Tafuta

Kwa bahati mbaya Wakristo wengi huna tunaadhimisha sherehe nyingi za kiliturujia bila kuzihusianisha na maisha yetu kama Wakristo. Kwa bahati mbaya Wakristo wengi huna tunaadhimisha sherehe nyingi za kiliturujia bila kuzihusianisha na maisha yetu kama Wakristo. 

Historia Fupi ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Mtakatifu Maria Alakoki

. Sherehe hii ilianza kuadhimishwa na Kanisa zima katika kalenda yake ya liturujia mnamo mwaka 1856 kwa idhini ya Baba Mtakatifu Pius IX. Bwana Wetu Yesu Kristo anamtajia Mt. Margareta Maria Alakoki mambo ya kufanya kama sehemu ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu: matendo ya malipizi, kupokea Ekaristi Takatifu, kupokea Ekaristi katika Ijumaa za kwanza za mwezi, kuhudhuria ibada ya Saa Takatifu. Hii ni siku pia ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa mapadre

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia

Kuanzishwa kwa Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni matokeo ya Bwana Wetu Yesu Kristo mwenyewe kumtokea Mt. Margareta Maria Alakoki na kumfafanulia umuhimu wa ibada hii kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Sherehe hii ilianza kuadhimishwa na Kanisa zima katika kalenda yake ya liturujia mnamo mwaka 1856 kwa idhini ya Baba Mtakatifu Pius IX. Bwana Wetu Yesu Kristo anamtajia Mt. Margareta Maria Alakoki mambo ya kufanya kama sehemu ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu: matendo ya malipizi, kupokea Ekaristi Takatifu, kupokea Ekaristi Takatifu katika Ijumaa za kwanza za mwezi, kuhudhuria ibada ya Saa Takatifu (Holy Hour). Haya yote yanaakisi upendo na huruma ya Yesu vilivyotoka katika Moyo wake Mtakatifu. Yesu Mwenyewe anasema “Moyo wangu ni kiti na makao ya Huruma ya Mungu iliyofunuliwa katika mateso, kifo na ufufuko wangu. Nimefungua Moyo wangu kama chemchem hai ya Huruma, ambayo roho zote zinachota uzima, na zinaijongea bahari hii ya Huruma kwa tumaini kuu.” Ufafanuzi na uelewa wa “Moyo wa Yesu”: Katika lugha ya Kibiblia na katika uelewa wa Kiyahudi “moyo” unabeba maana kubwa sana: Moyo ni kiini cha uzima wa mtu; moyo ni makao ya hisia, nia, matamanio, makusudio, mipango na mikakati yote ya mwanadamu. Hivyo kwenye Biblia (na hata katika zama hizi zetu) ni kwamba hisia zote za mwanadamu zatoka moyoni: upendo, furaha, huruma, huzuni, hasira, uchungu, mahangaiko na nyinginezo kama hizi. Kadhalika tukumbuke kuwa katika fani ya uandishi na lugha kuna mbinu ya uandishi iitwayo kwa kimombo “synecdoche” (a figure of speech in which a part is made to represent the whole or vice versa)- yaani kinatajwa kiungo kimoja tu cha mwili kumaanisha mwili mzima - unataja jicho, kwa mfano, lakini humaanishi jicho tu peke yake bali mwili mzima. Mbinu hii ya uandishi imetumika pia katika Biblia.

Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya neema
Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya neema

