Tafuta

Askofu Simon Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda na Dk.Paulo Ruffini,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano,wakati wa Mkutano Mkuu wa AMECEA,Dar Es Salaam 2023 Askofu Simon Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda na Dk.Paulo Ruffini,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano,wakati wa Mkutano Mkuu wa AMECEA,Dar Es Salaam 2023 

Kanisa la Tanzania limeenzi miaka 60 ya Hati ya Mtaguso II wa Vatican!

Ni kwa namna ipi nzuri tutaweza kuiishi hati ya Sacrosanctum Concilium ya Mtaguso II wa Vatican?Ni swali ambalo lilijibiwa katika hotuba ya Askofu Masondole wa Jimbo la Bunda Tanzania wakati wa Kongamano kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya Hati ya Sacrosantum Concilium ya Mtaguso wa Pili wa Vatican,kuanzia Julai Julai 31 hadi 4 Agosto.

+Simon C. Masondole,PhD SL, Askofu wa Bunda.

Katika fursa ya maadhimisho ya miaka 60 ya Hati ya Sacrosantum Concilium ya Mtaguso wa Pili wa Vatican, Kanisa la Tanzania limeandaa Kongamano kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 4 Agosti 2023, katika makao makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC). Katika Kongamano hilo Askofu Simon C. Masondole, wa jimbo Katoliki la Bunda, Tanzania  alitoa hotuba yake kwa washiriki wa kongamano hilo, ambao walikuwa ni mapadre, watawa, na  walei wa vyama vya kitume kutoka sehemu mbali mbali za Majimbo ya Tanzania. Radio Vatican, inachapisha hotuba yake kamili ambayo alijikita na mada: Ni kwa  namna ipi nzuri tutaweza kuiishi hati ya Sacrosanctum Concilium ya Mtaguso II wa Vatican?

Katika kuishi na kuadhimisha miaka 60 ya Sacrosactum Cconcilium, ni uwezo wa kutawala maamuzi, matendo, kumbukumbu, mawazo na utashi au akili ya mwingine kupitia nguvu ya maamuzi. Vifanano vya concilium ni maneno na matendo kama vile (congressus, coetus, concursus na conventus); yote yakimaanisha kusanyiko au kutano. Toka ilipotolewa hati hii Sacrosanctum Concilium inakuwa ndiyo mwongozo wa maisha ya liturujia ya Kanisa, kusanyiko la waamini na riti (ibada) katika maadhimisho yote ya sakramenti na visakramenti. Miaka 60 ya Sacrosanctum Concilium katika liturujia ya Kanisa la Tanzania kuna mengi ya kusema. Kwa njia hiyo Sacrosanctum Concilium ni jina na hati juu ya liturujia na maadhimisho iliyotungwa na kuandikwa na mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano yaani (Concilium Oecumenicum Vaticanum Secundum) uliodumu kuanzia manmo mwaka 1962 hadi 1965 chini ya Mtakatifu Papa Paulo wa VI. Hati hii ilipitishwa rasmi na mababa wa mtaguso huu kwa kupigiwa kura za ndiyo 2,147 dhidi ya 4 zilizosema hapana na hivyo kutangazwa rasmi na papa Paulo wa VI tarehe 04 Desemba mwaka 1963 kama mwongozo rasmi wa mambo yote yahusuyo maadhimisho na liturujia ya kanisa ikiwa ni hati ya kwanza kati ya 16 tunda la mtaguso huu.

Kwa nini iwe hati ya Kwanza? Mababa wa mtaguso walijitambua kuwa katika kikao hiki walikusanywa na Mungu kama watu wake na kanisa lake ili waitende kazi yake hivi kwamba Mungu ambaye kwa kujifunua na kuwaita watu wake anataka wamfuate, wahongoke, wamwabudu na kumtolea sadaka kwanza kabla ya mengine (Mwanzo 12:7, Kutoka 3: 6. Kwamba mababa wa mtaguzo walikusudia kuanza na kile ambacho ni kanuni na asili ya maisha, uwepo na mwito wetu yaani kuanza kwa kujiweka chini ya Mungu aliye mwanzo wetu, kuishi kwetu, kutenda kwetu na mwisho wetu kupitia liturujia iliyo utumishi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu.  Mababa wa mtaguso walilenga kutufundisha kuwa liturujia ni utumishi wetu mbele ya Mungu, na kuwa kila kitu walichotaka kukifanya katika mtaguso huu kililenga kumtambua na kumtambulisha Mungu kama kiini cha yote. Mababa wa mtaguso walilenga kutufundisha kuwa hati zingine zitakazofuata itakuwa ni mwendelezo wa liturujia yaani kuyaishi na kuyashuhudia yale tunayoadhimisha katika liturujia kwavile liturugia ni kazi ya Mungu - Opus Dei.  Mwisho napenda niseme kuwa kwa kuanza na sacrosanctum concilium mababa wa mtaguso walitaka kutufundisha kuwa liturujia ndiyo uwanja wa maadhimisho ambapo maarifa au sayansi zote nyingine zinakuja kushiriki, kuhudumu au kutumika. Wazo hili ilikuwa ni kusudio la wazi la kuweka vizuri nafasi ya utumishi wetu na ya maarifa yetu mbele ya Mungu ambayo ndiyo liturujia kama tutakavyoona sasa.

