Tafuta

Ujumbe wa Yohane Mbatizaji katika Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio unafupishwa kwa ujumbe wa kutubu na kubatizwa kwa kuwa ufalme wa mbinguni ukaribu. Ujumbe wa Yohane Mbatizaji katika Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio unafupishwa kwa ujumbe wa kutubu na kubatizwa kwa kuwa ufalme wa mbinguni ukaribu.  

Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa: Tubuni na Kubatizwa!

Ni Yohane Mbatizaji aliyekuwa sauti iliayo nyikani, akiwahubiria na kuwaalika Wayahudi kubadili maisha yao kwa maana ya kuenenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Aliwabatiza kwa kuwaalika kufanya toba na wongofu wa ndani. Mwinjili Mathayo leo anatuonesha jinsi Yohane Mbatizaji alivyokuwa mtu wa nidhamu kali katika maisha yake binafsi. Aliishi na kuhubiri jangwani. Tubuni!

Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.

Amani na Salama! Majilio ni kipindi cha kutoka katika ukale na kwenda jangwani, ili tuweze kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu! Mt. 3:1-12. Sehemu ya Injili ya leo tunakutana na Yohane Mbatizaji, ambaye habari zake tunazipata si tu katika Maandiko Matakatifu, bali hata kutoka kwa mwanahistoria Giuseppe Flavio anayetuambia kuwa alikuwa ni mtu mwema na mwenye hofu kubwa ya Mungu. Ni Yohane Mbatizaji aliyekuwa sauti iliayo nyikani, akiwahubiria na kuwaalika Wayahudi kubadili maisha yao kwa maana ya kuyanyoosha, ndio kuenenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Aliwabatiza kwa kuwaalika kufanya mabadiliko ya maisha yao, yaani toba na wongofu wa ndani. Hata Mwinjili Mathayo leo anatuonesha jinsi Yohane Mbatizaji alivyokuwa mtu wa nidhamu kali katika maisha yake binafsi. Aliishi na kuhubiri jangwani. Hivyo chakula chake kilikuwa ni kile cha kawaida kinachoweza kupatikana jangwani, na hata mavazi yale ni yale waliyovaa wachungaji waliokuwa wanabaki jangwani ili kuhimili mazingira magumu ya: joto, baridi na hata wanyama wakali wa nyikani. Kwa kifupi Yohane Mbatizaji ni kielelezo cha jinsi tunavyopaswa kujiandaa kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni mwaliko wa kuishi kwa tahadhari kuu na hasa kutualika nasi kuishi maisha ya kiasi. Kutoka katika maisha ya anasa na starehe ili tuweze kwenda jangwani kuweza kuisikia sauti ya Mungu. Jangwani ni mahali pa kujitenga na anasa na starehe za dunia, lakini hasa ni mahali pa kuingia ndani ili tuweze kuisikia sauti ya Mungu, ili tuweze kukutana na Mungu.

Ingieni katika jangwa la maisha ya kiroho, ili mpate kutubu na kuongoka
Ingieni katika jangwa la maisha ya kiroho, ili mpate kutubu na kuongoka

Ujumbe wa Yohane Mbatizaji katika Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio unafupishwa kwa ujumbe wa kutubu na kubatizwa kwa kuwa ufalme wa mbinguni ukaribu. Ni shime kubwa kwa waliomsikiliza Yohane Mbatizaji kiasi cha kuwafanya kutoka katika nchi ile ya ahadi na kurejea tena jangwani, maisha waliyopitia babu zao. Ndio mwaliko wa kipindi cha Majilio, kwani ni Kairos, ili nasi leo tuweze kuishi tena maisha na hali ile ya kumngojea Mwokozi. Ni kipindi cha kufanya mabadiliko ya kweli ya maisha yetu, yaani metanoia. Kufikiri na kuenenda sio kwa mantiki zetu bali kwa ile ya Mungu mwenyewe itokanayo na Neno lake kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu. Jangwani ni sehemu ya ukiwa na ukimya mkuu ili kila mmoja aweze kufikiwa na ile sauti ya Mungu. Ni mahali pakuweza kila mmoja wetu kuingia ndani mwake na kubaki na Mungu pekee. Leo tunaishi katika ulimwengu wenye kelele za kila aina, ila kwa kipindi hiki cha majilio ni fursa tena nyingine ya kwenda jangwani. Kwa nini Yohane Mbatizaji anakuwa ni sauti inayolia nyikani, kwa nini jangwani? Ni swali tunaloweza kujiuliza hata nasi leo, kwa nini niwe sauti ya Mungu iliayo nyikani? Ulimwengu wetu ndio nyika na jangwa ambalo tunaalikwa kwenda kuwa sauti ya Mungu ili watu wote wapate kukutana na Mungu, ni jangwa mahali pale ambapo bado hakuna uwepo wa Mungu, hakuwa imani ya kumkiri Mungu. Hivyo, Majilio ni mwaliko wa kila mmoja wetu kutoka na kwenda jangwani, ili kuwa sauti ya Mungu kama Yohane Mbatizaji

