Tafuta

Mwaliko wa Kristo anayesema: “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.” Mwaliko wa Kristo anayesema: “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.”  

Tafakari Dominika ya 14 ya Mwaka A: Nira: Amri Mpya ya Upendo

Katika Uyahudi, Torati ya Musa pamoja na sheria zote zilizoambatana nazo zilifahamika pia kwa jina la “Nira”, tafsiri rahisi ya Nira ni lile jembe la ng’ombe la kulimia. Yesu anaposema “jitieni nira yangu mjifunze kutoka kwangu” anawaalika wafuasi wake kuupokea upendo kama sheria mpya inayoongoza namna ya kuishi. Anaalika kujifunza kutoka kwake kwa maana yeye ameuishi upendo hadi upeo wake wa mwisho pale Msalabani. Ni Dominika ya Utume wa Bahari!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika ya 14 ya mwaka A wa Kanisa inatupatia mwaliko wa Kristo anayesema “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.” Anaelemewa na mzigo mtu anayebeba mzigo unaozidi uwezo wake wa kustahimili. Lakini pia anaelemewa yule asiyejua kwa nini lazima abebe mzigo huo. Anaposema Yesu “nami nitawapumzisha” anasema yote anayotamani kusikia yule aliyechoka, yule asiyeona msaada katika kuubeba mzigo wake na yule asiyejua sababu na manufaa ya kuubeba mzigo anaoubeba. Leo pia Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kumshukuru Mungu kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini sadaka ya watu hawa ambao wakati mwingine: haki, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali za maisha.

Hii ni Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2023
Hii ni Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2023

UFAFANUZI WA MASOMO: Kama kawaida ya kipindi hiki, tunaianza tafakari kwa kuyapitia kwa ufupi masomo yote matatu ili kuona ni kitu gani yanachozungumzia. Somo la kwanza, lenyewe linatoka katika kitabu cha Nabii Zakaria (Zak 9:9-10). Tunasikia maneno ambayo kwa kawaida huwa yananukuliwa na Injili ya dominika ya Matawi. Ni kuhusu ujio wa mfalme; mfalme mwenye haki na mshindi lakini anayepanda punda na mwanapunda. Ni mfalme asiye na maelekeo ya vita: silaha za kivita yeye anazivunja, hapandi farasi mnyama wa vita na habari anayoitangaza yeye ni moja tu – Amani. Picha hii ilikuwa ni picha tofauti kabisa na wafalme ambao Israeli ilikuwa inawaona katika kipindi cha unabii wa Zakaria lakini ndiyo ilikuwa ni picha ya mfalme Israeli aliyemtamani. Mfalme huyo waliyemtamani ndiye waliyemwita masiya. Kumbe, somo hili ni unabii wa kimasiya. Ndiyo maana mwinjili Mathayo anaposimulia tukio la Yesu kuingia Yerusalem kwa shangwe, injili tunayoisoma siku ya dominika ya Matawi, ananukuu unabii huu wa Zakaria kuonesha kuwa yule mfalme ambaye taifa lilikuwa linamsubiri ndiye huyu Yesu mwana wa Daudi. Somo la pili linatoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 8:9, 11-13). Tunasikia kitu ambacho kwa haraka haraka hatuoni uhusiano wa karibu na somo la kwanza. Mtume Paulo anazungumzia utawala wa mwili na utawala wa roho. Anawaasa wafuasi wa Kristo wasitawaliwe na matendo ya mwili bali watawaliwe na matendo ya roho kwa sababu kwa ubatizo wamemvaa Kristo na wamempokea Roho wa Kristo. Anasema matendo ya mwili yana hali ya kufa kwa sababu mwili hufa. Matendo ya roho, yenyewe hayafi kwa sababu Roho wa Kristo anao uwezo wa kuyafanya hai yale yanayoweza kufa.