Kumbe tunapoadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu hatuutazami “moyo wake tu kama moja ya viungo vya mwili” bali tunamtazama Yesu mzima aliyetupenda, aliyeteseka, aliyehuzunika, aliyefadhaika na aliyekufa kwa ajili ya dhambi zetu. Hivyo tunapofanya sherehe na ibada kwa heshima ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kimsingi tunauheshimu na kuuabudu Moyo wa Yesu uliojaa upendo na uliokuwa tayari kuteseka, kuhuzunishwa, kudharauliwa, kuonja uchungu na mahangaiko kwa ajili ya dhambi za wanadamu. Hata hivyo kwa nini tuutazame hasa Moyo wa Yesu? Jibu la swali hili linatoka kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki kifungu namba 478 kinachosema: “[Yesu] Ametupenda wote kwa moyo wa kibinadamu. Kwa sababu hiyo, Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa sababu ya dhambi zetu, na kwa ajili ya wokovu wetu, unachukuliwa kama alama na ishara kuu ya mapendo yake yasiyo na mipaka ambayo kwayo Mkombozi, ambaye ni Mungu, anampenda Baba wa Milele na watu wote bila kikomo.” Kumbe “Moyo Mtakatifu wa Yesu” ni alama na ishara kuu ya mapendo ya Yesu kwa pande mbili: upendo usio na kikomo kwa Mungu Baba na upendo usio na kikomo kwa watu wote. Yesu alimpenda sana Baba yake wa mbinguni kwa kuwa mtii mpaka mauti; Yesu alitupenda watu wote hadi kufikia hatua ya kuteswa, kufa, kufufuka na kupaa mbinguni kwa ajili yetu. Hivyo tunapaswa kuuheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kuwa ni Moyo wa Mungu-mtu: ni moyo wa kimungu na ni moyo wa kibinadamu. Uhusiano wa kutobolewa Moyo Mtakatifu wa Yesu na kupasuka kwa pazia la hekalu:

Moyo wa Yesu Makai ya upendo na huruma ya Mungu
Moyo wa Yesu Makai ya upendo na huruma ya Mungu

Katika muundo wa Hekalu la Yerusalemu kulikuwa na chumba kidogo mahali patakatifu (katika madhabahu) kilichoitwa “Patakatifu pa Patakatifu”. Aliyeruhusiwa kuingia Patakatifu pa Patakatifu ni kuhani mkuu (siyo kuhani wa kawaida). Na tena, kuhani mkuu aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa mwaka wakati wa siku iliyoitwa Siku ya Upatanisho (The Day of Atonement). Chumba hicho (yaani Patakatifu pa Patakatifu) kilitenganishwa na sehemu nyingine za hekalu kwa pazia. Pazia hili ndilo liliitwa pazia la hekalu na ambalo lilipasuka kuanzia juu hadi chini mara baada ya kifo cha Yesu (rejea Mk. 15:38). Kitendo cha kupasuka kwa pazia la hekalu kina uhusiano gani na kutobolewa kwa moyo wa Yesu? Waraka kwa Waebrania unatupa maana mpya ya pazia la hekalu: pazia la hekalu ni mwili wa Yesu (rejea Waebrania 10:19-20). Kama ambavyo pazia lilipasuka kule hekaluni, pazia jingine la hekalu (yaani mwili wa Yesu) linapasuliwa kwa mkuki ubavuni/moyoni. Pazia hili (mwili wa Yesu) linapasuliwa kwa mkuki moyoni na kutoa damu na maji vinazoashiria sakramenti za ubatizo na Ekaristi ambazo kwazo hutuwezesha kumfikia Mungu kwa kutupatia uzima mpya. Kumwagika kwa damu na maji ni ishara ya kumwagika kwa neema ambazo Mungu anampatia mwanadamu ili kumpatia uzima mpya. Moyo wa Yesu ndio chemchem ya maisha ya uzima mpya. Pia tukumbuke kuwa ubavuni mwa Adamu alitoka Eva, ambaye ni chanzo cha dhambi na mauti, lakini katika ubavu wa Yesu kunatoka damu na maji, chanzo cha neema na uzima.

