Tafuta

Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi,  Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam , Tanzania Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam , Tanzania 

Tanzania:Shirika la wabenediktini watimiza miaka 25 wakiwa Mwanza

Askofu Mkuu J.T.Ruwa'ichi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Tanzania,akitoa mahubiri yake katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Masista Wabenediktini,Julai 15 huko Kawekamo,Mwanza,alisema:“Mmekuwa thabiti kwa miaka 25 tunawapongeza,sasa tunasema mmekuwa wakomavu,ila ukomavu huo usiishie miaka 25,endeleeni kusimamia habari njema na kuwa mashahidi wa Kristo.

Na Patrick P.Tibanga-Radio Mbiu Kagera & Angella Rwezaula,- Vatican

Watawa na wakristu wabatizwa wametakiwa kusimamia habari njema,kuwa mashahidi wa Kristu kwa watu wote ili ufalme wa Mungu ujengeke na watu wa Mungu watakatifuzwe. Wito huo ulitolewa na Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi,  Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam , Tanzania, wakati wa homilia yake katika maadhimisho ya  Jubilei ya miaka 25 ya Masista Wabenediktini, mnamo tarehe 15 Julai 2023 katika nyumba ya Kawekamo, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Tanzania.

Watawa watoe ushuhuda wa matakatifu

Katika homilia yake Askofu Mkuu Ruwa'ichi alisema kuwa, kila mbatizwa ni mpakwa mafuta anayetumwa kutangaza habari njema na kufanywa wanakanisa na wafuasi wa Kristo, hivyo kuwataka Watawa na waamini wakristo wote kutoa ushuhuda wa matakatifu na kusimamia kuitangaza habari njema, kuwa mashahidi wa Kristo katika mazingira na nyakati tofauti ili ufalme wa Mungu ujengeke na watu wa Mungu watakatifuzwe.

Kuwa kielelzo cha Umoja, Upendo na ushuhuda wa dhati

“Yesu amewaita kama watawa ndani ya Shirika maalum, hivyo mnatakiwa kuishi kwa Upendo, kuvumiliana na kushikamana na kutakatifuzana, katika Utawa, na ninawaomba muwe wakereketwa katika jangwa ni mahali maalum pa kuimarishwa”, alisema Askofu Mkuu Ruwa'ichi. Aidha Askofu aliwataka Watawa kuwa kielelezo cha Umoja, Upendo na Ushuhuda wa dhati kwa Watawa wote ili kanisa la Mungu duniani kote liendee kustawi na kuimarika ili ufalme wa Mungu uendelee kushamiri, na kuwa wakereketwa katika wito na ushuhuda.

Manabii wa uongo wapo zama zote

“Mmekuwa thabiti kwa miaka 25 tunawapongeza, sasa tunasema mmekuwa wakomavu, ila ukomavu huo usiishie miaka 25, endeleeni kusimamia habari njema na kuwa mashahidi wa Kristo. Katika mazingira na nyakati zetu ili ufalme wa Mungu ujengeke na watu wa Mungu watakatifuzwe,” alisema Askofu Mkuu Ruwa'ichi. Kwa kuhitimisha homilia alisema kwamba, manabii wa uongo wapo zama zote ambao wanawarubuni watu wa kuwaambia wanayotaka kusikia badala ya kuwaambia watu yale Mungu anayotaka kuwaaambia, wanawarubuni kwa habari za kugushi. Hivyo wakristo wote wanatakiwa kuwa makini nakuitambua vyema sauti ya mchungaji wao mwema.

Ushuhuda wa watawa kila kona ya dunia

Masista  hawa Wabenediktini wakifanya Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa nyumba yao ya  Masista wa Shirika hilo waliona ushuhuda wa  Sr Anthonia Nimirwa OSB na Sr Benedicta Nevumba OSB wakirudia nadhiri za Utawa katika Shirika la Wabenediktini katika nyumba ya Kawekamo, Mwanza.  Misa Takatifu ya Jubilei hiyo ilihudhuriwa na Askofu Mstaafu Bruno Ngonyaji wa Lindi, Askofu Simon Masondole wa Bunda, Askofu Michael Msoganzila wa Musoma, Askofu Flavian Kasalla wa Geita na Askofu Mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu la Mwanza, Askofu Mkuu Jude Ruwa'ichi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam aliyeongoza misa pamoja na Wakuu wa Mashirika mbali mbali ya Kitawa yaliyomo nchini Tanzania.

Shirika la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing lilianzishwa mnamo mwaka 1884, huko St. Ottilien nchini Ujerumani. Shirika hilo lilianzishwa na Padre Andreas Amrhein huko Ujuerumani, akiwa na lengo la kwenda kuinjilisha Neno la Mungu. Karama ya Shirika ni kuishi katika jumuiya chini ya kiongozi wa nyumba kama njia makini ya kujitakatifuza na kuendelea kuinjilisha, kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Shirika hili  limeenea karibu sehemu nyingi, miongoni mwa nchi hizo ni Kenya, Uganda, Brazil, Ufilippini, Angola, Korea, Namibia, Ujerumani, Marekani na Tanzania.

Wabenediktini wamefikisha miaka 25 tangu wafungue nyumba huko Kawekamo Mwanza
18 July 2023, 15:38