Tafuta

Katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Kanisa linasali kwa kuuelekea Moyo huu Mtakatifu wa Yesu ili mapendo yake yakae ndani ya ulimwengu ili uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Kanisa linasali kwa kuuelekea Moyo huu Mtakatifu wa Yesu ili mapendo yake yakae ndani ya ulimwengu ili uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.  (Vatican Media)

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Chemchemi ya Sakramenti za Kanisa

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni siku ya kuwatakatifuza mapadre. Mama Kanisa amechagua sikukuu hii iwe ni kwa ajili ya kuwatakatifuza mapadre waweze kujazwa neema na baraka tele zitokazo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa ajili ya kazi yao ya kichungaji inayodai upendo wa kujitoa bila kujibakiza. Tuwaombee mapadre ili maisha yao yawe ni Ekaristi, mkate unaomegwa katika jumuiya ili kufundisha, kuongoza na kutakatifuza watu wa Mungu katika safari yao.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu mwaka A wa kiliturujia. Sherehe hii huadhimishwa ijumaa ya dominika ya pili baada ya sherehe ya Pentekoste yaani Ijumaa baada ya Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Yesu - Ekaristi Takatifu tunayoisherehekea dominika ya pili baada ya Pentekoste. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya kichungaji inayohusu Kanisa katika ulimwengu “Gaudium et spes” unatualika kuitazama dunia katika mtazamo chanya na kuweka chachu ya Injili kama Kristo alivyoweka chachu ya mapendo kwa njia ya umwilisho wake. Kwa sababu hiyo, katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Kanisa linasali kwa kuuelekea Moyo huu Mtakatifu wa Yesu ili mapendo yake yakae ndani ya ulimwengu ili uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Katika Moyo Mtakatifu wa Yesu yamo mapendo yote ya Mungu anayotupenda sisi wanadamu. Msalabani moyo huu ulifunguliwa alipochomwa ubavu kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji chemichemi ya neema na baraka za kimungu kwa maisha yetu ndiyo maana katika sala ya mwanzo katika Liturujia ya Sherehe hii Padre anasali akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, tunaona fahari juu ya Moyo wa Mwanao mpenzi, na kukumbuka jinsi alivyotupenda kwa mapendo yake makuu. Tunakuomba utujalie kupata neema tele katika chemchemi hiyo ya baraka za mbinguni”. Kumbe tunapoadhimisha sherehe hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunakumbuka mapendo yake kwetu sisi wanadamu aliyotupenda hivi, hata akajitoa afe msalabani ili atukomboe kutoka utumwa wa dhambi na mauti kama unavyoashiria wimbo wa mwanzo ukisema; “Makusudi ya Moyo wake ni ya vizazi na vizazi. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti na kuwahuisha wakati wa njaa” (Zab. 33:11,19).

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchem ya neema, huruma na baraka zote
Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchem ya neema, huruma na baraka zote

Ni siku ya kuwatakatifuza mapadre. Mama Kanisa amechagua sikukuu hii iwe ni kwa ajili ya kuwatakatifuza mapadre waweze kujazwa neema na baraka tele zitokazo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa ajili ya kazi yao ya kichungaji inayodai upendo wa kujitoa bila kujibakiza. Tuwaombee mapadre ili maisha yao yawe ni chachu kwa maisha ya watu wote, yawe ni Ekaristi, mkate unaomegwa katika jumuiya. Tunaweza kusema ni sikukuu pia ya kutakatifuzwa kwa waamini wote, maana mapadre si kwa ajili yao wenyewe bali wameitwa na kuchaguliwa na Mungu kwa mambo yamuhusuyo Mungu na watu wake. Tuwaombee waamini walei wanaushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ulimwenguni kote, ili maisha yao yaakisi upendo halisi wa kimungu kwa ulimwengu. Sherehe hii pia inatualika kujichunguza na kujitafiti kama kweli tumekuwa na moyo wa shukrani kwa mapendo ya Kristo kwetu sisi wanadamu kwa kuyaishi vyema mafundisho yake. Na kama tumekosa shukrani sababu dhambi zetu, basi tuombe msamaha na kufanya malipizi yatupasayo kama sala ya mwanzo inavyosisitiza ikisema; “Ee Mungu, umetujalia kwa rehema zako hazina isiyopimika ya upendo wako katika moyo wake Mwanao uliojeruhiwa kwa dhambi zetu. Tunakuomba utujalie tumtolee heshima ya ibada yetu na malipizi yatupasayo”. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (7:6-11). Somo hili linatueleza ni sababu gani Mwenyezi Mungu alilichagua taifa la Israeli kuwa taifa teule. Kwa kinywa cha Musa Mungu anawaambia waisraeli kuwa aliwapenda si kwa kulazimishwa na mtu awaye yote wala kitu chochote, wala wingi wao, wala uzuri wao, bali kwa upendo na huruma yake ili kutimiza makusudio yaliyokuwa katika moyo wake tangu milele na kujifunua kwake kwa binadamu wote. Musa kwa kutambua hili anawaalika kuishika sheria ya Mungu na hukumu zake kwani ni kamilifu na humpa mtu uhai mpya (Zab. 19:7).

