Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 13 ya Mwaka A wa Kanisa: Neno linatualika tuzame katika imani, tujikite katika kumtumikia Mungu na katika ufuasi. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 13 ya Mwaka A wa Kanisa: Neno linatualika tuzame katika imani, tujikite katika kumtumikia Mungu na katika ufuasi.  

Tafakari Neno la Mungu Dominika 13 ya Mwaka A: Imani, Huduma na Masharti ya Ufuasi

Dominika ya 13 ya mwaka A wa Kanisa linaletwa kwetu Neno linalotualika tuzame katika imani, tujikite katika kumtumikia Mungu na katika ufuasi. Injili inayoongoza tafakari ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Mathayo kifungu ambacho ni sehemu ya mafundisho ya kimisionari ya Yesu. Ni mafundisho ya kimisionari kwa sababu ni mausia ambayo Yesu anawapa wafuasi wake kabla hajawatuma waende kutangaza Neno lake wakimtangulia kule ambako alikusudia kwenda!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika ya 13 ya mwaka A wa Kanisa linaleta kwetu Neno linalotualika tuzame katika imani, tujikite katika kumtumikia Mungu na katika ufuasi. Injili inayoongoza tafakari ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Mathayo kifungu ambacho ni sehemu ya mafundisho ya kimisionari ya Yesu. Ni mafundisho ya kimisionari kwa sababu ni mausia ambayo Yesu anawapa wafuasi wake kabla hajawatuma waende kutangaza Neno lake wakimtangulia kule ambako alikusudia kwenda Yeye mwenyewe. Ufafanuzi wa Masomo kwa ufupi: Ufafanuzi wetu wa masomo ya dominika hii unaanza na somo la Injili(Mt 10:37-42). Yesu anasema apendaye baba au mama kuliko mimi hanistahili, apendaye mwana au binti kuliko mimi hanistahili wala yule asiyechukua msalaba wake kunifuata hanistahili. Baba na mama wanawakilisha chimbuko, historia au kule tulikotoka. Tunaweza kusema pia kuwa wanawakilisha asili ya utu wetu. Sasa Yesu anasema mtu anayejishikamanisha na hayo kiasi cha kuona kuwa Yesu hana nafasi katika asili yake, hafai kuwa mfuasi wake. Kama binadamu tuna asili yetu, tuna chimbuko letu lakini kabla ya hayo yote sisi asili na chimbuko letu ni Mungu mwenyewe. Historia yetu haiwezi kukamilika kama haitatambua uwepo wa Mungu. Watoto wanawakilisha matumaini yajayo, wanawakilisha kesho yetu.

Watoto ni tumaini la kesho!
Watoto ni tumaini la kesho!

Sasa Yesu anasema yeye anayejishikamanisha na mambo yajayo; mipango, matumaini n.k kiasi cha kumpa Kristo nafasi ya pili hafasi kuwa mfuasi wake. Tunapaswa kuiandaa kesho yetu na huu ni wajibu wetu wa msingi lakini kuiandaa kesho yetu bila kutambua kuwa kuna kesho ya maisha ambayo Kristo anatualika kuiangalia tutakuwa tunakosa kipengele muhimu sana katika maisha yetu. Msalaba ndio maisha ya sasa na maisha ya kila siku. Ndiyo njia ambayo Yesu aliitumia kuuokoa ulimwengu na ndiyo njia anayomwalika kila mmoja wetu akimpa msalaba wake. Sasa Yesu anasema yule anayetamani kuishi maisha yake ya kila siku kwa kuuepuka na kuukimbia msalaba wa Kristo kwa gharama yoyote ile, hafai kuwa mfuasi wake. Sehemu hii ya kwanza ya mausia ya Yesu kama tunavyoyapokea katika Injili hii, tunaweza kusema kuwa yanawahusu wafuasi wa Yesu  lakini hasa zaidi wale wanaopokea utume mbalimbali katika Kanisa lake. Anayetaka kuwa mtumishi wake, aliyekwisha kuupokea tayari utumishi anapaswa kujibandua kutoka katika kujishikamanisha na yaliyopita, yajayo na yaliyopo hasa wakati ule ambayo hayo yote hayampi Yesu wala hayaupi utume wake nafasi ya kwanza. Katika nafasi ya pili, Yesu anawaahidia tuzo wale wanaompa Yeye nafasi ya kwanza katika maisha. Anasema atakayewapokea wao atakuwa amempokea Yeye mwenyewe. Yeye atakayewapa walau kikombe cha maji ya baridi, atapata thawabu yake. 

Huduma kwa watumishi wa Mungu ni muhimu.
Huduma kwa watumishi wa Mungu ni muhimu.

