Tafuta

Frt Dominick Merichiro Mahinini aliyekuwa ametwa nyara huko Nigeria. Frt Dominick Merichiro Mahinini aliyekuwa ametwa nyara huko Nigeria. 

Frt.Mechior Mahinini,Kabla hatujapeleka habari njema kwa jirani lituguse

Umisionari ni zawadi kutoka kwa Mungu.Tunapokea bure na ni Mwaliko kutoa bure.Ni zawadi ambayo ndani yake kila mwamini au mbatizwa anatumwa na Bwana wetu Yesu Kristo kupeleka habari njema kwa wengine.Ni maneno ya Frt Melchior Domick Mmisionari na Afrika kutoka Tanzania aliyekuwa ametekwa nyara nchini Nigeria.

Na Angella Rwezaula, - Vatican

Katika Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni 2023 uliongozwa na kauli mbiu: "Mioyo inayowaka moto, miguu inayotembea," ukiwa unahakisi historia ya wafuasi wa Yesu walipokuwa njiani kuelekea Emau, kutoka Injili Luka (rej. Lk 24:13-35), mara tu baada ya kufufuka kwa Bwana. Siku ya Kimisionari kwa mwaka huu, iliadhimishwa Dominika tarehe 22 Oktoba 2023 katika makanisa yote Ulimwenguni kwa matendo mengi kila parokia katika kuenzi siku hii ya utume. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo alikazia kuwa: “Wafuasi hao wawili walikuwa wamechanganyikiwa na kufadhaika, lakini kwa kukutana kwao na Kristo katika Neno na katika kuumega mkate kulichochea ndani yao hamu na shauku ya kuanza tena safari kuelekea Yerusalemu na kutangaza kwamba Bwana alikuwa amefufuka kweli. Katika masimulizi ya Injili, tunaona badiliko hili kwa wafuasi kupitia taswira chache zinazo dhihirika: mioyo yao iliwaka ndani yao waliposikia Maandiko yakielezwa na Yesu, macho yao yalifunguliwa walipomtambua, na hatimaye, miguu yao ikashika njia.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo alibainisha kwamba: “Leo hii, kama ilivyokuwa wakati huo, Bwana Mfufuka anabaki karibu na wafuasi wake wamisionari na kutembea pamoja nao, hasa wanapohisi kuchanganyikiwa, kukatishwa tamaa, kuogopa fumbo la uovu linalowazunguka na kutaka kuwaelemea. Hivyo, “tusijiruhusu wenyewe kupoteza tumaini!” (Evangelii gaudium, 86). Bwana ni mkuu kuliko shida zetu zote, zaidi ya yote ikiwa tutakumbana nazo katika utume wetu wa kutangaza Injili ulimwenguni. Kwa maana mwishowe, utume huu ni wake na sisi si chochote zaidi ya watendakazi wenza wanyenyekevu, "watumishi tusio na faida” (taz. Lk 17:10).

Ushuhuda wa Frt Melchior Dominick Mahinini

Ndugu Msikilizaji/msomaji wa makala hii, ni katika muktadha huo ambapo Vyombo vya Habari Vatican News vilimfikia na kuhojiana na Frt. Melchior Dominick Mahinini wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, wajulikanao (White Fathers) kuelezea juu ya uzoefu wake na maana ya Umisionari. Frt. Dominick Mahinini, kutoka Tanzania bado anaendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa makuu aliyo mtendea mara baada ya kutekwa nyara mnamo tarehe 3 Agosti 2023 na mwenzake Padre Paul Sanogo(Mali) katika shambulio la parokia ya Mtakatifu Luka huko Gyedna Jimbo Katoliki la Minna, Mkoa wa Niger kaskazini ya kati mwa Nigeria na baadaye kuachiliwa huru. Kwa sasa yupo katika kituo chao cha Mafungo huko Nairobi nchini Kenya. Frt. Melchior katika mahojiano hayo anabainisha kuwa: “Umisionari ni zawadi kutoka kwa Mungu. Tunapokea bure na ni Mwaliko kutoa bure (rej. Mt 10,8). Ni zawadi ambayo ndani yake kila muumini au mbatizwa anatumwa na Bwana wetu Yesu Kristo kupeleka habari njema kwa wengine(rej Mt 28:19). Katika zawadi hii Yesu Kristo anatualika kujitoa kikamilifu kuwatumikia wengine kwa maneno na matendo yetu mema. Upendo ndiyo amri kuu ambayo ndiyo lazima itusukume kuwatumikia wenzetu wanaohitaji hizo habari njema za kimungu. Bikira Maria ni mfano mzuri wa mmisionari hodari anayepeleka habari njema kwa Elizabeth. Baada ya kuzipata habari hizo za matumaini toka kwa Mungu kupitia Malaika Gabriel hakuwa mchoyo na kuzificha bali anapeleka kwa jirani yake Elizabeth, (rej. Lk. 1:39 au [Rosari takatifu Matendo ya furaha, tendo la pili). Na ilikuwa ni kauli mbiu aliyochagua Baba Mtakatifu Francisko, iliyoongoza Siku ya Vijana Duniani 2023 (WYD)huko Lisbon 1-6 Agosti.

