Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Kumi na moja ya Mwaka A wa Kanisa: “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. Mwombeni Bwana wa Mavuno apeleke watendakazi shambani mwake.” Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Kumi na moja ya Mwaka A wa Kanisa: “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. Mwombeni Bwana wa Mavuno apeleke watendakazi shambani mwake.”   (Vatican Media)

Tafakari Dominika XI ya Mwaka A: Mavuno Ni Mengi, Lakini Watenda Kazi ni Wachache!

Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya Kumi na Moja ya Mwaka A wa Kanisa. Katika Injili tunayapokea maneno ya Yesu anayewaambia wanafunzi wake akisema “mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. Mwombeni Bwana wa Mavuno apeleke watendakazi shambani mwake.” Kristo Yesu anaona umati mkubwa na kguswa na mahitaji yao msingi. Sala na maombi yanayotolewa kwa imani na kwa kujiaminisha kwa Mungu yatajibiwa kwa wakati wake, salini!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapitia masomo ya Misa ya dominika ya 11 ya mwaka A wa Kanisa. Katika Injili tunayapokea maneno ya Yesu anayewaambia wanafunzi wake akisema “mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. Mwombeni Bwana wa Mavuno apeleke watendakazi shambani mwake.” Ufafanuzi wa Masomo : Masomo yote matatu ya dominika hii yanaonesha namna ambavyo Mungu anawahaingikia watu wake. Mungu anaguswa na mahitaji ya watu wake, yeye ni Mungu anayewatakia mema na hasa zaidi yeye ni Mungu anayewatafutia mema hayo. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Kutoka (Kut. 19:2-6a) linatupatia msingi wa Mungu kufanya yote hayo. Katika somo hilo tunasikia Mungu anamwambia waisraeli kuwa anataka kufunga nao agano ili wao wawe watu wake kweli na yeye awe Mungu wao. Anataka kuunda kwa njia yao ukoo wa makuhani na taifa teule, taifa takatifu. Tunaweza kujiuliza, sasa kama Mungu amewachagua waisraeli, sisi tunahusika nini? Israeli ni taifa ambalo Mungu alichagua kujifunua kwao kwanza ili kupitia wao aweze kuwafikia watu wote. Na ndivyo alivyofanya. Amewajenga katika imani, akakuza matumaini yao ya kumleta mwokozi na ulipofika utimilifu wa nyakati, Yesu Kristo akazaliwa kati yao. Mtume Paulo katika waraka kwa Warumi (Rum 9:6) anafafanua akisema neema hii ambayo Mungu aliwatangazia Waisraeli, kwa njia ya Kristo imefunuliwa kwa watu wote. Kumbe suala si Israeli kama Israeli bali ni utayari wa watu kuifungua mioyo yao kuipokea neema hiyo. Kwa maana hata ndani ya Waisraeli, sio Waisraeli wote kama kundi watakaookolewa bali ni wale watakaoifungua mioyo yao kuipokea neema ya Mungu katika Kristo. Kumbe hicho ambacho somo hili la kwanza linakitangaza kwa Waisraeli, ni kitu kile kile ambacho Mungu anakitangaza hata leo kwa watu wote. Yeye ni Mungu anayetaka mimi na wewe tuwe watu wake na yeye awe Mungu wetu. Tuishi tumeungana naye.

Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi shambani mwake.
Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi shambani mwake.

Somo la pili kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (5: 6-11) linaendeleza dhamira hiyo ya somo la kwanza. Ni somo linalokuja kutuonesha sasa huyu Mungu anayetaka kuwa karibu na watu, huyu Mungu anayetaka aingie katika maisha ya watu ili awaongoze kuchagua mema na kufikia mema amefanya nini ili kuitimiza azma hiyo? Somo linatuonesha kuwa alichokifanya Mungu ili kuitimiza azma hiyo ni kwamba alimtuma mwanae wa pekee Yesu Kristo ili ampatanishe mwanadamu kwa nguvu ya sadaka aliyoitoa msalabani. Kuna kitu cha pekee sana ambacho mtume Paulo anakigusia katika somo hili. Anasema Kristo ametoa sadaka yake na kufa msalabani wakati ambapo mwanadamu alikuwa dhaifu, wakati ambapo alikuwa ameipoteza thamani yake. Mtume Paulo anazungumza hivyo kuonesha kuwa katika hali ya kawaida, shujaa ni yule anayejitoa kwa ajili ya kuwaokoa watu wasio na hatia, watu wema . Ni nadra sana mtu kuwa shujaa kwa kujitolea kufa kwa ajili ya waovu. Kristo alichokifanya ndio hicho hasa, alijitolea kufa kwa ajili yetu kipindi ambacho tulikuwa waovu. Na sasa kama Kristo alifanya hivyo tulipokuwa dhaifu na mbali na Mungu, sasa ambapo tumepatanishwa na Mungu ataacha kushughulikia mahitaji yetu? Kwa mantiki hii basi, hili ni somo ambalo linakuja kuamsha imani na matumaini yetu kwa Mungu. Linakuja kutuhimiza kujiaminisha kwa Mungu, kuangalia yale aliyotufanyia hapo nyuma kama ni msingi wa kuendelea kumtumainia kwa yajayo.

