Tafuta

Kauli mbiu: “Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo: Miaka 50 ya Kujenga Kanisa Kama Familia ya Mungu Katika Nchi za AMECEA.” Kauli mbiu: “Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo: Miaka 50 ya Kujenga Kanisa Kama Familia ya Mungu Katika Nchi za AMECEA.”  

Barua ya Kichungaji Kwa Taifa la Mungu Jimbo Katoliki Mahenge: Gaudium Magnum 2023

Barua ya Kichungaji kwa Taifa la Mungu Jimbo Katoliki la Mahenge: “Gaudium Magnum” yaani “Ni Furaha Kubwa” anagusia kuhusu uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo ndogo, kiwe ni kipindi cha kupyaisha imani kwa: Sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mwaka 2024 Ni Mwaka Wa Ekaristi Takatifu sanjari na Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa mjini Quito nchini Equador kuanzia tarehe 8-15 Septemba 2024.

Na Askofu Agapiti Ndorobo, Jimbo Katoliki la Mahenge, Tanzania.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, tarehe 20 Agosti 2023 linazindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, huko Lilongwe, nchini Malawi na kufuatiwa na warsha ya siku tatu juu ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo pamoja na Ulinzi wa Mtoto. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu: “Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo: Miaka 50 ya Kujenga Kanisa Kama Familia ya Mungu Katika Nchi za AMECEA.” Ni katika muktadha huu, Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge, Tanzania katika barua yake ya kichungaji kwa Taifa la Mungu Jimboni Mahenge aliyoipatia jina “Gaudium Magnum” yaani “Ni Furaha Kubwa” anagusia kuhusu uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo ndogo, kiwe ni kipindi cha kupyaisha imani kwa: Sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mwaka 2024 Ni Mwaka Wa Ekaristi Takatifu sanjari na Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa mjini Quito nchini Equador kuanzia tarehe 8-15 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe huu wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, mwaliko wa kukuza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

AMECEA inazindua maadhimisho ya Jubilei ya JNNK 20 Agosti 2023
AMECEA inazindua maadhimisho ya Jubilei ya JNNK 20 Agosti 2023

“GAUDIUM MAGNUM” Ni furaha kubwa tunapotambua na kuona wazi kuwa Mwenyezi Mungu anatupenda. Katika kutupenda, Mungu anatujalia nafasi ya kuyatafakari makuu anayotutendea katika safari yetu ya kiroho. Wapendwa Taifa la Mungu, Kanisa Barani Afrika na kwa namna ya pekee kanda ya AMECEA linajipambanua kama familia ya Mungu. Tunawatangazia rasmi Jubilei ya miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Maadhimisho ya jubilei hiyo yanaanza rasmi mwezi Julai 2023 na kilele chake kitakuwa mwezi julai mwaka 2024. Kauli Mbiu inayoongoza maadhimisho hayo ni: “JUMUIYA NDOGONDOGO ZA KIKRISTO: MIAKA 50 YA KUJENGA KANISA KAMA FAMILIA YA MUNGU KATIKA NCHI ZA AMECEA.” Katika Jimbo letu la Mahenge, uzinduzi wa maadhimisho hayo umefanyika tarehe 27 Julai 2023 katika Kanisa kuu Kwiro. Tunaagiza kwamba: kila parokia iandae utaratibu wa uzinduzi rasmi katika ngazi zote yaani uzinduzi kiparokia, kivigango na kwa namna ya pekee katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Tunapendekeza kwamba, katika parokia zote ambako hatujafika kwa ziara za kichungaji na utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara, kufanyike maandalizi ya kuwezesha uzinduzi katika ngazi ya parokia au kigango husika uendane na tukio la utoaji wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara mwaka huu 2023. Aidha utaratibu maalumu utaandaliwa kwa zile parokia ambako tumekwishatoa Kipaimara mwaka huu 2023.

Pyaisheni imani kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa
Pyaisheni imani kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa

Katika Maadhimisho haya ya Jubilee ya Miaka 50 ya JNNK, kila parokia iandae utaratibu utakaowezesha kufanyika kwa mikutano maalumu ya kutafakari uhai wa jumuiya zetu na kwa namna ya pekee uelewa wa watu juu ya dhana nzima ya JNNK. Ifanyike tahmini ya kina juu ya mafanikio na changamoto tunazopaswa kuzifanyia kazi katika Jimbo letu la Mahenge. Yatolewe pia mapendekezo ya namna ya kuzitatua changamoto hizo kadili ya mazingira yetu. Tunaaagiza kwamba tathmini hizo zitufikie kupitia Idara yetu ya kichungaji na zitajadiliwa kwenye mikutano yetu ya kichungaji jimboni. Wapendwa katika Kristo Bwana, tunaagiza kwamba: SALA MAALUMU YA JUBILEI isaliwe na wanajumuiya wote wanapokutana pamoja kusali na kutafakari Neno la Mungu. Aidha, yatolewe mafundisho ya Imani na kuwahimiza waamini kuziishi kweli za Imani yetu hasa maisha ya Sakramenti hususani; NDOA TAKATIFU, SAKRAMENTI YA UPATANISHO NA EKARISTI TAKATIFU. Maadhimisho haya ya Jubilee ya Miaka 50 ya JNNK yatumike kama fursa muhimu ya kukuza Imani yetu na kuimarisha uhai wa Jumuiya zetu Jimboni Mahenge. Mapadre na watawa tushiriki katika mikutano hii muhimu.

Ni wakati wa kuziishi kikamilifu kweli za imani: Ndoa, Ekaristi na Upatanisho
Ni wakati wa kuziishi kikamilifu kweli za imani: Ndoa, Ekaristi na Upatanisho

Wapendwa Taifa la Mungu, katika jimbo letu la Mahenge, sherehe za kufunga maadhimisho ya Jubilei hii ya miaka 50 ya JNNK yatafanyika mwezi Julai mwaka 2024. Ndugu zangu katika Kristo, kwa waraka huu pia, tunawatangazia rasmi kwamba mwaka wa Bwana 2024 ni mwaka wa Ekaristi Takatifu. Hivyo kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 15 mwezi Septemba kutakuwa na Kongamano la 53 la Kimataifa la Ekaristi Takatifu katika mji wa QUITO nchini EQUADOR. Aidha hapa nchini Tanzania kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika katika Kanda yetu ya Mashariki katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Tumwombe Mungu afanikishe shughuli zote za maadhimisho hayo muhimu na tujiandae kushiriki kwa hali na mali. Mwanzoni mwa mwaka 2024 kutafanyika uzinduzi rasmi wa maadhimisho hayo. Tutawatangazia tarehe rasmi ya uzinduzi huo.

Tunawatakia Baraka tele katika maadhimisho haya yote.

Ndimi katika Utumishi,

+ Agapiti Ndorobo

Askofu Jimbo la Mahenge, Tanzania.

Mahenge Gaudium Magnum
02 August 2023, 14:18