Tafuta

Jumatatu tarehe 3 Julai 2023 imezinduliwa Warsha ya Siku nne ya “Uangalizi wa Wanawake Duniani” inayofanyika, Dar es Salaam, Tanzania, ili kuwawezesha wanawake wa kiafrika kuwa na mustakabali usio na unyanyasaji. Jumatatu tarehe 3 Julai 2023 imezinduliwa Warsha ya Siku nne ya “Uangalizi wa Wanawake Duniani” inayofanyika, Dar es Salaam, Tanzania, ili kuwawezesha wanawake wa kiafrika kuwa na mustakabali usio na unyanyasaji.  

Wanawake Wakatoliki Barani Afrika: Warsha Dhidi ya Ukatili, Ubaguzi na Nyanyaso

Jumatatu tarehe 3 Julai 2023 imezinduliwa Warsha ya Siku nne ya “Uangalizi wa Wanawake Duniani” inayofanyika, Dar es Salaam, Tanzania, ili kuwawezesha wanawake wa kiafrika kuwa na mustakabali usio na unyanyasaji. Warsha hii ya pili kufanyika Barani Afrika imeandaliwa na Kikundi cha Utafiti wa Masuala ya Wanawake Duniani (WWO – World Women Observatory) kilichopewa jina la “Mtandao wa Kiafrika dhidi ya Ukatili na Ubaguzi wa Wanawake. Hatua za kwanza."

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - WUCWO, Dar es Salaam, Tanzania.

Wanawake Wakatoliki Wajenzi Stadi wa Mahusiano ya Udugu wa Kibinadamu kwa Amani ya Ulimwengu! Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza utume wa Wanawake Wakatoliki Duniani kwa mwaka 2023-2027. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumatatu tarehe 3 Julai 2023 amezindua Warsha ya Siku nne ya “Uangalizi wa Wanawake Duniani” inayofanyika, Dar es Salaam, Tanzania, ili kuwawezesha wanawake wa kiafrika kuwa na mustakabali usio na unyanyasaji. Warsha hii ya pili kufanyika Barani Afrika imeandaliwa na Kikundi cha Utafiti wa Masuala ya Wanawake Duniani (WWO – World Women Observatory) kilichopewa jina la “Mtandao wa Kiafrika dhidi ya Ukatili na Ubaguzi wa Wanawake. Hatua za kwanza." Warsha hii inapania pamoja na mambo mengine, kuwaletea wanawake Barani Afrika mabadiliko chanya kwani sehemu kubwa ya waathirika ni wanawake wasionekana wa unyanyasaji na ubaguzi anasema, Mónica Santamarina, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC. Anakaza kusema: "tunatekeleza mradi unaolenga kutokomeza ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wanawake Barani Afrika, kwa ajili ya mabadiliko ya kitamaduni na kijamii." Shirika la Kimataifa la Kuchunguza Wanawake (WWO), linalenga pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha mitandao ya ushirikiano kati ya dini, madhehebu pamoja na mashirika ya kiraia ili kutekeleza shughuli za mafunzo na maendeleo ili kuwajengea uwezo wanawake Barani Afrika. Warsha hii ni mwendelezo wa warsha iliyofanyika nchini Kenya kunako mwaka 2022. Hii ni fursa ya kuimarisha mtandao wa mashirika ya kiulimwengu na Bara la Afrika. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Afrika katika risala yake amegusia kuhusu hadhi na utu wa wanawake, maono na malengo ya Shirika la Kimataifa la Kuchunguza Wanawake (WWO), Barani Afrika na mwishoni ni ombi maalum kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dr. Doroth Gwajima na Mama Evaline Malisa Ntenga
Dr. Doroth Gwajima na Mama Evaline Malisa Ntenga

