Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani: Hakika ya Uwepo wa Kristo Miongoni Mwa Watu Wake
Na Padre Octavian Onesmo Hinju, C.P - Morogoro, Tanzania.
UTANGULIZI: Maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Wito: Neema na Utume.” Huu ni mwaliko wa kutafakari kwamba, watu wameumbwa, kwa upendo, kwa ajili ya upendo na kwa upendo. Mimi ni utume katika dunia hii, hiyo ndiyo sababu ya kuwepo kwangu mimi katika ulimwengu, kuwa pamoja na wengine na kwa ajili ya wengine. Tunaitwa kuwa wamoja ili kuunda jumuiya ya wamisionari mitume kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia upendo kwa ajili ya wengine kwa kutambua kwamba, neema na utume ni zawadi na dhamana. Wito ni sauti ya ndani inayomwita mtu kufuata mtindo fulani wa maisha. Mungu anaita watu ili awashirikishe kazi zake mwenyewe (Ebr. 5:1-5). Katika kutekeleza hilo, Mungu yupo huru kumwita na kumtumia yule ampendaye. Namna hii ya utendaji wa Mungu ni kinyume kabisa na namna ya kibinadamu. Mungu anayo namna ya kuangalia ambayo ni tofauti kabisa na ya wanadamu “akini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo” (1 Sam 16:7). Namna hii ya utendaji wa Mungu ni ngumu kuielewa kwa akili ya kawaida kwa kuwa Mungu hutumia vitu dhaifu na vinyonge kudhihirisha utukufu wake. Mt. Paulo anasema kuna hazina katika vyombo vya udongo (2 Kor. 4:7).
Uwepo wa watu wanaoitikia wito wa Mungu ni dhihirisho wazi kuwa, wito ni hakika ya uwepo wa Kristo Yesu kati ya watu wake ili kwa sadaka ya misa takatifu, huduma na majitoleo ya watumishi wake waaminifu katika utume wa Kanisa na kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali, Yeye mwenyewe aendelee kuambatana nao na kujidhihirisha kati yao kwa namna ya neno lake na katika kuumega mkate (Lk. 24:31); ili Kristu aendelee kuwa ni kiungo na ishara ya mapendo makuu ya kimungu. Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican kila mwaka Dominika ya nne ya Kipindi cha Pasaka Mama Kanisa anaadhimisha “Siku ya Kuiombea Miito Mitakatifu Katika Kanisa.” Miito mitakatifu ni zawadi na tunu msingi ya uhai, utume na uinjilishaji wa kanisa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kwa namna ya maisha ya wito watawa na mapadre wengi wameendelea kwa nyakati zote kuitikia sauti ya MUNGU inayoendelea kuwaita kwa maneno ya Nabii Isaya kwamba “nimtume nani, naye ni nani atakaye kwenda kwa ajili yetu? Ndipo nilipo sema mimi hapa nitume mimi (Is. 6:8). Mapadre na watawa kwa maisha na majiundo yao wamekuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya KRISTU Yesu anayewatuma akisema “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, Mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyo waamuru ninyi (Mt. 28:19-20). Kimsingi Wito ni sauti ya kimungu ndani ya moyo wa mtu; ndivyo pia walivyoulizana wanafunzi wa Emau, “je mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko? (Lk. 24:32).
Ni mguso wa pekee katika nafsi; Ni sauti inayo hitaji jibu ‘mimi hapa nitume Bwana (Is. 6:8). Vile vile wito ni zawadi ya MUNGU kwetu wanadamu ili tuweze kutambua uwepo wake katika hija na safari ya maisha yetu ya kiroho (Lk. 24:15). Wito ni tunda la Imani kwa MUNGU, fumbo la upendo na ukarimu wake kwetu, MUNGU anayewapenda watu wake upeo kiasi cha kuwakirimia wingi wa neema na baraka zake. Wito ni fumbo la kujitoa kama anavyofundisha Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa “unapokuwa umezamishwa katika ule upendo mkuu, huwezi kukaa mbali na kutazama mambo, ila ni lazima uingie katika fumbo la kujitoa kwa upendo mkubwa, ni lazima ujiruhusu mwenyewe kuunguzwa katika moto ule na kuchomwa kama dhabihu ya sadaka safi ya upendo wa KRISTU.” Aina za miito: Zipo aina nyingi sana za miito. Katika nafasi yetu ya leo napenda tutafakari juu ya aina chache; wito mkuu, wito wa maisha na wito wa kazi. Wito mkuu- huu ni wito ambao ni mama wa miito mingine yote. Wito mkuu ni ule wa kuwaita watu wote kuwa watakatifu (Law. 18:1; Mt 5:48). Katika wito wa maisha, hapa ndipo tunapoangalia miito mbalimbali kama vile, wito wa ndoa, wito wa kitawa, wito wa Ukasisi/upadre. Hata hivyo, Wito wa maisha hautengani na wito mkuu. Wito wa kazi. Hapa pia watu wanapata mivuto mbalimbali ya kazi. Wengine wanapenda kuwa waalimu, marubani, wafanyabiashara, matabibu nk.
