Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 17 ya Mwaka A: Thamani na gharama ya Ufalme wa Mungu Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 17 ya Mwaka A: Thamani na gharama ya Ufalme wa Mungu 

Tafakari Dominika ya 17 Mwaka A wa Kanisa: Thamani na Gharama za Ufalme wa Mungu

Wazo kuu katika masomo ya dominika hii ni thamani, gharama na utamu wa kuwa katika ufalme wa Mungu. Kumbe kuacha vyote na kufanya kila linalowezekana ili kuupata ufalme wa Mungu ni kwa maana zaidi katika maisha kwani kunatuhakikishia uzima wa milele. Ndivyo sala ya mwanzo inavyosistiza ikisema; “Ee Mungu, wewe ndiwe mlinzi wa wenye kukutumaini; pasipo wewe hakuna lililo thabiti, hakuna lililo takatifu. Utuzidishie huruma yako; utusimamie!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 17 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Wazo kuu katika masomo ya dominika hii ni thamani, gharama na utamu wa kuwa katika ufalme wa Mungu hakuwezi kufananishwa na kitu kingine chochote. Kumbe kuacha vyote na kufanya kila linalowezekana ili kuupata ufalme wa Mungu ni kwa maana zaidi katika maisha ya mwanadamu kwani kunatuhakikishia uzima wa milele. Ndivyo sala ya mwanzo inavyosistiza ikisema; “Ee Mungu, wewe ndiwe mlinzi wa wenye kukutumaini; pasipo wewe hakuna lililo thabiti, hakuna lililo takatifu. Utuzidishie huruma yako; utusimamie, utuongoze. Na sasa tutumie vema mambo ya dunia, hali tumeambata na ya milele.” Somo la kwanza ni la kitabu cha kwanza cha Wafalme (1Fal. 3:5, 7-12). Mfalme Sulemani alipoenda kuhiji huko Gibeoni kilometa chache kutoka Yerusalemu, ili aweze kumsifu Mungu kwa kumtolea sadaka na kuomba ulinzi wake katika utawala wake; Mungu anamtokea na kumwambia; “Omba upendacho nami nitakupa” (1Fal. 3:5). Sulemani anaomba busara na hekima ili aweze kuliongoza vyema taifa lake akisema; “Mpe mtumishi wako moyo wa hekima ajue kutofautisha jema na baya” (1Fal. 3:9). Sulemani aliomba hekima yaani mwanga wa kuelewa mpango wa Mungu na uwezo wa kutekeleza mpango huo, moyo mpole ili aweze kuongozwa na Mungu wakati wote. Katika sala yake alimshukrani Mungu kwa uwezo na utajiri aliyourithi kutoka kwa baba yake Daudi. Lakini pia alikuwa na hekima kiasi cha kutambua kwamba hizi zilikuwa hazina zenye kupita uwezo wake; kuongozwa na Mungu ilikuwa hazina ya kweli. Mungu alikubali ombi lake, akamwongezea fahari, mali na maisha marefu kwani moyo uliomnyenyekevu hufungua milango ya Mungu.

Ufalme wa Mungu ni hazina kubwa
Ufalme wa Mungu ni hazina kubwa

Mungu akamwambia; “Kwa kuwa hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako, tazama nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe”. Chaguo la Sulemani ni mwangwi wa maneno ya Yesu yasemayo; “Tafuteni kwanza ufalme wa Mungu, mengine yote mtapewa kwa ziada”. Je, Mungu akitokea nyakati hizi akakuambia omba lolote utaomba nini? Kumbuka daima maneno ya mzaburi katika wimbo wa mwanzo akisema; “Mungu yu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani. Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo” (Zab. 68:5-6). Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi Mtume (Rum. 8:28-30). Mtume Paulo katika somo hili anaeleza kwa nini ufalme wa Mungu ni kitu cha thamani kubwa. Ni kwa sababu tumechaguliwa na Mungu kuwa katika ufalme wake. Chaguo la Mungu la kutuchagua ni la tangu zamani (Rom 8:29), kuanzia mwanzo (Ef 1:9). Mungu alitujua na kutuchagua tangu milele. Hivyo maisha yetu yamo katika umilele wa Mungu. Tumeshirikishwa uzima huu kwa njia ya Kristo. Ni vyema kuyasikiliza maneno halisi ya Mtume Paulo. Naye anasema; “Twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza”. Kumbe Mungu alitufanya kuwa watu wake kabla hata hatujazaliwa kabla ulimwengu haujaumbwa. Wakati wote amekusudia tuwe katika ufalme wake na kushiriki uzima na furaha yake.

