Sinodi huko Suva-Fiji imehitimishwa na uhakika wa kusikilizwa kilio cha dunia
Na Angella Rwezaula;- Vatican.
Ni kwa Juma zima walisindikizwa na tafakari ya maombi na utambuzi kuhusu mwitikio wao kama maaskofu wa Bara huku wakisaidiwa na Hati kitendea Kazi ya Hatua ya Bara ya Sinodi. Ni kwa mujibu wa mwakilishi wetu wa Vatican News, Sr Bernadette M. Reis, fsp, aliyefuatilia Mkutano wa Kibara uliofunguliwa Dominika tarehe 5 Februari kwa washiriki ambao waliwalikisha Mabaraza ya Maaskofu wa Australia, New Zealand, Papua New Guinea na Visiwa vya Solomon pamoja na visiwa vya Pasifiki ambao umehitimishwa Ijumaa tarehe 10 Februari 2023 huko kisiwa cha Suva- Viji. Kwa mujibu wake alibanisha kwamba kwa hakika wazungumzaji mbalimbali na kundi la wataalimungu walitoa michango yao mikubwa kuhusu mada tatu zilizoainishwa kwa ajili ya kutafakari kwa kina ambazo zilikuwa ni: “sinodi, utunzaji wa bahari na malezi kwa ajili ya utume”.
Katika makabiliano hayo wajumbe waliweza hata kuzunguka katika mazingira yao ya ndani na wakipitia liturujia mbili zilizojaa tamaduni na mila za Kifiji. Vile vile waliweza kufanya ziara kwenye mto wa ndani na njia ya bahari ambazo ziliruhusu wale walioshiriki kuona hata uharibifu uliofanywa dhidi ya asili, kupitia mazoezi ya uchimbaji na mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla. Pamoja na hayo pia washiriki walifurahia onesho la moja kwa moja lililojumuisha muziki, dansi na historia zinazosimulia tabia ya nchi zote za Bara hilo la Visiwa ambamo waweza kusikia kweli vilio vya watu wa visiwa hivyo wanamoishi na bahari.
Umuhimu wa kujaza mapungufu katika suala la wanawake
Katika mahojiano ya mwisho, na Askofu Mkuu Peter Loy Chong Mkuu Suva na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Pasifiki (CEPAC) lililokuwa mwenyeji wa Mkutano wa kibara alisema jinsi alivyofurahishwa na kuridhishwa na matokeo ya Mkutano huo. Yeye aliweza kuhisi nguvu katika mkutano huo na alitoa shukurani zake kwa Sekretarieti inayoundwa na walei wengi wao wakiwa ni wanawake ambao waliweza kuandaa na kufanikisha Mkutano huo. Akizungumzia kuhusu jibu la Hati ya Kitendea Kazi kwa Hatua ya Bara, Askofu Mkuu alibainisha kwamba maaskofu wa visiwa hivyo walitoa mchango wao na kujaza kile walichofikiri ni mapungufu. Pengo moja alilobainisha lilikuwa ni kuhusu wanawake na suala la jeuri za nyumbani, ambalo alithibitisha kuwa ni tatizo kubwa kwa visiwa vya Fiji na Papua New Guinea, lakini hata Australia.”
Sr. Nathalie:Roho Mtakatifu amevuma katika watu waliokusanyika Suva
Kwa upande wa Sr. Nathalie Becquart, Katibu Mkuu Msaidizi wa Sekretarieti ya Sinodi, alielezea Mkutano huo kama tukio zuri na la kina. Kwa upande wake alielezea alivyoguswa moyo aliposhuhudia Maaskofu wakitoa “sauti” kwa Kanisa katika sehemu hiyo ya dunia na roho yao ya umisionari. Kwa hiyo ,Sr Nathalie alisema kwamba hata hivyo Sinodi tayari imepachikwa kwa njia nyingi na alihisi Kanisa la visiwa hivyo kupitia uzoefu wake hapo na kwamba limesikiliza kwa kina sauti ya maskini, kilio cha dunia, kilio cha bahari na kilio cha watu wakati huo linajaribu kujibu wito huo wa Mungu kwa kuendelea kuwa Kanisa lililo karibu na watu katika muktadha huo, ili kusisitizia malezi kwa ajili ya utume na kuwa zaidi na zaidi Kanisa la Sinodi. Kiukweli alisema, inawezekana kutafakari kazi ya Roho kwamba inavuma juu ya bahari na kupitia mioyo ya watu waliokusanyika huko Suva.
Katika taarifa yao iliyotolewa Ijumaa tarehe 10 Februari 2023, wakati wa kuhitimisha Mkutano huo, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki wa Visiwa vya Australia walibainisha kuwa: “imekuwa ni furaha kubwa kwa Maaskofu wa wa Bara hili kukusanyika Fiji kwa Juma hili kwa ajili ya kusali na kuzingatia utume wetu wa pamoja, kama wachungaji Wakuu wa Kanda yetu. Kama tulivyowaombea watu wetu, tumekuwa tukifahamu maombi ambayo wamekuwa wakitoa kwa ajili ya kusanyiko letu na huduma yetu. Kusanyiko letu limetoa fursa kwetu kusali pamoja, kujenga uhusiano wa kidugu, kujifunza kutoka kwa mtu mwingine na kuzingatia changamoto za kawaida za kichungaji.”
Katika Mkutano huo wa Sinodi wa Juma moja ambao ulihitimishwa tarehe 10 Februari 2023 kwa kuadhimisha Misa Takatifu, wachungaji hao wa ndani hatimaye wametumwa kwa upya kwa ajili ya utume wa kimisionari katika maeneo yao yote ya visiwa vyao. Kutokana na hili ni matazamio yao ya kuwepo katika maadhimisho ya kikao cha kwanza cha Sinodi kitakachofanyika mwezi Oktoba 2023 mjini Vatican huku wakitambua kuwa sauti zao zimesikika!