Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani ya Kanisa Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani ya Kanisa 

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu Kiini cha Imani ya Kanisa

Mama Kanisa anatufundisha kuwa Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna Nafsi Tatu zisizogawanyika katu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho. Hizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili. Utatu Mtakatifu ni moyo na kiini cha imani yetu ya kikristo. Ishara ya Msalaba ni ufupisho wa Kanuni ya Imani juu ya Mungu Baba Muumbaji, Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayetakatifuza malimwengu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Fummbo la Utatu Mtakatifu. Sherehe hii tunaiadhimisha Jumapili baada ya Sherehe Pentekoste iliyohitimisha kipindi cha Pasaka na tukarudi katika kipindi cha kawaida cha mwaka wa kiliturujia katika juma la nane na sherehe hii ya Utatu Mtakatifu tunaiadhimisha katika jumapili ya 9 la kipindi cha kawaida. Itakumbukwa kuwa tuliishia juma la saba katika kipindi cha kawaida tukaanza kipindi cha kwaresima kwa jumatano ya majivu na baadae Pasaka na baada ya sherehe ya Pentekoste iliyofunga kipindi cha Pasaka tukaanza wiki ya juma la 8 na Jumapili ya 10 kipindi cha kawaida tutaadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Kumbe masomo ya jumapili ya 8, 9 na 10 kipindi cha kawaida mwaka A 2023 hatutayatafakari kwasababu masomo ya sherehe hizi yanachukua nafasi yao. Mama Kanisa anatufundisha kuwa Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna Nafsi Tatu zisizogawanyika katu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho. Hizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili. Utatu Mtakatifu ni moyo na kiini cha imani yetu ya kikristo. Ni fumbo asili la imani na maisha ya Kikristo. Ndiyo maana Misa na sala zote katika Kanisa Katoliki zinaanza na kumalizika kwa maneno haya: “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” ambayo ni namna fupi kabisa ya kumkiri Mungu mmoja katika nafsi tatu. Katika hii sala rahisi hivi, tunakiri kile tunachokiamini kwa kirefu katika Kanuni ya Imani katika sehemu kuu tatu tukisema: “Nasadiki kwa Mungu mmoja Baba Mwenyezi, mwumba wa mbingu na Dunia… Nasadiki kwa Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu…Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima…”

Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani ya Kanisa
Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani ya Kanisa

Tunasadiki haya yote siyo kwa sababu ya utambuzi wa akili zetu bali kwa kuwa Mungu mwenyewe ametufunulia hivyo. Na kwa kuwa ni fumbo la imani, imani tu yaelewa ndiyo maana katika sala ya koleta Padre anasali akisema; “Ee Mungu Baba, uliwafumbulia watu fumbo lako la ajabu, hapo ulipompeleka Neno wako na Roho Mtakatifu ulimwenguni. Utujalie kuutambua utukufu wa Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli na kuabudu Umoja wa Mungu katika enzi ya fahari yake”. Kiuhalisia akili zetu za kibinadamu haziwezi kulielewa kikamilifu fumbo hili la Utatu Mtakatifu. Hatuwezi tukamjua wala kumuelewa na kumuelezea Mungu jinsi alivyo na kwa namna inayositahili. Ndiyo maana hata masomo tunayosoma katika liturujia ya sherehe hii hayalengi kutufafanulia waziwazi juu ya fumbo hili bali yanatuonyesha umoja wa Utatu Mtakatifu katika Fumbo la wokovu wetu. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kutoka (Kut. 34:4b-6, 8-9). Somo hili linatueleza kuwa kama Mungu angekuwa Bwana mwenye haki tu, hatungekuwa na tumaini la wokovu. Lakini Yeye ni Bwana na mwingi wa huruma na fadhili. Kwa hiyo tunatumaini kwamba ingawa sisi tu watu wadhambi tena wenye shingo ngumu, atatusamehe uovu wetu tunapoukiri na kuomba msamaha kwa moyo wa majuto na hivyo anatustahilisha kuingia katika utukufu wa ufalme wake huko mbinguni. Somo la pili ni la Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2Kor. 13:11-14). Katika somo mtume Paulo anapohitimisha waraka huu anawaasa Wakorinto waliokuwa waachane na tofauti zinazowafanya watengane na wajitahidi kuishi kwa umoja akisema; “Hatimaye ndugu kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa busu takatifu…Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu Baba. Na ushirika wa Roho Mtakatifu vikae nanyi nyote.” Kumbe, somo hili linatueleza kuwa pendo la Mungu limedhihirika kwetu katika neema ya Yesu Kristo. Na neema ya Yesu inafanya kazi yake katika Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hivi ukombozi wetu ni kazi ya Utatu Mtakatifu. Mapato ya kazi ya Utatu Mtakatifu ni furaha, amani, upendo, mshikamanoo na umoja.

Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani, matumaini na mapendo
Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani, matumaini na mapendo

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 3:16-18). Sehemu hii ya Injili inatueleza kuwa Mungu na Mwanawe na Roho Mtakatifu ambaye anaitwa Upendo ni Utatu Mtakatifu. Ukombozi wetu umetoka kwa Baba na Roho Mtakatifu na umetekelezwa na Yesu Kristo. Sisi lazima tusadiki katika Utatu huo tukitaka kuokoka. Tukikataa kusadiki tunajihukumu wenyewe sababu tunajitenga na Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Ndiyo maana katika utangulizi wa sherehe hii Padre anasali akisema; “Ee Bwana, Baba mwema, Mungu Mwenyezi wa milele. Wewe pamoja na Mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa nafsi, ila katika Utatu wa umungu mmoja. Mambo tunayoyasadiki juu ya utukufu wako kwa sababu ya ufunuo wako, twayasadiki pia juu ya Mwanao na juu ya Roho Mtakatifu pasipo tofauti ya kutengana. Nasi tunapoungama Umungu wa kweli na wa milele, tunaabudu nafsi zilizo mbalimbali za Mungu mmoja zenye utukufu ulio sawa”. Mtakatifu Tomaso wa Akwino kuhusu fumbo hili la Utatu Mtakatifu anakiri kutolifahamu kwa undani wake akisema; “waficha Umungu msalabani na ubinadamu Altareni, mafahamu yangu yadanganya ninapokuona na kugusa.” Naye Mtakatifu Augustino anasema; “Inatupasa kusadiki kwa sababu Mungu ametufunulia”. Kumbe lengo la tafakari hii katika sherehe ya Utatu Mtakatifu siyo kuwaelewesha namna ambavyo nafsi tatu za Utatu Mtakatifu zilivyoungana na kufanya Mungu mmoja bali ni kutafakari huruma ya Mungu inavyojidhihirisha kwa njia ya Utatu Mtakatifu katika maisha yetu kwa upendo mkubwa kwetu sisi wanadamu kama wimbo wa mwanzo unavyosema: “Asifiwe Mungu Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; kwa sababu ametufanyizia huruma yake”. Kumbe kwa Utatu Mtakatifu tunafunuliwa upendo, wema, ukuu, mamlaka, huruma na asili ya Mungu. Ni katika Utatu Mtakatifu ndimo tunamopata ufupisho na simulizi la asili yetu tangu kuumbwa na Mungu Baba hata kukombolewa kwa njia ya Yesu Kristo, nafsi ya pili ya Mungu, na kutakaswa kwa njia ya Roho Mtakatifu, ndimo zinamolala sala zetu na matumaini yetu kufikia utimilifu wa upendo kwa kuungana na yule aliye asili ya upendo. Kumbe kwa vile Utatu Mtakatifu una asili moja iliyo sawa, vivyo hivyo una utendaji mmoja ulio sawa. Lakini kila nafsi ya Mungu inatekeleza kazi yake ya pamoja kufuatana na hali yake kama nafsi. Hivyo matendo yote ya nafsi za Mungu ni mamoja, yaani Utatu Mtakatifu ndio ulioumba, uliotukomboa na unaotakatifuza.

Ishala ya Msalaba ni muhtasari wa Kanuni ya Imani.
Ishala ya Msalaba ni muhtasari wa Kanuni ya Imani.

Sisi tunashirikishwa katika umoja huo wa mapendo ya kimungu kwa sababu katika ubatizo tumetiwa muhuri usiofutika kwa jina la Utatu Mtakatifu tulipobatizwa kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Hivyo inatupasa kuwa na umoja na mapendo kati yetu sisi wenyewe na kati yetu na Mungu katika Utatu Mtakatifu. Mapendo kati yetu sisi wenyewe yanapaswa yaonekane katika maisha yetu ya kila siku popote pale tulipo tukisaidiana kwa hali na mali, tukiishi kwa umoja, amani na upendo tukilenga hasa katika kutafuta maisha ya utakatifu (LG. 40). Umoja na upendo kati yetu na Mungu katika utatu wake, unajidhihirisha katikati yetu kwa njia ya sala ambayo ni moja ya nguzo muhimu sana ya maisha yetu ya kiroho. Sala inaleta umoja na kudumisha uhusiano mzuri na mwenyezi Mungu, kwa hiyo ni muhimu kusali katika familia na katika jumuiya zetu ndogondogo za Kikristo na zaidi sana kushirika katika maadhimisho ya Misa Takatifu. Kumbe, Sherehe hii inatuhimiza tuwe wamoja katika maisha yetu tukisaidiana katika taabu na raha. Tujenge familia zenye umoja thabiti unaosimikwa katika upendo. Ni kutoka katika umoja wa kifamilia ndipo tunaweza kuwa na umoja katika nyanja zingine za maisha yetu na kuishi kwa kupendana. Tumuombe Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, watukirimie fadhila ya mapendo katika maisha yetu. Na hii iwe ni sala yetu; Eee Mungu kwa upendo wako umetuumba, umetupenda daima mpaka kushuka kwetu pamoja na kuwa tulikuasi, ukatufia kifo cha aibu msalabani, ukatuimarisha ili tutangaze ukuu wako. Lakini bado tuko wakaidi kwa kutotii mausia yako. Huruma yako isiyo na mipaka, na upendo wako usiobagua uzidi kumiminika ndani mwetu mpaka hapo tutakapoungana nawe huko mbinguni. Ndivyo sala baada ya komunyo inahitimsiha maadhimisho haya ikisema; “Ee Bwana Mungu wetu, Sakramenti hii tuliyoipokea ituletee afya ya mwili na roho, na kutuwezesha kuungama Umoja wa Mungu katika Utatu Mtakatifu wa milele”. Nasi kwa imani tunasema; Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote na milele, Amina.

Sherehe Utatu Mtakatifu
01 June 2023, 08:13