Tafuta

Warsha la Ukatili wa Kijinsia Barani Afrika, Unyanyasaji wa kijinsia majumbani; maazimio na jinsi ya kuendeleza mradi huu. Warsha la Ukatili wa Kijinsia Barani Afrika, Unyanyasaji wa kijinsia majumbani; maazimio na jinsi ya kuendeleza mradi huu. 

Mtandao wa Afrika Dhidi ya Ukatili na Ubaguzi wa Wanawake, Hatua ya Kwanza!

Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Barani Afrika, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania anapembua kwa kifupi yale yaliyojiri wakati wa: Ufunguzi wa Warsha la Ukatili wa Kijinsia Barani Afrika, Unyanyasaji wa kijinsia majumbani; maazimio na jinsi ya kuendeleza mradi huu, ili kutokomeza kabisa ukatili wa kijinsia Barani Afrika.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Dar Es Salaam, Tanzania.

Utangulizi: Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Barani Afrika, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania katika makala hii anapembua kwa kifupi yale yaliyojiri wakati wa: Ufunguzi wa Warsha la Ukatili wa Kijinsia Barani Afrika, Unyanyasaji wa kijinsia majumbani; maazimio na jinsi ya kuendeleza mradi huu, ili kutokomeza kabisa ukatili wa kijinsia Barani Afrika. Wanawake wakatoliki wajenzi stadi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu kwa amani ya Ulimwengu! Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, (WUCWO, UMOFC) na Mradi wa Kikundi cha Uangalizi wa Masuala ya wanawake Duniani (WWO) uliopo chini ya WUCWO wakishirikiana na WAWATA liliwakaribisha wajumbe wawakilishi wa wanawake na wa mashirika ya kitawa kutoka kote Barani Afrika, kushiriki warsha ya siku nne kwa nia ya kujenga mtandao unaolenga kukabiliana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia (GBV). Warsha hiyo ilifanyika jijini Dar Es Salaam, Tanzania kuanzia tarehe 3 hadi 6 Julai 2023. Warsha hii ni mwendelezo wa Warsha iliyofanyika Nairobi, Kenya mnamo mwei Mei 2022, ambapo WUCWO pamoja na wataalam wabobezi wa masuala ya unyanyasaji waliridhia kuanza utafiti ili kukusanya taarifa zitakazoweza kubaini ukubwa wa tattizo la ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia na hivyo kuamua mwelekeo wa kazi ya WWO barani Afrika. Matokeo ya Utafiti huo yalishirikishwa wajumbe wa Warsha mwanzoni mwa warsha ili kuwa na mtazamo wa Pamoja.

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Afrika
Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Afrika

Ufunguzi wa Warsha la Ukatili wa Kijinsia Barani Afrika: Kongamano hilo lilianza kwa adhimisho la Ibada ya Misa ya ufunguzi iliyoongozwa na Padre Dkt. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambaye alisisitiza umuhimu wa wanawake katika kanisa. Alibainisha kwamba hakuna wokovu bila wanawake, kwa kuwa wokovu wa wanadamu ulizaliwa na mwanamke; Aliendelea kusema kwamba Maria Magdalena, mwanamke, alikuwa wa kwanza kushuhudia ufufuo. Alitoa shukrani kwa wanawake kwa kazi nzuri wanayofanya kama wanafunzi na wafuasi wa Kristo, akieleza kwamba wanawake ni chombo cha mabadiliko ya kweli ulimwenguni. Kwa upande wake Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam akiongoza Ibada ya Misa takatifu siku ya pili ya warsha alisema kwamba mabadiliko ya nyakati hayapaswi kuwa sababu ya kupuuza maadili ya msingi ambayo yanatufanya sisi kuwa Wakristo. Alionya dhidi ya nyakati zilizo katika hatari ya kupoteza wokovu na akabainisha kuwa wanawake, yaani mama, ndio ufunguo wa utunzaji wa maadili hayo. Askofu Mkuu aliwakumbusha washiriki kwamba hawako peke yao, Mama Bikira Maria anatuombea, na Yesu ni kimbilio letu. Kwa Upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Warsha hii lilifunguliwa na Dkt Dorothy Gwajima Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Mhe. Dkt Dorothy Gwajima aliwakaribisha wajumbe wote Tanzania na kuwahimiza kufurahia yote ambayo Dar es Salaam inatoa. Alieleza kuguswa kwake na kazi inayofanywa na WAWATA katika kuwakutanisha wanawake ili kukabiliana na masuala yanayowakumba wanawake nchini Tanzania. Aliendelea kutabainisha ukweli kwamba ni jukumu la serikali ya Tanzania kuendelea kutafuta ufumbuzi wa masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na kuwakaribisha WUCWO na wajumbe wote kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kufanikisha malengo ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kuwa uhalisia.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi akiwa na baadhi ya wajumbe
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi akiwa na baadhi ya wajumbe

