Tafuta

2023.09.04 Katika ziara ya Kitume Papa alizindua nyumba ya upendo kwa ajili ya kukaribisha wengine. 2023.09.04 Katika ziara ya Kitume Papa alizindua nyumba ya upendo kwa ajili ya kukaribisha wengine.  (Vatican Media)

Dominika ya 25 ya Mwaka A:Mungu yu karibu na watu wake siku zote

Ujumbe wa masomo ya Domenika hii ni wa faraja na matumaini kwani Mungu anajifunua na kutuonyesha jinsi alivyo karibu nasi watu wake siku zote na nyakati zote.Mastahili ya kuurithi ufalme wa Mungu yanatokana na huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika kutimiza nyajibu na ahadi za ubatizo wetu na kuishi kwa upendo.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 25 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya domenika hii ni wa faraja na matumaini kwani Mungu anajifunua na kutuonyesha jinsi alivyo karibu nasi watu wake siku zote na nyakati zote na kila amwitaye na kumwomba msaada wake Yeye humsikiliza na kumpatia mahitaji yake kadiri ya mpango wake na makusudi yake, kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Bwana asema: Mimi ni wokovu wa watu wangu, wakinililia katika taabu yoyote nitawasililiza, nami nitakuwa Bwana wao milele”. Ahadi hii ni kwa wale wote wanaoishi kwa upendo maana upendo ni utimilifu wa sheria zote za Mungu kama sala ya mwanzo inavyosema; “Ee Mungu, umeziweka katiba zote za sheria takatifu katika amri ya kukupenda wewe na jirani. Utuwezeshe kuzishika amri zako tupate kustahili kuufikia uzima wa milele”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 55:6-9). Somo hili linatilia mkazo juu ya ukuu wa huruma ya Mungu kwa watu wake wanaotubu dhambi zao na kumrudia Yeye. Mungu daima yu karibu na watu wake na kwa kuwa ni mwenye huruma, wakitubu na kumrudia Yeye kwa moyo wote, anawasamehe. Ujumbe huu wanapewa waisraeli wakiwa utumwa Babeli. Itakumbukwa kuwa Taifa hili teule la Mungu, lilipelekwa utumwani kwa watu wake kukosa uaminifu kwa Mungu. Wakiwa utumwani na baada ya kutafakari vyema mahusiano yao na Mungu, walitambua kuwa walikosa sana na kwasababu waliona kuwa dhambi yao ni kubwa mno, walikata tamaa, wakakosa matumaini ya kurudi tena katika nchi yao ya ahadi maana walifikiri kuwa Mungu hawezi kuwasamehe uovu wao. Katika hali hii, Mungu kwa kinywa cha nabii Isaya anawafariji na kuwapa matumaini kuwa huruma Yake ni ya milele, hivyo wakitubudu dhambi zao na kuomba msamaha atawasamehe. Nabii Isaya anasisitiza kusema; “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu; mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; na amrudie Bwana. Naye atamrehemu; na arejee kwa Mungu wetu, naye atamsamehe kabisa”.

Huu ni ujumbe wa faraja na matumaini kwetu kuwa daima Mungu yu karibu nasi naye ni mwenye huruma. Hivyo tukitubu dhambi zetu, tukaghairi uovu wetu na kumrudia Yeye kwa moyo wote, atatusamehe maana Yeye hatendi kama binadamu atendavyo kwani Nabii Isaya anasema kuwa; Mawazo ya Mungu si mawazo yenu na njia zake si njia zenu. Kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia Zake zi juu sana kuliko njia zenu na mawazo Yake kuliko mawazo yenu. Kumbe katika shida na mahangaiko yetu hatupaswi kukata tamaa na kusema kuwa Mungu yu mbali nasi hatusikilizi bali tumtafute maadamu anapatikana, tumwite maana yu karibu atatusikiliza, lakini sharti ni moja kuziacha njia zetu mbaya na mawazo yetu maovu na kumrudia Yeye kwa moyo wa majuto na toba, Naye ataturehemu na kutusamehe kama anavyosisitiza mzaburi katika wimbo wa katikati (Zab. 145:2-3, 8-9, 17-18).

Somo la pili ni la waraka wa mtume Paulo kwa wafilipi (Flp. 1:20-24, 27). Mtume Paulo aliandika barua hii akiwa gerezani akiishukuru jumuiya ya wafilipi kwa msaada waliompatia. Katika sehemu ya barua hii ambayo ni somo la pili dominika ya 25A, anaeleza kilicho ndani ya moyo wake kwa wakristo wafilipi kuwa ndani mwake kuna pande mbili zinazokinzana; kwa upande mmoja ni kutaka kuendelea kuhubiri injili, habari njema ya wokovu ili watu wengi zaidi wawezi kuongoka na kuingia katika ufalme wa Mungu na kwa upande mwingine ni hamu ya kuiona siku ya kifo chake atakapopa nafasi ya kuwa na Kristo milele yote mbinguni ikiwadia upesi. Katika hali hii Mtume Paulo anajimwaga na kujikabidhi mzima mzima, roho, mwili na akili yote mikononi mwa Mungu akisema kuwa iwe ni kuishi au kufa yote ni sawa, maadamu Kristo atukuzwe. Basi nasi tunaalikwa kujimwaga wazima wazima, kujiachilia na tukijikabidhi kwa Mungu katika hali zote maana tukiwa naye tuko salama zaidi.

