Tafuta

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro, hivi karibuni ametoa Daraja ya Ushemasi wa mpito kwa Wamisionari kumi na mmoja wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi, Kanda ya Tanzania. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro, hivi karibuni ametoa Daraja ya Ushemasi wa mpito kwa Wamisionari kumi na mmoja wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi, Kanda ya Tanzania. 

Askofu Msimbe Atoa Daraja ya Ushemasi Kwa Wamisionari 11 wa C.PP.S., Tanzania

Askofu Msimbe amewataka kujivika hekima na busara kwa kutambua kwamba, wao ni wahudumu wa Neno, watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Neno na busara hii inahitajika ili kuwaondolea watu watu wa Mungu hofu, mashaka na manung’uniko; iwasaidie kuratibu maisha na utume wao, kadiri ya mwongozo wa Kanisa. Pili, Mashemasi wawe ni watu wema na wenye busara, huku wakijitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma.

Na Angela Kibwana, - Morogoro

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa isiyoweza kufutika na hufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mashemasi ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo kwa njia ya maisha ya wakfu! Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro, hivi karibuni ametoa Daraja ya Ushemasi wa mpito kwa Majandokasisi kumi na mmoja wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Kola, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Askofu Msimbe ametoa Daraja ya Ushemasi kwa wamisionari 11.
Askofu Msimbe ametoa Daraja ya Ushemasi kwa wamisionari 11.

Katika wosia wake kwa Mashemasi wapya, Askofu Msimbe amewataka kujivika hekima na busara kwa kutambua kwamba, wao ni wahudumu wa Neno la Mungu, watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Neno na busara inahitajika ili kuwaondolea watu wateule wa Mungu hofu, mashaka na manung’uniko; iwasaidie kuratibu maisha na utume wao, kadiri ya mwongozo wa Mama Kanisa. Pili, Mashemasi wanapaswa kuwa ni watu wema na wenye busara, huku wakijitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma na ukarimu, tayari kuwaganga wale waliopondeka na kuvunjika moyo. Injili ya upendo, huduma na ukarimu isimikwe katika kanuni maadili na utu wema. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., amesema licha ya Shirika la Damu Azizi ya Yesu kupata mashemasi 11 kwa wakati mmoja, hitaji bado ni kubwa zaidi kwa Kanisa na kwamba, huduma za kiroho bado ni kubwa mno kwa kuwa mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, ni wajibu kwa wabatizwa wote kuendelea kuhamasisha ukuaji wa miito katika majimbo yote. “Sijasikia katika majimbo yote nchini Tanzania kwamba kuna Jimbo ambalo limetosheka na mapadre, bado majimbo yote yanahitaji mapadre yakiwemo Mashirika mbalimbali ya kitawa na kazi za kitume kwa sababu hitaji la huduma za kiroho ni kubwa, hivyo, tumwombe Bwana wa mavuno aongeze watenda kazi katika shamba lake.” Licha ya neema ya kupata idadi hiyo kubwa ya mashemasi, watambue kwamba Kanisa linawahitaji sana pamoja na Shirika lao kwa ujumla, kwa kuwa utume wa Kanisa na Shirika unapanuka na kuwa na tija kutokana na ongezeko la watenda kazi katika shamba la Bwana.