Unyanyasaji wa Kijinsia majumbani: Jopo la wabobezi kutoka kwa wanawake wanaofanya kazi na waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia Pamoja na wasomi walizungumza mambo mbalimbali yanayohusiana na sababu na suluhisho la unyanyasaji wa majumbani. Hisia zinazoungwa mkono na wao wote zinaonyesha kuwepo kwa tatizo la unyanyasaji wa majumbani katika jamii nyingi, hata kwa muktadha tofauti. Walizungumzia uwepo wa matabaka katika jamii zetu ambayo mara nyingi husababisha wanawake kuwa waathirika wakuu wa unyanyasaji wa nyumbani na kwamba, mara nyingi kuwa mikononi mwa wenzi wao. Utafiti unaonesha kuwa sababu kubwa za unyanyasaji majumbani ni pamoja na imani za kidini na kitamaduni, upatikanaji duni wa elimu kwa watoto wa kike na ndoa katika umri mdogo. Manyanyaso ya kiuchumi: Mazingira ya kitamaduni, kielimu, na kidini ya wanawake wengi Barani Afrika yanaoneshwa, miongoni mwa mambo mengine, kama sababu kuu za unyanyasaji wa kiuchumi dhidi ya wanawake. Wasichana wanafundishwa kuwa waangalizi wa nyumba, kutokuwa na fursa ya kupata mirathi kutoka kwa wazazi wao na kutopewa fursa ya kupata elimu rasmi imetengeneza mazingira ambayo yanawafanya kuwa katika mazingira magumu wenza wao ambao wanasimamia mali za familia na kuleta mkate. Hii ilichambuliwa kama kisababishi cha wanawake kunyanyasika kiuchumi kuanzia kunyimwa mahitaji ya msingi ili kuhakikisha utegemezi kwa wenzi wao. Hata hivyo, hii ni aina ya unyanyasaji haitolewi taarifa. Ripoti ya utafiti unaoendelea: Washiriki walipata fursa ya kutazama filamu fupi ya wasioonekana (invisibles) waliojitolea kuelezea hadithi za kuathirika kwao na unyanyasaji wa nyumbani. Lengo la uchunguzi/utafiti lilikuwa kuonyesha kazi ambayo tayari imefanywa katika kukusanya simulizi/taarifa za wanawake na kuboresha dodoso lililotumika kukusanya taarifa. Baada ya filamu hiyo timu hiyo ilipitia kwa mara ya pili mwongozo uliopo na dodoso la kukusanya taarifa na kufanya marekebisho ambayo yatafanya mwongozo huo kuwa na ufanisi zaidi kwa mtazamo wa kiafrika.

