Tafuta

Mkutano mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani unanogeshwa na kauli mbiu: “Wanawake Wakatoliki Wajenzi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu Kwa Amani ya Ulimwengu.” Mkutano mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani unanogeshwa na kauli mbiu: “Wanawake Wakatoliki Wajenzi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu Kwa Amani ya Ulimwengu.”  

Ujumbe Maalum Kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania: Uhai, Maadili na Utu Wema

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Tanzania, anakazia umuhimu wa kusimama kidete: kutetea, kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mwaliko kwa waamini kujikita katika maadili na utu wema pamoja na Mkutano mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, kuanzia tarehe 14-19 Mei 2023, huko Assisi, Italia.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - WAWATA, Dar Es Salaam, Tanzania.

Ujumbe Maalum kwa WAWATA: Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Tanzania, lakini zaidi wanawake, anakazia umuhimu wa kusimama kidete: kutetea, kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mwaliko kwa waamini kujikita katika maadili na utu wema pamoja na Mkutano mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, kuanzia tarehe 14-19 Mei 2023, huko Assisi, nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Wanawake Wakatoliki Wajenzi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu Kwa Amani ya Ulimwengu.” Tarehe 25 Machi 2023, Mama Kanisa sehemu mbalimbali za dunia ameadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari na Malaika Gabrieli kwamba atakuwa ni Mama wa Mungu sanjari na Siku ya Kutetea Uhai na Utakatifu wa Maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni ujumbe makini unaonesha kwamba, maisha ni matakatifu na kila mtu anayo haki ya kuishi. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo.

Ujumbe maalum kwa WAWATA: Uhai, Maadili na Utu wema
Ujumbe maalum kwa WAWATA: Uhai, Maadili na Utu wema

Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II bado anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watetezi wa Injili ya uhai kwa ajili ya maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo! Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, “Theotokos” ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Jibu la Bikira lilikuwa, “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana.” Malaika Gabrieli akamjuza pia matendo makuu ya Mungu aliyomtendea binamu yake Elizabeti, kiasi cha kutoka kwa haraka kwenda kumtembelea na huo ukawa ni ufunuo wa siri kubwa iliyokuwa imefichika mjini Nazareti, tukio la kiimani, akajiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu ili kumwezesha kuandika historia ya ukombozi kwa kukubali wito wa Mungu. Bikira Maria akawa ni chombo cha imani kwa sababu aliamini kile alichoambiwa na Bwana. Elizabeti akamwona Bikira Maria kuwa kweli ni Mama wa Mungu, kwa sababu alikua amejaa neema “Fide plena.” Mwenyezi Mungu atujalie neema na baraka za kuweza kufurahia mafanikio ya wengine; atuwezeshe kuwa ni vyombo, mashuhuda na vichocheo vya mafanikio ya jirani zetu.

Bikira Mama wa Mungu na Kanisa awe ni kielelezo cha utume wa WAWATA
Bikira Mama wa Mungu na Kanisa awe ni kielelezo cha utume wa WAWATA

Kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 ni: "Tunawaombea Mjaliwe Kufanywa Imara Katika Utu..." Efe 3: 16. Ujumbe huu unachota utajiri kutoka katika Neno la Mungu, Mafundisho ya Kanisa juu ya Utu, Uundwaji wake, Kufanywa imara katika utu; Na jinsi ya kuuvua utu wa kale. Unakazia umuhimu wa Neno la Mungu, Sala, Toba na Wongofu wa ndani. Kipindi hiki cha Pasaka, kama Wanawake Wakatoliki, tunapaswa kumweka Bikira Maria kuwa kama kioo cha maisha na utume wetu. Bikira Maria tangu mwanzo alikubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake; akawa kweli ni Mama wa Mungu, akaandamana naye katika maisha, lakini zaidi katika Njia ya Msalaba, kiasi hata cha kuthubutu kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Huu ndio mwaliko tunaopewa na Mama Kanisa na kwa namna ya pekee na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., mintarafu malezi na makuzi ya watoto wetu wanaokabiliana na changamoto katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Huu ni mwaliko wa kufanywa upya utu wa ndani; kwa kuheshimu, kulinda na kudumisha kanuni maadili na utu wema; kulinda na kutunza uadilifu wa uumbaji dhidi ya utamaduni wa kifo. Ikumbukwe kwamba, tunaweza kuunda na kukuza utu wetu wa ndani kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti; kufunga kwa ajili ya kudhibiti vilema vyetu na hatimaye, kushiriki katika matendo ya huruma kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kimsingi hizi ni nguzo kuu za Kipindi cha Kwaresima, Siku Arobaini za kutembea katika jangwa la maisha ya kiroho, tayari kufufuka na Yesu Kristo na hivyo kuanza kutembea katika mwanga wake kama vyombo na mashuhuda wa imani.

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha

Jambo la msingi la kujiuliza, Je, Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 imenisaidia kuku ana kukomaa: kiutu, kimaadili na kiimani? Je ni mambo yepi ninayopaswa kuyaendeleza kama sehemu ya mchakato wa ukuaji na ukomavu wangu katika maisha na utume wangu kwa familia, jamii na Kanisa? Ni mambo yepi ninayopaswa kuyazika? Ni wakati wa kuendeleza yale mema na matakatifu ambayo Mwenyezi Mungu amenikirimia katika Kipindi hiki cha Kwaresima. Ninapenda kuchukua fursa hii, katika Kipindi hiki cha Pasaka kuwaalika watu wa Mungu nchini Tanzania, lakini kwa namna ya pekee wanawake, kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza: imani, maadili na utu wema. Ni wakati wa kuwa karibu zaidi na watoto pamoja na vijana wetu, ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ari, ujasiri, moyo mkuu na unyenyekevu. Tayari tumo kwenye mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Mchakato huu uliwezeshe Kanisa kujenga umoja katika tofauti zake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuanzia tarehe 14-19 Mei 2023 kunafanyika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC huko mjini Assisi nchini Italia. Basi nichukue fursa hii kuwaalika watu wa Mungu nchini Tanzania na hasa zaidi wanawake kuombea mafanikio ya mkutano huu unaoongozwa na kauli mbiu: “Wanawake Wakatoliki Wajenzi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu Kwa Amani ya Ulimwengu.” (Catholic Women Artisans of human fraternity for World Peace.) Basi tuendelee kuombeana ili tuwe kweli vyombo na wajenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu; tuyafie madhaifu na mapungufu yetu ya kibinadamu, tayari kufufuka pamoja na Kristo Yesu, ili siku ile atakapotuita kutoka huku Bondeni kwenye machozi, aweze kutukaribisha kwenye Ufalme wake wa milele.

WAWATA 2023
11 May 2023, 14:10