Tafuta

Kumbe tunaalikwa kuchagua kutenda yaliyo mema na kuacha kutenda yaliyo mabaya ili tuendelee kuishi katika nuru ya utakatifu tuliyoipokea kwa njia ya ubatizo Kumbe tunaalikwa kuchagua kutenda yaliyo mema na kuacha kutenda yaliyo mabaya ili tuendelee kuishi katika nuru ya utakatifu tuliyoipokea kwa njia ya ubatizo  (ANSA)

Tafakari Dominika 13 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukarimu Unalipa!

Masomo yanatupa fundisho la kujifunza kuchagua yale yanayotupa nafasi ya kubaki katika muungano na Mungu wetu mtakatifu ili nasi tuweze kudumu na kubaki katika utakatifu kwanza kabisa katika maisha ya hapa na duniani na baadae katika maisha ya umilele mbinguni na kuyaacha yale yote yanayoweza kututenga na Mungu wetu mtakatifu na hivyo kushindwa kuishi kitakatifu hapa duniani na hivyo kuyakosa maisha ya utakatifu milele yote mbinguni. Ukarimu unalipa!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 13 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yakitumia lugha ya biashara ya kupata faida na hasara yanatupa fundisho la kujifunza kuchagua yale yanayotupa nafasi ya kubaki katika muungano na Mungu wetu mtakatifu ili nasi tuweze kudumu na kubaki katika utakatifu kwanza kabisa katika maisha ya hapa na duniani na baadae katika maisha ya umilele mbinguni na kuyaacha yale yote yanayoweza kututenga na Mungu wetu mtakatifu na hivyo kushindwa kuishi kitakatifu hapa duniani na hivyo kuyakosa maisha ya utakatifu milele yote mbinguni. Kumbe tunaalikwa kuchagua kutenda yaliyo mema na kuacha kutenda yaliyo mabaya ili tuendelee kuishi katika nuru ya utakatifu tuliyoipokea kwa njia ya ubatizo, tulipoondolewa dhambi kwa gharama ya malipo ya damu azizi ya Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa maisha yetu.

Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki
Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki

Somo la kwanza ni la kitabu cha pili cha Wafalme (2Waf 4:8-11, 14-16). Somo hili linatufundisha kuwa tukiwahudumia kwa upendo watumishi wa Mungu tutapata baraka tele katika maisha yetu. Hili linajidhihirisha kwa mwanamke tajiri Mshunemu aliyemhudumia Nabii Elisha kwa kumpa chakula kila alipopita nyumbani kwake. Zaidi sana walitenga chumba cha yeye kupumzika na kulala ikiwa alichelewa kurudi katika kazi zake. Kwa shukrani Elisha anamwagulia kupata mtoto ingawa yeye na mume wake walikuwa wazee. Somo hili ni sehemu tu ya simulizi zima linalopatikana katika kitabu cha pili cha wafalme 4:8-37. Simulizi hili linatueleza kuwa kwa ukarimu wake huyu mwanamke alijaliwa mtoto wa kiume kama zawadi, amabyo ilikuwa ni tamaa na hamu ya moyo wake iliyodumu kwa miaka mingi. Lakini baadae huyo mtoto alikufa kwa ugonjwa wa kiharusi naye Elisha alimfufua na hivyo kurudisha tena furaha ya huyu mama. Zaidi ya hayo, yule mwanamke alimwamini zaidi Mungu kwa sababu ya zawadi hii ya thamani kubwa aliyomjalia kwa huduma aliyoitoa kwa nabii. Kumbe somo hili linatufundish kuwa Mungu atatupa zawadi kubwa zaidi kwa matendo madogo madogo ya ukarimu kwa jirani zetu tunayoyafanya kwa moyo wa upendo. Hivyo tunapaswa kuwa na hamu wakati wote ya kufanya matendo ya huruma kwa ndugu zetu tukiamini kuwa tutalipwa zaidi kwa kufanywa warithi wa uzima wa milele mbinguni ambayo ndiyo zawadi kubwa zaidi.

Wekezeni katika ukarimu kwani inalipa!
Wekezeni katika ukarimu kwani inalipa!

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 6:3-4, 8-11). Katika somo hili Mtume Paulo anatufundisha thamani ya Sakramenti ya ubatizo na matunda yake tunayoyapata tukiipokea kwa moyo wa toba na imani. Ni kwamba ubatizo wetu in ishara au alama inayoashiria kufa kwetu kuhusu dhambi na kufufuka kwetu pamoja na Yesu Kristo. Huku kufa kuhusu dhambi na kufufuka na Kristo ni sawa na kuingia katika ushirika na Kristo, ushirika wa uhakika na mkamilifu wa kufa na kufufuka naye. Ushirika huu tunaouingia kwa njia ya ubatizo kwa jina la Yesu Kristo ni kwa maondoleo ya dhambi na tunamtapokea Roho Mtakatifu (Mdo 2:38). Ushirika huu ni kama vile wa kibiashara ambapo mmoja anasaidiwa kulipa deni asiloweza kulilipa yeye mwenyewe kwa namna yoyote ile. Kumbe tulipoingia ushirika na Yesu tulifutiwa deni la dhambi kwa thamani ya damu yake Yesu. Ndivyo anavyosisitiza mtume Petro katika fundisho hili hili akisema: “Kumbukeni fidia iliyolipwa kuwaweka kwenu huru, siyo fedha wala dhahabu bali kwa damu azizi ya Mwanakondoo asiye na doa ambaye ni Kristo (1Pet 1:18). Kile tulichochangia katika ubatizo wetu ni kukiri dhambi zetu na kufanya toba na hata. Tusingekuwa tumetubu asingetupa roho wake ambaye alitusukuma kutubu. Gharama aliyolipa Yesu kwa ajili yetu ni kutushirikisha uzima wake mwenyewe, uzima wa kiroho. Alitushirikisha Baba yake, kumfanya awe baba yetu pia. Alitushirikisha sisi pia mwili na damu yake katika Ekaristi Takatifu. Alituahidia kwamba siku ya kifo chetu, tutashiriki kwa ukamilifu urithi wake mbinguni (Rum 8:17). Kwa hivi tuishi kadiri ya uzima mpya na tusitende tena dhambi. Ndivyo inavyosisitiza sala ya mwanzo ikisema; “Ee Mungu umependa kutufanya sisi tuwe wana wa nuru kwa neema uliyotufadhilia. Tunakuomba utujalie tusifunikwe na giza la udanganyifu, bali tukae daima peupe katika nuru ya kweli."

