Tafuta

Limefanyika Kongamano la Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Kitaifa katika Jimbo Katoliki Kondoa, Tanzania kuanzia Juni 22-26 mwaka huu 2023 Limefanyika Kongamano la Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Kitaifa katika Jimbo Katoliki Kondoa, Tanzania kuanzia Juni 22-26 mwaka huu 2023 

Kongamano la Utoto Mtakatifu Kitaifa Kondoa Lapanda Mbegu ya Umisionari!

Kongamano la Tano la Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Kitaifa limeadhimishwa Jimboni Kondoa kuanzia tarehe 22-26 Juni 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ushirika na utunzaji wa mazingira" na kuwahusisha watoto wa Shirika la Utoto Mtakatifu kutoka majimbo yote 34 ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania ambapo idadi ya washiriki ilikuwa 5,562; Watoto walikuwa 4,707 walezi 792, Wakurugenzi wa PMS 34 na wasaidizi wao 29 ambao ni mapadri, watawa na walei.

Na Sarah Pelaji, - Kondoa, Tanzania.

Limefanyika Kongamano la Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Kitaifa katika Jimbo Katoliki Kondoa kuanzia Juni 22-26 mwaka huu 2023. Kongamano hilo limehusisha watoto wa Shirika la Utoto Mtakatifu kutoka majimbo yote 34 ya Kanisa Katoliki nchini ambapo idadi ya washiriki ilikuwa 5,562 ambapo Watoto walikuwa 4,707 walezi 792, wakurugenzi wa PMS ngazi ya jimbo 34 na wasaidizi wao 29 ambao ni mapadri, watawa na waamini walei. Kongamano hilo limeongozwa na kauli mbiu ‘Ushirika na utunzaji wa mazingira.’ Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa PMS Taifa Padri Jovitus Mwijage amesema kuwa, kongamano hilo limekuwa la kihistoria kwani limewakilishwa na watoto kutoka majimbo yote 34 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Kongamano hilo la Kitaifa lilifunguliwa kwa adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Rais wa PMS nchini Askofu Mkuu Damian Dallu huku homilia ikitolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa Mhashamu Bernardin Mfumbusa. Askofu Mfumbusa aliitambulisha kaulimbiu ya Kongamano hilo ambayo ilikuwa’ Ushirika na Utunzaji wa Mazingira’ huku akiwakaribisha Watoto wamisionari na mahujaji Jimboni Kondoa. Mwishoni mwa Maadhimisho hayo Jimbo Kuu Katoliki Tabora lilikabidhi Msalaba wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu kwa Jimbo Katoliki Kondoa. Msalaba huo utakaa Jimboni Kondoa hadi maadhimisho ya Kongamano lijalo la Kitaifa ambapo Jimbo la Kondoa litakabidhi kwa Jimbo litakalochaguliwa kuwa mwenyeji wa kongamano la sita lijalo. Baada ya Misa Takatifu ya Ufunguzi, mada mbalimbali ziliwasilishwa kama vile ‘Ushirika’ iliyowasilishwa na Padri Edward Ijengo kutoka Jimbo Katoliki Kondoa, ‘Utunzaji wa Mazingira’ iliyowasilishwa na Ndugu John Sulle-OFM Cap. Siku ya pili ya Kongamano hilo ilianza kwa Ibada ya Misa Takatifu kisha uwasilishwaji wa mada mbalimbali ikiwemo mada ya ‘Katekesi ya Sakramenti za Upatanisho na Ekaristi’ iliyotolewa na Padri Zefrine Msafiri. ‘Ulinzi na Wajibu wa Mtoto kwa Wazazi’   iliyowasilishwa Padri Paulinus Mligo kutoka Idara ya Ulinzi wa Mtoto TEC na ‘Malezi ya Mtoto’ iliyowasilishwa na Bw na Bi Paschal Maziku. Pia ilifanyika Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu na watoto wakashiriki pia katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho. Zaidi ya hayo, maazimio mbalimbali yaliyotokana na kaulimbiu hiyo yalitolewa na watoto wenyewe, kama vile kuhakikisha kwamba wanalipa kipaumbele suala la utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Msalaba wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu uko Kondoa
Msalaba wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu uko Kondoa

