Tafuta

Askofu Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki la Ifakara, ametoa daraja takatifu ya ushemasi kwa mashemasi 24 kutoka mashirika mbalimbali ya kitawa yanayofanya utume nchini Tanzania. Askofu Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki la Ifakara, ametoa daraja takatifu ya ushemasi kwa mashemasi 24 kutoka mashirika mbalimbali ya kitawa yanayofanya utume nchini Tanzania. 

Majandokasisi 24 Wapewa Daraja Takatifu ya Ushemasi Jimboni Morogoro: Huduma!

Askofu Libena hivi karibuni ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24 kutoka katika Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yanayotekeleza dhamana na wajibu wake wa kitume na kimisionari ndani na nje ya Tanzania. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Jimbo Katoliki la Morogoro. Amewataka Mashemasi wapya katika maisha na utume wao, kumtukuza Mwenyezi Mungu na kuhudumia Matakatifu.

Na Angela Kibwana, - Morogoro

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu imegawanyika katika Madaraja makuu matatu: Daraja ya Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Daraja ya Ushemasi “Diakonia” huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa: Shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha ya wakfu! Utume na dhamana ya Mashemasi katika maisha ya Kanisa ni kwamba, wao ni wasaidizi wa karibu wa Maaskofu mahalia katika huduma ya Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa kadiri ya daraja lao na hasa zaidi wadau wakuu katika utekelezaji wa matendo ya huruma kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, watu ambao Kristo Yesu aliwapatia kipaumbele cha kwanza. Huu ni wito na mwaliko wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake.

Shemasi anawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya Neno na Sakramenti za Kanisa
Shemasi anawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya Neno na Sakramenti za Kanisa

Wito huu ni kwa ajili ya mafao ya Kanisa na wala si fursa ya mtu kujitafuta mwenyewe. Ni katika muktadha huu, Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania, hivi karibuni ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24 kutoka katika Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yanayotekeleza dhamana na wajibu wake wa kitume na kimisionari ndani na nje ya Tanzania. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Jimbo Katoliki la Morogoro. Amewataka Mashemasi wapya katika maisha na utume wao, kumtukuza Mwenyezi Mungu na kuhudumia Matakatifu huku wakiwa chini ya Makuhani kwa ajili ya kumtolea Mungu sadaka ya sifa na shukrani. Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu katika kuwahudumia na kuwatakatifuza watu wa Mungu, ili hatimaye wamjue Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai na hatimaye kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari waamini kumrudia Mungu kwa njia ya Kanisa. Watambue kwamba, wanatenda kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kwa kuwa wahudumu wa Neno la Mungu na maskini. Kumbe, Mashemasi wanapaswa kuwa ni watu wema, wenye kujawa na nguvu ya Roho Mtakatifu na hekima ili waweze kutenda kwa busara na kamwe wasigubikwe na hekima ya dunia hii inayofupishwa kwa maneno “Ponda mali kufa kwaja.”

Mashemasi wajenge urafiki na Kristo Yesu ili kuwahudumia maskini na wanyonge.
Mashemasi wajenge urafiki na Kristo Yesu ili kuwahudumia maskini na wanyonge.

Mashemasi katika maisha na utume wao waongozwe na hekima ya kimungu kabla ya kutenda jambo lolote, ili kuchagua yale mambo yanayomfurahisha Roho Mtakatifu na kuepukana na mambo yale yanayomhuzunisha Roho Mtakatifu. Walimwengu wanahitaji huduma makini kutoka kwa Mashemasi. Hii inatokana na ukweli kwamba, walimwengu wamegubikwa na uchoyo, ubinafsi, uchu wa mali na madaraka, kiasi cha kutokumwangalia Mungu tena. Kumbe, Kanisa linawahitaji Mashemasi watakaotangaza na kushuhudia katika maisha yao kweli za Kiinjili bila woga wala makunyanzi. Huu ni mwaliko kwa Mashemasi wapya kumruhusu Roho Mtakatifu kutenda kazi ndani mwao, ili waweze kuwa kweli ni mwanga na chumvi ya kuyakoleza malimwengu. Mashemasi ni wahudumu wa Neno, viongozi wa sala na huduma kwa maskini na wagonjwa. Huu ni mwaliko kwa Mashemasi kuwatumikia na kuwahudumia watu wa Mungu kwa furaha, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu. Mashemasi wanapaswa kutekeleza huduma yao kwa kuyaishi Mashauri ya Kiinjili: Utii, Ufukara na Useja; mambo wanayopaswa kuyamwilisha katika vipaumbele vya maisha yao, tayari kuzaa matunda mengi. Kwa hakika Mashemasi wamewekwa wakfu kwa ajili kutangaza na kukoleza tumaini la Injili na kamwe wasiwe wasikilizaji tu, bali wahudumu wa Injili.

Askofu Libena ametoa Daraja ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24 Morogoro
Askofu Libena ametoa Daraja ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24 Morogoro

Wakati huo huo, Mheshimiwa Padre Isdory Ndekumanya, Mwenyekiti wa walezi na Makamu wa Askofu Jimbo Katoliki la Morogoro upande wa Watawa, amekazia umuhimu wa ujenzi wa umoja na ushirika kati ya walezi na mafrateri walioko Chuo hapo, ili hatimaye, waweze kufikia ndoto yao ya kuwa ni Mapadre wa Kanisa Katoliki, jambo la msingi ni umoja na ushiriano na wakuu wa Mashirika katika malezi na makuzi ya Majandokasisi. Umoja na ushirikiano huu unapaswa kuonesha na Maaskofu mahalia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Waamini waendelee kusali na kuwaombea Mashemasi wapya ili siku moja waweze kusimama na kuwahudumia watu wa Mungu kama Mapadre. Hii ni changamoto ya kuendelea kutangaza na kushuhudia wema, hekima, busara na maongozi ya Mungu kwa ajili ya kulistawisha Kanisa. Kwa upande wake, Shemasi Evodius Carlos Mtove, OFMCap. A., amewashukuru wazazi na walezi walioshiriki kikamilifu katika mchakato wa majiundo yao kwa hali na mali. Amewaomba waamini kuwakumbuka na kuwaombea ili waweze kuishi na kuhudumia kwa upendo zaidi. WSala na sadaka za waamini ziwasindikize katika huduma kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre
Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre

Mashemasi wapya wanaotumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mungu nchini Tanzania na ulimwengu katika ujumla wake ni: Evodius Carlos Mtove OFMCap, Leonard Lugandya CM, Alberto Mapunda OFMCap, Yohana Joseph Mwamgogo CM, Peter Leopold Ulaya OCD, Sewanyana Joseph CMF, Simon Tumusiime CMF., Setas Amedeus Kereti OFMCap, George Wawero SDS, Nicas Fabian Mrosso OFMCaP, Mwasa Joseph MSFS, Francis Moses SDS, Essau Edward Nyiriri CM, Raphael Edward Kappi OFMCap. Wengine ni Michael Christian Mwambogo OCD, Ken Omondi CMF, Priscus Selestin Bahati OFMCap, Godwin Nanalo MSFS, Jeminus Gosbert Rwiza SDS, Nelson Dominick Shirima CMF, Mubbo Ivan MSFS, Christian Ravelonirina OCD, Lukas Wasembe OFMCap., pamoja na Abraham Mutoro MSFS.

Mashemasi Morogoro
26 October 2023, 14:24