UFUPISHO WA SURA ZINZAOUNDA SACROSANCTUM CONCILIUM

1.      Sura ya Kwanza: Kanuni jumuishi za kuipata na kuikuza liturujia takatifu

2.      Sura ya Pili: Fumbo takatifu sana la Ekasisti.

3.      Sura ya Tatu: Sakramenti nyingine na visakramenti.

4.      Sura ya Nne: Ofisyo ya Kimungu.

5.      Sura ya Tano: Mwaka wa Kiliturujia

6.      Sura ya Sita: Muziki Mtakatifu.

7.      Sura ya Saba: Sanaa Takatifu na Nakshi Takatifu.

MTUGUSO WA II WA VATICAN NA HATI YAKE SACROSANCTUM CONCILIUM

Baba mtakatifu Yohane wa XXIII aliyejulikana kama Papa/Baba mwema kwa kiitaliano (Papa buono) alitangaza kuja kwa mtaguso huu wa pili wa vatican mnamo tarehe 25 Januari 1959. Mababa wa mtaguso walipokutana walianza maramoja kuandika hati hii ambayo iliwachukua muda wa kutosha. Lengo la mtaguso katika kuandika hati hii kama tunda lake la kwanza ilikuwa ni kuwa njia ya kuhuisha, kuboresha na kuhaisha maisha ya kiroho ya Kanisa, hati hii pia ilikusudiwa kuwa nafasi ya upatano na wakristo waliojitenga na Roma ili kuungana nayo katika kutafuta umoja wa kikristo. Sababu nyingine zaweza kuonwa kutoka katika historia ya makuzi ya Kanisa na liturujia yake ambazo tayari zilishapelekea kuitishwa kwa mitaguso mingine mingi ikiwemo ile ya Trento na Vaticano ya I. Papa Pius IX katika kuitisha mtaguso wa kwanza wa Vaticano mwaka 1869 hadi 1870, alikusudia kushughulika na matatizo yaliyozushwa na nyakati mpya akimaanisha uhuria katika fikra (ratinalism), uhuru (liberalism) na ufisadi (materialism).

Sababu nyingine twaweza kuziona kuwa ni zile zilizoletelezwa na upinzani, uhasi na utengano kama vile Luthero, Zwingli, Kelvin, Arius, uangilikana na vingine. Mwondoko wa kiliturujia yaani movimento liturgico ni sababu nyingine zinazotoka ndani ya kanisa katoliki lenyewe, ulioanzishwa na wasomi wa kikatoliki ukiasisiwa na mwanaliturujia Aboti Ildefons Herwegen wa Ujerumani, na kudakwa na mwanaliturujia Odo Casel wa Ujerumani, na kisha ukaenea katika madhehebu mengine ya kianglikana, kilutheri na ya kiprotestanti ukidai maboresho katika namna ya kuabudu. Odo Casel akiwa ameanza kisomo chake katika liturujia, alitafiti uwezekano wa mwanzo wa liturujia ya Kikristo kuwa umetokana pia na ibada za kipagani, akiiona liturujia kama tendo na hitaji kumbakumba la kiutu na kidini kwa watu wa ulimwengu wote. Katika chapisho lake la Kanisa liombalo - (Ecclesia Orans) la mwaka 1918, Odo Casel aliona ufanano wa maadhimisho na madhehebu ya kikristo kutoka katika ibada na namna za kale za kuabudu za dini za kipagani za kigriki na kirumi. Wazo hili lilipata umaarufu na washabiki wengi na kuzua hisia za utafiti miongoni mwa wasomi na viongozi wengi wa kanisa akiwemo Pius Parsch wa Klosternuburg Austria. 

