Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa, waamini wanaalikwa kutafakari Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu; Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa, waamini wanaalikwa kutafakari Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu;   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Dominika ya IV Kwaresima: Fumbo la Mateso Katika Maisha ya Mwanadamu!

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa, waamini wanaalikwa kutafakari Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu; upofu wa maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu, kazi ya uumbaji, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili inayosimikwa katika uchaji, ibada na udumifu tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Waamini wawe kweli ni mashuhuda wa ukuu na utukufu wa Mungu maishani mwao

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli) – Italia.

Katika Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameganga na kuponya dhambi za binadamu; akamhurumia na hatimaye, kumkirimia maisha mapya. Kristo Yesu amegeuza hofu, taabu, mahangaiko na mashaka ya binadamu kuwa ni chemchemi ya imani, mapendo na matumaini. Pasaka ni ufunuo wa mapenzi mema ya Mungu kwa binadamu! Hii ni kwa sababu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni tukio la kihistoria na wala “si mambo ya kufikirika wala Hekaya za Abunuwasi”. Ndiyo maana baada ya ufufuko wa Kristo Yesu, waamini wanaambiwa “Msiogope.” Liturujia ya neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa, waamini wanaalikwa kutafakari Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu; upofu wa maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu, kazi ya uumbaji, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili inayosimikwa katika uchaji, ibada na udumifu tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. SOMO LA KWANZA: 1 Sam 16:1b, 6-7, 10-13°. Somo letu la kwanza linatufikishia ujumbe kuwa “Mungu humchagua yoyote anayemtaka kwa kazi yake na hivyo kila mmoja anayo nafasi katika mpango wa Mungu.” Baada mfalme Sauli kuasi na kukiuka matakwa ya Mungu (rejea 1Sam 15:10-35), Mungu alimtuma Samweli katika nyumba ya Yese ili kumpaka mafuta Daudi kuwa mfalme. Hata hivyo kwa vigezo vya kibinadamu Daudi anaonekana “kutostahili kuwa mfalme” maana Samweli aliyetumwa kuchagua mfalme katika wana wa Yese alijikita zaidi kuangalia vigezo vya nje nje tu: uzuri wa sura pamoja na marefu na mapana ya mtu- mwonekano wa nje wa mtu. Hata Yese mwenyewe hakuwa na wazo la kumleta mtoto wake mdogo wa nane (yaani Daudi) ambaye alikuwa ameenda kuchunga kondoo. Yawezekana hakumleta Daudi kwa sababu aliona ya kuwa bado ni kijana mdogo sana, hivyo kwa vyovyote vile asingestahili kupakwa mafuta ili awe mfalme. Na zaidi yupo huko kondeni akichunga kondoo, kazi iliyofanywa na watu duni.

Mwenyezi Mungu anaangalia moyo wa mwanadamu!
Mwenyezi Mungu anaangalia moyo wa mwanadamu!

Samweli na Yese walitumia macho na vigezo vya kibinadamu na hivyo kuona Daudi hastahili kupakwa mafuta na kuwa mfalme. Hata hivyo, Mungu atajichagulia Daudi, ambaye mwanzoni hakufikiriwa kabisa maana alionekana kutokidhi vigezo vyao. Yule ambaye hakidhi vigezo vya kibinadamu, ndiye ambaye anakidhi vigezo vya Mungu maana “wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.” Hivyo Samweli na Yese walikuwa vipofu (upofu wa roho) maana hawakuweza kuona mpango wa Mungu ndani ya Daudi, hawakujua kuwa Mungu ana mpango wa kumleta Masiha kupitia ukoo wa Daudi, hawakujua ya Daudi, mchungaji wa kondoo, ameteuliwa kuwa mchungaji wa kondoo wa Mungu (taifa la Israeli) kwamba kuchunga kondoo ilikuwa ni fursa kwa Daudi kujifunza uongozi wa kundi la Waisraeli. Ama kweli macho ya Mungu siyo macho ya wanadamu. Upofu wao uliwafanya kuona tu mambo ya nje nje tu badala ya kutazama kwa undani zaidi. Hata hivyo kwa kumchagua Daudi Mungu anafungua macho yao (anawaponya upofu wao wa kiroho). Kuna msemo usemao “umdhaniaye siye, ndiye; umdhaniaye ndiye, siye.” Hata sisi tunasumbuliwa na mambo wawili: kwanza, tunayo hulka ya kufikiri watu wanafaa kwa kazi fulani kwa sababu tu ya vigezo vionekanavyo kwa nje nje tu (ongea yake, utajiri wake, uzuri wake, kazi yake, elimu yake na mengineyo); Pili, tunayo hulka ya kuwapuuza na kuwadharau watu na kuwaona hawafai kwa sababu tu tumetazama vigezo vya nje nje tu (vaa yake, umri wake mdogo, elimu yake ndogo, uwezo wake mdogo, kazi yake duni na mengineyo) badala ya kuingia ndani zaidi na kutambua kwamba kila mtu anaweza kutumika kwa kadiri ya mpango wa Mungu licha ya mapungufu yake aliyonayo kwa kadiri ya mwono wetu wa kibinadamu. Matatizo haya mawili hutufanya kuwa vipofu: kushindwa kuona mema ya wengine, kushindwa kuona thamani aliyonayo kila mtu mbele ya Mungu na ya kwamba Mungu humchagua yeyote anayemtaka kwa kazi yake. Sisi tunatazama sifa za nje tu lakini Mungu hutazama sifa za ndani. Tunapaswa kuruhusu Mungu/Kristo atuponye upofu huu wa kiroho tulionao kama alivyomponya mtu ayelizaliwa kipofu katika Injili yetu ya leo.