WITO WA KIKASISI/KIPADRE: Padre ni mwanaume mkatoliki, aliyeteuliwa na Mungu kwa kazi ya Mungu kwa wanadamu. Kwa maneno mengine, Padre/kuhani anatwaliwa kutoka kwenye kundi la wanadamu kwa ajili yao katika mambo yanayomhusu Mungu (Ebr 5:1-5). Dira ya makuhani ni kushiriki katika kazi ya wokovu. “Maana Mungu hakumtuma Mwana limwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye” (Yn. 3:17). Yesu alihubiri habari njema ya Ufalme, alichagua na kuunda jumuiya ya mitume wake, akakamilisha kazi ya ukombozi kwa njia ya msalaba na ufufuko wake. Kwa njia ya Mitume, tunahusishwa kwa namna fulani kwenye kazi ya wokovu, kuifanya iendelee kutendeka kila wakati na kila mahali ulimwenguni.[1] Bila padre, mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo kinakosa maana. Kwani ni kwa njia ya padre sadaka ya Kristo inaendelea kutendeka ulimwenguni.[2] Kutokana na kazi kuu tatu za padre yaani kazi ya kikuhani, ya kifalme na ya kinabii, padre, anawajibu wa; • Kutangaza Habari Njema bila kukoma, kuifafanua katika namna ambayo ujumbe wa neno la Mungu unakuwa hai bila kupoteza maana. Kutoa sadaka ile Yesu aliyoitoa katika karamu ya mwisho, na kiuhalisia pale msalabani, kwa ajili ya msamaha wa dhambi zetu. Mtu anaye sikia, kutambua na kuufuata wito, ni yule tu aliyeonja kupendwa sana na KRISTU hivyo daima ametamani na kuwa tayari kurudisha shukrani ya pendo kwa pendo kama anavyo zungumza Padre Innocent Bahati Mushi, OFM Cap katika kitabu chake cha Fadhila na tunu za maisha ya wakfu akisema kwamba “wao walio tambua wito wao na kuufuata wametaka zaidi kuwa kama YESU KRISTU Mkombozi wetu kuhuishwa na kugeuzwa kwa ndani kabisa na kuwa viumbe wapya Katika KRISTU.” Kwa njia ya Yesu Kristu, wito ni mwendelezo wa historia ya Pasaka ya kikristo. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu aliye mlezi wa kwanza wa miito mitakatifu.