Wawata Jimbo kuu la Dar es Salaam
Wawata Jimbo kuu la Dar es Salaam

Ukosefu wa elimu kwa mtoto wa kike: Wabobezi walijadili namna ya kukabiliana na suala la ukosefu wa elimu kwa mtoto wa kike, na kuzungumzia thamani ya kuwaelimisha wasichana huku wakiwasilisha mipango mbalimbali ya wanawake wakatoliki, walei na mashirika ya kitawa kukuza uundaji wa upatikanaji wa elimu. Jambo hili lilitiliwa mkazo na jopo ambalo lilitoa takwimu za kazi zinazofanywa na baadhi ya mashirika yaliyowakilishwa katika warsha hii, pamoja na simulizi ya ufanisi ulipatikana. Takwimu hizi ziliarifu majadiliano ya kikundi ambayo yalilenga kubuni njia za kuboresha mbinu za kuelimisha na kuwapa ujuzi wanawake vijana katika muktadha tofauti. Msaada wa Kisheria: Mwakilishi wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Hakimu Nabwike Mbaba, alitoa mada kuhusu umuhimu wa kutumia mfumo wa utoaji haki kama utaratibu wa kuwalinda wanawake. Alibainisha baadhi ya mipango inayotumiwa na TAWJA kujenga uelewa juu ya huduma za kisheria zilizopo pamoja na upatikanaji wa mahakimu wanawake zaidi ya 400 na majaji ambao ni sehemu ya mtandao. Aidha, ametaja haja ya kufanya sera ziendane na sheria, kwani kuna pengo katika utekelezaji wa sheria ambazo hatimaye zitafanya maisha ya wanawake kuwa bora. Alihimiza ushirikiano kati ya kanisa na vyombo vya kisheria ili kuweza kufikia lengo ya WWO kwa ufanisi na kwa haraka zaidi.    Maazimio: Warsha ilimalizika kwa kuweka maazimio na namna ya kuendelea na mradi. Tunamshukuru Mungu kwa mwitikio wa washriki wote kuweka kuendelea na mradi huu, kukuza kazi ya WWO kupitia kushawishi mabalozi wapya na kuendelea kusikiliza kilio cha moyoni cha huyu mwanamke wa kiafrika aliesukumizwa pembezoni. Washiriki wote waliahidi kuendelea kufuata nyayo za mtangulizi wetu Mama Bikira Maria wa kupiga vita unyanyasaji na ubaguzi katika bara la Afrika na sehemu nyingine ya ulimwengu na kwa hivyo kuweka ahadi ya kuendelea kuitikia wito wa kuwatumikia wengine kaka Mama Bikira Maria alivyoitikia wito kuwa Mama wa mkombozi, na daima majibu yetu yatakuwa ya Ndio: ‘FIAT.’  

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi akitoa mahubiri
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi akitoa mahubiri

Jinsi ya kusonga mbele: Kuundwa kwa vikundi 7 vya kikanda ili kurahisisha kazi ya WWO. Vikundi hivi vitakutana mara kwa mara ili kushirikishana uzoefu na pia utekelezaji wa malengo waliyojiwekea. Vikundi vyote vya kikanda vimejitolea kuendelea kushawishi kupata mabalozi wapya kujiunga na mtandao wa kampeni mathubuti ya kupambana na kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia. Tunategemea kupata mabalozi Zaidi ya 500 katika kipindi cha Julai na Oktoba 2023.    Kuwashirikisha mashirika ya maendeleo ya jamii, watekelezaji wa sheria, mashirika ya dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, wizara za serikali, wabunge, na mahakama kusaidia kazi ya mtandao huu wa WWO na kuhakikisha mafanikio katika malengo ambayo mtandao unatafuta kufikia katika nchi husika na Bara la Afrika kwa ujumla.  WWO kuendelea na kutoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike. Kuhamasisha maafisa wa serikali wenye ushawishi kuunga mkono juhudi za WWO katika utekelezaji wa sheria ambazo zinalenga kuwasaidia waathirika, kuwezesha utoaji wa elimu ya ufundi itakayowawezesha kufanya shughuli za ujasiriamali kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.     Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC) Padri Florence Rutaihwa aliushukuru ujumbe huo kwa kuuchagua kufanyia kongamano hili hapa jijini Dar es Salaam. Alisema kwamba kazi inayofanywa ni kazi nzuri na kwamba tunapaswa kuendelea kujitahidi kurekebisha mapungufu yote ya ukosefu wa usawa ikiwa tunataka kufanikisha lengo la ukristo wetu tulioitiwa kwani Kristo alikuja kueleta usawa na kuondoa matabaka. Napenda sasa niwatakie nyote safari njema ya kurudi nyumbani. Mizigo yenu iliyojaa upendo iwe furaha kwa ndugu zenu na marafii zenu watakaowapokea mkirudi nyumbani. Ni matumaini yetu tutapata nafasi ya kuwakaribisha tena hapa Tanzania, nchi iliyojaa maziwa na asali ikiwa pia ni kisiwa cha amani. Tunawakaribisha kwa moyo wote.  Tunasema kwa lugha yetu Kiswahili: Karibu sana! Mama Evaline Malisa Ntenga – Makamu wa Rais Kanda ya Afrika ya WUCWO na mwenyeji wa warsha hii kwa mwaka 2023.

Wanawake Wakatoliki Afrika
12 July 2023, 15:57