Sababu zingine ni udhaifu wa liturujia ya Trento uliotokana na ugumu wa lugha ya kilatini, riti kutokuwa mvuvumko na madhehebu kutojulikana kwa wote. Mijengo ya makanisa na mahala pa maadhimisho kutokuwa faawote hasa katika makanisa ya uhispania na kwingineko pia ilikuwa ni sababu iliyowaacha watu bila ushirikitunduizi huku wakibaki kuwa na kiu na njaa ya kushibishwa na liturujia ya wakati huo. Yote haya ulikuwa ni mwendelezo wa vurugu na uhitaji ambao mtaguso wa pili wa vaticano na hati yake sacrosanctum concilium vilitakiwa kuja na kutoa majibu kwa watu na nyakati. 

MPITIO RASHIA JUU YA HATI HII

Kwa kutoa hati hii sacrosanctum concilium YA mtaguso wa II wa Vatican ulikusudia yafuatayo:

1.   Kupandikiza nguvu ikuayo daima katika maisha ya kikristo.

2. Kujiasili kwa ufasaha na ipasavyo katika mwito na mahitaji ya nyakati kupitia utamadunisho. Wazo na nia hii vilikusudia kuruhusu tafsiri ya hati,  machimbukomsingi na riti za kiliturujia kutoka katika lugha ya kilatini kwenda katika lugha na vilugha. Utamadunisho pia ulilenga kuruhusu mabadiliko yaguse yale mambo yawezayo kubadilishwa yaliyo katika riti na madhehebu.

3. Kupandikiza vinasaba muhimu viwezavyo kukuza umoja katika tofauti miongoni mwa waamini, madhehebu na riti mbalimbali za liturujia ya kanisa Katoliki. Mambo haya yalikusudiwa kuhusisha umoja uzingatiao tofauti katika sala ya kanisa, kalenda ya liturujia, mavazi ya liturujia, muziki mtakatifu, sanaa takatifu, mionekano, miondoko ya kiliturujia, ishara na alama zitumikazo katika liturujia yetu.

MAANA YA LITURUJIA:

Mababa wa mtaguso wa pili wa Vatikano, katika hati ya sacrosanctum concilium wanaielezea liturujia kama kazi ya kumwabudu Mungu inayotendwa na watu wake katika kusanyiko la ibada katika kusudio la ushiriki hai ulio chanya na wenye ujuo ili kumwabudu, kumsifu, kumtukuza, kumshukuru na kumwomba Mungu. Sasa ni lazima kujua kuwa liturujia yetu inajipambanua kama kazi au utumishi wa watu mbele ya Mungu wao. Kinyume chake pia ni sahihi yaani liturujia pia ni kazi ya Mungu mbele ya watu wake. Hapa, mababa wa mtaguso wanakusudia kutufundisha kuwa ili liturujia mahususi ifanyike na ipate maana na matunda yake inamwitaji Mungu awepo, na tena wawepo watu katika kusanyiko na katika mahali fulani, na tena ndani ya muda fulani. Vitu vingine vya msingi na muhimu ni uwepo wa rito, madhehebu na vifaa vya kiliturujia. Kwa kifupi sasa twaweza kusema kuwa liturujia inamwitaji mtu, mwanadamu au mwamini katika utajiri wa utamaduni wake aje katika utumishi mbele ya Mungu.

Maana na mtazamo wa liturujia kama utumishi wa watu mbele ya Mungu unaasiliwa kutoka katika neno λείτουργία la lugha ya kigiriki. Neno hili λείτουργία (leitourgia) lina mwunganiko wa maneno mawili ya kigiriki lēito likimaanisha hadhara, kundi au jumuiya na ergo likimaanisha kutenda au kufanya kazi. Katika mtazamo wa kale wa kigiriki neno leitourgia lilimaanisha kazi, huduma au zamu ya watu mbele ya miungu, jamuhuri, au mfalme. Wazo hili la utumishi au huduma lilimaanisha pia kazi ya kucheza michezo au kufanya maonesho mbele ya watu katika kumbi. Watu waliokusanyika wanamaanishwa kupitia neno leos au laos. Mwadhimishi au mtu aliyetoa huduma aliitwa leitourgos.