Hivyo tukio la wito ni muungano wa kimungu na Roho Mtakatifu mfinyanzi wa miito yote. Kwa nyakati zote, Roho huyo ameendelea kuwagusa na kuwaita wakristu wabatizwa wake kwa waume katika maisha na chaguo hili la pekee sana. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wanaotikia wito wanarudia tena kwa ujasiri maneno ya Nabii Yeremia wakisema kuwa “umenihadaa Ee Bwana, nami nikahadaika (Yer. 20:7). Roho ndiye anaye toa shauku ya mtu kujibu wito mtakatifu akisema “fingere me secundum voluntatem tuam, Domine" ‘nifinyange utakavyo Ee Mungu.” Padre Innocent Bahati anaendelea kufundisha akisema kwamba “ni Roho ndiye anayeongoza ukuaji wa shauku ya kuitikia wito, akiisaidia ikomae katika mrejesho chanya na kuiwezesha kutafsiriwa katika matendo, ni yeye anayeumba na kuipa mioyo ya wale walioitwa kufanana Zaidi na Kristo aliye fukara, mtii na mwenye usafi kamili na kuufanya utume wa Kristo kuwa utume wao.” Katika kuisikia sauti ya KRISTU na “kwa kuruhusu wenyewe waongozwe na Roho Mtakatifu katika safari yao ya utakaso isiyo na kikomo, siku baada ya siku wale wote waliotwa na kwa namna ya pekee watawa na mapadre, basi waendelee kulandana na Kristo na kuendeleza historia ya uwepo wa pekee wa Bwana Mfufuka. (V.C, 19). Sambamba na ukweli huo, akitafakari juu ya wito wa Nabii Elisha Dominika ya 13 ya Mwaka C wa kanisa katika kipindi cha kawaida, Padre William Bahitwa anafundisha akisema kwamba “Wito una madai ya kudumu na changamoto zake kulingana na hali na maisha. Kwa asili yake, Mwito unabadilisha maisha ya mtu kumuelekea Kristo, mwito mtakatifu ni mwaliko wa kujibandua na malimwengu na kujikita kwa Kristo bila kugeuga ugeuka. Hata hivyo, mwito unazo sadaka zake na magumu yake yanayohitaji uimara na ujasiri wa kuyakabili kwa nguvu zake anayeita, mwito ni mwaliko wa kuupokea bila kuchelewa. Lengo la mwito wa kimungu ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Asili ya Wito: Mpendwa msikilizaji, wito asili yake ni MUNGU mwenyewe ambaye kwa upendo mkuu hapo kale alimwita kwanza baba yetu wa Imani Abrahamu alipomwambia kuwa ‘Ondoka katika nchi yako, acha jamaa yako na nyumba ya baba yako, uende katika nchi nitakayokuonesha. Nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka. Anayekubariki, nitambariki; anayekulaani, nitamlaani. Kwako wewe, nitayabariki mataifa yote ya dunia (Mwz. 12:1-3). Lakini hata leo kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu mwenyezi MUNGU Bwana wa historia na nyakati zote ameendelea kuwaita watu mbalimbali ili waendeleze kazi yake Kristu mwenyewe kama alivyofanya “kwenye karamu ya mwisho usiku ule alipotolewa Mkombozi wetu aliweka sadaka ya mwili na damu yake takatifu; yaani Ekaristi. Alifanya hivyo kwa ajili ya sadaka yake Msalabani ambayo ingekuja kuadhimishwa milele ili kumpa mchumba wake yaani kanisa kumbukumbu ya kifo na ufufuko wake; Sakramenti ya upendo, ishara ya umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya kipaska ambapo KRISTU twampokea, tukijazwa neema na hakika ya utukufu ujao (S.C, 47). Kumbe basi kwa kuiombea miito mitakatifu tunajihakikishia wachungaji watakao endela kumshusha KRISTU kati yetu nasi kupandishwa mpaka altare ya mbinguni. Kwa Sakramenti ya daraja takatifu katika Kanisa, ambayo ni tunda la wito mtakatifu “kila kazi ya kitume inahuishwa na kuelekezwa kwake KRISTU mwenyewe. Mapadre kama KRISTU MWINGINE, kupitia mwili wake yaani kanisa katika Roho Mtakatifu wajitoe maisha yao kwa ajili ya watu. Kwa hiyo wanaalikwa na kuongozwa kujitoa kwa kazi zao na vyote vilivyo umbwa na yeye (P.O).
