Tafuta

Askofu Edward Mapunda: Mtakatifu Yohane Paulo II ni Kielelezo cha Maisha ya Uchaji, Ibada, Imani na Utakatifu Askofu Edward Mapunda: Mtakatifu Yohane Paulo II ni Kielelezo cha Maisha ya Uchaji, Ibada, Imani na Utakatifu 

Askofu Edward Mapunda: Mt. Yohane Paulo II: Uchaji, Ibada, Imani na Utakatifu wa Maisha

Mtakatifu Yohane Paulo II ni kielelezo cha maisha ya Uchaji, Ibada, Imani na Utakatifu kwa Kanisa linalosafiri. Kwa ushuhuda wa maisha yake alidhihirisha imani yake kwa Bwana wetu Yesu Kristo wazi wazi bila hofu na uoga wowote huku akiamini kuwa Kristu daima anabaki kuwa mlinzi na mtetezi wake mbele ya Mungu Baba Mwenyezi (Rej. Mt 10:32). Katika tafakari yake kuhusu maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, Askofu Edward Mapunda alikazia matumaini.

Na Damian Kongwa, - Dar Es Salaam 

Mama Kanisa Mtakatifu kila ifikapo tarehe 22 Oktoba kila mwaka anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yohane Paulo II Papa. Kanisa Katoliki linasadiki katika ushirika pamoja na watakatifu “Communio Sanctorum” kwa kuheshimu kumbukumbu ya wakazi wa mbinguni kwa sababu ya mfano wao kwani kama ushirika kati ya wakristo duniani unavyotusogeza karibu zaidi na Kristo, ndivyo umoja pamoja na watakatifu unavyotuunganisha na Kristo, zinakotoka kama chemichemi, neema zote na uzima wenyewe wa Taifa la Mungu (Rej. KKK 957). Katika ukatoliki wake “Catholicism” Kanisa la mbinguni na duniani linaunganika pamoja kama watoto wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristu (Rej. Efe 3: 14-15). Mababa wa Kanisa katika Mtaguso wa Pili wa Vatican wanafundisha kuwa “ilimpendeza Mungu katika wema na hekima yake kujifunua mwenyewe na kulidhihirisha fumbo la mapenzi yake. Katika fumbo hilo kwa njia ya Kristo, Neno la Mungu aliyefanyika mwili, katika Roho Mtakatifu, wanadamu wanapata njia ya kumwendea Baba na kushirikishwa hali ya kimungu (Rej. Dei verbum 2). Ukristo wetu unatudai kuishi maisha ya utakatifu na amani na watu wote kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Mungu bila ya maisha kama hayo (Rej. Ebr 12:14). Kwa mifano ya maisha ya watakatifu tunakumbushwa siku zote asili, umuhimu, thamani na kusudi la Mungu kwetu huku tukijibidiisha katika tumaini la kurithishwa uzima wa milele mbinguni. Kusanyiko la watakatifu mbinguni linaunda kundi la mashahidi ambao hawachoki kuliombea Kanisa linalosafiri hapa duniani ili liweze kufikia ile taji ya utukufu mbinguni. Wito wa Utakatifu unatudai kukesha siku zote huku tukingojea ujio wa pili wa Bwana Wetu Yesu Kristu (Rej. Mt 24:42).

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alikuwa na Iba kubwa kwa B. Maria
Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alikuwa na Iba kubwa kwa B. Maria

Ni katika muktadha huu, Dominika ya 29 ya Mwaka A wa Kanisa tarehe 22 Oktoba 2023, Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima na kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye ni mwombezi na msimamizi wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II Ununio Jimbo Kuu la Dar es Salaam iliyoambatana na kubariki Grotto ya Mama Bikira Maria.  Katika mahubiri yake yaliyojikita katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, mafundisho kuhusu Mama Bikira Maria na Maadhimisho ya Dominika ya kimisionari, Askofu Edward Mapunda alisisitiza wajibu wa waamini kusimama kidete katika kuchuchumilia utakatifu, kudumu katika ibada kwa Mama Bikira Maria, kuombea shughuli mbalimbali za kimisionari na kuwa wakarimu kwa Kanisa kwa kuchangia utume, ustawi na maendeleo ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II ni kielelezo cha maisha ya Uchaji, Ibada, Imani na Utakatifu kwa Kanisa linalosafiri. Kwa ushuhuda wa maisha yake alidhihirisha imani yake kwa Bwana wetu Yesu Kristo wazi wazi bila hofu na uoga wowote huku akiamini kuwa Kristu daima anabaki kuwa mlinzi na mtetezi wake mbele ya Mungu Baba Mwenyezi (Rej. Mt 10:32). Katika tafakari yake kuhusu maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, Askofu Edward Mapunda alikazia kuwa Mtakatifu Yohane Paulo II anatupatia waamini matumaini ya kuwa Watakatifu na kuufikia uzima wa milele na hivyo kamwe waamini hawapaswi kukata tamaa. Mwenyezi Mungu anataka mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake aufikie uzima wa milele. Ni ukweli kwamba mwanadamu si mkamilifu lakini anakamilishwa kwa neema ya Mungu pekee na msaada wa Roho Mtakatifu.