Sasa niseme kuwa kuaanzia karne ya 16 neno na jina hili liturujia liliasiliwa na kuchukuliwa na Kanisa Katoliki likimaanisha kuwa liturujia ni tendo la utumishi wetu la kumwabudu Mungu litendwalo na kusanyiko la watu mbele ya Mungu katika wakati na mahali fulani. Katika maana hii ni lazima tutambue kuwa zawadi ya neema ya Mungu inategemea tendo la mwanadamu. Andrea Grillo anafafanua kuwa teologia inaitegemea sana elimujamii yaani antropologia na inatenda kwa usaidizi wa sayansi au elimu na maarifa mengine . Katika liturujia watu wanakuja mbele ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao wakionesha afya zao, furaha yao, uzuni au maumivu yao. Kwa upande mwingine kusanyiko la waamini wanaohudumu mbele ya Mungu wanaonesha munganiko wa mwilifumbo wa Kristo. Hivyo liturujia inakuwa ni uwanja ambapo umoja huu au mwunganiko huu unaoneshwa na kuadhimishwa pia. Liturujia ni locus theologie na kwa upande mwingine Theolojia ni (locus liturgicus - theologia est locus liturgicus).

Sasa, hapa ni sharti tugundue kuwa utumishi wetu katika liturujia na liturujia yenyewe vimeuganika na mazoea au maonjo ya kidini aliyonayo mtu mwamini kama vile kasisi, mtawa, au mlei mbele ya sakramenti. Napenda niseme kuwa hapa tunaangalia utendaji –performance na ushiriki (participation) kwa kila mmoja katika kazi ya kuhudumu kiliturujia. Ni lazima pia tujumuishe umuhimu wa eneo la maadhimisho – (space) kama tukakavyoona mbeleni kukimaanisha majengo ya ibada au mahali pengine pafaapo, bila kusahau muda – time utumikao katika maadhimisho. Muda katika liturujia ni kitu cha lazima na ni tunda la majitoleo ya kila mshiriki katika uhiari wake na ubinafsi wake yaani ad libitum. Huu ni muda wa kutolea na kutumia au kutumika kama sadaka mbele ya Mungu ukisukumwa na upendo unaopambwa na uchaji alionao mwamini mbele za Mwenyezi Mungu wake.

KISHINDO CHA SACROSANCTUM CONCILIUM

Baada ya hati hii kupitishwa na kupokelewa na jumuiya za makanisa mbalimbali, twaweza kuona kuwa meza ya neno la Mungu na madhehebu yake vilitajirishwa zaidi kwa neno la Mungu. Kutojua maandiko matakatifu kulionekana ni kutomjua Kristo Yesu. Kardinali Francis Arinze anataja yafuatayo kama mafanikio:

1.      Kubuniwa kwa mzunguko wa miaka mitatu wa masomo ya biblia katika liturujia.

2.      Kuhuishwa zaidi kwa maisha ya kanisa kupitia liturujia yaani masomo, kalenda, sala, alama na ishara za kiliturujia.

3.      Kuingizwa kwa vitu zaidi toka tamaduni na sayansi katika liturujia.

4.      Kutafsiriwa hati hii katika lugha na tamaduni mbalimbali.

5.      Kuhimizwa kwa ushiriki hai na chanya wenye ujuo katika liturujia.

6.      Waamini walei kupewa ushiriki zaidi katika huduma za kiliturujia.

7.      Liturujia kuwa na mwono wa siku za mwisho zaidi - eschatological.

MABADILIKO YALIYOLETWA NA SACROSANCTUM CONCILIUM

Kutokana na kuja kwa hati hii yafuatayo ni mabadiliko yaliyoletwa na ujio wake:

1. Ushiriki hai na chanya wenye ujuo katika liturujia ulihimizwa sasa. Wazo hili na himizo hili vilikusudia kuona kuwa tendo la kiliturujia halikuwa tu tendo la kuangaliwa kama ilivyo katika kumbi za maonesho au viwanja vya michezo bali la kushirikwa na kila mmoja kupitia kuimba, kuitikia, kusali, kuhudumu, miondoko, mionekano, mikao nk.

2.  Liturujia ya Misa Takatifu iliboreshwa kuwahusisha walei pia.

3. Mabadiliko katika uga wa maadhimisho uliohusisha mkao wa altare na mwonekano wa kasisi mwadhimishi. Sasa altare ililetwa katikati ya kanisa. Awali kasisi aliadhimisha Misa Takatifu akiwa amewatega mgongo waamini na hivo kuwafanya kuwa watazamaji.