Thamani na gharama za Ufalme wa Mungu
Thamani na gharama za Ufalme wa Mungu

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 13:44-52). Sehemu hii ya Injili ni mwendelezo wa mafundisho ya Yesu kuhusu ufalme wa Mungu kwa mifano tunayoisoma katika sura ya 13 ya Injili ya Mathayo. Domenika hii Yesu anatumia mifano mitatu ya mwisho amabyo ni mfano wa lulu yenye thamani, hazina iliyofichika na juya/neti, kueleza habari za ufalme wa Mungu. Kwa mifano ya hazina na lulu anaelezea dhamani ya ufalme wa Mungu. Na kwa mfano wa wavu anasisitiza kuwa siyo watu wote wanaoingia katika Kanisa lake wataokoka katika hukumu ya mwisho. Ni wale wasiojiweka katika hali njema ya kiroho wataukosa ufalme huu. Ufalme wa Mbinguni ni nini? Ufalme wa Mbinguni ni hali ya uwepo wa Mungu unaoleta furaha kwa wale walioko ndani yake. Ufalme huu unaanza kujengeka na kudhihirika hapa ulimwenguni, na baadaye kukamilika Mbinguni. Hapa ulimwenguni, mtu anakuwa katika ufalme wa Mungu pale anapoishi katika uwepo wa Mungu na kutimiza mapenzi ya Mungu. Kanisa ni chombo cha kuueneza ufalme wa Mungu na kuwaleta watu ndani mwake. Kwa maana hiyo, mtu anaweza akawa ndani ya Kanisa lakini yupo nje ya Ufalme wa Mungu kama haweki juhudi kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Tunasali katika sala ya Baba yetu tukisema; “Ufalme wako ufike utakalo lifanyike duniani kama mbinguni” (Mt 6:10). Kuingia katika umoja wa Kanisa ni mwaliko wa awali wa kuingia katika ufalme wa Mungu. Tunaingizwa katika juya (neti). Kazi inayobaki ni kuhakikisha tunadumu katika kutenda mema mpaka mwisho wa maisha yetu ili wakianza kuchambua vilivyo katika juya ama neti hii basi tukutwe tukiwa tunafaa.

Ufalme wa MUngu ni sawa na lulu ya thamani
Ufalme wa MUngu ni sawa na lulu ya thamani

Hakuna kilicho kizuri kama kuwa ndani ya Ufalme wa Mungu. Lengo la maisha ya binadamu ni kuwa na furaha. Furaha ni hali ya kuridhika inayoletwa na tendo jema. Matendo mema ni matendo yanayoendana na mapenzi ya Mungu. Hivyo, kutimiza mapenzi ya Mungu kunaleta furaha na kiuhalisi ndiyo kuwa katika Ufalme wa Mbinguni. Hivyo, kuwa katika Ufalme wa Mbinguni kunaleta furaha. Hii furaha tunaanza kuionja tukiwa hapa duniani kwa kutenda matendo mema na pia furaha hii itakamilika katika Ufalme wa Mungu mbinguni baada ya maisha ya hapa duniani. Kwa hiyo, lengo la maisha yetu linapaswa kuwa ni “kuuona uso wa Mungu na kuwa na furaha ya milele”. Mzaburi anasema; “Ilikuwa hamu ya Moyo wangu kuuna uso wa Bwana”. Mtume Paulo anasisitiza akituonya kwa kusema; “Kama lengo la maisha yetu lipo katika vitu vya ulimwengu huu, basi sisi ni watu wakusikitikiwa sana” (1Kor 15:19). Ndiyo maana katika Injili Yesu analinganisha Ufalme wa Mungu na “kitu cha thamani kubwa”, “lulu iliyo njema au hazina kubwa sana.” Ufalme wa Mungu unajitokeza katika maisha yetu ya kawaida. Historia inasema kuwa waisraeli walikuwa na kawaida ya kuficha vitu vya thamani ardhini katika mashamba yao wakati wa misukosuko ya kivita, maisha yalipokuwa hatarini. Pia iliwawia wevi na wanyang’anyi vigumu kugundua mali imelala wapi. Mwenye mali alipokufa bila kumuonesha mrithi, au alipokaa mbali muda mrefu, mali ilidumu ardhini. Kama mtu aliigundua mali iliyofichwa katika shamba la mwingine, hakuwa na haki ya kuitwaa mali ile kama yake. Njia ya kuipata mali hiyo ilikuwa kulinunua shamba ili liwe mali yake. Baada ya kufanya hivyo hazina zote chini ya ardhi zinakuwa zake. Katika mfano huu mkulima aliyeiona hazina aliificha zaidi ili ibaki salama hadi hapo atakapokamilisha mipango ya kumiliki shamba. Ni kawaida mtu anakuwa na furaha sana pale anapopata kitu cha thamani kubwa na anaona kuwa mengine yote aliyonayo si kitu. Kwa urahisi furaha na hiari, mtu huvitoa vitu vya zamani ili avipate vipya. Kwa furaha anauza yote aliyonayo na ananunua lile shamba lenye hazina. Vivyo hivyo enzi zile lulu zilikuwa na thamani sana, hata kuzidi dhahabu, ziliuzwa kwa bei kubwa. Wafanyabiashara walisafiri mbali kuzisaka lulu. Mfanyabiashara alikuwa tayari kuuza yote aliyonayo ili kuipata lulu ya thamani.

