Tafuta

2023.03.02 Hatua ya kibara ya Sinodi Barani Afrika inayofanyika nchini Ethiopia. 2023.03.02 Hatua ya kibara ya Sinodi Barani Afrika inayofanyika nchini Ethiopia. 

Sinodi,Afrika:Ni wakati wa kushirikiana na kushikamana kwa Kanisa la Afrika

Wakristo Barani Afrika wajitahidi kupanua hema ya ushiriki wa watu wa Mungu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu,kwa ari na moyo mkuu.Ni kutoka katika hotuba za utangulizi tarehe 2 Machi 2023 katika uzinduzi wa Sinodi awamu ya II ya kibara huko Addis Ababa,Ethiopia. Afrika,ithamini maisha ya sala na utambuzi wa waamini walei.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Addid Ababa.

Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika Sala, kusikiliza, kung’amua na kutekeleza kwa Pamoja. Hii ni sala inayoliwezesha Kanisa kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na ikolojia fungamani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa la Kisinodi linajikita katika wongofu wa kisinodi wenye mwelekeo wa kimisionari, kwa kusikilizana na kutembea Pamoja kama watu watakatifu na wateule wa Mungu Barani Afrika. Huu ni utangulizi uliotolewa Alhamisi tarehe 2 Machi 2023 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya uzinduzi wa maadhimishi ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu inayoongozwa na kauli mbiu: Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushirikina Utume na Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, mjini Addis Ababa kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho ya Sinodi Barani Afrika.

Makundi yakijadiliana baada ya hotuba ya ufunguzi wa Sinodi barani Afrika
Makundi yakijadiliana baada ya hotuba ya ufunguzi wa Sinodi barani Afrika

Kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kuna haja kwa waamini kujikita katika mchakato wa ukweli na awaze, ili kujenga umoja wa Watoto wa Mungu, wanaoshiriki kikamilifu katika Maisha na utume wa Kanisa. Tayari kwa upande   wake Kardinali Jean Claude Hollerich, Mwezeshaji mkuu wa Sinodi ya 16 ya Maaskofu alikuwa asema, huu ni mwaliko wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko wa kumwomba Roho Mtakatifu ili aliwezeshe Kanisa kujizatiti katika kusimamia, haki, amani na ikolojia fungamani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni ulimwengu ambao unaendelea kushuhudia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Baadhi ya watoa mada katika sinodi ya kibara huko Ethipia
Baadhi ya watoa mada katika sinodi ya kibara huko Ethipia

Kumbe, Mama Kanisa hana budi kutioa majibu muafaka yanayosadifu na kukata kiu cha watu wa Karne ya Ishirini na moja kwa kuzama katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho. Kanisa Barani Afrika halina budi kubaini vipaumbele vya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo, kwa kuzingatia tunu msingi za Maisha ya watu wa Munhgu Barani Afrika. Huu ni wakati wa wongofu wa kisinodi na kimisionari unaoratibiwa na kusimamiwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Ni katika muktadha huu, Kanisa halina budi kujitambulisha kama Kanisa linalo Sali na limesimikwa katika maongozi ya Roho Mtakatifu. Bila Roho Mtakatifu, maadhimisho ya Sinodi yatageuka na kuwa ni majadiliano ya kisiasa kwa kuvutana ili kupata mshindi, kati ya waafidhina na wasiopenda mabadiliko ndani ya Kanisa.

Kwa upande wake Padre Rafael Simbine anasema, Maadhimisho haya ni kwa ajili ya kuandaa Hati ya Kanisa la Bara la Afrika, itakayochangia katika maandalizi ya Hati ya Kitendea Kazi, (Intrumentum Laboris) kwa ajili ya Mkutano wa Sinodi ya 16 ya Maaskofu itakayoadhimishwa mwezi Oktoba 2023 kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Hiki ni kipindi cha kuomba maongozi ya Roho Mtakatifu, Kusali na Kumsikiliza Roho Mtakatifu anasema nini kwa Kanisa la Bara la Afrika. Ni wakati wa kushirikiana na kushikamana, kama kielelezo cha kukua na kukomaa kwa Kanisa Baran Afrika kwa kutambua vipaumbele vya maisha na utume wake Barani Afrika, kwa kuthamini maisha ya sala na utambuzi wa waamini walei kama wadau katika uinjilishaji. Hii ni Sinodi ya kusherehekea Imani, ari na mwamko wa kimisionari tayari  kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu.

Washiriki wa Mkutano wa Sinodi barani Afrika
Washiriki wa Mkutano wa Sinodi barani Afrika

Askofu Lucio Muandula, Makamu wa kwanza wa Rais, SECAM, katika hotuba yake ya ufunguzi amebainisha safari ya Kisinodi iliyoanzishwa kunako mwaka 2021 kwa kuwashirikisha watu wa Mungu kuanzia kwenye Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na sasa imefikia katika awamu ya Kibara na hatima yake ni Mwezi Oktoba 2023 tayari kuandaa Hati ya Kitendea Kazi (Instrumnentum Laboris). Ni wakati muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu ili kupata maana iliyokusudiwa ya maadhimishoi ya Sinodi ingawa kwa waafrika wengi, tayari kuna miundombinu ya Kisinodi. Huu ni wakati wa kumsikiliza Roho Mtakatifu pamoja na waamini kutembea kwa pamoja huku wakiheshimiana na kuthaminiana, tayari kushiriki kazi na utume wa Uinjilishaji na uwajibikaji ndani na nje ya Bara la Afrika. Mang’amuzi ya Kisinodi yalisaidie Kanisa Barani Afrika kujenga utamaduni wa kusikiliza na kutenda kwa ukarimu katika: Sala, Liturujia na Maisha ya kila siku ya waamini, ili hatimaye kutangaza na kushuhudia Habari njema ya wokovu.

Padre Giacomo Costa, SJ. amelitaka Kanisa la Afrika kujikita katika mchakato wa kusikiliza kwa makini, kujifunza kutoka kwa watu wa Mungu, kugusa amana na utajiri pamoja na tunu msingi za maisha ya Kanisa. Ni wakati wa kutembea kwa pamoja kama Watoto wa Kanisa, kujifunza na kushirikiana tayari kujenga utamaduni wa majadiliano ya maisha ya kiroho, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalokita mizizi na utume wake katika wongofu na majadiliano,m kwa kufikiri na kutenda kwa umoja na ushiriki mkamilifu swa Watoto wote wa Mungu. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau, wakristo wajifunze kutoka kwa Kristo Yesu, ili kutafasiri matukio mbalimbali kwa mwanga wa Maandiko Matakatifu, tayari kusimulia na kushuhudia Injili, tayari kujikita katika wongofu wa kimisionari.

Ni wakati wa ujenzi wa utamaduni nwa kusikiliza, kung’amua na kutenda kwa mwanga wa Roho Mtakatifu. Ni jambo la muhimu kwa waamini kukazia kwa namna ya pekee maisha ya sala, tafakari na ukimya, kushirikishana na hatimaye kwa pamoja kutambua vipaumbele vinavyopaswa kufanyiwa kazi katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisan la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume unawaowahamasisha wakristo  kutambua dhamana na wito wao unaowashirikisha: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo Yesu. Wakristo Barani Afrika wajitahidi kupanua hema ya ushiriki wa watu wa Mungu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa ari na moyo mkuu.

Ufunguzi wa Sinodi huko Addis Ababa
02 March 2023, 17:15