Tafuta

Masomo ya dominika hii yanatilia makazo kuhusu utulivu wa Mungu katika kujifunua na kujionesha kwake kwa mwanadamu anayehangaika na papara nyingi katika maisha yake. Masomo ya dominika hii yanatilia makazo kuhusu utulivu wa Mungu katika kujifunua na kujionesha kwake kwa mwanadamu anayehangaika na papara nyingi katika maisha yake.   (ANSA)

Tafakari Dominika 19 ya Mwaka A wa Kanisa: Imani ya Kweli na utulivu wa Mungu

Makazo ni kuhusu utulivu wa Mungu katika kujifunua na kujionesha kwake kwa mwanadamu anayehangaika. Hili linajidhihirisha jinsi Mungu alivyomtokea Eliya na kuongea naye katika upepo wa utulivu katika mlima horebu na jinsi Yesu alivyotuliza dhoruba katika ziwa Galilaya na kuwaokoa wanafunzi wake, huku Petro akiomba naye aweze kutembea juu ya maji, lakini kwa papara na kuona shaka baada ya Yesu kumruhusu kutembea juu ya maji alianza kuzama: Imani haba

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 19 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatilia makazo kuhusu utulivu wa Mungu katika kujifunua na kujionesha kwake kwa mwanadamu anayehangaika na papara nyingi katika maisha yake. Hili linajidhihirisha jinsi Mungu alivyomtokea Eliya na kuongea naye katika upepo wa utulivu katika mlima horebu na jinsi Yesu alivyotuliza dhoruba katika ziwa Galilaya na kuwaokoa wanafunzi wake, huku Petro akiomba naye aweze kutembea juu ya maji, lakini kwa papara na kuona shaka baada ya Yesu kumruhusu kutembea juu ya maji alianza kuzama kwa kuwa na imani haba. Imani thabiti kwa Mungu ni ya muhimu ili kupata msaada wake. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Wafalme (1Waf. 19:9, 11-13). Somo hili linatusimulia jinsi Nabii Eliya alivyokutana na Mungu katika pango la mlima Horebu alipokimbilia kwenda kujificha, kujiepusha na adha na dhuluma za papara za Yezebeli mke wa Ahabu, mfalme wa Israeli aliyetafuta kumuua. Sababu za kutaka kumuua ni kuuwawa kwa manabii wa Baali na watu baada ya kushindwa katika shindano la kujua Mungu wa kweli ni yupi kati ya Mungu wa Israeli na Baali, ambapo Elia alishinda baada ya Mungu wa Israeli kushusha moto toka mbinguni na kuzichoma dhabihu zilizoandaliwa kitu ambacho Baali alishindwa kufanya alipoombwa na manabii wake. Adha na dhahama hizi za kutaka kuuawa anazishuhudia Elia mwenyewe baada ya kuulizwa na Mungu; “Unafanya nini hapa?” Naye akajibu; “Naona uchungu na wivu, ewe Mungu wa majeshi, kwasababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!” (1Waf. 19:10).

Petro alianza kuzama kwa kuwa na imani haba!
Petro alianza kuzama kwa kuwa na imani haba!

Itakumbukwa kuwa nyakati fulani katika Agano la Kale, Mungu alijifunua kwa watu wake, katika ngurumo na radi, moto na matetemeko ya nchi ili kuwafanya watu watambue ukuu na uwezo wake. Eliya alipokuwapo ndani ya pango palitokea dhoruba kubwa, radi na tetemeko la nchi, lakini Mungu hakujitokeza kwake kupitia ishara hizi, bali alijionesha katika upepo mtulivu. Mungu akaongea na Eliya kama mtu anavyoongea na rafiki yake; kwa sauti ya upole na utulivu akimhakikishia kuwa yupo pamoja naye hata kama yuko kimya. Mungu anamwonyesha Eliya kuwa hawakomboi watu kwa kuwapatiliza kwa moto, matetemeko, upepo mkali, kwa kuwatesa au kuwauwa. Yeye si Mungu wa kisasi bali ni Mungu wa msamaha na amani. Katika hali hii, imani ya nabii Eliya kwa Mungu iliimarika, akawa na ujasiri wa kusimama mbele zake na kumshuhudia kuwa Yeye ni Mungu wa kweli ndiyo maana anakumbukwa kama nabii mkubwa zaidi baada ya Musa. Itakumbukwa kuwa ni Musa na Eliya ndio walitokea na kuongea na Yesu kuhusu kifo chake katika tukio la kugeuka sura kwa Yesu mlimani Tabor (Mt. 17:3). Imani ya Eliya kwa Mungu ilimfanya awe mwaminifu katika kazi ya Mungu. Naye Mungu alikuwa upande wake daima kama wimbo wa mwanzo unavyosisitiza kusema; “Ee Bwana, ulitafakari agano lako, usisahau milele uhai wa watu wako walioonewa. Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, usiisahau sauti ya watesi wako” (Zab. 74 :20, 19, 22, 23).  Kumbe ni katika utulivu na ukimya wa kutafakari, ndipo Mungu anajitokeza na kuongea nasi.

