Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 26 ya Mwaka A wa Kanisa: Toba nw ongofu wa ndani; unyenyekevu; upendo katrika kutekeleza mapenzi ya Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 26 ya Mwaka A wa Kanisa: Toba nw ongofu wa ndani; unyenyekevu; upendo katrika kutekeleza mapenzi ya Mungu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 26 ya Mwaka A: Toba, Upendo, Haki na Unyenyekevu

Katika mwendelezo wa mafundisho ya Kanisa kuhusu upendo, Mtume Paulo leo anatuongezea kipengele muhimu. Kipengele hicho ni kuwa ili kuuishi upendo kikamilifu ni muhimu kuwa mnyenyekevu. Upendo na unyenyekevu ni tunu mbili zinazokamilishana, moja ikiiangazia nyingine na moja ikiijenga nyingine. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na haki! Umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza maisha mapya katika mwanga wa Kristo!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 26 ya mwaka A wa Kanisa.  Masomo kwa Ufupi: Somo la kwanza (Ez 18:25-28) ni kutoka kitabu cha nabii Ezekieli. Ni somo ambalo Mwenyezi Mungu anawaalika watu watubu na kumrudia. Tunapoliangalia vizuri somo hili tunaona kuwa ni kama Mwenyezi Mungu anawabembeleza waisraeli watubu. Anawasihi akiwaonesha kuwa Yeye haonei mtu; mtu mwenye haki anapoiacha njia yake ya haki na kuingia katika maisha ya dhambi, atakufa katika dhambi zake. Bali yule mtu mwenye dhambi akiyaacha maisha yake ya dhambi na kumrudia Mungu, basi ataishi  Kwa nini Mwenyezi Mungu anazungumza hivi kwa kinywa cha nabii Ezekieli? Anazungumza hivi kwa sababu kipindi cha kihistoria cha unabii huu ni kile ambacho waisraeli walikuwa ndio tu wamepelekwa utumwani Babeli. Katika kipindi hicho cha kwanza kwanza cha mateso na mahangaiko ya utumwa, walianza kumnung’unikia Mungu. Walisema Yeye sio mwenye haki, njia zake sio sawa na hawezi kuwatetea dhidi ya watesi wao wanaohatarisha maisha na ustawi wao. Ni hapa Mungu anawajibu na kuwaambia “msiseme kwamba njia za Bwana sio sawa enyi nyumba ya Israeli. Njia za Bwana ni sawa. Ni njia zenu ambazo sio sawa”. Mungu anawakumbusha kuwa Yeye ni mwaminifu na sio kigeugeu hata awaangamize bure. Leo anawaonesha kuwa kupelekwa kwao utumwani ni mwaliko wa toba na kumrudia. Anawasihi watambue kuwa toba yao ndio kuishi kwao.

Toba na wongofu wa ndani
Toba na wongofu wa ndani

Somo la pili (Waf. 2:1-11) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Mtume Paulo anauandika waraka huu akiwa kifungoni Roma. Katika somo la leo anawaandikia kuhimiza upendo wa kindugu kati ya wakristo, upendo anaowaalika kuchota msingi wake katika unyenyekevu wa Kristo ambaye alikuwa yu na namna ya Mungu lakini alijishusha akajinyenyekeza akawa mtii hadi kifo cha Msalaba. Katika mwendelezo wa mafundisho ya Kanisa kuhusu upendo, Mtume Paulo leo anatuongezea kipengele muhimu. Kipengele hicho ni kuwa ili kuuishi upendo kikamilifu ni muhimu kuwa mnyenyekevu. Upendo na unyenyekevu ni tunu mbili zinazokamilishana, moja ikiiangazia nyingine na moja ikiijenga nyingine. Paulo anaonesha kuwa ni unyenyekevu wa Kristo ulioubeba upendo wake mkubwa kwa wanadamu, upendo uliopelekea kujitoa kwake kwa kifo cha Msalaba ili kuwaokoa. Basi mkristo anayetaka kuuishi upendo hana budi kujifunza unyenyekevu.