Mama Maria kama mtume wa kwanza ulivyoeleza ni mfano mzuri kimisionari na hodari katika kupekeka habari njema; je uhusiano wake na yeye hukoje hasa kwa kuzingatia changamoto uliyopitia? Bikra Maria amekuwa upande wangu siku zote. Amekuwa ni mwombezi wangu hasa wakati wa changamoto. Hajawahi kuniangusha pale ninapoomba msaada wake katika utume wangu. Na kwa hiyo kama wamisionari jukumu letu ni kusambaza upendo usio na masharti. Kutangaza Amani, kuleta upatanisho palipo na migogoro na kutangaza Msamaha badala ya chuki. Kwa kumwiga Yesu ni vema tutoe faraja kwa walio jeruhiwa kiroho, kuleta matumaini ya kuiona kesho kwa walio kata tamaa ya kuishi tena. Kuleta uponyaji wa mwili na Roho kwa wagojwa. Pia kuwalea wazee, yatima na wajane kwa kuwasikiliza, kwa kuwa mara nyingi wangetamani wasikilizwe lakini wanatelekezwa tu.

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akikazia juu ya sanaa ya kusikiliza na zaidi wazee vile vijana kwa kuwasindikiza na kuwasaidia kufanya mang’amuzi yao…

Ndiyo kama Kardinali Charles Lavigerie Mwanzilishi wa Shirika letu anavyo sisitiza kwamba, kuwa karibu na watu ambao tumetumwa kwao ni muhimu. Yeye alipendekeza wamisionari wake kuwa vitu vyote kwa watu wote. Kuwa mitume na si chochote ila mitume. Kabla hatujapeleka habari njema kwa jirani zetu ni Bora neno la Mungu lituguse sisi wenyewe tupate uponyaji na baadae twende kuwaponya wengine. Hii ni kwa sababu Mtu hawezi kutoa kitu ambacho hana. Ili kuimarika zaidi katika kazi ya umisionari ni lazima Yesu Kristo awe ndiye kioo chetu (Kiini, kitovu). Inatakiwa tumtazame yeye na kazi zake zote, ziakisi yeye. Lazima tuguswe  vile alivyojitoa kwa ajili ya watu wote bila kujibakiza. Kama wafuasi wake ni muhimu na tuombe hiyo Neema. Pia ni lazima tuwaenzi na kuyaenzi yale wamisionari wa kwanza, wazee wetu walitenda kwa kuongozwa na Mungu. Mafanikio Yao ni lazima yawe kigezo cha kututia Moyo katika utume wetu. Na hivyo kama Utume wa Kanisa kwa vijana ni kweli kwamba unajikita katika mambo makuu matatu hasa ya kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia wafanye mang’amuzi makini katika maisha na wito wao kuanzia chini.Kama wamisionari, tunajua wazi kwamba vijana kiukweli ni amana na utajiri wa Kanisa na Jumuiya nzima inayaowazunguka. Kwa kufanya hivyo hasa ni wazazi kwa kushirikiana vyema na wazee (Babu na Bibi) wanaweza kweli kuwasaidia malezi na mfundo yao ya mwanzo ili yawe bora zaidi na kwa kizazi kipya, kwa kujali mila na utamaduni zinazojikita zaidi katika majadiliano, sanaa ya kusikiliza kama Papa anavyopenda kuhimiza kila wakati katika mikutano mbali mbali na miito yake.

Kwa uzoefu wako wa utume wa kimisionari, jambo la kwanza ili kutimiza wajibu au kupokea utume ni kitu gani ambacho unashauri?

Kwa kuwa kuna Raha na Msalaba katika kuwatumikia wengine ni heri tuanze na Sala pia kwa kuhitimisha na Sala kwa Mwenyezi Mungu. Sala iwe ni ufunguo wa kufungulia Baraka zote kutoka kwa Mungu. Pia iwe ni funguo ya kupambana na changamoto na vizingiti, vyote vinavyoweza kutukatisha tamaa na kuturudisha nyuma kiimani. Bado Mwanzilishi wetu wa Shirika anatueleza kuwa: “Wamisionari lazima waamini kwamba hakuna jambo zito na la kudumu litakalofanywa bila Sala ya uaminifu na kujitolea katika utume.”(Cardinal Charles Lavigerie). Katika Ubatizo wetu hapa tulifanyika kuwa watoto wa Mungu, Makuhani na Manabii. Sote tumetumwa na kupokea zawadi hiyo ya umisionari. Yesu Kristo anatusihi tusiogope wala kuteteleka maana Yeye ndiye nguvu yetu kwani yupo pamoja nasi kila wakati alisema Yeye mwenyewe (rej Mt 28:18-20.) Ni kweli usemayo maana nimeona katika vyombo vya kidigitali hasa katika jukwaa la Youtube ukiwa unapiga kinanda au kufanya mikutano mbali mbali ya kutoa ushuhuda na zaidi, hata siku mara moja ulipoachiwa huru, ulionekana kufurahi Ni kweli kwa sasa ninaendelea kutafakari juu ya Ukuu wa Mungu katika tukio zima na kuendelea kutoa shukrani kwake. Bikira Maria Mama yetu awe ni mwombezi wetu. Amina.

FRT MAHININI NA USHUHUDA WA KIMISIONARI

Ndugu Msomaji wa Vatican News, hayo ndiyo yalikuwa ni mahojiano na Frt. Merchior Dominick, Mahihini  wa Shirika la Wamisonari wa Afrika wajulikanao (White Fathers), lakini kwa kuhitimisha ni vema kama itakupendeza hata kusikiliza mahojiano yake  mara baada ya kuachiwa huru akizungumza na Jugo Media mjini Dar Es Salaam Tanzania, ambayo tunayachapisha hapa.

Ushuhuda Kamili wa Frt Mahinini
30 October 2023, 15:07