Tafuta

Mashemasi wanaotarajiwa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre Jimbo Katoliki la Same tarehe 6 Julai 2023 ni: Shemasi Vincent Msoffe, Shemasi Michael Viano, Shemasi James Singo na Shemasi Emmanuel Lucas. Mashemasi wanaotarajiwa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre Jimbo Katoliki la Same tarehe 6 Julai 2023 ni: Shemasi Vincent Msoffe, Shemasi Michael Viano, Shemasi James Singo na Shemasi Emmanuel Lucas. 

Upadrisho Jimbo Katoliki la Same, Tanzania: Mapadre ni Mawakili wa Siri za Mungu

Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki la Same, Tanzania anatarajia tarehe 6 Julai 2023 kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa: Shemasi Vincent Msoffe, Shemasi Michael Viano, Shemasi James Singo na Shemasi Emmanuel Lucas. Hawa sasa wanapaswa kuwa ni mfano bora wa Kristo Yesu Mchungaji mwema; wahudumu wa Sakramenti za Huruma ya Mungu; Watumishi na Mawakili wa siri za Mungu; wanatumwa kuinjilisha na kuinjilishwa, tayari kusadaka maisha yao kwa Kristo!  

Na Vincent Patrick Msofe, - Same, Kilimanjaro, Tanzania

Mapadre wanapaswa kuwa ni mfano na kielelezo cha Kristo Mchungaji mwema kwa kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; sadaka inayojionesha katika mchakato wa maisha na utume wa Kipadre, kwa kujikita katika huduma makini kwa Familia ya Mungu wanayoihudumia. Waamini wanatambua na kuthamini sadaka ya maisha ya Wakleri wanaojitosa bila ya kujibakiza; wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa wanaotekeleza dhamana na wito wao katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu. Wawe ni viongozi wanaoonesha dira na njia ya kufuatwa na wala si watu wanaotoa amri na kuendelea “kuponda maisha.” Mapadre wanaojisadaka barabara ni mfano mwema katika maisha ya kiroho na wengi wanaweza kuwatambua Mapadre wa namna hii kuwa kweli ni “Watu wa Mungu” ambao hawajamezwa na malimwengu na kutopea huko huko! Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya mtindo na ushuhuda wa maisha yake, anaendelea kujenga na kuimarisha wanafunzi katika shule ya Kristo Yesu, kielelezo makini kinachopata chimbuko lake, Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na huduma ya upendo kwa kuwaosha wanafunzi wake miguu, ili kuendeleza dhamana na wito huu kwa Familia ya Mungu. Wito na maisha ya Kikristo, yanawachangamotisha Mapadrec kutoka katika undani na ubinafsi wao, tayari kuwaendea wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kuwatangazia Injili ya Furaha, Imani na Matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Miito ya Upadre nchini Tanzania imeongezeka maradufu.
Miito ya Upadre nchini Tanzania imeongezeka maradufu.

Hapa Wakristo wote wanakumbushwa kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki katika: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo, hivyo wanapaswa kutambua kwamba, wao pia ni wamisionari wanaotumwa Kuinjilisha na kuinjilishwa kwa njia ya mifano bora na utakatifu wa maisha. Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!

Shemasi Vincent Patrick Msofe akiwa Roma 2019-2022
Shemasi Vincent Patrick Msofe akiwa Roma 2019-2022

Mimi ni Shemasi Vincent Msoffe, mtoto wa Patrick Msoffe na Esther Mtera kutoka Jimbo Katoliki la Same, Tanzania. Mnamo tarehe 27/06/1995 nilizaliwa nikiwa mtoto wa pili wa familia yetu yenye watoto wanne. Nilipata Elimu ya awali mnamo mwaka 2000 hadi mwaka 2001. Mnamo mwaka 2002 hadi mwaka 2008 nilipata elimu ya Msingi katika shule ya kata ya Vingunguti mkoani Dar es Salaam. Huku nikiendelea na sala na malezi ya wito wangu, kwa msaada wa mapadre, wazazi wangu na marafiki zangu hatimaye, Mnamo mwaka 2009 nilipokelewa kwenye Kituo cha Malezi Dido, Jimbo Katoliki la Same ambako nililelewa kwa mwaka mmoja kabla ya masomo ya sekondari. Mnamo mwaka 2010 nilianza masomo ya sekondari kwenye Seminari ya Roho Mtakatifu Chanjale, Jimboni Same na nilihitimu masomo ya Sekondari mnamo mwaka 2013. Mwaka 2014 niliendelea na masomo ya Kidato cha tano na sita katika seminari hiyohiyo na kuhitimu mnamo mwaka 2016. Baada ya kuhitimu masomo ya Kidato cha tano na sita, mnamo mwezi Mei mwaka 2016 nilipokelewa katika Nyumba ya Malezi ya Mtakatifu Yohane Bosko, Jimboni Same. Mnamo Mwezi Septemba mwaka 2016, nilitumwa kwenda Seminari Kuu ya Bikira Maria Malkia wa Malaika, Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi kwa masomo ya Falsafa na nilihitimu mnamo mwezi Juni mwaka 2019.

Roho Mtakatifu apende kuwaimarisha Mapadre wapya katika huduma
Roho Mtakatifu apende kuwaimarisha Mapadre wapya katika huduma

Na Mwaka huohuo mwezi Agosti, 2019 Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki la Same alinituma Roma, Italia kwa masomo ya Taalimungu katika Chuo cha Kipapa cha Malkia wa Mitume na nilienda kupokea malezi katika Seminari ya Kipapa ya Bikira Maria Mama wa Kanisa Mjini Roma. Mnamo mwezi Agosti 2022 nilirejea nyumbani, Jimboni Same na nilitumwa kufanya utume katika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Bwambo. Baada ya utume kwa kipindi cha Miezi mitano, Mnamo tarehe 12 mwezi Januari mwaka 2023 nilipewa daraja ya Ushemasi wa Mpito Jimboni Same. Baada ya Ushemasi nilitumwa kufanya utume katika Nyumba ya Askofu, Jimboni Same. Napenda Kumshukuru Mungu kwa neema na baraka zake nyingi anazonijalia na nawaomba muendelee kuniombea hasa wakati huu ninapojiandaa kupokea daraja ya Upadre mnamo tarehe 6 ya mwezi Julai mwaka 2023 pamoja na Mashemasi wenzangu wa Jimbo Katoliki la Same; Shemasi Michael Viano, Shemasi James Singo na Shemasi Emmanuel Lucas.

Shemasi Vincent Msoffe
05 July 2023, 15:56