Wanawaisraeli walisafiri jangwani kwa muda wa miaka 40, ndio kusema muda mrefu, ni lengo na shabaha ya Mungu kutumia muda huo mrefu ili awaunde na kutengeza kuwa wana na Taifa lake teule ili kwa njia yao watu wa mataifa mengine yote waweze kumjua Mungu. Jangwani ni kipindi cha maandalizi na matayarisho ya kuwa Taifa moja chini ya maongozi ya Mungu pekee. Jangwani pia ni mahali ambapo huwezi kuweka makazi au makao ya kudumu, ni sehemu ya mpito, hivyo kubaki na mambo ya msingi tu tunayoyahitaji kwa maisha yetu. Leo tunaishi katika ulimwengu wa kumiliki na kukumbatia kila aina ya mali na utajiri wa ulimwengu huu. Sisi rafiki zake Kristo tunaalikwa kurejea jangwani, kuishi kwa yale ya msingi na kutojilimbikizia mali na utajiri bali kutumia yote tunayojaliwa kwa upendo kwa wengine wanaosafiri pamoja nasi. Hivyo, Majilio ni mwaliko wa kuangalia tena aina ya maisha yetu mintarafu vitu na mali. Je, sisi ni watumwa wa mali na vitu? Kama ndio basi tunaalikwa kurejea jangwani, kujiona hapa duniani sisi ni mahujaji na wasafiri. Jangwani ni mahali ambapo tunaalikwa kuungana ili kusafiri kwa pamoja. Ni mahali ambapo kila mmoja wetu anamjali mwingine na kuona fahari kubaki katika muungano na mshikamano wa upendo na mwingine. Maisha ya Kikristo utambulisho wake ni katika upendo wa kweli kwa Mungu na kwa jirani. Mahtama Gandhi alipowaangalia Wakristo alipenda kusema: “Kama wangeliishi kweli Injili, basi nami ningejiunga nao.”

Toba na wongofu wa ndani; kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu
Toba na wongofu wa ndani; kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu

Ni mwaliko wa Majilio wa kuwa ni mashuhuda wa Injili sio tu kwa maneno yetu bali zaidi sana kwa matendo na ushahidi wa maisha yetu ya siku kwa siku. Hakika ni kwa maisha yetu zaidi tunaweza kumtangaza Kristo kuliko maneno yetu. Mwanafalsafa Jacque Maritain katika kujenga hoja za Kifalsafa juu ya uwepo wa Mungu alisema: “Mkristo wa kweli! Huyo ni hoja ya uthibitisho juu ya uwepo wa Mungu. Na matokeo yake Mkristo mbaya huyo ni uthibitisho wa hoja inayokinza uwepo wa Mungu” Ni wajibu wa kila mmoja wetu kama Mbatizwa kwenda kuwa Wainjilishaji, kuwa wapelekaji wa Habari Njema ya Wokovu, lakini hilo litafanikiwa ikiwa sisi wenyewe ni Habari Njema, ikiwa sisi wenyewe ni mifano mema na mizuri ya imani yetu. Na huu ndio wito na mwaliko wa kipindi hiki cha neema cha Majilio, kubadili maisha yetu ili yaweze kuakisi kweli za Injili. Ni katika muktadha huo wa kurejea tena jangwani pembeni mwa mto ule Yordani tunaona Yohane Mbatizaji anawaalika wasikilizaji wake kutubu na kubatizwa. Ni mwaliko wa kubadili maisha yao, na ndio kubadili vichwa, namna na jinsi zao za kufikiri. Wanatoka Yerusalemu na miji yote ya Yuda, ndio kusema wanatoka katika ardhi ile waliodhani wapo huru, ili warudi tena nyikani kuweza kupata uhuru wa kweli. Uhuru wa kweli ni katika kupokea toba na kubatizwa, ni katika kubadili vichwa na kukubali kuongozwa na sauti ya Mungu, yaani Neno lake.