4. Muziki mtakatifu ulibadilika pia. Licha ya muziki wa kigregoriano kwendelea kuwa mahususi kwa liturujia ya kanisa, iliruhusiwa pia muziki, ghani na tungo toka kwa mataifa na jamii nyingine.

5. Sanaa takatifu iliyohusisha namna za mijengo ya makanisa kama vile romaniki, gotiki, reneshenti, na baroku zilichukuliwa mbadala na zile za kisasa na za jamii nyingine.

6. Kuthaminiwa kwa riti nyingine kama vile Ambrosiano, Armena, Kopta, Mozzarabi, Binzantino, Siro – Maraba/Malankara nk.

MAFUNDISHO YALIYOMO KATIKA SURA YA I, II NA III:

Sura hizi tatu zinahusika na kanuni msingi za kuirudisha na kuiendeleza liturujia takatifu.

1.  Kwamba asili na umuhimu wa liturujia katika maisha ya kanisa ni Mungu. Liturujia ni kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya watu. Mungu aabudiwe na mtu atakatifuzwe. Liturujia yetu ni kwa ajili ya utukufu wa  Mungumtatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tumjue Mungu tumwabuduye katika Utatu Mtakatifu:

1.1.  MUNGU BABA: Mungu Baba ni nafsi ya kwanza ya Mungu. Anajifunua katika kila mtu na watu wote au mataifa yote. Anajifunua pia katika maumbile ya vituasili. Kwa mara ya kwanza na zilizofuata katika historia ya wokovu wetu alijifunua kwa Abraham, Isaka, Yakobo, Musa na mitume. Leo kabila zote na dini zote tunamjua Mungu. Kwa wayahudi yeye ni El Shadai, kwetu ni Nyamuhanga, Katonda, Lesa, Murungu nk. Sifa na majina yake ni Mjuayote, Mwenyenguvu, Mwezayote, Upendo nk. Waakani wa Ghana wanamjua kama Borebore - Mfinyazi na Wahaya wa Tanzania wanamjua pia kama– mwenye macho mengi kama tenga - Owamaisho nk’olugega.

1.2. MUNGU MWANA: Mungu mwana ni nafsi ya pili ya Mungu. Yeye ni mwana wa Mungu n ani Mungu kweli sawa na Baba na Roho Mtakatifu. Anaitwa Neno wa Mungu – Logos. Ni yeye alijifanya mwanadamu katika fumbo la umwilisho na akatwaa mwili kwa kutungwa mimba katika tumbo la mama Bikra Maria. Alizaliwa kama mtoto wa kiume kule Bethlehemu jina lenye maana nyumba ya mkate na akalelewa katika familia ya Nazareth ya Mama Maria na Mmewe Mwenyeheri Yosefu. Alifundisha watu Injili yaani Habari Njema ya wokovu alipokuwa na umri wa miaka 30 na akauawa kwa kuteswa, kusulubiwa na kuwambwa msalabani alipokuwa na umri wa miaka 33. Baada ya siku 3 za kalenda ya kiyahudi za kukaa kaburini alifufuka na kisha siku 40 alipaa mbingu katika ahadi ya kutuletea Mungu Roho Mtakatifu na ile ya kurudi tena ili kuuhukumu ulimwengu na kutwaa walio watu wake kwa uzima wa milele na waovu kwa mateso ya milele.

1.3. MUNGU ROHO MTAKATIFU: Mungu Roho Mtakatifu ni Mungu nafsi ya Tatu ya Mungu. Yeye ni sawa na Baba na Mwana na ni tunda la upendobadilishana wao. Yeye ni Pneuma yaani pumzi ya Mungu. Anaitwa pia Mfariji, Mwalimu, Kiongozi, Roho wa Mungu, Kidole cha Mungu, Kiagano cha Mungu nk.