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 20:1-16). Katika sehemu hii ya injili Yesu akitumia mfano wa vibarua, anatufundisha kuwa wema wa Mungu upo kwa watu wote hata kwa wakosefu wanaotubu, kinyume na mafundisho ya Mafarisayo waliofikiri kuwa wokovu ni kwa ajili tu ya taifa teule la Israeli, tena sio kwa waisraeli wote bali kwa wale tu wanaoshika sheria na amri za Mungu kikamilifu kama zilivyotolewa na Musa, wao wakiwa ni mfano bora. Katika kutoa fundisho hili, Yesu anamfananisha Mungu na mmiliki wa shamba la mizabibu anayewaajiri watu kufanya kazi katika shamba lake kwa muda tofauti tofauti. Kadiri ya desturi ya kiyahudi, ilipofika jioni ilikuwa ni lazima mtu alipwe kwa kazi aliyoifanya. Tunasoma hivi katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati; “Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni ndugu yako mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Bwana dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi” (Kumb. 24:14-15). Na kiwango ambacho mtu alilipwa ilipaswa walau kimsaidie kupata mahitaji muhimu ya siku moja ambayo gharama zake zilikuwa ni denari moja. Ndiyo maana mmiliki wa shamba la mizabibu katika Injili alipatana na vibarua wake kuwalipa denari moja kwa kila mmoja. Na ni kweli ilipofika jioni aliwalipa wote kila mmoja denari moja licha ya kuwa walifanya kazi kwa mda tofauti tofauti. Hii ni tofauti kabisa na uelewa wetu sisi wanadamu ambapo malipo ni lazima yalinganishwe na uzoefu wa wa kazi, kiasi cha kazi na muda wa kufanya kazi. Ndiyo maana vibarua walioajiriwa mapema walimnung’unikia mwajiri wao kwa kuwalipa kiwango sawa na wale waliofanya kazi kwa mda mfupi, ambapo kimsingi wanaolalamika hawana sababu kwa kuwa haki yao wameipata kadiri ya makubaliano kwamba watapokea denari moja.

Fundisho kuu tunalopata katika mfano huu ni kuwa wema wa Mungu ni sawa kwa wanadamu wote, hauna mipaka, kipimo cha mda wala ubaguzi wowote ule maana mbele za Mungu, binadamu wote ni sawa na hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine. Mbele za Mungu hatuna haki ya kudai chochote kutoka kwake maana yote tuliyonayo ni vyake; maisha yetu na vitu tulivyo navyo ni zawadi kutoka kwake. Na kuingia katika ufalme wa Mungu kunategemea tu huruma yake maana hakuna binadamu aliye mkamilifu ambaye anaweza kudai haki ya kuurithi. Zaidi sana kuingia katika ufalme wa Mungu ni zaidi ya kushika sheria. Ndiyo maana kijana tajiri alipomwendea Yesu na kumwuliza nifanye nini niweze kuupata uzima wa milele, Yesu alimjibu shika amri. Naye akamjibu nimezishika tangu ujana wangu. Yesu akamwambia nenda ukauze vyote ulivyo nanyo uwape maskini nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate. Yule kijana akaondoka kwa huzuni. Kumbe kushirika sheria tu haitoshi. Mwanadamu hawezi kudai haki ya kuupata uzima wa milele kwa kushika sheria tu.  Mastahili ya kuurithi ufalme wa Mungu yanatokana na huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika kutimiza nyajibu na ahadi za ubatizo wetu na kuishi kwa upendo.

Basi tujitahidi kujiepusha na dhambi za wivu kwa kumlalamikia Mungu kwa wema na huruma yake isiyo na mipaka. Bali sisi tujikite zaidi katika kutenda matendo mema kwa moyo wa upendo tukiwasaidia watu wengine wapate mahitaji yao ya kila siku kadiri ya uwezo aliotujalia Mungu nasi tutapata dhawabu yetu mbinguni.  Na hivyo sala ya kuombea dhabihu inayosema: “Ee Bwana, tunakuomba uwe radhi kuzipokea dhabihu zetu sisi taifa lako; utujalie kupata katika sakramenti takatifu hayo tunayoungama kwa imani” itasikilizwa na Mungu. Nayo sala baada ya Komonyo inayosema; “Ee Bwana, sisi unaotuburudisha kwa sakramenti zako, utuinue kwa msaada wako wa siku zote, tupate matunda ya ukombozi kwa njia ya mafumbo yako na mwenendo wetu” itapata kusikilizwa.

Tafakari ya Dominika 25 ya Mwaka A
21 September 2023, 16:09