Mashemasi wakitakiana amani na mapadre
Mashemasi wakitakiana amani na mapadre

Askofu Msimbe amesema kuwa katika Jimbo Katoliki Morogoro bado kuna uhitaji mkubwa wa mapadre katika parokia, kwa kuwa kila parokia kuna padre moja pekee licha ya kuwa na vigango vingi zaidi na wengine wamelazimika kuhudumia parokia mbili kwa kuwa idadi haitoshelezi. Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwashukuru na kuyapongeza mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanayofanya utume jimboni Morogoro. Alisema kuwa baadhi ya waamini wanafikia hatua ya kukasirika na kuwalaumu mapadre hasa wanapokosa huduma za kiroho vigangoni na parokiani, bila kujua changamoto wanazopitia mapadre kwa sababu wanazidiwa na majukumu, hasa kusoma misa vigangoni na jumuiyani kwa kuwa ziko parokia zenye vigango zaidi ya 15 ambavyo vinategemea huduma za mapadre hao hao. Wakati huo huo, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., amewaomba wamisionari hao kuwa na utayari kufanya utume wao popote watakapopangiwa na wakuu wao wa Shirika, wakubali kutumwa hata katika nchi za Ulaya ambapo kuna uhaba mkubwa wa mapadre ambapo wanahitaji msaada wa mapadre kutoka Afrika. “Ninyi ni wamisionari tambueni mnahitajika mjiandae kufanya huduma hizo mahali popote na wakati wowote mnapotumwa katika nchi mbalimbali duniani, nendeni mkafanye kazi kwa nidhamu, uadilifu na uaminifu.

Askofu Msimbe, Mashemasi na Watawa
Askofu Msimbe, Mashemasi na Watawa

Wajihadhari na tamaa ya fedha, vitu na mali, hali ambayo itawafanya wachanganyikiwe na hivyo kupoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha na wito wa kipadre. Kamwe wasikubali kuweka kando mambo ya kiroho na kutanguliza maslahi binafsi yaani: umiliki wa mali na fedha. Wajitahidi kutoa huduma ya maisha ya kiroho kwa usawa, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza kwani hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Watu wa Mungu wanathamini sana huduma halisi kuliko maneno na porojo! Mashemasi wajitahidi kuwafundisha watu kwa mifano ya maisha mema, adili na matakatifu; wawaeleze watu kweli za Kiinjili na kwamba, kwa njia ya Daraja Takatifu ya Ushemasi wao ni wasaidizi kwanza kabisa wa Maaskofu pamoja na Mapadre katika: Huduma ya Altare: Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwagawia watu wa Mungu Mafumbo ya Kanisa kadiri ya taratibu, sheria na kanuni zilizowekwa na Mama Kanisa. Wawe ni waalimu wa Katekesi, watoe Sakramenti za Kanisa na kuongoza Ibada za mazishi na watende yote kwa msaada wa Mungu kwa kutambua kwamba, wameitwa na kutumwa kuwahudumia watu wa Mungu, huku wakifuata mfano wa Kristo Yesu, Mchungaji mwema.

Mashemasi wajenge urafiki na Kristo Yesu ili kuwahudumia maskini na wanyonge.
Mashemasi wajenge urafiki na Kristo Yesu ili kuwahudumia maskini na wanyonge.

Askofu Msimbe amewakumbusha mashemasi hao 11 kutekeleza huduma yao katika hali ya useja ambayo itakuwa ishara ya kichocheo cha upendo wa kichungaji na chemchemi yenye kuzaa matunda mengi hapa duniani ili wawe huru zaidi kumtumikia Mungu na wanadamu. Pamoja na hayo amewaomba mashemasi wasikubali kugeukia mbali na tumaini la Injili wakiambatana na Kristo Yesu kwa moyo usiogawanyika, wasikubali kuwa wasikilizaji pekee, bali wawe wahudumu wa Neno wajidhihirishe kama watu wasio na doa wala lawama mbele za Mungu na wanadamu. Katika kutoa huduma mashemasi watambue kwamba ndio wajibu wao mkubwa na wa kwanza ambao unaaongozwa na unyenyekevu, wanatakiwa pia kuhakikisha vitabu vya kuongozea ibada vinaandaliwa kwa usahihi, wajue vizuri masomo ya misa husika ili wasivuruge watu wafanye kila jambo kwa uhakika. Wajitayarishe pia kutunza matakatifu katika altare wajue ni mahitaji gani yanayotakiwa wakati wa misa, hasa divai na hostia takatifu pamoja na kuvitambua vifaa vyote vinavyohifadhia matakatifu hayo ili kutayarisha kwa usahihi vipaji hasa kujua uwiano wa maji na divai ili Misa iweze kuwa halali.