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma ya Mungu
Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma ya Mungu

Umuhimu na maana ya sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu katika Maisha ya waamini: Kwa bahati mbaya Wakristo wengi huna tunaadhimisha sherehe nyingi za kiliturujia bila kuzihusianisha na maisha yetu kama Wakristo. Sherehe na mafumbo mengi ya imani yetu yanabaki kusherehekewa tu kwa nyimbo za midomoni, vifijo na shamrashamra bila kuacha alama yeyote katika maisha yetu kama Wakristo. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu inatudai kulinganisha “Moyo wa Yesu” na mioyo yetu: Moyo wa Yesu ulijaa upendo (Yn. 13:1), Moyo wa Yesu ulikuwa wazi kutoa msamaha (rejea Lk. 23:34), Moyo wa Yesu ulikuwa na furaha (rejea Lk. 10:21; Yn. 11:15), Moyo wa Yesu ulijaa huruma (rejea Lk. 7:13). Swali kubwa la kujiuliza ni hili: Je, mioyo yetu ni sawa na Moyo wa Yesu? Je, mioyo yetu ina upendo unaodhihirishwa katika matendo? Je, mimi na wewe tunakuwa tayari kusamehe pale tunapokosewa au kutendwa pasipo haki? Je, mioyo yetu ina huruma pale tunapoona binadamu wenzetu wanaumia, wanateseka au wana huzuni zitokanazo na maisha? Je, moyo wako una furaha katika Kristo? Yote katika yote Moyo wa Yesu ni kielelezo cha upendo na huruma ya mungu kwa watu wote. Ni katika Moyo wa Yesu tunaheshimu na tunakiri upendo wa Mungu kwa wanadamu, utashi wake wa kuukomboa ulimwengu pamoja na kukiri na kuomba huruma yake isiyo na kikomo. Moyo wa Yesu ni kielelezo cha Upendo na Huruma ya Mungu. Tunarudishaje upendo wa Kristo uliotoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu? Tunaishije Huruma ya Mungu iliyotoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu? Tunapaswa kujua wazi kuwa upendo unahusisha pande mbili: kutoa upendo na kupokea upendo. Kama Yesu Kristo alitupenda hadi kukubali kufa mauti ya aibu msalabani, nasi hatuna budi kuwa tayari kupokea upendo huu na kuwa tayari kurudisha upendo huu kwake kwa njia ya kutimiza mapenzi ya Mungu.

Moyo Mtakatifu wa yesu
Moyo Mtakatifu wa yesu

Lakini upendo huu tuliopokea kutoka kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu tunapaswa kuwapatia na wenzetu pia. Kama Moyo wa Yesu unafunua Huruma ya Mungu kwetu, kadhalika nasi tunapaswa kuishi Huruma ya Mungu katika maisha yetu: kujongea Sakramenti na Kitubio, kutoa msamaha kwa nafsi zetu wenyewe na kwa wengine. Hata hivyo, tunapaswa kuutazama Moyo wa Yesu katika upande wake wa pili: Moyo wa Yesu ulisononeka na kulia kwa sababu ya watu wa Yerusalemu kutoamini (rejea Lk. 19:41); Moyo wa Yesu ulipatwa na huzuni na mahangaiko (Mt. 26:37-38), Moyo wa Yesu ulipatwa na hasira- hasira inayotokana na ugumu wa mioyo ya watu (Mk. 3:5), Moyo wa Yesu ulipatwa na uchungu na hata kulia kwa uchungu (Yn. 11:35). Upande huu wa pili wa Moyo wa Yesu unatufundisha nini? Moyo huu wa Yesu unatufundisha kuwa kuna nyakati mioyo yetu itakuwa na huzuni na mahangaiko, kuna nyakati mioyo yetu itajaa uchungu na vilio na mengineyo kama hayo. Tunapokumbana na hali hizi za maisha tukumbuke kuwa sisi sio wa kwanza kupitia hali hizo. Jambo la msingi ni kuchota nguvu kutoka katika Moyo wa Yesu ambao nao ulipitia hali hizo pasipo kukata moyo. Ni katika Moyo wa Yesu ndimo kuna majibu ya matatizo yetu yote, ni katika Moyo wa Yesu tunapata dawa ya magonjwa yetu ya kiroho na kimwili, ni katika Moyo wa Yesu tunapata nafuu ya matatizo yetu na ni katika Moyo wa Yesu tunapata nguvu ya kufanya malipizi ya makosa yetu. Moyo wa Yesu utusaidie kuishi maisha ya imani, matumaini na mapendo.

17 June 2023, 08:21