Tafuta

Tafakari Dominika IV ya Kipindi cha Kwaresima: Upofu wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili: Ushuhuda amini wa imani ni muhimu katika ulimwengu mamboleo Tafakari Dominika IV ya Kipindi cha Kwaresima: Upofu wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili: Ushuhuda amini wa imani ni muhimu katika ulimwengu mamboleo  (Vatican Media)

Tafakari Dominika IV Kwaresima Mwaka A: Upofu wa Maisha ya Kiroho, Kimaadili na Kiutu!

Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima ni dominika ambayo inafahamika pia kama dominika ya furaha. Maneno ya wimbo wa mwanzo katika dominika hii ndiyo yanayodokeza furaha hiyo yakisema “furahi Yerusalemu na shangilieni ninyi nyote mmpendao.” Furaha inayozungumziwa hapa ni furaha ya Pasaka. Huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari kwa kina kuhusu Fumbo la Mateso ya mwanadamu; upofu wa maisha ya kiroho na ushuhuda wa imani na matumaini.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Dominika ya nne ya Kipindi cha Kwaresima ni dominika ambayo inafahamika pia kama dominika ya furaha. Maneno ya wimbo wa mwanzo katika dominika hii ndiyo yanayodokeza furaha hiyo yakisema “furahi Yerusalemu na shangilieni ninyi nyote mmpendao.” Furaha inayozungumziwa hapa ni furaha ya Pasaka. Kwa dominika tumefika nusu ya safari ya Kwaresima na tunaalikwa kuanza kuyaamsha matumaini yetu ya kuifikia siku hiyo ya Pasaka, siku ya kuadhimisha ukombozi wetu, siku ya furaha kuu. MASOMO YA MISA KWA UFUPI: Katika dominika hii tunasoma Injili kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 9:1-41). Ni kifungu ambacho Yesu anamponya mtu ambaye alikuwa kipofu tangu kuzaliwa. Na kabla hata uponyaji wenyewe haujaelezwa, kuna swali ambalo Yesu anaulizwa na wanafunzi wake: “ni yupi aliyetenda dhambi hadi huyu mtu azaliwe kipofu, je ni yeye mwenyewe au ni wazazi wake?” Hili ni swali ambalo linagusa kipengele kigumu sana katika maisha ya mwanadamu: kwa nini mateso katika maisha! Wayahudi walikuwa na imani kuwa mateso ni matokeo ya dhambi. Na kutokana na tafsiri ambazo walizoyapatia Maandiko Matakatifu, mfano katika kitabu cha Kutoka pale Mungu anaposema “Bwana Mungu wako ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana maovu ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao... (Kutoka 20:5), waliamini kuwa mtu anayeteseka leo kama sio yeye aliyefanya dhambi, basi ni dhambi walizofanya wazazi au babu na bibi zake.

Fumbo la Mateso na mahangaiko ya binadamu halina majibu ya mkato.
Fumbo la Mateso na mahangaiko ya binadamu halina majibu ya mkato.

Mantiki au tafsiri hii ilikwama pale ambapo anayeteseka alikuwa ni mtu mwema au alikuwa ni mtoto mchanga au kama huyu wa injili ya leo ambaye alizaliwa kipofu. Yesu anapolijibu swali hilo haweki mkazo juu ya sababu ya kuteseka. Yeye anaweka mkazo juu ya lengo au matokeo ya mateso ambayo mwanadamu anayapitia. Ni kama Yesu anasema kuwa mateso ya mwanadamu ni fumbo ambalo mwanadamu kwa upeo wake hawezi kulielewa wala kulieleza kinagaubaga. Anapoliingia ili kulichunguza ni lazima kuna mahala yatakosekana majibu. Ni fumbo analolijua Mungu mwenyewe na ndiyo maana kwa kuonesha fumbo hilo mwanadamu hubaki tu kusema ni “mapenzi ya Mungu”. Yesu haweki mkazo juu ya sababu ya mtu huyo kuzaliwa kipofu. Anawatoa tu wasiwasi wanafunzi wake akisema sio yeye aliyetenda dhambi wala si wazazi wake waliotenda dhambi. Mkazo anaouweka Yesu ni juu ya lengo au matokeo ya mateso ya mwanadamu. Na katika hili anasema huyo amezaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake. Wito wake anayemwamini Kristo ni kujiuliza wakati wa mateso, ni namna gani kwa mateso haya kazi ya Mungu inadhihirika ndani yangu? Ni katika kutokukata tamaa, ni katika uvumilivu na saburi, ni katika kuendelea kutumia juhudi, akili na maarifa ambayo Mungu huyo huyo ametupatia ili maisha yaweze kuendelea.