Katika mazingira ya kisinodi tukiongozwa na kauli mbiu yake yaani: Umoja, Ushiriki na Utume, wito uwe kwetu kifungo cha umoja na mshikamano wa kidugu na kikristu. Kama alivyo tualika Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022 alitutaka tuendelee kutafakari kwa pamoja maana pana ya “wito” ndani ya muktadha wa Kanisa la Kisinodi, Kanisa linalomsikiliza Mwenyezi Mungu na Ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kukuza moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana, ili kujenga familia ya kibinadamu, kuponya majeraha yake na kuiongoza kwenye maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu aliendelea kukaza kwamba watu wa Mungu kutembea kwa pamoja kama kielelezo cha Kanisa la Kisinodi kwa kutambua kwamba, kila mwamini ni mdau katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kila Mkristo daima ni mfuasi mmisionari. Wakristo wanaitwa kusimama kidete kuwalinda ndugu zao na mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko kwa waamini kuutazama Uso wa Mwenyezi Mungu anayewaita kuwa watakatifu, kwa kutambua kwamba, utakatifu ni wito kwa watu wote unaowawezesha kutumia karama na fursa mbalimbali wanazowezeshwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Tunapoendelea kusherehekea ufufuko wa KRISTU, tuwasindikize kwa sala zetu kwa namna ya pekee watawa na wachungaji wetu ili waweze daima kuiga mfano wa YESU KRISTU MCHUNGAJI Mwema. Ili kwake waweze kujisadaka katika maisha yao ya kila siku kwa ajili ya ukombozi wa roho zao na za wale waliowekwa chini yao. Daima watambue kwamba ‘pasipo KRISTU hawawezi kulifanya jambo lolote’ (Yn. 15:5). Kwa njia ya malezi na majiundo yao ya upadre na utawa waendelee kutambua na kujua lengo hasa la maisha ya wito, kwamba ni kutolea maisha yao sadaka hai na timilifu kwa ajili ya Kristo na watu wake, na kwamba hakuna jambo jingine liwalo lolote linalowapa nguvu, faraja na furaha kama kutambua ukweli kwamba ni kwa muungano na KRISTU ndipo nao wanaweza kuwa ‘Alter Christi’ yaani Kristu mwingine miongoni mwa watu waweze pia kutumia nguvu, vipaji, akili na maarifa waliyojaliwa na MUNGU kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kwa utumishi wa huduma kwa watu wake kama anavyo tufundisha Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa “namna pekee ya kumrudishia MUNGU shukrani ni kutumia vipawa na karama alizo tujalia kuwatumikia wanadamu wenzetu.”
Wakisindikizwa kwa sala zetu, nguvu, mwangaza na uvuvio wa Roho Mtakatifu kwa namna ya maisha na utume wao waendelee kumrudishia mwenyezi MUNGU sifa na shukrani; yeye anayewapitisha katika mapito yote ambayo ni hatua muhimu katika maisha na utume. Tumwombe MUNGU aendelee kugusa na kufungua mioyo ya vijana wengi waisikie sauti ya KRISTU nafsi mwao waitikie na wawe tayari siku zote kujiunga na majiundo ya kitawa na kikasisi lakini Zaidi sana macho ya Imani yao ili waweze kweli kuona kile ambacho YEYE mwenyewe anataka kama wachungaji wema waendelee kuchota katika kila hatua ya kutumikia katika shamba lake. Kwa kufanya hivyo, Mwenyezi Mungu aendelee kila siku kuwavumilia ili wawe kati ya wale wanaojongea Altare yake mara zote kumshusha KRISTU MWOKOZI kati ya watu kwa sakramenti takatifu ya Ekaristi. Ili waamini wakichagizwa na Imani thabiti waendelee kuonja ukuu wa huruma na upendo wake wa kibaba ambao kwao twajua fika hatuna chochote cha pekee kuustahili. Kwa sadaka ya maisha ya wito mtakatifu, jamii ya waamini iendelee daima kujivunia kuwa katika tunza yenye kujali. MUNGU ROHO MTAKATIFU aliye mfinyanzi mkuu wa miito mitakatifu aendelee kutukumbusha kumwomba MUNGU BABA mwenyezi aendelee kufinyanga watumishi wengi Zaidi kwa ajili ya shamba lake kwa uvumilivu na upendo mkubwa awasaidie kuwa atakavyo yeye, wajitambue na kumtambua yeye aliye Mungu wa pekee na kweli (Yon. 17:3) wanaye mtumikia, dominika hii ya miito iwakumbushe kujitoa kwa ajili ya Kanisa lake na watu wake na hasa kwa namna ya maisha na mafundisho ya kanisa. TUMSIFU YESU KRISTU.
[1] Yohane Paulo II, Mafungo kule Ars kwa ajili ya Mapadre, Mashemasi na Waseminari, Oktoba 6, 1986.
[2] Mt. Yohane Maria Vianey, Cure d’ Ars, sa Pense, son Coeur, 1958.