SHUKRANI: Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, sisi Wanawake Wakatoliki Afrika tunakushuru sana kwa kutenga muda katika ratiba yako ngumu kushiriki nasi siku hii muhimu tunapokutana pamoja kwa lengo moja kuu la kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mheshima Rais Mama Samia Suluhu Hassan ya kuwa sauti ya wasio na sauti… “the voice of the voiceless.” Katika kupitia Vipaumbele vyako 8 katika bajeti ya mwaka huu 2023/24, vipo vipaumbele viwili vinavyoendana na mradi wetu wa World Women’s Observatory (WWO): Kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiuongozi na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wazee; Kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum, huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia na huduma za msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa majanga mbalimbali na makundi mengine yenye uhitaji katika jamii. Hayo mawili yanaendana na kipaumbele namba moja cha WUCWO kwa kipindi cha 2023 – 2027, cha kutokomeza ukatili wa aina zote dhidi ya wale wote waliosukumizwa pembezoni mwa jamii na wasio na sauti. WAWATA NI NINI: Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, WAWATA (Wanawake Wakatoliki Tanzania) ni Jumuiya inayowaunganisha Wanawake Wakatoliki, Tanzania Iliyoundwa rasmi chini ya muundo wa Kanisa Katoliki.  Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972 umoja huu umekuwa na jukumu la kuwaweka Wanawake pamoja ili kutatua changamoto wanazokumbana nazo kila siku katika kulea familia. Tunashirikiana na Kanisa kutoa elimu ya kiroho ili kujenga familia yenye maadili na hivyo Taifa lenye uwajibikani. Tunatoa pia elimu ya kumsaidia mama kufanya shughuli za kiuchumi kuchangia pato la familia na Taifa. Kauli mbiu ya WAWATA ni ‘KWA UPENDO WA KRISTO, TUTUMIKIE NA KUWAJIBIKA.” WAWATA ni mwanachama hai wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani (World Union of Catholic Women Organisations, WUCWO); hivyo tunashiriki kikamilifu katika kutunga sera na kupendekeza vipaumbele vya muda mrefu na muda mfupi.

Wajumbe wa Mtandao wa Kiafrika Dhidi ya Ukatili na Ubaguzi wa Wanawake
Wajumbe wa Mtandao wa Kiafrika Dhidi ya Ukatili na Ubaguzi wa Wanawake

HADHI NA UTU WA MWANAMKE (Woman Dignity). Tamaduni nyingi katika nyakati za nyuma hazikumpa mwanamke nafasi stahiki katika jamii. Tukiangalia hata utamaduni wa taifa teule haukutambua nafasi na hadhi ya mwanamke, mfano katika kuhesabu watu – walihesabu wanaume tu bila wanawake na watoto. Tunasoma katika Maandiko, mathalani, watu waliokula mikate na samaki yapata elfu tano bila kuhesabu wanawake na watoto (Yn. 6: 11 -35). Ama mfano wa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi anahukumiwa yeye tu. Mwanamme aliyekuwa na uhusiano naye hatajwi kana kwamba yeye hahusiki (Yn. 8: 4 – 11). Kwa hivi mwanamke hakupewa nafasi stahiki katika jamii. Ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo ulinyanyua hadhi ya mwanamke. Kwanza kabisa, Yesu mwenyewe kama Mungu ameshuka hapa duniani kupitia kwa Mwanamke Mama Bikira Maria. Zaidi ya hayo mtangulizi wake, aliyemtayarishia njia, yaani Yohane Mbatizaji amezaliwa na mwanamke wa kawaida tu, maskini. Mungu ameanza mpango wa kumkomboa mwanadamu kupitia hawa wanawake. Bwana wetu Yesu Kristo amekuja kunyanyua hadhi ya mwanamke. Katika muktadha kama huo Kanisa Katoliki likifuata tabia ya mwasisi wake linatambua sana nafasi ya mwanamke. Kanisa linatambua mchango mkubwa na karama mbali mbali za wanamke. Na kweli kama jamii inavyokiri palipo na mwanamke kuna maendeleo, Kanisa limekuwa likitambua nafasi na mchango wa wanawake katika juhudi mbalimbali za kumkomboa mwanadamu kimwili na kiroho.