1.4. MTU/MWANDAMU: Huyu ni roho-mwili. Bonaccorso Giorgio anatufundisha kuwa mwili wa mtu yaani σώμα kwa kigiriki umeunganika maramoja na nyama yake yaani (σάρξ), na roho yake yaani  (ψυχή) kutengeneza nafsi yaani mtu άνθρωπος. Na hivi mtu ni άνθρωπος ψυχικός ikimaanisha mtu asili au mlimwengu (Tazama, Il corpo di Dio, 24-25). Mwili huu alionao mtu ni ule unaoelezwa pia kama basar kwa kiebrania. Huu ni mwili tuwezao kuujua kuwa mwili wa kiumbeasilia ikiwa na maana mwili kama/wa mwandamu. Ni mtu huyu katika roho-mwili ajaye mbele ya Mungu katika adhimisho akitumia vitu vya utamaduni wake au akiwa katika utamaduni wake, afya yake njema ya roho na mwili au katika magonjwa, maumivu, uzuni, masikitiko, matatizo na mahitaji ya kijamii na anamwabudu Mungu kwa kutumia vifaa ambavyo ni tunda la teknologia na utamaduni wake au wa jamii fulani.

1.5. MAHALI PA MAADHIMISHO: Hitaji hili linamaanisha lazima ya kuwepo mahala pa kuazimishia liturujia. Yaweza kuwa makanisa katika ukubwa na udogo wake, ukumbi, darasa, ufukwe, mlima, eneo tambarare au mti ambapo Misa Takatifu itaadhimishwa.

1.6. MUDA: Muda ni sehemu ya lazima ya adhimisho. Adhimisho la kiliturujia linahitaji muda wa kuanza na kumalizika. Riti, madhehebu na matendo yote katika liturujia yanafanyika katika muda  na tena ndani ya muda maalum.

1.7. RITO: Rito ni namna ya kutenda katika kumwabudu Mungu. Rito hukamilika kama kazi ya mwanadamu yaani waamini katika nafasi zao za ushiriki. Rito inaundwa na mfululuzo wa madhehebu yatendwayo ndani ya muda. Rito ni kiunganishi kati ya Mungu na watu wake, Mwumba na viumbe wake, liturujia na teolojia tena kati ya teolojia na athropolojia na kati ya liturujia au teologia na sayansi nyingine katika kumwabudu Mungu na kumtakasa mwanadamu. Hapa liturujia inakuwa uwanja wa teolojia locus theologie. Kwa upande mwingine teolojia yaani kada nyingine zote za teolojia zinakuja kutumika katika liturujia. Ni liturujia inayoiishi na kuitenda teologia kupitia mwunganiko na mfululizo wa madhehebu. Kwa maneno mengine teolojia inatendwa katika adhimisho la kiliturujia. Liturgy applies what the dogmatic knowledge and other theological sciences have elaborated because participates as such to the truth of revelation and faith in Christ . 

1.8.  MADHEHEBU: Madhehebu ni namna ya kutenda ndani ya muda jambo fulani katika adhimisho na tena kwa kufuata nidhamu fulani. Kwa umoja, mwunganiko na mfululizo wake madhehebu yanatengeneza rito. Katika liturujia madhehebu ni matendooneshi takatifushi au ponyaji yanayotendwa ndani ya muda.

1.9. VIFAA VYA MAADHIMISHO: Hapa tunataja Misale ya Altare, Kitabu cha Masomo, Kalisi, Siborio, mkate, divai, maji, kisafishavikombe, kikaushamikono, pala, koropolare, ufunguo wa taberinakulo, altare/meza, kisomeo/ambo, stendi ya kasisi mwazimishi, chetezo, ubani, mavazi ya kasisi, msalaba wa maandamano, mishumaa, vyombo vya muziki, kengele na vinginevyo kulingana na sakramenti au kisakramenti kinacho adhimishwa.

1.10. NAKSHI: Nakishi au rangi  ni ishara zinazoonekana kwa macho na zina umuhimu sana katika kila nyanja ya maisha, matukio na shughuli za kila siku za mwanadamu. Katika dhana nzima ya kuhudumu kwetu mbele ya Mwenyezi Mungu yaani  kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumshukuru, nakshi na rangi katika liturujia au adhimisho zinakuwa pia ni sehemu ya lazima ya tukio hili. Liturujia ya kanisa Katoliki tokea zama zake za awali imetumia nakshi, rangi, michoro, sanamu kama moja ya ishara, alama, vioneshi vya uzuri na utambulisho wa  liturujia katika nyakati na matukio mabalimbali ya kiimani na kiibada yanayo adhimishwa.

1.11. KUSANYIKO LA WAAMINI: Hapa wanatajwa watu wa Mungu katika huduma na utumishi wao yaani kasisi mwazimishi, makasisi waazimishawenza, watawa, walei kama vile maakolito, wasomaji, watumikiaji, waimbaji, waimbishaji, waimbazaburi, wapiga vyombo vya muziki, walizi, wasimamizi wa ibada, wapigakengele, wasakristia, wafanyausafi nk.