Kama uthibitisho wa maneno hayo ya Yesu, somo la kwanza kutoka Kitabu cha pili cha Wafalme (2Fal. 4:8-11, 14-16a) kinatuonesha ukarimu ambao ametendewa Nabii Elisha kwa sababu tu ni mtumishi wa Mungu. Elisha alikuwa akipita mara kwa mara katika mji huo unaotajwa, mji wa Shunemu, akitokea kwake akienda kule ambako Mungu alimtuma kwenda kutolea unabii. Katika moyo wa ukarimu, mama mmoja wa mji huo anamkaribisha awe anapitia kwake ili kumpunguzia mwendo na adha za safari kulingana na mazingira ya wakati huo. Kwa mama huyo tendo hilo linageuka kuwa baraka.  Yeye na mumewe hawakuwa na mtoto, Elisha anamtabiria kupata mtoto na kweli mwaka uliofuata akajaliwa baraka hiyo aliyokuwa anaingoja kwa miaka mingi. Somo la pili linatoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 6:3-4, 8-11). Somo la leo linafafanua maanda ya ndani kabisa ya ubatizo. Tunafahamu kuwa ubatizo ni Sakramenti inayomwondolea mbatizwa dhambi ya asili na kumrudishia utukufu wa kuwa mwana wa Mungu, utukufu ambao ulipotezwa kwa dhambi ya Adamu. Katika somo la leo, mtume Paulo anaongeza kuwa anayebatizwa anazamishwa katika kifo cha Kristo na anainuliwa pamoja naye katika ufufuko wake. Kwa maneno mengine, Paulo anasema kuwa kwa sakramenti ya ubatizo, yule anayebatizwa anaunganishwa na fumbo la Pasaka, fumbo la kifo na ufufuko wa Kristo. Anapozamishwa katika maji au anapomwagiwa maji ya ubatizo anakufa, si katika mwili bali katika dhambi. Ili kama vile ambavyo kifo cha Kristo kiliishinda dhambi basi na yeye kwa nguvu ya ubatizo anatangaziwa ushindi dhidi ya dhambi. Anapozamishwa au anapomwagiwa maji anafufuka. Ili kama Kristo alipofufuka katika mwili, mbatizwa afufuke katika maisha mapya. Katika ubatizo tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo kwa sababu tunahakikishiwa ushindi dhidi ya dhambi na tunazaliwa katika maisha mapya. Na hii ndiyo inayotangaza hadhi mpya tunayoipata kwa njia ya ubatizo.

Kwa Ubatizo mwamini anazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu
Kwa Ubatizo mwamini anazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kupata ufafanuzi wa masomo ya dominika hii ya 13 ya mwaka A wa Kanisa, nawaalika sasa tuone kwa pamoja kile ambacho tunaweza kutoka nacho kama tafakari ya kutuongoza katika dominika hii. Binafsi nimeguswa sana na somo la Injili hasa pale ambapo Yesu anatualika tusijishikamanishe na yaliyopita, yajayo au hata yaliyopo kiasi cha kumuweka yeye kando. Ninachojiuliza ni kuwa maneno haya ya Yesu ambayo inabidi kuyapokea katika uzito wake yanamaana gani katika mazingira na maisha yetu ya leo? Yanatutaka tuishi vipi katika ulimwengu wetu wa leo pamoja na yote yanayotuzunguka? Katika nafasi ya kwanza naona kuwa kuna baadhi ya vitu huwa tunavishikilia kiasi ambacho tunashindwa kupiga hatua kwenda mbele. Na linapokuja sasa suala la imani, wakati mwingine inakuwa ni ngumu hata kulipokea Neno la Mungu. Tunalisoma Neno, tunalisikia likitangazwa kwetu lakini hatuwezi kulipokea kwa sababu tu haliendani na kile ambacho tumekishikilia katika maisha. Hivi vitu vinaweza kuwa ni mfumo wa maisha, picha yenyewe ya namna ya kuishi, viwango vya kipi kinafaa na kipi hakifai n.k. Yesu leo anatuchokoza tukubali kubadilishwa na Neno lake. Neno la Mungu haliji kutuondolea maisha, linatusaidia tuishi maisha kamili, haliji kutuondolea furaha au utulivu maishani, linakupka kutupa amani na furaha ya moyo. Tulipe nafasi katika maisha yetu. Katika nafasi ya pili, hayo mambo aliyoyagusia Yesu katika Injili, yaani yaliyopita, yajayo na yaliyopo kuna wakati yanatufunga tunakuwa kama mateka wa maisha yetu wenyewe. Wapo wanaokosa uhuru na amani leo kwa sababu ya mambo fulani yasiyopendeza waliyoyapitia katika historia zao, wapo watu ambao ni mateka wa maisha ya kesho kiasi kwamba ni kama vile leo hawaioni na hawaiishi na wapo ambao ni mateka wa maisha yaliyopo kana kwamba hakuna kesho na kana kwamba hawana historia. Kristo anataka kutuweka huru kutoka katika utumwa wa namna hiyo ndiyo maana anatuambia tumpe Yeye nafasi ya kwanza na tulipe nafasi ya kwanza Neno lake. Mtakatifu Padre Pio alizoea kuwaasa waamini wake akisema ikabidhi historia yako iliyopita kwa Huruma ya Mungu, yakabidhi maisha yako ya leo katika Neema ya Mungu na ikabidhi kesho ya maisha yako katika Maongozi ya Mungu nawe utaionja amani katika maisha yako. Nakutakia tafakari njema ya dominika ya 13 ya mwaka A wa Kanisa.

Liturujia D13
01 July 2023, 09:27