Papa Francisko akiwa na wajumbe wa WUCWO mjini Vatican
Papa Francisko akiwa na wajumbe wa WUCWO mjini Vatican

WORLD WOMEN OBSERVATORY (WWO) NI NINI: Baada ya miaka mingi ya mashauriano, uchunguzi na majadiliano, Umoja wa Mashirika ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO) uliamua kuunda, kwa msingi wa majaribio, Kikundi cha Utafiti wa Masuala ya Wanawake Duniani (WWO – World Women Observatory). Kufikia leo, hakuna kikundi chini ya mwavuli wa Kanisa kilichohusika moja kwa moja na uangalizi wa wanawake ambao unajumuisha kila aina ya wanawake ulimwenguni bila kujali Imani zao, hasa wale ambao kwa kawaida "hawana sauti" na "hawaonekani." Uangalizi ambao unafuata kanuni za ukweli na utaratibu wa asili wenye sura ya kiMungu wa kusikiliza kutoka moyoni, ambao maono yake yanakumbatia mafundisho ya kijamii ya Kanisa na ambayo yanatuonyesha ukweli wa wanawake katika maeneo mbalimbali ya sayari yetu, ikiwa ni pamoja na mahitaji yao makubwa, changamoto wanazopitia pamoja na ustahimilivu wao na uwezekano mkubwa wa mafanikio. WWO inajaribu kuziba ombwe hili.

Papa Francisko alikabidhiwa utafiti wa Amerika ya Kusini Juni 2022
Papa Francisko alikabidhiwa utafiti wa Amerika ya Kusini Juni 2022

MAONO YETU: Kuwaibua Wanawake, hasa wale walio katika mazingira magumu zaidi, ambao wanaonekana "hawaonekani", kwa upande wa mateso yao na uwezo wao, ili kuhamasisha na kuzalisha mikakati ya kichungaji na Kanisa, ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kiraia, sera za umma na Mataifa, na michango ya ajenda ya kimataifa ambayo inapendelea maendeleo ya kibinadamu ya wanawake na ya familia zao, jamii, na taifa lote. MALENGO YA WWO: Mheshimiwa Dkt Dorothy Gwajima, Malengo ya WWO ni Pamoja na: Kuwa kitovu cha taarifa zinazohusu ukweli wa Maisha ya wanawake ulimwenguni ndani na nje ya kanisa. Kwamba maarifa na uelewa yaliyopatikana katika mradi huu yanaleta mwanga na kuwekwa kwenye agenda ya kimataifa manyanyaso na visa vya kunyimwa haki wanawake pamoja na uwezo wa mwanamke huyu. Kuwezesha, kuhamasisha na kukuza vitendo vya kichungaji ili kuwa na mchango kwenye uhalisia wa mwanamke kijamii, kitamaduni, na kisiasa ya wanawake na wale wanaowazunguka. WWO AFRIKA: Utafiti wa majaribio ulifanyika Amerika ya kusini kuanzia 2021 na ripoti ikakabidhiwa kwa Baba Mtakatifu siku ya familia duniani iliyoiadhimishwa tarehe 12 Juni 2022 Roma Italia. Utafiti na mtandao Barani Afrika ulianza mwezi Mei 2022 kwa Warsha na mafunzo yaliyofanyika jijini Nairobi. Kupitia ushirikiano huu, tuliweza kuwafikia wanawake 10,000 na kuwahoji Wataalamu 270 barani Afrika kati ya Agosti 2022 hadi Aprili 2023. Timu hiyo pia ilitembelea Afrika Magharibi na kurekodi makala ambayo ilitazamwa kwa mara ya kwanza kwenye hadhira na Baba Mtakatifu tarehe 13 Mei 2023 siku ya WUCWO duniani. Matokea ya utafiti huo yatachambuliwa kwa kina katika Warsha hii kwa lengo la kutafuta mbinu bora ya kuwaibua wahanga na kuwasaidia kujikwamua kuendana na mazingira, tamaduni zetu Waafrika. Aidha tunaendelea kutengeneza mtandao wa kukomesha utamaduni huu mbaya.