Mwaliko wa kuboresha maisha ya kiroho
Mwaliko wa kuboresha maisha ya kiroho

Somo hili linatuambia nini sisi siku ya leo? Ni somo linalotupa ujumbe juu ya umuhimu wa maisha ya kiroho. Maisha ya kimwili, au yale tuliyozoea kuita maisha ya kawaida, maisha ya kila siku, ni maisha yanayopaswa kujengwa juu ya msingi wa maisha ya kiroho. Asiye na maisha ya kiroho ana hatari ya kuyaishi maisha yake ya kawaida kijuu juu sana pamoja na hatari ya kuyumbishwa na vionjo mbalimbali maishani. Maisha ya kiroho si tu msaada unaomfanya mtu aishi kama mtoto wa Mungu bali pia humuwezesha mtu kuyasimika maisha yake katika msingi imara. Kuupokea ujumbe wa somo hili ni kutambua vitu mbalimbali vinavyosaidia kukuza na kuimarisha maisha ya kiroho: kuuishi uwepo wa Mungu katika sala, Misa Takatifu na maisha ya sakramenti pamoja na kushiriki yale yanayoitwa mazoezi ya kiroho: mafungo, hija, uchaji mbalimbali katika vyama vya kitume n.k. Tukiingia sasa katika somo la Injili (Mt 11:25-30) tunaupokea mwaliko wa Yesu anayesema “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.” Wachambuzi wa Maandiko Matakatifu wanafafanua kifungu hiki cha Injili wakionesha namna ambavyo Yesu anaweka amri yake ya mapendo sambamba na Torati ya Musa.

Kristo Yesu ni mpole na mnyenyekevu wa moyo
Kristo Yesu ni mpole na mnyenyekevu wa moyo

Katika Uyahudi, Torati ya Musa pamoja na sheria zote zilizoambatana nazo zilifahamika pia kwa jina la “Nira”, tafsiri rahisi ya Nira ni lile jembe la ng’ombe la kulimia. Yesu anaposema “jitieni nira yangu mjifunze kutoka kwangu” anawaalika wafuasi wake kuupokea upendo kama sheria mpya inayoongoza namna ya kuishi. Anaalika kujifunza kutoka kwake kwa maana yeye ameuishi upendo hadi upeo wake wa mwisho pale msalabani. Ndiyo maana mahala pengine anasema “hakuna aliye na upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake wa ajili ya rafiki zake.” Anaposema “nira yangu ni rahisi na mzigo wangu ni mwepesi” anautofautisha upendo na Torati ya Musa ambayo ni nzito na ngumu kuitimiza. Upendo anaouhimiza nao ni mzigo, sio kitu rahisi wala cha lele mama, lakini ni mzigo ambao mtu akiubeba hadi mwisho anapata raha na amani katika nafsi yake. Hii ni Injili basi ambayo kwetu leo inatualika kumpokea Yesu kama kitulizo cha mizigo au majukumu tunayobeba katika maisha yetu. Ni hapa ambapo somo la Injili linaunganisha dhamira ya somo la kwanza la ya somo la pili. Kuujenga ufalme wa amani, kutamani haki na ushindi bila kutumia njia za vita nk kunahitaji kuwa na undani wa maisha ya kiroho, na undani huo anayetupatia ni Kristo.

Ujenzi wa Ufalme wa haki, amani na maridhiano
Ujenzi wa Ufalme wa haki, amani na maridhiano

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News,  baada ya kuyachambua masomo ya dominika hii ya 14 ya mwaka A wa Kanisa, ni wakati sasa wa kuona kile tunachoweza kutoka nacho cha kutuongoza katika maisha. Ninaguswa kuusisitizia mwaliko wa Kristo alitupatia katika somo la Injili akisema “njooni kwangu”. Wengi tunapopokea mwaliko wa namna hii tunasuuzika moyo, tunafarijika kusikia Yesu akituita atupe pumziko. Lakini swali tunalobaki nalo linakuwa “ni namna gani niende kwa Yesu”? Yesu anasema “mimi ni mpole na mnyofu wa moyo”, maneno yanayoakisi mojawapo ya misingi ya ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ndiyo maana, katika namna nyingi ambazo mwamini anaweza kumuendea Yesu apate pumziko, ninapenda kugusia leo njia ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu iliyo pia njia ya kujiweka Wakfu kwa Moyo huo. Kiini cha ibada hii ni kule kujikabidhi kwa Yesu kwa njia ya sala ya kujiweka wakfu, akijibidiisha kuupendeza na kuutukuza Moyo Mtakatifu wa Yesu akitumaini kujazwa na neema ya ahadi zake. Ibada hii, ambayo pamoja na mambo mengine, inaalika kuiishi kila ijumaa ya kwanza ya mwezi katika moyo wa ile Ijumaa Kuu ambapo Moyo wa Yesu ulitobolewa ili kutukomboa, imekuwa kwa watu wengi sana chanzo cha wongofu na utakatifu. Ni changamoto hii ambayo ninakuachia ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kama tayari unaiishi ibada hii na umekwisha jiweka wakfu kuzidi kujibidiisha na kujikita ndani yake. Kama bado wakati haujafika ni vizuri kuanza kujielimisha juu ya ibada hii ili pale moyo wako utakapokuwa tayari, kadiri ya mapenzi ya Mungu, uweze kuukabidhi kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kama namna ya kuupokea mwaliko wake. Nakutakia tafakari njema ya dominika hii.

Liturujia D 14
08 July 2023, 14:57