Tafuta

2023.03.05 Vipaumbele muhimu kwa bara la Afrika vilivyotokana na majadiliano ya awamu ya kibara huko Addis Ababa, Ethiopia 2023.03.05 Vipaumbele muhimu kwa bara la Afrika vilivyotokana na majadiliano ya awamu ya kibara huko Addis Ababa, Ethiopia 

Sinodi:Kanisa la Kisinodi katika umoja na utofauti wake,utajiri wa familia ya Mungu

Wajumbe wa Maadhimisho ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu Ukanda wa Afrika, Ijumaa na Jumamosi wakiwa wamekusanyika katika makundi 15 wamesali na kutafakari na hatimaye wakaibuka na vipaumbele 15 vya Kanisa Barani Afrika.Baada ya tafakari ya kina,vipaumbele hivyo vikapembuliwa kwa makini na hatimaye kubaki vipaumbele 8.

Na Padre Richard A. Mjigwa,C.PP.S., – Addid Ababa.

Kama familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani, utawala bora na kwamba, rasilimali za Afrika ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Afrika. Tunu msingi za maisha ya Kiafrika hazina budi kupewa uzito unaostahili katika nyaraka na mafundisho ya Kanisa hususan, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, umoja na mshikamano, ukarimu, majadiliano na uwajibikaji wa pamoja. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi hauna budi kusimikwa katika utamadunisho, liturujia na ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Kanuni auni, ushirika na umoja wa watu wa Mungu.

Wakati wa Misa takatifu Jumamosi 4 Machi 2023 huko Addis Ababa
Wakati wa Misa takatifu Jumamosi 4 Machi 2023 huko Addis Ababa

Kanisa la Kisinodi liwahusishe na kuwashirikisha watu wote wa Mungu bila ubaguzi. Malezi na majiundo ya awali na endelevu kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha ya utume wa Kanisa, ili kujenga miundo mbinu itakayoliwezesha Kanisa Barani Afrika kutembea bega kwa bega na kwa ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.  Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi hauna budi kufumbatwa katika tunu msingi za maisha ya watu wa Mungu: Uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Haki ya tabianchi, ni changamoto inayohitaji wongofu wa ikolojia unaopaswa kumwilishwa katika maisha na utumje wa Kanisa. Kuna haja ya kukuza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kuhusu ndoa na familia pamoja na kuangalia changanoito zake, ili kuzipatia suluhu ya kudumu katika mwanga wa tunu msingi za Kiinjili  na utu wema.

Washiriki wa Mkutano wa Sinodi huko Addis Ababa
Washiriki wa Mkutano wa Sinodi huko Addis Ababa

Wajumbe wa maadhimisho ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu Kanda ya Bara la Afrika, Jumamosi tarehe 4 Machi 2023 wameshiriki katika Ibada ya Liturujia Takatifu katika Madhehebu ya Kiithiopia, iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Kuzaliwa Bwana, iliyoongozwa na Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa, Ethiopia. Hii ni ibada iliyokuwa na ushiriki mkubwa wa waamini katika kuimba na kuitikia sala mbalimbali kwa njia ya nyimbo na tenzi za rohoni. Liturujia ya Neno la Mungu imeadhjimishwa kwa ibada na uchaji mkubwa, kwa kukazia umoja, ushiriki na utume wa Kanisa. Katika mahubiri yake, Askofu Musie Ghebrerachiorghis wa Jimbo la Emdibir, amekazia umoja na utofauti kama amana na utajiri wa familia ya Mungu Barani Afrika kama unavyoshuhudiwa katika ibada na madhehebu, mila, desturi na tamaduni mbalimbali Barani Afrika, lakini wote wanaunda na kujenga familia ya Mungu inayowajibikiana. Kanisa Barani Afrika bado ni hain a lina nguvu sana.

Washiriki wa Sinodi walei na watu wa dini pamoja huko Addis Ababa
Washiriki wa Sinodi walei na watu wa dini pamoja huko Addis Ababa

Kumbe Kanisa halina budi kuendelea kujikita katika mchakato wa utamadunisho na uinjilishaji na kamwe familia ya Mungu Barani Afrika isikubali kuyumbishwa na hatimaye kukengeuka kwa madai ya demokrasia na utandawazi usiokuwa na mvuto wa mashiko kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Tunu msingi za maisha ya watu wa Mungu Barani Afrika ziwasaidie waamini kuwajibika barabara kadiri ya miito yao na nyajibu walizojitwalia kwa Sakramenti ya Ubatizo: Ukuhani; Unabii na Ufalme, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa ndani na nje ya Bara la Afrika. Ahadi za Ubatizo, ziwawezeshe waamini kukabiliana na shida, matatizo, changamoto na fursa zinazojitokeza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi kati ya hizi ni: Ukosefu wa haki, amani na maridhiano kati ya watu; Ujinga, umaskini na maradhi. Ukabila, udini na misimamo mikali ya kidini na kisiasa: Uchoyo, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Kikundi kikijadili masuala ya mkutrano huko Addis Ababa
Kikundi kikijadili masuala ya mkutrano huko Addis Ababa

Kumekuwepo na vitendo vya kigaidi vinavyohirishia amani, usalama na mafungano ya watu mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika. Watu wa Mungu Barani Afrika wanahimizwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, maridhiano na mnajadiliano katika ukweli na wazi. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hata wakristo ni wadau wakubwa katika uvunjaji wa misingi ya haki, amani na utawala bora. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi uwawezeshe waamini kuwa na mwelekeo mpya, tayari kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili na utu wema. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ujitahidi kutoa majibu muafaka kwa changamoto mbalimbali zinazoibuliwa na Familia ya Mungu Barani Afrika.

Sinodi ya Kibara huko Addis Ababa
Sinodi ya Kibara huko Addis Ababa

Maadhimisho ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu yanaadhimishwa katika kipindi hiki cha Kwaresima, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa kujizatitiZaidi katika maisha ya sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Kufunga na kumwilisha sadaka na majitoleo hayo katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wongofu wa ndani usaidie ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho. Maadhimisho haya yajenge umoja, ushiriki na utume wa familia ya Mungu Barani Afrika. Mwishoni mwa Ibada hii iliyoshuhudia ushiriki mkamilifu na ibada ya watu wa Mungu nchini Ethiopia, Makardinali wote walioshiriki walitoa baraka zao za kitume kwa watu wa Mungu Barani Afrika, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwakirimia waja wake amani ya kudumu.

05 March 2023, 12:06