Washiriki wa warsha Jijini Dar es Salaam baada ya Misa takatifu, Kurasini
Washiriki wa warsha Jijini Dar es Salaam baada ya Misa takatifu, Kurasini

OMBI KWA SERIKALI: Mheshimiwa Waziri, tunapofanya Warsha hii tunatambua hii ni hatua ya awali kabisa katika harakati zetu kama Wanawake Wakatoliki Barani Afrika kuwafikia na kuwaibua wale waliosukumizwa pembezoni. Kwa hakika juhudi zetu haziwezi kufanikiwa bila msaada na kuungwa mkono na serikali ambayo ina mkono mrefu.  Hivyo basi, tunaiomba Serikali kupitia Wizara yako itusaidie na kuimarisha mambo yafuatayo: Tanzania iliridhia Mkataba wa Haki za Mtoto wa mwaka 1991, ambao uliweka umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18, na Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) mwaka 1985, ambao unazitaka nchi kuhakikisha uhuru na ridhaa kamili ya ndoa. Hata hivyo sheria ya Ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971 imeweka umri wa chini wa ndoa kwa wasichana kuwa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi, na 18 kwa wavulana. Pamoja na sheria hiyo, tunazidi kuiomba Wizara yako ijaribu kutilia mkazo juu ya suala la kuwataka wazazi waone umuhimu wa watoto kupata elimu kwanza badala ya kufikiria kuwaozesha mapema. Kuweka utaratibu sahihi na wa haraka kuanzia ngazi za chini ili kufikisha taarifa za unyanyasaji/ ukatili zinazofanywa na jamii kwa makundi yote. Kuchukua hatua kali na kwa haraka za kinidhamu kwa wale wote wanaohusika na vitendo vya ukatili kwa makundi yote kwa ujumla na kuendelea kutoa elimu na kukemea masuala ya ukatili nchini kote.

Washiriki wa warsha wakati wa Ibada ya Misa Takatifu
Washiriki wa warsha wakati wa Ibada ya Misa Takatifu

TAMATI: Napenda kumalizia kwa kukushuruku Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zinazofanywa na wizara yako chini ya serikali ya Mheshimiwa Daktari Mama Samia Suluhu Hassan katika kutokomesha vitendo ya ukatili na unyanyasaji kwa makundi yote. Tunakuahidi kuendelea kushirikiana na Wizara yako katika kushiriki shughuli za Maendeleo na vipaumbele vya serikali katika kuifikia Tanzania tunayoitamani UTAMBULISHO – KWA MAKUNDI: Wafadhili wa WWO Afrika: Wajumbe wa Bodi ya Wanawake Wakatoliki Duniani kutoka kanda ya Afrika: Bi Doris Makhubu – Eswatini, Cecilia Asobayire – Ghana, Florence Namata – Uganda, Lucy Joceylin – Malawi, Marie Salome – Cameroon, Mary Gonsum – Nigeria, Theresa Arama – Mali, Veronica Lebona – South Africa (Beatrice Tavares – Senegal, Titi Kamano – Gunea). Wawakilishi wa WUCWO: Afrika Kusini, Benin, Burkinafaso, Cameroon, Chad, Congo, Eswatini, Ethiopia, Gabon, Ghana, Kenya, Malawi, Nigeria, Rwanda, Senegal, Sudan ya Kusini, Tanzania (Wenyeji), Togo, Uganda, Zambia, Argentina, Italia, Hispania.

Naye Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania, TEC katika hotuba yake ya kuwakaribisha wajumbe wa wasrha ya siku nne, nchini Tanzania amegusia kuhusu mchango wa wanawake wakatoliki katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; mchango wa wanawake wakatoliki katika kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema na kwamba, wanawake wakiwezeshwa vyema, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika changamoto mamboleo zinazoendelea kuwasumbua walimwengu.

Warsha Dar
03 July 2023, 17:45