Matembezi ya kilometa tano yalivyoweka historia Kondoa: Misa Takatifu ya kilele cha Kongamano hilo la Kihistoria ilitanguliwa na hija ya kimisionari ambapo watoto na washiriki wote wakiwemo Maaskofu walifanya matembezi ya hija ya mwendo wa kilomita tano katika mji wa Kondoa, maandamano ambayo yalistajabisha watu wa Kondoa kwa wingi wa watoto waliovalia sare zenye rangi nyeupe na njano huku wakishika mabango ya kongamano yaliyowasilishwa kijimbo. Maandamano hayo yaliyokuwa na watu takribani elfu tano yaliongozwa na bendi ya Watoto wa Utoto Mtakatifu kutoka Jimbo Katoliki la Zanzibar waliokuwa wanaongozwa na maaskari kutoka Zanzibar waliowafanyia mafunzo. Watoto hao wakiwa na maaskofu, mapadri, watawa na walezi walionesha nyuso za furaha huku wakiimba na kucheza kwa uchangamfu. Vigelegele, ngoma na makofi vilisikika katika mji wa Kondoa na kusababisha wenyeji wa mji huo kusimama pembeni mwa barabara na kustaajabu huku watoto wao wakivutiwa na kuwafuata watoto mahujaji hadi Kanisani. Hakika maandamano hayo ya hija yaliacha alama na kusia mbegu ya umisionari Jimboni Kondoa. Baada ya maandamano ndipo iliadhimishwa Misa Takatifu ya kufunga iliyoongozwa na Rais wa PMS Taifa Askofu Mkuu Damian Dallu huku Rais wa TEC Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga akitoa Homilia. Mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu, Majimbo yote 34 yalipewa cheti cha ushiriki katika Kongamano hilo la tano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu.

Ibada ya Misa Takatifu ilichangamka sana kwa ushiriki wa watoto
Ibada ya Misa Takatifu ilichangamka sana kwa ushiriki wa watoto

Shuhuda za Watoto: Mtoto Elizabeth Malwa alieleza kuwa Kongamano hilo limempa hamasa ya kukuza imani yake baada ya kupata mafundisho mbalimbali hasa kujua haki za Watoto. “Wapo Watoto wenzetu wanayimwa ruhusa ya kushiriki kwenye mafundisho ya utoto mtakatifu huko majimboni hasa parokia za vijijini huko Dodoma. Wengi wananyimwa kushiriki makongamano haya kwani wazazi wao wanasema wanapaswa kubaki nyumbani wafanye kazi. Kuhudhuria kongamano ni uvivu. Tunawaasa wazazi wawapatie watoto haki ya kushiri masuala mbalimbali ya kiimani pamoja na watoto wenzao ili kupata uzoefu kutoka kwa wengine. Pia wasitumikishe sana watoto na kazi ambazo hazilingani na umri wao,” amesema. Mtoto Neema John kutoka Jimbo Katoliki Ifakara alisema amestaajabishwa kukutana na Watoto wenzake na kupata marafiki wapya kutoka majimbo mbalimbali. Ameiomba jamii kuwapenda watoto kwa kuwalea, kuwasikiliza, kuwaheshimu na kuwapatia mahitaji yao msingi. Mtoto Edward Yohana amesema amefurahishwa kuona Maaskofu wengi wakiambatana nao katika kongamano pamoja na mafundisho mbalimbali. Amependa jinsi Watoto walivyoachiwa majukumu ya kuimba na kuongoza liturujia ya nyimbo wenyewe ili waweze kukuwa wakitambua wajibu wao katika Kanisa. Wakati wa sherehe watoto walikuwa na wakati wa burudani ikiwa ni pamoja na; michezo ya kuigiza, nyimbo, kushirikishana mambo mbalimbali, kusikiliza na kucheza muziki wa Kanisa na wa kiulimwengu, kukutana na marafiki wengine kutoka majimbo mbalimbali nk. Walezi wamepongeza Kongamano hilo wakisema limekuwa la kustaajabisha kwani watoto walikuwa wengi. “Kazi iliyofanyika ni kubwa kwani kuratibu Watoto wote hawa si kazi ndogo lakini kila kitu kimeenda sawa, changamoto ni ndogo za kawaida. Tunaomba Kongamano lijalo ikiwezekana kila Askofu wa Jimbo ashiriki ili Watoto wao wasijione wapweke hasa kwenye utambulisho,” amesema Mr Elias Mbuya. Katibu wa Utoto Mtakatifu Kitaifa Sr. AnnaGladnes Mruma amemshukuru Mungu kwa kufanikisha Kongamano hilo kwani watoto waliweza kusafiri salama katika safari zao za kwenda na kurudi majimboni. Isitoshe, ilikuwa ni furaha kubwa kwao kwani kwa kipindi chote cha kongamano hilo, watoto walifurahi sana. Watoto walijaliwa afya njema na wale watoto wachache waliopata shida ya afya walipewa huduma ya kwanza na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Viongozi wa Utoto Mtakatifu wameshiriki kwa karibu sana.
Viongozi wa Utoto Mtakatifu wameshiriki kwa karibu sana.