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha

SOMO LA PILI: Efe. 5:8-14: Yesu ambaye ni nuru ya ulimwengu amekuja ili tusiendelee kuishi gizani bali kuishi katika nuru. Huu ndio ujumbe ambao Mtume Paulo anawafikishia Waefeso na sisi sote ambao tumempokea Kristo aliye nuru ya ulimwengu. Lakini je, nini kitakachodhihirisha kwamba sisi ni watoto wa nuru? Ni matendo yetu: wema, haki na kweli. Haya anayozungumzia Paulo ndiyo nguzo za maisha ya Kikristo. Ikiwa maisha yetu ya Kikristo hayadhihirishi wema, haki na kweli, basi tuwe na uhakika kuwa bado tupo gizani, bado tupo usingizini. Tutende haki: tuache dhuluma, tusipindishe haki ili kuwakandamiza wanyonge; tusimamie ukweli bila kuogopa macho na maneno ya watu maana ukweli utatuweka huru na tutendeane wema: tusaidiane, tutakiane mema na tujali mahitaji ya wengine. SOMO LA INJILI: Yn. 9:1-41: Katika Injili tunasikia simulizi la kuponywa kwa mtu aliyezaliwa kipofu. Katika tukio hili la uponyaji wa kipofu Yesu anatumia tope. Mara nyingi katika Injili tunamwona Yesu akiponya kwa kutumia neno lake tu. Hata hivyo katika Injili ya leo tunamwona Yesu akimponya kipofu tangu kuzaliwa kwa kutumia tope: Yesu anatengeneza tope kwa kutumia mate na kumpaka kipofu machoni. Kwa kawaida tope hutengenezwa kwa kuchanganya maji na udongo (Yesu kwa upande wake anatema mate chini kwenye udongo na kutengeneza tope, anachanganya mate na udongo). Tukitaka kuelewa kwa nini Yesu alitumia tope basi yatupasa kurudi kwenye simulizi la uumbaji, hasa Mwanzo 2:7: “Basi, Mwenyezi Mungu akamuumba mwanaume kwa mavumbi ya udongo.” Kama ambavyo Mungu alimuumba mtu kwa tope (kwa udongo), Yesu naye anatumia tope kuonesha kuwa anamuumba upya huyu kipofu- anamuumba upya kiroho ili awe kiumbe kipya. Sisi nasi tuna upofu wa roho. Mungu yupo tayari kutuumba upya na kutufanya kuwa viumbe vipya kwa nguvu ya Roho wake Mtakatifu.

Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu!
Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu!

Kutoka katika Injili ya leo tunachota mafundisho yafuatayo: (1) Yesu ni nuru ya ulimwengu, amekuja ili tupate nuru. Tukio la kuponywa kwa kipofu lina matukio makubwa mawili ndani yake: tukio la kuponywa upofu wa macho ya kawaida na tukio la kuponywa kwa upofu wa kiroho. Yaani mtu huyu alikuwa na upofu wa aina mbili: upofu katika macho yake ya kibaiolojia na upofu wa roho. Tukisoma tu kwa haraka haraka tutaishia kuona uponyaji wa ugonjwa wa upofu wa macho ya kawaida. Hata hivyo tukisoma kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu tutagundua kuwa mtu huyu alikuwa pia na upofu wa roho: upofu wa kushindwa kumtambua Kristo. Upofu wa kiroho ulimpelekea mtu huyu kumtambua Yesu kama “mtu tu wa kawaida kama watu wengine.” Anapoulizwa: Macho yako yalifumbuliwaje? Yeye alijibu: Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona. Kwa sababu alikuwa kipofu wa roho aliishia kumwona Yesu kama mtu tu wa kawaida kama wengine: “mtu yule aitwaye Yesu…” Lakini Yesu hatua kwa hatua anamponya upofu wa roho ambao unampelekea kumtambua Yesu hatua kwa hatua: kutoka hatua ya kumuona Yesu kama mtu wa kawaida hadi kufikia kiwango cha kumtambua Yesu kama Nabii, baadaye Mtu wa Mungu na mwishoni Bwana na kisha anamsujudia. Kristo anayafungua macho ya kiroho ya mtu kipofu hatua kwa hatua: kumjua Mungu siyo shughuli ya siku moja au ya muda fulani bali ni shughuli endelevu inayokuja hatua kwa hatua. Tusibaki katika hatua moja tu bali tumruhusu Mungu taratibu hatua kwa hatua ajifunue kwetu. Na wala tusiwe na haraka ya kutaka kuyaelewa mafundisho yote ya imani kwa mkupuo mmoja.  Tunaporuhusu nguvu ya Yesu ifanye kazi ndani yetu tunaponywa upofu wa roho: upofu wa kushindwa kumwona Yesu aliye Mwana wa Mungu.

