Tafuta

Ni kitu gani kilicho cha msingi katika maisha yangu ambacho nikikipata sitahitaji tena kitu kingine chochote? Ni kitu gani kilicho cha msingi katika maisha yangu ambacho nikikipata sitahitaji tena kitu kingine chochote?  

Tafakari Neno la Mungu Dominika 17 ya Mwaka A Kanisa: Ufalme wa

Yesu anatoa mifano miwili ya vitu vya thamani. Cha kwanza ni hazina iliyofichwa shambani. Mtu alipoigundua hazina hiyo alitamani kuipata. Ona ni thamani gani iliyokuwa nayo hiyo hazina hadi yule aliyeiona alikwenda kuuza vyote alivyonavyo ili anunue shamba lote. Mbele ya hazina hiyo vyote alivyokuwa navyo havikuwa tena na maana, akaviuza. Akaamua anunue shamba zima. Solomoni aliomba hekima, yaani kuwa karibu na Mwenyezi Mungu katika maisha!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika ya 17 ya mwaka A wa kanisa yanatualika tuupokee ujumbe wake tukijiuliza swali la msingi katika maisha na safari yetu ya imani: ni kitu gani ninachokitafuta? Ni kitu gani ninachohangaika ili nikipate niridhike? Ni kitu gani kilicho cha msingi katika maisha yangu ambacho nikikipata sitahitaji tena kitu kingine chochote? Tukiongozwa na swali au maswali hayo, tuyaangalie sasa walau kwa kifupi masomo yote matatu ya dominika hii. Ufafanuzi wa Masomo: Tukianza na somo la Injili ambayo inatoka kwa Mwinjili Mathayo (Mt 13:44-52), Yesu anatoa mifano miwili ya vitu vya thamani. Cha kwanza ni hazina iliyofichwa shambani. Mtu alipoigundua hazina hiyo alitamani kuipata. Ona ni thamani gani iliyokuwa nayo hiyo hazina hadi yule aliyeiona alikwenda kuuza vyote alivyonavyo ili anunue shamba lote. Mbele ya hazina hiyo vyote alivyokuwa navyo havikuwa tena na maana, akaviuza. Akaamua anunue shamba zima. Kwa sheria za Kiyahudi za wakati huo aliyemiliki ardhi alimiliki pia na vyote vilivyo chini ya ardhi. Hivyo kununua shamba kulimhakikishia kuwa hazina iliyofichwa shambani humo kwa hakika itakuwa yake.  Mfano wa pili unafanana na huo wa kwanza. Katika mfano huu kitu chenye thamani ni lulu, madini ambayo mfanya biashara alipoyaona naye alikwenda kuuza vyote alivyonavyo ili ayanunue. Mbele ya lulu hiyo, mbele ya madini hayo vyote alivyokuwa navyo mfanya biashara huyo havikuwa tena na thamani. Aliuza vyote kwa kuwa aliamini akiipata lulu hiyo au akiyapata madini hayo atakuwa amepata vyote.

Ufalme wa Mbinguni ni hazina iliyofichika sana
Ufalme wa Mbinguni ni hazina iliyofichika sana

Mifano hii miwili kwa namna fulani inatoa pia picha ya maisha yetu kuhusu yaliyo matamanio, vipaumbele na kama tulivyotangulia kujiuliza mwanzoni, kile kitu au vile vitu ambavyo katika maisha tunavitafuta ili kuwa na amani ya roho. Dhamira hii tunaikuta pia katika somo la kwanza ambalo linatoka katika kitabu cha kwanza cha Wafalme (2Fal 3:5, 7-12). Mungu anamtokea Mfalme Solomon na anamwambia “omba utakalo nikupe.” Kwa Solomoni, kama ambavyo ingekuwa kwa yeyote kati yetu hii leo, huu haukuwa mtihani mwepesi. Nafasi Mungu anayompa Solomoni ni kwenda kuangalia kile kitu ambacho kwa wakati ule na daima kimekuwa ndio matamanio yake kukipata. Ni kama Mungu anamwambia Solomoni ile hazina uliyoiona imesitirika shambani au ile lulu ya thamani ambayo katika maisha yako umetamani daima kuuza vyote ili uipate ni ipi? Omba sasa hivi nikupe. Solomoni anaomba hekima. Katika uyahudi, hekima ilifahamika kama mto unaotiririka kutoka kwa Mungu mwenyewe, chanzo che hekima ni Mungu. Aombaye hekima, kwa maneno mengine aliomba maongozi ya kimungu. Anapoomba hekima, kwa maneno mengine Solomoni anaomba ukaribu na Mungu. Ombi la Solomoni linampendeza Mwenyezi Mungu naye anampa hekima pamoja na mengine ambayo hata hakuyaomba. Fundisho tunalolipata kutoka katika somo hili katika muungano na somo la injili ni kuwa yeye ambaye katika vitu vyote humtafuta Mungu, kwa njia ya Mungu huvipata vitu vyote. Mungu ndiyo ile hazina iliyofichika katika shamba, Mungu ndiyo ile lulu ya thamani ambayo inafaa kabisa kuuza vyote tulivyonavyo ili kumpata.