2. MAAGANO: Mungu ndiye aadhimishwaye katika liturujia ya Agano la Kale na ya Agano Jipya. Kwamba liturujia ya Agano la Kale ilikuwa ni utangulizi, kivuli na mwangwi wa kazi ya Kristo Yesu katika Agano Jipya yaani katika kuokoa au kukomboa na katika kumpa Mungu Baba utukufu kamili usio na waa. Kupitia mateso, kifo ufufuko na kupaa mbinguni, Kristo ameikamilisha bila dosali kazi ya Mungu ya kutukomboa na kutupata tena kama watoto wake. Hii ina maana kuwa mateso ya Kristo yametibu na kuponya mateso yetu, kifo cha Kristo kimeua kifo chetu – what causes heals it, au il simile cura il simile kufufuka kwake kuliturudishia maisha na uzima wetu.

3. MITUME: Kwamba liturujia yetu imejengwa pia juu ya kazi na matendo ya mitume yaani yaliyofanya na kufundisha juu ya sadaka ya Bwana na kuziishi sakramenti.

4. SAKRAMENTI NA VISAKRAMENTI: Kwamba katika adhimisho la kiliturujia Mungu anatenda kupitia nguvu yake katika sakramenti za kanisa, uwepo wake katika watumishi wake, uwepo wake katika neno lake, sala na nyimbo, kusanyiko la watu wake na yeye (Matayo 18:20), vielelezo, picha na visakramenti. Ni katika  liturujia, kwayo na hasa katika sadaka ya kimungu ya ekaristi, kazi ya wokovu wetu inakamilika.

5. KANISA: Kwamba ni katika liturujia, waamini wanajaliwa kuonesha katika maisha yao na kwa ndugu zao fumbo la Kristo na ile hulka iliyo kweli asili ya kanisa la kweli. Hii inamaana watu wawezeshwe kujua kuwa kanisa kwa asili ni la kimungu na la kiutu, lionekanalo na lenye ukweli usioonekana, lenye juhudi katika kutenda na lenye kutafakari daima. Kwamba kanisa lipo ulimwenguni lakini katika hali ya hija na mpito kuelekea mbinguni. Katika lenyewe ubinadamu wake unaelekezwa kwa umungu na chini yake. Uhalisia wa kionekanacho kwa kisichoonekana, tendo kwa tafakari na ulimwengu huu kwa ule ujao.

NAMNA NJEMA YA KUIISHI SACROSANCTUM CONCILIUM

Ni kivipi tunaitwa kuiishi vema hati hii? Mababa wa mtaguso wanatuelekeza tujue kuwa wao walinuia kuongeza nguvu zaidi katika maisha ya kikristo na ya kiliturujia. Hii inamaana kuwa liturujia katika vile vipengee vyake vinavyoweza kubadilika au kubadilishwa bila kuathiri yale ya msingi ni sharti ijiasili kwa ukaribu zaidi na mahitaji ya nyakati zetu na maisha yetu. Hapa mababa wa mtaguso wanataka kutufundisha kuwa liturujia yetu ni lazima itoe majibu kwa mahitaji ya watu na ipoze kiu au kushibisha njaa ya wana wa Mungu katika maisha yao. Lakini hapa twaweza kuzusha maswali kadhaaa ya kujiuliza: Twaweza kusemaje leo juu ya kundi la watafuta tiba? Vipi wagonjwa watembeao na matatizo yao kwa kihaya “abatanyamile balweile”? vipi wasaka miujiza? Watafuta mafanikio? Je, twaweza kujioji, sakramenti yetu ya Mpako wa wagonjwa inakizi mahitaji leo? Mbona wapo wakanyaga mafuta? Je sala zilizomo katika liturujia mahususi ya kanisa zinakidhi mahitaji? Zinashibisha njaa yetu? Je, tunasoma neno la Mungu?

