Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka na hivyo kuiandikia familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, wito wa kutafuta na kudumisha amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka na hivyo kuiandikia familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, wito wa kutafuta na kudumisha amani.  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini: Ujumbe wa Amani

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka na hivyo kuiandikia familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, wito wa kutafuta na kudumisha amani, baada ya kuangalia muktadha wa hali halisi kwa sasa Sudan ya Kusini; mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu Sudan Kongwe, mwelekeo wa kiekumene wa amani nchini Sudan ya Kusini sanjari na ujenzi wa Kanisa mahalia Sudan ya Kusini. Amani ni jina jipa la maendeleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini “South Sudan Catholic Bishops, SSCBS” hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka na hivyo kuiandikia familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, wito wa kutafuta na kudumisha amani, baada ya kuangalia muktadha wa hali halisi kwa sasa Sudan ya Kusini; mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu Sudan Kongwe, mwelekeo wa kiekumene wa amani nchini Sudan ya Kusini sanjari na ujenzi wa Kanisa mahalia Sudan ya Kusini. Ujumbe huu unanogeshwa na kauli mbiu “Umwangalie sana mkamilifu, umtazame mtu mnyofu maana mwisho wake mtu huyu ni amani.” Zab 37: 37. Maaskofu wanakumbusha kwamba machafuko yalianza kutimua vumbi kwa miaka ya hivi karibuni na kuanza kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wa Mungu Sudan ya Kusini na Sudan Kongwe wakianza kuteseka sana. Hii ikiwa ni watu kupoteza maisha, mali na vitu pamoja na uharibifu mkubwa wa vitu na mali; mambo ambayo yameathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi. Vita hii imesababisha wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu. Haya ni mapambano, kielelezo cha mapambano ya kuwania mali na madaraka. Ni vita kati ya Majenerali wawili Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Sudan (SAF), na Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti, mkuu wa Kikosi cha Dharura (RSF). Majenerali wawili hao walifanya kazi pamoja, na kufanya mapinduzi pamoja sasa vita vyao vya kuwania madaraka vinasaimbaratisha Sudan. Vita hii ya wenyewe kwa wenyewe ni ya waasimu wawili. Jeshi la Sudan Kongwe, Alhamisi, tarehe 11 Aprili 2019 liliipindua Serikali iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Omar Al Bashir na kujitwalia madaraka. Aliyekuwa Rais wa Sudan Kongwe, Omar Al Bashir akazuiliwa nyumbani kwake na kwamba, majadiliano yaliendelea ili kuunda Serikali ya mpito!

Jitihada za diplomasia za kuleta amani na utulivu Sudan ya Kusini
Jitihada za diplomasia za kuleta amani na utulivu Sudan ya Kusini

Maaskofu wanasema, watu wa Mungu wanahitaji demokrasia inayosimikwa kwenye Serikali ya kiraia na kwamba, wanajeshi wanaolumbana kuhusu uchu wa madaraka wanapaswa kuheshimu utashi wa watu wa Mungu nchini Sudan. Kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, uporaji na ubakaji wa wanawake na wasichana. Watu wanakosa mahitaji yao msingi kama chakula na maji safi na salama; watu wanakosa nishati ya umeme kwa ajili ya maendeleo yao. Silaha kubwa kubwa zinatumika kwa ajili ya maangamizi ya watu wa Sudan. Haya ni mambo ambayo kamwe hayawezi kukubaliwa na wapenda amani, kumbe, Maaskofu wanalaani mambo yote haya. Vita ya Sudan inaihusisha pia Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kujizatiti katika majadiliano ili kuleta suluhu ya amani na hivyo kumaliza tofauti zilizopo. Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini wanapenda kuonesha mshikamano wao na viongozi wa Kanisa Sudan Kongwe pamoja na watu wateule wa Mungu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kongwe. Maaskofu wanawapongeza wananchi ambao kwa miaka mingi wamesimama kidete kupinga utawala wa kijeshi nchini Sudan na kwamba, hawa raia wanapaswa kutambulikana na Jumuiya ya Kimataifa, ili waweze kupatiwa msaada wanaohitaji, wanapoendelea kusimama kidete kudai: haki, amani na demokrasia ya utawala wa kiraia. Maaskofu wanapenda kuonesha mshikamano na watu wa Mungu wanaokimbia vita Sudan Kongwe na kwamba, kwa msaada wa Shirika ya Misaa la Kanisa Katoliki Caritas Sudan ya Kusini, wataendelea kuwahudumia wakimbiji, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Maaskofu wanapenda kuchukua fursa hii, kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa mshikamano wa huruma na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Sudan Kongwe pamoja na kuiomba Serikali ya Sudan ya Kusini kuonesha pia moyo wa mshikamano kama ilivyo pia kwa nchi jirani ambazo zimefungua mipaka yake kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Sudan Kongwe.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe Sudan ya Kusini imepelekea majanga
Vita ya wenyewe kwa wenyewe Sudan ya Kusini imepelekea majanga