Fumbo la mateso na majaribu ya maisha kwa binadamu
Fumbo la mateso na majaribu ya maisha kwa binadamu

Sasa tukirudi katika uponyaji wenyewe ambao Yesu anaufanya, Mababa wa Kanisa kwa namna ya pekee Mtakatifu Augostino, Mtakatifu Ambrosi na Mtakatifu Yohane Krisostomu, kuhusu Injili hii wao wanazungumzia upofu sio ule wa kimwili bali wanaiona injili hii kama kifungu kinachozungumzia upofu wa kiroho. Uponyaji wa upofu huu ni kazi ambayo Yesu mwenyewe anaendelea kuifanya hadi leo, kuwatoa watu katika giza la maisha na kuwaleta katika nuru ya mwanga wake. Mtu huyu aliyezaliwa kipofu, kwanza kabisa anawakilisha binadamu wote ambao tunazaliwa na dhambi ya asili, dhambi inayoondolewa kwa ubatizo.  Lakini pia hata baada ya ubatizo, pale giza la maisha linapoisonga na kuizima nuru ya Kristo ndani mwetu, tunarudi kuishi katika giza. Matendo ya alama ambayo Mwinjili Yohane anayatumia kuonesha uponyaji, ni matendo ambayo hata leo yanaonesha maana ya uponyaji ambao Yesu anaendelea kuufanya ndani yetu. Tukijikita tu katika ishara mbili, ishara ya kwanza ni ile ambayo Yesu anatema chini, anatengeneza tope na kumpaka machoni. Tope au udongo ni alama ya uumbaji, kwa sababu Adamu aliumbwa kutokana na udongo. Hii ni ishara inayoonesha kuwa kumpokea Kristo, kuupokea mwanga wake maishani, kuongoka na kumgeukia Yeye ni kama kuumbwa upya. Na anayefanya kazi ya kutuumba upya ni huyo huyo Yesu. 

Mwaliko wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Nuru ya Mataifa.
Mwaliko wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Nuru ya Mataifa.

Katika alama ya pili, Yesu anamwambia “nenda ukajioshe katika bwawa la Siloamu”. Hii ni alama muhimu sana inayoonesha maana ya muujiza katika Injili ya Yohane. Tangu ule muujiza wa kwanza katika Injili ya Yohane ambayo ni wa harusi ya Kana ambapo Maria aliwaambia watumishi “chochote akachowaambia fanyeni”, Mwinjili Yohane anaonesha kuwa muujiza ni pale ambapo mtu anakuwa tayari kufanya kile anachoagiza Yesu. Muujiza kumbe ni tokeo la imani, ni tokeo la kutumaini na hasa zaidi ni tokeo la kujikabidhi katika mapenzi ya Mungu. Masomo mawili yanayotangulia somo hili la Injili, yaani somo la kwanza kutoka Kitabu cha Kwanza cha Samweli (1Sam. 16:1b,4,6-7,10-13) na somo la pili kutoka barua ya Paulo kwa Waefeso (Ef. 5:8-14) yanatupa dhamira ya wito wa imani yetu. Katika somo la kwanza, tunaona namna Mungu alivyomwita na kumchagua Daudi kuwa mfalme wa Israeli. Mungu anamwambia nabii Samweli “Bwana haangalii kama binadamu, yeye huutazama moyo.” Kwa namna hii Daudi akapakwa mafuta mbele ya kaka zake wote ambao Bwana hakuwachagua. Somo la pili linakuja kutuonesha wito kama huo wa Daudi katika maisha ya mkristo. Kama ambayo Daudi alichaguliwa, kila mkristo amechaguliwa na ameitwa kutoka gizani aishi katika nuru ya Bwana. Wito anaoitiwa ni kuyakataa na kuyakemea matendo ya giza. 

Simameni kidete dhidi ya upofu wa maadili na utu wema.
Simameni kidete dhidi ya upofu wa maadili na utu wema.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo na kupata ufafanuzi wake, nawaalika sasa tuingie katika tafakari yake fupi kuona kati ya mengi ambayo masomo ya leo yametupatia, tunaweza kuchota lipi. Ninaguswa kutafakari nawe ujumbe wa Mtume Paulo tulioupokea katika somo la pili, ujumbe unaozungumzia wito wetu wakristo, wito wa kuyakemea matendo ya giza. Paulo ambaye katika mausia kama haya mara nyingi amekuwa anayataja matendo maovu kwa jina, leo hayataji. Anasema yapo yanayotendeka ambayo ni aibu hata kuyanena. Hayataji kwa sababu uovu ni uovu; na kwa asili mwanadamu ameumbwa na akili na utashi wa kutambua lililo jema la kufuata na lilio baya la kuepuka. Na utambuzi huu unazidi kukua pale mwanadamu anapoupokea ufunuo wa Mwenyezi Mungu. Agizo hili la Mtume Paulo ni muhimu sana kwetu wakristo hasa katika kipindi hiki ambacho mwanadamu anaonekana kuweka pembeni uwezo wake wa asili wa kutambua jema na baya na tena kuupuuzia ufunuo wa Mwenyezi Mungu na kujiweka yeye kuwa kipimo cha kuamua lipi ni jema na lipi ni baya. Na kwa bahati mbaya zaidi hakomei hapo, anaanza kuchochea kuwa lile lililo ovu lipokelewe na jamii nzima, lishabikiwe na lihimizwe. Uovu ni uovu. Lililo ovu ndani ya dhamiri na machoni pa Mwenyezi Mungu haliwezi kugeuga kuwa jema kwa kupigiwa kura au kwa ithibati ya kisayansi au kwa maamuzi ya wengi.  Mtume Paulo leo anatuambia “amka wewe usinziae”. Pokea dhamana ya wito wako wa Ukristo, uyakimbie matendo ya giza na uyakemee. Na anahitimisha kwa kusema “na Kristo atakuangaza.” 

Liturujia D4 Kwaresima
17 March 2023, 16:32