Mwenyezi Mungu anaongea na waja wake kutoka katika dhamiri zao
Mwenyezi Mungu anaongea na waja wake kutoka katika dhamiri zao

Ili kuisika sauti ya Mungu akiongea nasi tunahitaji sio tu ukimya wa kutokuongea bali pia utulivu wa nafsi na akili katika kumtafakari Mungu na makuu yake. Kumbe katika kusali hatupaswi kupiga kelele, kulialia na kurukaruka kwa fujo mbele za Mungu, bali kwa moyo tulivu na wa unyenyekevu, tunapaswa kusali mbele za Mungu. Tukumbuke daima kuwa Mungu ni Baba yetu mwema anayetusikiliza kila tumwitapo sisi wanae kama sala ya mwanzo inavyotilia mkazo ikisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, sisi tunathubutu kukuita baba. Ututhibitishie moyoni mwetu neema ya kuwa wana wako, tupate kustahili kuingia katika urithi uliotuahidia”. Somo la pili ni la Waraka Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 9:1-5). Katika somo hili Mtume Paulo kwa kuapa kuwa hasemi uongo bali kwetu tupu na Roho Mtakatifu akiishuhudia dhamiri yake, anaelezea huzuni na maumivu aliyonayo moyoni kwa kuwa Wayahudi ndugu zake, waliokirimiwa kipekee na Mungu kwa kuchaguliwa na kuandaliwa vizuri kumpokea Yesu Kristo Masiya aliyezaliwa kwao, wao walimkataa Yeye aliye njia pekee ya wokovu ambaye torati na manabii walitabiri kuja kwake na ametoka katika ukoo wao. Ni mwaliko kwetu kujitafakari pia kama mienendo yetu baada ya kulipokea neno la wokovu, Bwana wetu Yesu Kristo kwa sakramenti ya ubatizo, na tunaendelea kumpokea katika Ekaristi Takatifu, mwili na damu yake, chakula chetu cha kiroho na mafundisho mengi tunayopata, kama tunaishi kweli haya tuliyoyapokea au tumekaza shingo na kuwa wakaidi. Kama tumekuwa wakaidi, basi tujue kuwa tumepotea, na huzuni hii ya Mtume Paulo inatuhusu na sisi.

Tunahitaji imani thabiti ili kupata huruma na msaada wa Mungu
Tunahitaji imani thabiti ili kupata huruma na msaada wa Mungu

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 14:22-33). Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi Yesu alivyotembea juu ya maji ili kudhihirisha umungu wake, kwani kadiri ya Agano la Kale, watu walisadiki kuwa ni Mungu tu ndiye mwenye mamlaka yote juu ya maji kama alivyofanya kwenye bahari ya shamu alipowaokoa Waisraeli dhidi ya mkono wa Farao na majeshi yake yote, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kutembea juu yake bila kuzama. Kutembea kwake Yesu juu ya maji kulikuwa hakikisho kwa mitume wake kuwa yeye ni Mungu. Ndiyo maana walimsujudia wakisema; “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu”. Petro baada ya kuona hivyo aliomba naye atembee juu ya maji. Maana yake alitaka kufanana na Mungu. Yesu alimruhusu. Lakini kwa kuwa yeye si sawa na Mungu na kwasababu ya imani yake kuwa haba, aliona shaka akaanza kuzama, kisha akamlilia Yesu na kumwambia Bwana niokoe. Yesu akanyoosha mkono wake, akamshika, akamwokoa asizame. Nasi kila mara tunapokuwa katika taabu na mahangaiko, tunapoona tunazama na hatuna msaada mwingine, tuikumbuke hii sala ya Petro na kusema; “Bwana niokoe”. Naye atanyoosha mkono wake na kukuinua usizame na kuaibika. Tukumbuke daima kuwa Kristo yupo karibu nasi kila wakati kutusaidia katika shida zetu. Basi tumwombe Mungu atulize ghasia za Maisha yetu. Tukumbuke daima kuwa baada ya dhoruba kuna utulivu; baada ya dhiki kuna faraja. Ndiyo maana sala baada ya Komunio inahitisha kusema; “Ee Bwana, sakramenti yako tuliyopokea ituokoe na kututhibitisha katika nuru ya kweli yako”. Huu ndio utimilifu wa sala ya kuombea dhabihu inayosema; “Ee Bwana, uwe radhi kuzipokea dhabihu za Kanisa lako. Umetupatia kwa huruma dhabihu hizi ili tukutolee; na kwa enzi yako unavifanya kuwa fumbo la wokovu wetu”. Hili ndilo tumaini la maisha yetu ya kuingia katika wokovu wa Mungu mbinguni milele yote. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D19 Mwaka A
10 August 2023, 14:41