Moyo Mtakatifu wa Yesu Ufalme wake ufike.
Moyo Mtakatifu wa Yesu Ufalme wake ufike.

Upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu umeonekana katika hatua mbalimbali na kufunuliwa katika ukamilifu wake wote na kufikia kilele chake katika nafsi ya Bwana wetu Yesu Kristo, mwanae wa pekee. Agano la kale linatuonesha hatua za mwanzo kabisa za upendo wa Mungu kwa binadamu. Mungu ndiye anayeanza kupenda na upendo wake unaonekana katika kazi yake ya uumumbaji (Mw.1-2). Aidha upendo wa Mungu katika hatua zake za mwanzo umeonyeshwa kwa kule kuunda Taifa la Israeli ambalo alitaka lieneze ufalme wake duniani. Mungu amewaonyesha upendo wake kwa tendo la kuwatoa utumwani Misri na kuwafanya huru tena (Kumb.7:6-8). Zaidi sana Mungu aliwabariki na kuwapa nchi aliyowaahidi kwa sharti la wao kumpenda kwa moyo wote, kwa nguvu zao zote na kwa akili zao zote na kuzishika amri zake (Kumb.6:5;11:1). Kumbe chaguo hili la Mungu, lilikuwa maandalizi tu ya kutuonyesha upendo wake sisi wanadamu usio na mipaka aliotuonyesha kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo huu ni mwaliko pia kwa kila mkristo na awaye yote katika kupokea upendo utokayo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu na kuzishika amri za Mungu. Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Yohane kwa Watu Wote (4:7-16). Somo hili linatueleza asili ya Mungu. Mungu ni upendo. Kwa upendo yake alimtoa mwanae atukomboe kutoka utumwa wa dhambi na mauti ili nasi tushiriki katika mapendo yake. Somo hili linatupa agizo la kupendana sisi kwa sisi na kipimo cha upendo huo ni upendo wa kimungu kwa kuwa “Mungu ni Upendo” (1Yoh 4:8). Kipimo cha upendo wa kimungu anasema Baba Mtakatifu Francisko ni “kupenda bila kipimo”. Maana kupenda kwa kipimo inatuelekeza kupenda kwa faida binafsi yaani upendo wa “nipe nikupe” ulio sumu kwa maisha ya kikristo maana unatufanya tuangalie nyuma na hivyo kutokufaa kwa ufalme wa Mungu kama anavyosema Yesu mwenyewe; “Mtu atiaye mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu” (Lk 9:61-62). Kumbe upendo wa kimungu unatudai kujitoa bila kujibakiza na bila kipimo.

Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya mapendo yote ya Kimungu
Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya mapendo yote ya Kimungu

Ni upendo unaotudai kujitoa wazima wazima kwa ajili ya wengine kama Kristo alivyojitoa kwa ajili yetu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (11:25-30). Sehemu hii ya Injili inasisitiza juu ya fadhila kuu mbili; upole na unyenyekevu. “Jitieni nira yangu mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt 11:29a). Kumbe, ni kwa wale walio wanyenyekevu Mungu anajifunua kwao na kuwawezesha kulitambua pendo lake. Maana utambuzi wa pendo la Mungu hautegemei uwezo wa akili ya mwanadamu, bali unyenyekevu wa moyo, kujiepusha na kiburi na majivuno katika maisha yetu ya kila siku. Ndivyo inavyosisitiza sala baada ya komunyo; “Ee Bwana, tunakuomba sakramenti hii ya mapendo ituwashie upendo wako mtakatifu na kutuvutia siku zote kwa Mwanao, kusudi tuweze kumtambua yeye katika ndugu zetu.” Matunda ya fadhila hizi za upole na unyenyekevu wa moyo ni kile anachokitafuta kila mwandamu wa kila nyakati zote - raha: “Nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Mt 11:29b). Lakini sharti ni moja kuwa kama watoto wachanga. Maana kwa mtoto mdogo tunajifunza unyoofu, msamaha, mahusiano yasiyo na hila, umoja, utayari wa kupokea mapya na kusikiliza maagizo ya wakubwa. Ndivyo anavyosisitiza Yesu; “Kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga” (Mt 11:25). Yesu mwenyewe ambaye kwa asili alikuwa daima Mungu, hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu. Kwa unyeyekeu na hiari yake mwenyewe alijitwalia hali ya ubinadamu, akateswa na kufa kifo cha aibu msalabani ili atukomboe sisi wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti (Fil.2:6-8). Hii yote ni kwa sababu ya upendo wake kwetu sisi hata akautoa uhai wake. Kwa kufa kwake sisi tumekombolewa kama utangulizi katika sherehe hii unavyosisitiza; “Yeye aliinuliwa msalabani, akajitoa mwenyewe kwa ajili ya kutupenda sisi. Alichomwa ubavu akamwaga damu na maji, zipate kutoka humo sakramenti za Kanisa. Nasi sote tuvutwe na huo Moyo wazi wa Mwokozi, na kuchota kwa furaha neema katika chemchemi ya wokovu."

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchem ya neema, huruma na baraka zote
Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchem ya neema, huruma na baraka zote

Kumbe, Mungu alituchagua “ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo sawasawa na uradhi wa mapenzi yake” (Ef 1:5). Yesu “ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote” (Kol 1:15). Katika sala yake ya kikuhani Yesu aliomba kwa Baba kwa ajili ya watu wake aliowapenda upeo mambo makuu manne; uzima wa milele, kinga dhidi ya uovu, wadumu katika ukweli na wawe na umoja (Yn 17). Upendo huu ndiyo unatufanya kupenda kwa kutumikia, kupenda kwa kuhangaikia fanaka ya wengine, kupenda kwa kujali jirani zetu. Hivyo, katika adhimisho la Sherehe hii tulipokee agizo la kimungu la kujitia nira ya Yesu na kujifunza kwake, kwa fadhila za upole na unyenyekevu wa moyo ili tuweze kusaidiana, kusikilizana, kusameheana na kutiana moyo katika maisha yetu ya kila siku. Hii inapaswa kuanzia katika ngazi ya familia kuishi kwa umoja na uelewano. Na familia zikiimarika katika umoja na uelewano zinakuwa ni chachu ya umoja, amani na uelewano kati ya jamii. Kumbe dawa ya ugomvi, kutoelewana na kutokuaminiana ni upole na unyenyekevu wa moyo. Mwishoni mwa Litania ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tunasali kwa kiitikizano kinachosema: “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu! Ufanye mioyo yetu ifanane na moyo wako”. Basi tumwombe Mwenyezi Mungu aifanye mioyo yetu ifanane na Moyo Mtakatifu wa mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Upole na unyenyekevu wa Kristo uwe chachu ya maisha ya umoja badala ya kutengana, maisha ya msamaha badala ya visasi, maisha ya kutakiana mema badala ya mabaya, maisha ya kupendana badala ya chuki na maisha ya utakatifu badala ya dhambi. Tukumbuke daima kuwa fadhila za upole na unyenyekevu ndizo bakuli pekee la kupokelea upendo wa kimungu ndani mwetu unaotuletea furaha katika maisha ya sasa na yajayo. Heri na baraka tele zitokazo katika Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu
15 June 2023, 16:58