Mwanadamu ni kito cha thamani mbele ya Mungu
Mwanadamu ni kito cha thamani mbele ya Mungu

Wakati ambapo tunafanya tafakari hii juu ya hazina au lulu yenye thamani ambayo mwanadamu huitafuta katika maisha yake, somo la pili kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi linakuja kubadilisha kidogo mtazamo. Linakuja kutuonesha kuwa machoni pa Mungu sisi ndio hiyo hazina iliyositirika na sisi ndio hiyo lulu yenye thamani. Mtume Paulo anaonesha mambo ambayo Mungu ameyafanya ili kumvuta mwanadamu karibu naye na ni mambo yanayofanana fanana na kile alichofanya mkulima pale alipouza vyote alivyonavyo ili anunue shamba lenye hazina na pia yule mfanyabiashara ili anunue lulu yenye thamani. Mtume Paulo anasema wale ambao Mungu aliwachagua tangu asili, aliwaita, alipowaita akawahesabia haki na aliowahesabia haki akawatukuza. Kwa maneno haya mafupi, Mtume Paulo anaeleza historia nzima ya wokovu. Anaeleza yale aliyofanya tangu mwanzo kwa taifa lake teule. Anaposema aliwachagua tangu asili anazungumzia Agano ambalo Mungu aliliweka pamoja na waisraeli akiwachagua wao kutoka mataifa mengine. Kisha kuingia nao Agano aliwaita, yaani aliwajalia wito wa kumjua Kristo na kumpokea katika maisha yao. Wale waliompokea Kristo kwa imani akawahesabia haki, yaani akawakomboa kwa mastahili ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Wale aliowakomboa akawatukuza, yaani akawapa utukufu. Mungu huwashirikisha utukufu wake watakatifu walio mbinguni. Kuwapa watu utukufu maana yake ni kuwaingiza katika ufalme wake wa mbinguni ili wakae naye milele.  Yote hayo amefanya ili ampate mwanadamu aliye hazina na aliye lulu machoni pake. Sasa haya yote ambayo Mungu aliyafanya kwa taifa lake teule ndiyo anayoendelea kuyafanya hadi leo kwa njia ya Kanisa. Agano jipya na la milele linatangazwa kila dakika Kanisa linapoadhimisha sakramenti hasa Misa Takatifu, humo Mungu anaendelea kuita ili watu wamuongokee Kristo, wale wanaomuongokea Kristo anawahesabia haki, yaani anawajalia wokovu na wale anaowajalia wokovu anawaahidia uzima wa milele mbinguni watakaposhiriki utukufu wake.

Mwanadamu anahitaji kuwa karibu zaidi na Mungu
Mwanadamu anahitaji kuwa karibu zaidi na Mungu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasikiliza masomo ya dominika hii na kupata ufafanuzi wake, ni wakati sasa wa kurudia lile swali au maswali tuliyojiwekea mwanzoni: Ni kitu gani ninachohangaika ili nikipate niridhike? Ni kitu gani kilicho cha msingi katika maisha yangu ambacho nikikipata sitahitaji tena kitu kingine chochote? Tukiyaangalia kwa ukaribu masomo ya dominika hii, tunaona kuwa yenyewe yametupa majibu mawili au jibu moja lililo katika ngazi mbili. Ngazi ya kwanza ni kuwa tunahitaji kumtafuta kwanza Mungu katika maisha yetu. Tunahitaji kuwa karibu na Mungu katika maisha yetu kwani tukiwa karibu naye, tukimpata Yeye tumepata yote.  Ngazi ya pili ni nafsi yetu. Kama Mtume Paulo ametuonesha kuwa sisi ni hazina na sisi ni lulu machoni pa Mungu na kwamba Mungu hufanya yote ili kutupata, basi kitu tunachopaswa kukitafuta kwanza ni nafsi yetu. Yesu mwenyewe alisema “itamfaa nini mtu akiupata ulimwengu wote akaipoteza nafsi yake?” ili kuipata nafsi yetu, ili kutokuipoteza nafsi yetu tunaalikwa kuwa tayari kuuza vyote na si kufanya kinyume chake, yaani kuuza nafsi yetu ili tupate vyote. Nafsi yetu ni ya thamani, imeumbwa kwa thamani na imekombolewa kwa thamani. Kutoka katika jibu hili lililo katika ngazi mbili tunaweza kuendelea kushuka na kuona katika mazingira ya kawaida na mazingira tofauti tofauti ya kila siku ni kitu gani tuendelee kukitafuta na kukiweka mbele ili tu tusimpoteze Mungu na tusizipoteze nafsi zetu?  Hapo tutakuwa kama yule mtu mwenye nyumba ambaye Yesu anamzungumzia katika Injili. Yeye hutoka katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Nakutakia tafakari njema ya dominika ya 17 ya mwaka A kwa Kanisa. 

Liturujia D17
28 July 2023, 15:17