Ni bora tujue kuwa mtaguso na mababa wa mtaguso waliadhimu pia kukuza na kuendeleza chochote kile kilicho kwa ajili ya umoja wa wakristo. Wale wote wamwaminio Kristo ili wawe kitu kimoja (Yohane 21:19) na pia kutegemeza jitihada yoyote ile itakayosaidia kuwaita watu wote ndani ya zizimoja na chini ya mchungaji mmoja yaani kanisa moja. Je, leo tupo wamoja? Twasemaje juu ya wimbi la ulokole na ukarismatiki? Uneokatekumenato, je, ni tatizo baadhi yao kutaka kusali jumamosi jioni tu? Usabato? Vipi juu ya itikadi kali za kidini - fundamentalism? Mtaguso pia ulikusudia kuleta maboresho na kuikuza liturujia. Je, liturujia yetu ni moja? Vipi twasemaje juu ya tofauti ndogondogo tulizo nazo katika liturujia ya majimboni mwetu? Je, sala ya Mtakatifu Inyasi ni hitaji la lazima sasa la liturujia mahususi katika kanisa la Tanzania? Vipi twasemaje leo juu ya zile sala nyingi (Baba yetu, salamu Maria, sala ya kutamani, esala yo kwikilizya au ya kuzunya, sala baada ya komunio, nk)  zinazosaliwa kabla au baada ya komunio takatifu katika baadhi ya majimbo yetu? Je, twendelee na kutoshikana mikono wakati wa kutakiana amani au kutojibariki na maji ya baraka madhara yaliyosababishwa na janga la korona? Je, twendelee kuleta neno la Mungu katika maandamano kwa kubebwa na mtoto mdogo katika beseni au kalai? katika vijimtumbwi tena kwa kulindwa na sime, mikuki, mishali na marungu?

Ni bora tena tujifunze kujua kuwa liturujia siku kwa siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa, ikiwafanya hekalu takatifu la Mungu na makao yake katika Roho. Mwisho, mtaguso na sacrosanctum concilium  vinataka kutufundisha kuwa mama kanisa mtakatifu anathamini riti zote mama kanisa atumiazo katika liturujia kuwa sawa. Baadhi ya riti hizi ni Latini/Romani, Bizantine, Ambrosiano, kopta, Motharabi/mozzarabi, Maronite,  Siro Marankara/Maraba nk.

MASWALI YATOKANAYO:

1.  Je, kanisa la Tanzania na waamini wake wote tumefaulu kuinasa na kuiishi liturujia yetu katika hali na moyo wa ushiriki hai, chanya, wenye ujuo na tena wenye kuleta matunda?

2. Tunawezaje kuondosha mchanganyo – syncretism katika maisha ya kiliturujia?

3.  Kanisa la Tanznaia lifanye nini kufutilia mbali mwondoko wa kuzinyanyapaa sakramenti za kanisa na kutafuta majibu nje ya liturujia Katoliki?

MAAZIMIO YA KUFANYA:

1.  Tuimize zaidi mafundisho na mistagojia/ catechesis and mystagogy.

2. Tuimize mafundisho na kusindikizana/ kuleana kiroho na kichungaji.- (Pastoral and spiritual accompaniment).

3.  Tujitahidi kufisha desturi ya kumgawa mwumini katika roho na mwili – (Platonic dualism.)

HITIMISHO: ITE MISSA EST

Tumalizie kwa kusema kuwa tutaweza tu kuiishi vizuri na kwa mafanikio makubwa hati ya Sacrosanctum Concilium ya Mtaguso wa Pili wa Vaticano kwa kujua na kuuishi ukweli kuwa maneno yetu tuyaimbayo au kuyazungumza na hata ishara na mionekano yetu wakati wa liturujia takatifu vinapaswa kuunganika daima na mwili wa Kristo utuzungukao. Hii inamaanisha kuwa liturujia ni maisha na ili kuuishi ukristo wetu ni lazima katika maisha yetu ya kila siku tuwe na mwendelezo wa kile tulichokisikia na kukiishi katika liturujia. Ite missa est ni maneno ya kutuaga mwishoni mwa adhimisho lakini yakitutaka kuendeleza misa hii au adhimisho la misa maishani.  Katika adhimisho la liturujia twaweza kusimama, kuketi, kupigamagoti, kutembea, kuzungumza, kuimba, kufanya ishara, lakini daima katika mwunganiko na wengine karibu yetu na kamwe si katika namna yetu tutakayo sisi. Ni lazima tukumbuke daima kuwa katika liturujia takatifu tunakuja kushiriki katika kazi ya Mungu na ya watu wa Mungu na siyo kuunda kazi au liturujia yetu. Ni bora sana tujue kuwa kila matendo katika liturujia mahusisi ya Kanisa, mfano, rito ya Kilatini/Kirumi yana kile yanacho kimaanisha au kusudio linalofungua mlango wa Mungu kwetu.

11 August 2023, 15:14