Upendo kwa Mungu na jirani viwe ni utambulisho wa wakristo
Upendo kwa Mungu na jirani viwe ni utambulisho wa wakristo

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 10:37-42). Sehemu hii ya Injili inahusu masharti ya huduma kwa wale wanaotaka kumfuata Yesu. Sharti la kwanza ni gumu na la kukatisha tamaa kwa yeyote anayetaka kuingia katika utumishi wa Kristo. Sharti hili ni la kufanya uamuzi mgumu wa kuchagua na kuacha. Kumchagua Yesu na kuwaacha ndugu, wazazi, watoto, mke au mume, jamaa na marafiki au kumuacha Yesu na kuwachagua ndugu, wazazi, watoto, mke au mume, jamaa na marafiki. Ni wazi kuwa maisha yetu/uhai wetu, familia zetu, fedha na mali tulizo nazo kwa namna ya vitu hai na visivyo hai – yote haya yana thamani. Lakini hayo yote ni zawadi za Mungu kwa mwanadamu na tena ni mambo yanayodumu kwa kitambo kidogo tu. Kuna jambo la thamani zaidi kuliko haya - kubaki katika ufalme wa Mungu – kubaki katika muunganiko na Mungu aliye mtakatifu sana. Hakuna kitu chochote hapa duniani kinachoweza kuchukua nafasi yake. Ifahamike kuwa katika sehemu hii ya Injili Yesu hatuambii tutupe vitu tulivyonavyo au kuziacha familia zetu, kuyaacha maisha yetu na kadhalika. Anachotuambia hapa ni kwamba vyote ni vya thamani lakini kuna kitu cha thamani zaidi kuliko vyote nacho ni ufalme wa Mungu na kwamba tunapaswa kuwa tayari kuachilia mambo mengine yote kama yanakuwa kikwazo cha kubaki katika ufalme wa Mungu.

Huduma kwa maskini ni ufunguo wa utakatifu wa maisha.
Huduma kwa maskini ni ufunguo wa utakatifu wa maisha.

Kuna wakati katika maisha yetu tunaweza kuitwa kuchagua kati ya ufalme wa Mungu na zawadi nyingine za Mungu, hatupaswi kusita kuchagua ufalme wa Mungu kwanza na haki yake na kudumu katika muunganiko na Mungu baba yetu. Ndiyo maana sala baada ya Komunyo inatilia mkazo ikisema; “Ee Bwana, tunakuomba kafara hii takatifu tuliyokutolea na kuila itutie uzima wako. Hivyo tuwe tumeungana nawe siku zote kwa mapendo, tupate kuzaa matunda yenye kudumu daima”. Ndiyo maana Yesu anatuasa kuwekeza katika jirani zetu wahitaji kama njia ya uhakika ya kubaki katika muungano na Mungu. Yesu anaweka huduma tunazopaswa kuwatendea wengine katika makundi makuu matatu. Kwanza kabisa kuwapokea na kuwahudumia manabii ili kupata thawabu ya kinabii. Pili kuwapokea na kuwahudumia walio wadogo hata kwa kuwapa tu kikombe cha maji yaani kuwapatia mahitaji ya muhimu na lazima katika maisha ya kila siku wanaohitaji. Na tatu kuwa watu wa haki na kutetea haki za wanyonge. Katika huduma zote hizi hakuna inayooneka ndogo ikitendwa wa moyo wa upendo isiweze kuwa na faida kwa anayetendewa na anayetenda kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Kumbe kikombe kidogo cha maji hakina thamani yeyote kwa mtu mwenye kiu ya siku nzima. Lakini kama kikitolewa kwa ajili ya Bwana kinakuwa kikombe kikubwa cha maji ambacho ni cha thamani kubwa kwa uzima wa milele mbinguni. Kwa vile tumezungukwa na watu wakati wote hakuna wakati ambao hatuwezi kutoa huduma kwa mtu na hivyo kuongeza hazina yetu ya kiroho. Basi tujitahidi kuwa wakarimu kwa ndugu zetu wahitaji na tuyafanye matendo ya huruma kwa moyo upendo kwa ajili ya uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 13 Mwaka A

 

29 June 2023, 08:15