Kanisa linawahitaji watenda kazi waaminifu na watakatifu
Kanisa linawahitaji watenda kazi waaminifu na watakatifu

Tukiingia sasa katika somo la Injili (Mt 9:36-10:8) tunaweza kugusia mambo mawili ambayo yanaendeleza dhamira ya somo la kwanza na somo la pili. Jambo la kwanza, Yesu anaona umati wa watu waliokuwa wanamfuata na anaona uchovu na mahangaiko yao kama ya kondoo wasio na mchungaji. Hawa hawakuwa watu wasio na wachungaji au viongozi. Tatizo ni kwamba hakuna kiongozi au mchungaji aliyeweza kuona uchovu na mahangaiko ya watu hao. Huenda wao waliwaona kama mzigo, au kama kitega uchumi au kama wapiga kura, au kama eneo la kuonesha umahiri wao n.k. Hakuna aliyeona mahangaiko yao ila Yesu pekee. Hilo ni la kwanza. Jambo la pili ndilo hilo alilowaambia wanafunzi wake: “mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache”. Kundi lina viongozi, kundi lina wachungaji ambao ndio watendakazi, na watendakazi hao ni wachache. Ni wachache katika idadi? Ni wachache katika ubora? Ni wachache katika yote mawili, idadi na ubora? Hilo linahitaji tafakari. Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hapo hapo Yesu anakuwa kwa kwanza kuitikia hitaji hilo kwani anawachagua mitume kumi na wawili kati ya wanafunzi wake. Anawatuma waanze kwa kondoo waliotawanyika wa nyumba ya Israeli. Waponye wagonjwa, wafufue wafu, watakase wakoma na wawinge pepo wachafu. Wamepokea bure, watoe bure. Mungu anaguswa na mahitaji ya watu wake, Mungu anayashughulikia mahitaji ya watu wake.

Yesu akawaonea huruma na kuguswa na mahangaiko yao
Yesu akawaonea huruma na kuguswa na mahangaiko yao

Tafakari fupi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tumeupokea ujumbe wa masomo ya leo kuwa Mungu wetu ni Mungu anayejali na kuguswa na mahitaji yetu. Anaguswa na mahitaji ya kiroho na anaguswa na mahitaji ya kimwili na katika yote hututafutia mema na kutuongoza katika kuyafikia mema. Katika maisha yetu ya kila siku na hasa katika safari yetu ya imani ujumbe huu unatugusa vipi? Kwanza kabisa ujumbe huu unakuja kuthibitisha kwa mara nyingine tena kuwa Mungu wetu hayuko mbali na uhalisia wa maisha yetu kama tunavyodhani wakati mwingine. Anaona jitihada tunazofanya, anaona nia zetu njema, anaona magumu tunayopitia, anaona pia madhaifu na mapungufu yetu. Anazidi kutualika tuujenge ustawi wetu na maisha yetu kwa kujenga ukaribu naye. Jambo la pili ni kwamba ujumbe wa leo unatupatia uhakika kuwa sala zetu na maombi yetu kwa Mungu havipotei. Tukiwa na Mungu aliye karibu nasi kiasi hiki, Mungu anayetaka sote tuwe taifa lake teule na takatifu, basi kila mara tunapoingia ndani ya mioyo yetu na kumuomba kwa imani, tuna uhakika wa kusikilizwa. Tuombe nini kwa Mungu na tusiombe nini kwa Mungu? Kimsingi hatupaswi kuchuja sala za kupeleka kwa Mungu.

Kristo Yesu akaguswa na mahitaji yao ya kiroho na kimwili
Kristo Yesu akaguswa na mahitaji yao ya kiroho na kimwili

Katika sala tunapeleka mahitaji na hisia zetu za ndani, za kiroho na za kimwili na zote hizo tunaziweka mbele yake. Ni yeye katika mapenzi yake atatujibu kadiri ya uradhi wa mapenzi yake. Jambo la tatu na la mwisho, ni kuwa ujumbe wa leo unatualika tuishi tumeungana na Kanisa. Yesu katika kuhakikisha kuwa watu wake wahudumiwa, aliwasimika mitume. Nguvu na wajibu wa mitume hao inaendelea hadi leo ndani ya Kanisa. Ni ndani ya kanisa na kwa njia ya kanisa tunapata uhakika wa kuguswa na neema ya Mungu inayookoa. Kanisa ndiyo ile Sakramenti ya wokovu, yaani alama hai na inayoonekana inayobeba neema hai isiyoonekana. Nje ya Kanisa, alisema Mt. Cypriano, hakuna wokovu. Yeye anayesema anayo imani ya moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu na kwamba halihitaji Kanisa ana hatari ya kuipoteza hata hiyo imani aliyonayo. Mungu mwema na mwenye upendo mkubwa kwetu, atuhifadhi katika upendo wa kimungu siku zote za maisha yetu.

Liturujia Dominika II
16 June 2023, 16:12