Ufalme wa Mungu ni kitu cha thamani kubwa
Ufalme wa Mungu ni kitu cha thamani kubwa

Kumbe, anayetambua kuwa utawala wa Mungu ni kitu cha thamani kubwa, atafanya hivyo hivyo. Mtu anaamua kuyaacha ya zamani yaani mali, ndugu au marafiki ili awe na uraia mwema katika utawala wa Mungu. Mifano hii inatuhakikishia kuwa ukristo ni lulu yenye thamani kubwa kuliko mengine yote. Lakini tunahitaji Hekima ya kujua mapenzi ya Mungu. Ndiyo maana Solomoni alipoambiwa na Mungu aombe lolote “aliomba Hekima ya kupambanua mema na mabaya”. Hili ndilo tunaloliihitaji, maana ulimwengu huu umejaa vitu vingi vinavyong’aa. Tusipokuwa na hekima, tunaweza kudhani tumegundua hazina au lulu kumbe ni dhambi na mauti. Tunahitaji hekima ya kutambua kuwa kutimiza mapenzi ya Mungu kunaleta furaha ya kweli, kwanza hapa duniani na baadaye huko mbinguni. Kutimiza mapenzi ya Mungu si kazi rahisi kunahitaji gharama. Ndiyo maana Kristu anasema; “Anayetaka kuwa mfuasi wangu lazima ajikane mwenyewe abebe msalaba wake na anifuate” (Mt 16:24). Na Mtume Paulo anakazia kusema; “Maana Ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa tu, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo, humpendeza Mungu na kukubaliwa na watu” (Rum 14:17). Basi daima tumuombe Mwenyezi Mungu atujalie roho ya hekima na busara ya kuweza kujua kuwa ufalme wake ni wa dhamani kuliko malimwengu yote. Kama sala ya kuombea dhambihu inavyosisitiza kusema; “Ee Bwana, tunakuomba upokee vitu hivi ulivyotukirimia ambavyo tunakutolea. Nayo mafumbo haya matakatifu yatutakase hapa duniani kwa nguvu ya neema yako, na kutufikisha kwenye furaha za milele”. Nayo antifona ya wimbo wa komunio inatukumbusha jambo hili ikisema; “Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; maana hao watamwona Mungu” (Mt. 5:7-8). Huu ndio wokovu aliotuletea Kristo kama sala baada ya Komunio inavyohitimisha ikisema: “Ee Bwana, tumepokea sakramenti takatifu iliyo ukumbusho wa siku zote wa mateso ya Mwanao. Tunakuomba sakramenti hii aliyotujalia Mwanao kwa mapendo makuu ituletee wokovu.” Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika ya 17 ya Mwaka A
27 July 2023, 14:36