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba “wasomi” Sudan ya Kusini wanaendelea kuponda maisha kwa gharama za watu wa kawaida, hali ambayo kamwe, haitaleta haki, amani na ustawi wa watu wa Mungu. Madhara makubwa ya vita yanaendelea kusikika kila upande wa Sudan ya Kusini. Ukabila hauna mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini. Jambo la msingi ni kujenga Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Nchi bado inachechemea kutokana na kuyumba kwa uchumi, hali ya usalama wa raia na mali zao bado inatisha sana; kuna ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula na kwamba, amani ya kudumu ndiyo suluhu ya ufumbuzi wa changamoto zote hizi. Maaskofu wanahimiza dhana ya kuongoza kuliko kutawala, daima wakijielekeza katika kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini badala ya kuelemewa na masilahi binafsi. Vita, kinzani na migogoro inayoendelea huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Sudan Kongwe, DRC inaweza kuwa na madhara makubwa kwa Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2017 anasema, amani ni chachu ya maendeleo ya watu na kwamba, kinzani, misigano na utaifa usiokuwa na mashiko ni mambo yaliyokuwa yanatishia amani. Kumbe, vita, migogoro na kinzani mbalimbali zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika: sheria, haki, usawa, upendo; ukweli na uhuru, tunu ambazo zinaonesha umuhimu wa pekee hata katika ulimwengu mamboleo. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia kutotumia nguvu kuwa ndio unaopaswa kuwa ni mtindo wa maisha ya kisiasa ili kujenga na kudumisha amani duniani na anamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie watu kuchota tunu hizi msingi kutoka katika undani wa maisha yao.

Jitahada za kiekumene za kuleta amani nchini Sudan
Jitahada za kiekumene za kuleta amani nchini Sudan

Upendo na amani ziwe ni tunu ambazo zitasaidia kujenga na kudumisha mahusiano ya binafsi, kijamii na kimataifa. Huu ni mwaliko wa kuondokana na utamaduni wa kulipizana kisasi na kwamba, wahanga wanaweza kuwa ni wadau wa mchakato wa kutotumia nguvu kwa ajili ya ujenzi wa amani katika medani mbalimbali za maisha, ili kweli maamuzi, mahusiano, matendo na nguvu zote za kisiasa ziweze kujielekeza huko. “Umwangalie sana mkamilifu, umtazame mtu mnyofu maana mwisho wake mtu huyu ni amani.” Zab 37: 37. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuwa ni wajenzi wa haki, amani na mardhiano. Kanisa limechangia sana katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani Nchini Sudan Kongwe. Mchakato wa amani unasimikwa pia kwenye majadiliano ya kiekumene kwa Kanisa Katoliki kuendelea kushirikiana na kushikamana na Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai. Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini linabainisha kwamba, mwaka 2024, Kanisa Katoliki Sudan ya Kusini litaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake sanjari na maadhimisho ya Kongamano la 40 la Ekaristi Takatifu Kitaifa. Hii ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa wale wote ambao wamechangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika kipindi chote hiki. Wanawakumbuka viongozi wa Kanisa waliong’atuka hivi karibuni kutoka madarakani. Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini linabaianisha kwamba, kipindi cha Serikali ya Umoja wa KItaifa kinafikia ukomo wake Desemba 2024. Sasa ni wakati wa kukamilisha Katiba, ujenzi wa Jeshi la Umoja wa Kitaifa, kujiandaa kwa zoezi la Sensa ya Wat una Makazi ya Mwaka 2024 pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wasiokuwa na makazi maalum wanarejea kwenye makazi yao mapema iwezekanavyo. Yote haya yanahitaji moyo wa toba na wongofu wa ndani na kuendelea kujizatiti kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mung una kuendelea kutangaza Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo! 

Ujumbe Sudan ya Kusini

 

 

13 July 2023, 15:45