waamini 75 walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, wamepigwa chapa ya mhuri wa Roho Mtakatifu, anayewaimarisha kuwa kweli ni askari wa Kristo Yesu, tayari kusimama kidete kuilinda, kuitetea na kuineza imani yao kwa njia ya matendo yenye mvuto na mashiko kwa watu wanaowazunguka. Kwa njia ya Kipaimara, wameimarishwa na sasa wanapaswa kuwajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Waamini waendelee kuboresha maisha yao kwa njia ya sala na ibada; kwa tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma. Wajitahidi kujiunga na vyama vya kitume, vitakavyowasaidia kuimarisha imani na maisha yao ya Kikristo! Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amewataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, watoto wao wanapata Sakramenti za Kanisa. Kwa sasa idadi ya Parokia zinazounda Dekania ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba zimefikia 12 pamoja na Parokia moja ambayo ni teule! Jimbo kuu la Dodoma kwa sasa lina Parokia 52. Waamini wanahimizwa kuitunza Parokia pamoja na Mapadre wanaowahudumia!

Parokia Kitovu cha Uinjilishaji
25 October 2023, 14:12