Upendo wa dhati unasimikwa katika unyenyekevu
Upendo wa dhati unasimikwa katika unyenyekevu

Injili (Mt 21:28-32) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Katika injili hii, Yesu anaeleza kwa njia ya mfano juu ya maana ya kutimiza mapenzi ya Mungu. Mfano anaoutoa ni ule wa baba aliyekuwa na wana wawili: akamwambia wa kwanza “nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu”,akajibu “siendi” lakini baadaye akajirudi akaenda. Wa pili akajibu “ndiyo, naenda” lakini hakwenda.  Mfano huu, Yesu aliutoa kwa wakuu wa makuhani na wazee. Alipenda wao wenyewe wajipime wajihoji na wajihukumu wanachukua nafasi ya mwana yupi kati ya hao wawili katika kuupokea ufalme wa Mungu. Kumbe katika nafasi ya kwanza alipenda kuwaonya juu ya ule tunaoweza kuuita ukigeugeu katika maisha au ile hali ya kusema neno na kutenda lingine. Katika nafasi ya pili, Yesu alitaka kuwaonesha kuwa kuupokea ufalme wa Mungu na kutimiza mapenzi yake ni kuwapokea wajumbe wa Mungu wanaotangaza ufalme huo. Yohane Mbatizaji alipokuja, wao kama wakuu wa makuhani na wazee hawakumpokea lakini wale walioonekana kuwa wadhambi walimpokea. Katika nafasi ya tatu, Yesu anafundisha kuupokea ufalme wa Mungu kwa toba. Ili kuuingia ufalme wa Mungu na ili kuyatimiza mapenzi yake ni muhimu kutembea katika njia ya toba na upyaisho wa maisha. Huu ndio mfano anaotupatia yule mwana wa kwanza ambaye awali alikataa kwenda kufanya kazi shambani lakini baadaye alijirudi akajikosoa akaenda.

Vikwazo: Kumkataa Yesu, Kutimiza Mapenzi ya Mungu na Kutokutubu!
Vikwazo: Kumkataa Yesu, Kutimiza Mapenzi ya Mungu na Kutokutubu!

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kupata ufafanuzi wa masomo ya dominika ya leo, nawaalika tuichote tafakari yetu kutoka katika somo la injili, somo linalotupatia tafakari juu ya ni nini maana ya kutimiza mapenzi ya Mungu. Katika tafakari hii fupi ninapenda tuangalie kutoka katika injili hiyo vikwazo au vizuizi vitatu vinavyoweza kutuzuia kupiga hatua katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Kikwazo cha kwanza ni kumkataa Kristo, cha pili ni kutanguliza matakwa yetu binafsi na cha tatu ni kutokutubu. Injili imetuonesha kupitia mfano wa wale wana wawili kuwa ni vigumu kuyatimiza mapenzi ya Mungu ikiwa tunamkana Kristo. Kumkana Kristo ndio kulikataa Neno lake na kuwakataa wajumbe ambao Kristo mwenyewe anawatuma katika safari ya maisha yetu. Na hiki ni kizuizi katika safari ya kutimiza mapenzi ya Mungu. Kizuizi cha kutanguliza matakwa binafsi kinatokea pale ambapo tunashindwa kuuweka wokovu wetu na wa wenzetu kuwa ni kipaumbele cha kwanza katika maamuzi na chaguzi tunazozifanya katika maisha yetu. Hii hutokea hasa pale ambapo tunashindwa kuona kuona kuwa kila ambacho Mungu anatuagiza kufanya kinahusiana moja kwa moja na wokovu wetu na wa wenzetu. Inatokea kuwa wokovu huu sisi tunauona kuwa uko mbali sana kuja na hivi kutupa nafasi ya kufanya tuyatakayo sisi kwanza kabla ya kuongozwa na makusudi mapana ya Mwenyezi Mungu. Kikwazo cha tatu cha kutokutubu huvijumuisha vikwazo vyote na kutuzuia kujirekebisha na kutumainia neema ya Mungu katika kurekebisha makosa na udhaifu ambao umetuingiza katika makosa na kupunguza neema ya utakaso ndani yetu. Tafakari ya dominika hii ichochee basi ndani yetu neema na kukuza ari ya kutimiza kwa ukamilifu mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Nakutakia tafakari njema ya dominika ya 26 ya mwaka A Kanisa!

D26 Mwaka A
29 September 2023, 15:30