Kumbukumbu ya miaka 45 tangu Papa Yohane Paulo achaguliwe
Kumbukumbu ya miaka 45 tangu Papa Yohane Paulo achaguliwe

Askofu Edward Mapunda amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa Katoliki linatosha kwa ajili ya uzima wa milele na hivyo waamini hawapaswi kutangatanga na kuyumbishwa katika imani bali wabaki imara katika imani wakifata mifano ya Watakatifu ambao waliweza kushinda vishawishi na mitego ya shetani na hatimaye kufanikiwa kupata tuzo la uzima wa milele mbinguni kama Mtakatifu Yohane Paulo II. Ni wito na mwaliko kwa waaamini wote kuiishi imani na miito yao kwa uaminifu. Waamini wanapaswa kuheshimu utu wa mwanadamu kama vile Mtakatifu Yohane Paulo II alivyojali na kuheshimu uhai wa kila mwanadamu. Kanisa linatutaka kuheshimu si tu maisha yetu binafsi bali pia na maisha ya watu wengine. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa mtetezi wa Amani. Maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II yanatufundisha kuwa watu wa amani nyakati zote huku tukitambua kuwa amani ni tunda la haki, alisisitiza Askofu Edward Mapunda. Sambamba na kusherehekea sikukuu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Askofu Edward Mapunda alibariki Grotto ya Mama Bikira Maria iliyojengwa kwa michango ya waamini kwa kipindi cha miaka miwili tangu mwaka 2021. Mababa wa Kanisa Katika Mtaguso wa Pili wa Vatican wanafundisha kuwa Bikira Maria ni Mama yake Kristo Yesu, ambaye ni mwana wa Baba wa milele. Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kweli kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Kanisa linamwita kuwa ni Eva mpya kutokana na utii wake kwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria ni kielelezo cha Imani na ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kwa imani na utii wake thabiti, Bikira Maria alipewa upendeleo wa pekee kuweza kushiriki kazi ya ukombozi. Askofu Edward Mapunda aliwapongeza waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa majitoleo, sadaka na michango yao katika ujenzi wa Grotto na kuwaasa kuwa watu wa bidii katika Ibada kwa Mama Maria Mama wa Mungu “Theotokos” na Mama wa Kristo “Christokos”. Waamini wanaalikwa kuwa na utamaduni wa Sala na Ibada kwa Mama Bikira Maria, Mama wa Huruma aliye msaada na makimbilio ya wakosefu.

Kumbukumbu ua kutabaruku Kanisa
Kumbukumbu ua kutabaruku Kanisa

Askofu Edward Mapunda aliwakumbusha waamini kuwa Dominika ya 29 ya Mwaka A wa Kanisa imewekwa maalum na Mama Kanisa kuwa Dominika ya Kimisionari. Ujumbe wa Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni unanogeshwa na kauli mbiu “Mioyo inayowaka moto na miguu inayotembea” (Rej. Lk 24:13-35). Baba Mtakatifu anabainisha jinsi ambavyo katika kazi ya kimisionari Neno la Mungu huangaza na kubadili mioyo ya waamini. Kristo Mfufuka bado anabaki na kutembea na wafuasi wake ili wasikate tamaa. Umuhimu wa kulifahamu Neno la Mungu, Sakramenti ya Sadaka ya Yesu Msalabani, ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wawe tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kwa kujikita katika wongofu wa kimisionari. Katika ujumbe huu Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote ulimwenguni kutambua wito wao wa kuwa Wamisionari na kutangaza Neno la Mungu kwa Imani kwa sababu Kristo Yesu mfufuka anaendelea kutembea nao siku zote kama alivyotembea na wafuasi wa Emau. Waamini wanatumwa kutangaza Injili na kumshuhudia Kristo kwa imani na matendo siku zote (Rej. Mt 1:8).  Askofu Edward Mapunda alikazia kuwa Waamini ni wadau wa muhimu sana katika utume wa Kanisa Katoliki ambalo kwa asili yake ni Kanisa la Kimisionari na kuwashukuru kwa michango yao mbalimbali wanayotoa katika kuchangia shughuli za Kimisionari.  Kwa upande wake, Padre Emmanuel Haule, CM Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II Ununio amewaasa wanaparokia kujibidiisha katika Sala na Ibada kwa Mama Bikira Maria kwa kutenga muda na kufika mara kwa mara kwenye Grotto kusali kwa maombezi ya Mama Bikira Maria kwa kufuata mfano wa maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II. 

26 October 2023, 15:11