Askofu Mfumbusa: maisha ya sasa na kesho yanategemea tunavyolinda mazingira leo: Askofu Bernardini Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa ambaye ndiye mwenyeji wa Kongamano hilo amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuchagua jimbo lake kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la kitaifa. Ameeleza kuwa, Jimbo la Kondoa ni moja kati ya majimbo mapya ya Kanisa Katoliki nchini ambapo hadi sasa lina miaka 11 tangu lianzishwe. Hivyo alivyopata taarifa ya kuchaguliwa kupokea Kongamano hilo alipata wasiwasi lakini kongamano hilo limefanikiwa kwa msaada wa Mungu. “Jimbo letu linaundwa na Wilaya mbili ya Chemba na ya Kondoa likiwa na makabila zaidi ya kumi na kwa niaba yao ninawakaribisha watoto na walezi wao kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki. Tujisikie nyumbani na kuishi kwa umoja, upendo na amani ambazo ni tunu zetu kama Taifa la Tanzania ambazo tuliachiwa na waasisi wa nchi yetu,” amesema. Amewashukuru wazazi wote waliotoa watoto wao kushiriki kongamano hilo na kuwaamini watu wa Kondoa kwamba wanaweza kuwatunza watoto wao kwa siku hizo chache za kongamano. Ameelezea ujumbe wa Kongamano hilo kitaifa wa “ushiriki na mazingira” akisema kuwa mada ya mazingira ni nzito inayozungumzwa na ulimwengu kwa sasa ambapo mwaka 2022 Kanisa Katoliki liliendesha mkutano wa AMECEA ambao ulijadili kwa kina namna ya utunzaji bora wa wa mazigira nyumba ya wote. “Nasi katika kongamano tutafakari kwa kina namna ya kuyaheshimu na kuyatunza mazingira ikiwemo ardhi. Shughuli za wanadamu ndizo zinasababisha uharibifu wa mazingira ukiwemo ukataji miti hovyo. Ndiyo maana Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” unabainisha kwamba, mazingira ni nyumba ya wote na binadamu asipoitunza anaiharibu kwa mikono yake mwenyewe. Kwa hivyo kupitia kongamano hili ninawaalika watoto kutafakari kwa makini mada ya mwaka huu ya ushiriki na mazingira mkitambua kuwa maisha yenu ya sasa na yale ya kesho yatategemea sana tunavyolinda mazingira leo. Mmekuja hapa kusali na kujiombea wenyewe, kuliombea taifa letu ili tuweze kuwa watu wa kujali na kutunza mazingira nyumba ya wote. Mmekuja kulinda umoja wetu kama taifa na tukitoka hapa kila mtu awe mmisionari na kuelimisha wengine kuhusu utunzaji bora wa mazingira,” amesisitiza.

Braza la Maaskofu Katoliki Tanzania liliwakilishwa barabara
Braza la Maaskofu Katoliki Tanzania liliwakilishwa barabara

RAIS WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA: Tuwe mashuhuda wa Imani katika matendo: Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, amewapongeza watoto walioshiriki kongamano hilo huku akisema amestaajabishwa na ukomavu wa imani ya watoto hao kwani hata baada ya maandamano ya kilometa tano walirudi kwenye Misa Takatifu wakiwa na uchangamfu uleule. Aidha amewasisitiza kujali utu wa mwanadamu kwa kupenda kujali wengine zaidi ya vitu. Amesema mara nyingi mwanadamu anashindwa kutoa ushuhuda wa imani yake, elimu na ubinadamu wake kwa sababu ya hofu. Hofu ya kuogopa kutofanikiwa katika maisha hivyo kwa kuondoa aibu inamlazimu afanye mambo kinyume na taratibu za Mungu na jamii. Amesema kuwa, mara nyingi maamuzi mengi yasiyokuwa na busara yanachochewa na hofu. Hofu inamfanya mwanadamu ashindwe kustawisha ushirika, ashindwe kutunza mazingira, ashindwe kuikiri imani yake kwa matendo na kukiuka misingi ya ubinadamu wake. Pia hofu inamfanya mtu asiwe na uthubutu na asiwe mbunifu. Amewataka watoto hao kuondoa hofu na kuwa wajasiri ili wawe na uthubutu wa kuikiri imani yao kwa vitendo. Amewasisitiza wawe wasikivu kwa wazazi na walezi wao, wasikivu kwa Mungu na kwa Kanisa ili wapate busara ya kupata ujasiri wa kulinda utu wao na wengine na kuwa kizazi bora kwa maisha ya sasa na yale yajayo.

Kauli mbiu "Ushirika na Utunzaji wa Mazingira
Kauli mbiu "Ushirika na Utunzaji wa Mazingira

Kongamano hilo la kihistoria lilihudhuriwa na Maaskofu kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania akiwemo Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC Mhashamu Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya,  Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa nchini ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea Mhashamu Damian Dallu, Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa Mhashamu Bernardin Mfumbusa, Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge  Mhashamu Agapit Ndorobo, Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar  Mhashamu Augustino Shao CSSp., Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga  Mhashamu Liberatus Sangu, Askofu wa Jimbo Katoliki Tunduru-Masasi Mhashamu  Filbert Mhasi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Prosper Lyimo, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Stephano Msomba, OSA na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu Mhashamu Anthony Lagweni.

Kongamano Kondoa
01 July 2023, 14:26