Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda Ya Tanzania: Uchaguzi Mkuu: Padre Vedasto Ngowi
Na Padre Dominic Mavula, C.PP.S., na Ndahani Lugunya, - Dodoma, Tanzania.
Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., ni Shirika la Kitume lililoanzishwa na Mtakatifu Gaspar del Bufalo kunako tarehe 15 Agosti 1815 na kulisimika katika nguzo kuu tatu: Maisha ya kijumuiya, tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu na Utume. Utume: kama mhimili wa kwanza wa wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu ni kuendeleza utume wa Mtakatifu Gaspari wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mhimili wa pili ni maisha ya jumuiya, ambapo wamisionari huishi pamoja daima, hasa utume unapowaruhusu kufanya hivyo. Katika kukamilika katika hilo, Wamisionari huunganishwa na kuongozwa na kifungo cha upendo badala ya nadhiri. Mhimili wa tatu ni Tasaufi ya Damu Takatifu. Kristo Yesu aliyemwaga Damu yake Azizi ni alama ya upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote. Na tasaufi ya Damu Azizi ndiyo inayowahamasisha wamisionari mpaka leo hii kuunganisha maisha na kujenga maisha ya jumuiya wakitembea huko na huko wakiwa wameshikamana na wale wanaoteseka na kutafuta maridhiano kila kinaposikika kilio cha damu katika dunia hii iliyogawanyika. Kwa kifupi kilio cha damu ndiyo tasaufi dhahiri ya Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na daima wanajitahidi kusikiliza na kutoa majibu muafaka kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.
Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania kuanzia tarehe 10 hadi 13 Julai 2023 wamekuwa wakiadhimisha mkutano mkuu wa tatu wa Shirika sanjari na uchaguzi mkuu ambapo Mheshimiwa Padre Vedasto Ngowi amechaguliwa kuwa Mkuu wa Kanda, Padre Achileus Mutalemwa, Makamu, Padre Felix Mushobozi, Katibu mkuu, Padre Dominic Mwaluko, Mhazini na Padre Richard Kungi, Mshauri. Uchaguzi kuu umesimamiwa na Mheshimiwa sana Padre Emanuele Lupi, C.PP.S. Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni. Katika mahubiri yake ya kumsimika Padre Vedasto Ngowi kuwa Mkuu wa Kanda, amewataka wamisionari kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni utume unaowataka kutoka nje ili kukutana na watu wa Mungu, tayari kuweka agano lao vyema na Kristo Yesu, kwa kujenga mahusiano na mafungamano shirikishi kati ya kiini cha Damu Azizi na wapokeaji. Wamisionari wawe na nguvu ya kuelekea kiini cha Agano na kwamba, wote wanaalikwa kukinywea kikombe kimoja, ili kujenga ushirika, na hatimaye waweze kuwa mwili mmoja, roho moja na nia moja kama walivyokuwa wale Wakristo wa Kanisa la mwanzo.
Uongozi mpya wa Shirika unapewa jukumu la kushuhudia na kutangaza matumaini kwa wanashirika waliopondeka na kuvunjika moyo; watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho sanjari na utakatifu wa maisha; ili harufu hii ya utakatifu iwafuate na kuwaambata watu wa Mungu wanaowahudumia. Hii ni changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Shirika na Kanisa katika ujumla wake, huku wakijitahidi kufuata nyayo za Kristo Yesu aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika wimbi la dhambi na mauti. Waendelee kujitoa kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: Kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani katika medani mbalimbali za maisha. Kwa upande wake, Padre Vedasto Ngowi, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania ambaye amechaguliwa kwa mara ya pili amewashukuru wamisionari wote waliomwamini na hivyo kumchagua tena kuwaongoza kwa awamu ya pili. Ni matumaini yake kwamba, wamisionari waliomwamini watashirikiana na kushikamana naye katika kuliongoza Shirika nchini Tanzania. Amewaomba wanashirika na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake ili kusudi atende kile kinacho mpendeza Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko pia kwa wanashirika kuwa waaminifu na waadilifu kwa wito, maisha na utume wao. Viongozi waliochaguliwa watakuwepo madarakani kwa muda wa miaka minne yaani kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka 2027.