Kama wamisionari wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili
Kama wamisionari wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili

Kwa upande wake Mheshimiwa sana Padre Emanuel Lupi, C.PP.S., Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni amewaasa mashemasi hao namna ya kuuangalia Msalaba wa Kristo Yesu ili uwe faraja kwao wanapokutana na changamoto na magumu mbalimbali katika utume na kuwaomba wawe waadilifu na waaminifu zaidi, ili waweze kusikia na kusema mengi zaidi kuhusu huduma na Msalaba wa Kristo Yesu ndani ya Kanisa. Kadhalika amewaomba wawe waaminifu katika utumishi wao waweze kusikia na kusema mengi kuhusu Msalaba wa Kristo na pia wawe waaminifu kwa Maisha yao yote kwa kuwa Mungu anahitaji sana uaminifu wao: “Kanisa na Shirika linahitaji sana uaminifu wenu, watu wote wanahitaji uaminifu wenu, tutakuja kuhukumiwa kwa namna ambavyo tunawajibika kwa hii kazi tunayokabidhiwa” alihitimisha wosia wake Padre Emanuel Lupi, C.PP.S., Mkuu wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni.

Wamisionari wazalendo wa C.PP.S ni matunda ya kazi ya kimisionari
Wamisionari wazalendo wa C.PP.S ni matunda ya kazi ya kimisionari

Wakati huo huo, Mheshimiwa Padre Vedasto Ngowi, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania amewaomba mashemasi hao kutekeleza majukumu yao kwa: uadilifu na uaminifu ili kuwawezesha waamini kuuona Uso wa huruma ya Mungu. Amewashukuru wazazi na walezi walioshiriki malezi na makuzi ya mashemasi hao katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasindikiza katika safari ya kutambua miito yao, huku akiwaomba waamini kuwaombea na kuwasindikiza kwa sala ili hatimaye waweze kufikia Daraja Takatifu ya Upadre. Hata hivyo ametumia fursa hii kuwataka mashemasi wote 11 kurudi katika vituo vyao vya kazi walivyokuwepo awali kabla ya kupewa daraja hiyo: Shemasi Abelhard Dimosso ataendelea kufanya utume katika nyumba ya malezi ya mtumishi wa Mungu Yohane Merlin, Miyuji jimbo kuu Katoliki la Dodoma. Shemasi Abibon Rukiza ataendelea kufanya utume katika Parokia ya Mtakatifu Anna Simiyu, Jimbo Katoliki la Mbulu. Shemasi Aidan Mtui atafanya utume katika Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki la Singida. Shemasi Appolonius Byarugaba atafanya utume katika Parokia ya Benaco Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara. Shemasi Bonaventure Maro atafanya utume katika Parokia ya Mtakatifu Yuda Thadeus Gunyoda Jimbo Katoliki Mbulu. Shemasi Ernest Shirima atafanya utume katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II Shanwe Jimbo Katoliki la Mpanda. Shemasi Gregory Ndeshilo atafanya utume Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki la Singida. Naye Shemasi James Makinda atafanya utume Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Mtongani Jimbo kuu la Dar es Salaam. Na Shemasi Joseph Richard Msumeno atafanya utume nyumba ya Malezi ya Pili ya Shirika iliyopo Kinda, Jimbo Katoliki la Morogoro. shemasi Livinus Benedicto atafanya utume katika Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Chibumagwa, Jimbo Katoliki la Singida na shemasi Revocatus Gimbuya atafanya utume katika parokia ya Bikira Maria Malkia wa Damu Azizi ya Yesu, Kisasa Jimbo kuu Katoliki Dodoma.

Mashemasi C.PP.S

 

11 July 2023, 14:43