Kristo Yesu aguse na kuponya upofu wa maadili na utu wema
Kristo Yesu aguse na kuponya upofu wa maadili na utu wema

Ni upofu wa roho unatusababisha kushindwa kuona nguvu ya Mungu na hivyo kukimbilia nguvu za wanadamu; ni upofu wa roho unatusababisha kushindwa kuona utu na thamani ya wengine na hivyo kuwalinganisha na vitu; ni upofu wa roho unaotusababishia kushindwa kuona mateso na mahangaiko ya wenzetu. Wakati kipofu huyu akiponywa upofu wake wa roho, Mafarisayo waliendelea kubaki katika upofu wao wa roho: walishindwa kumtambua Yesu kama Mwana wa Mungu. Kristo aliye nuru ya ulimwengu ayafumbue macho yetu ili yapate kumtambua katika uhalisia wake. (2) Tunapaswa kuitetea imani yetu kwa uthabiti, bila uwoga na kwa hoja za kiimani. Tofauti na wazazi wake ambao walijibu mambo kirahisi kwa hofu ya Wayahudi, aliyeponywa upofu alikuwa thabiti katika kutetea kile alichoshuhudia juu yake. Aliweza kupangua hoja kwa hoja, tena bila kuogopa Mafarisayo. Ni lazima nasi kukabiliana na hoja dhaifu za kiimani kwa hoja nzito za kiimani bila uwoga. Wakatoliki tunashtumiwa kuwa tu waoga wa kutetea imani yetu kwa hoja. Inawezekana kuna ukweli ndani yake. Inawezekana kwa sababu ya kukosa uthubutu au kwa sababu hatujataka kuichimba zaidi imani yetu ili kuweza kujenga hoja nzito na dhahiri. Hata sisi kuna wakati tunakosa uthabiti wa kutetea imani yetu kama wazazi wa kipofu kwa kuogopa hoja, vitisho na maneno ya wapinzani wetu. Na tena kuna wakati tunaacha kujibu hoja na tunaanza kushambulia mtu. Tusiwe wepesi wa kukwepa hoja kama Mafarisayo ambao walipozidiwa “waliacha kujadili hoja na wakaanza kujadili mtu” (badala ya kuishambulia hoja wanaanza kumshambulia mtoa-hoja kwa kutafuta madhaifu yake ili hoja yake ionekane dhaifu): “Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe watufundisha sisi?”

Kristo Yesu awe ni dira na mwongozo wa maisha adili
Kristo Yesu awe ni dira na mwongozo wa maisha adili

Haya yote yalikuwa ni visingizio baada ya kuona wanaambiwa ukweli na hawana hoja ya kujibu. Ni hulka ya mwanadamu kukataa ukweli na badala yake huanza kumchambua mtoa-hoja. Mtume Petro anasema, “Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu” (1 Pet. 3:15). Hata hivyo ili kuweza kutetea imani yetu kwa uthabiti tunahitaji kuichimba na kuifahamu imani yetu kwa kina huku tukisaidiwa na neema ya Mungu. (3) Tunapaswa kuondokana na imani na mawazo potofu. Wayahudi waliamini kuwa mtu akiwa na mapungufu yoyote katika mwili wake basi ni kwa sababu amepewa adhabu na Mungu baada ya ama yeye mwenyewe au wazazi wake kutenda dhambi (rejea kutoka 20:5). Kwa kadiri ya mtazamo wao, “ulemavu wowote” ni laana kutoka kwa Mungu. Bado baadhi yetu tuna mawazo na imani kama hawa Wayahudi. Ni imani potofu, ujinga na ushamba kufikiri kuwa mtoto akizaliwa na ulemavu wa viungo au ulemavu wa ngozi ni laana ama mtoto akitanguliza miguu badala ya kichwa wakati wa kuzaliwa basi ni laana, na ati mtu akizaa watoto mapacha ni laana tu. Tunapaswa kuondoa mawazo haya potofu na ya kijinga. Kwa nini mtu anazaliwa na mapungufu au ulemavu au magonjwa? Jibu la Yesu li wazi: “ili kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake,” yaani kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Tukijua kwa dhati ukweli huu tutaimba kwa furaha na matumaini antifona ya mwanzo: “Furahi, ee Yerusalemu, na mkusanyike, ninyi nyote mmpendao. Furahini kwa furaha, ninyi nyote mliokuwa na huzuni, mpate kushangilia, na kushibishwa kwa utamu wa faraja zake.”

18 March 2023, 09:15