Yohane Mbatizaji anawatambua Mafarisayo na Masadukayo kama uzao wa nyoka, kwa mafundisho na namna zao za maisha kuwa ni kinyume na mapenzi ya Mungu na Sura ya Mungu. Nao waliofika pale nyikani wanaalikwa kuzaa matunda yapasayo toba. Haitoshi kuwa wazaliwa wa Ibrahimu bali tunaalikwa sote kushiriki kuwa wana wa Mungu ndio kushiriki ufalme wa Mungu, kuwa wana wa ufalme huo. Yohane Mbatizaji anawachangamotisha kuona lililo la muhimu sio dini bali kuwa na imani ya kweli; na ndio changamoto hata ya nyakati zetu kwani mara nyingi tumepigania kuwa wenye dini na tusahau kuwa dini ya kweli inajengwa katika imani. Imani ndio kukutana na Mungu kwa nafasi ya kwanza, kuwa wajumbe wa Mungu na kujituma sisi wenyewe kupeleka mapenzi na mipango yetu, iwe vile ninataka mimi mambo yawe na sio kadiri ya Mungu. Ni wazi ni hoja ambayo itahitaji muda mwingine ili tuweze kuona tofauti bayana kati ya dini na imani. Ni hatari kuwa wenye dini bila imani! Lugha ya Kiapokalipsia inayotumika katika somo la Injili Dominika ya Pili yua Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa naomba ieleweke kuwa sio lengo na shabaha ya Mungu kumwangamiza mwanadamu. Naomba tuepuke kila mara tafsiri potofu za Neno la Mungu ambazo zinatupotosha kuiona Sura ya Mungu wa kweli. Ilikuwa ni lugha ya kawaida kwa nyakati zile za Yesu, na wasikilizaji walielewa aina ile ya uandishi na lugha, hivyo nasi leo ili kupata ujumbe kusudiwa hatuna budi kusaidiwa na wataalamu wa Maandiko Matakatifu, hivyo nawasihi tuepuke kila mara kutoa au kupokea tafsiri zinazokinzana na Sura ya Mungu.

Ubatizo wa Toba na Maondoleo ya Dhambi; Ubatizo wa Roho Mtakatifu
Ubatizo wa Toba na Maondoleo ya Dhambi; Ubatizo wa Roho Mtakatifu

Yohane Mbatizaji anawatahadharidha wasikilizaji wake juu ya ujio wa yule atakayebatiza si kwa maji bali kwa moto. Moto ni ishara inayotumika kuleta mwanzo mpya kwa kutekeza ulimwengu ule wa kale na mabaya yote, ni mwaliko wa mwanzo mpya katika ukamilifu wake. Ubatizo wa moto ndio unaotufanya sasa sisi kuwa viumbe vipya, kuweza kuondolewa dhambi zetu na kufanyika kweli wana wa Mungu. Si tu ishara ya nje bali ni ubatizo unaotuwezesha kuwa wapya kwa maana halisi. Moto pia ni ishara ya uwepo wa Mungu, ndio Ubatizo wa kweli ni kukutana na Mungu, ni kuingia katika mahusiano ya ndani na ya kirafiki na Mungu. Kama ambavyo wana wa Israeli walivyoalikwa kutoka katika nchi yao, hivyo nasi leo kila mmoja wetu anaalikwa kutoka katika hali na mtindo ule wa maisha tunaojisikia kuwa tupo huru na nyumbani ili tuweze kwenda jangwani na kuanza maisha mapya, maisha ya kuishi katika kumsikiliza Mungu, kubaki kuishi kwa yale ya msingi tu na si kujilimbikizia. Kuishi tukijua tupo njiani na safarini, tupo katika malezi na majiundo ili tuweze kuingia sasa nchi ile ya ahadi, nchi ya maziwa na asali, ndio katika ufalme wa Mungu tunaoalikwa kuuishi kila siku za maisha yetu. Yohane Mbatizaji anatuambia kuwa ufalme wa Mungu umekaribia, sio kwa maana kuwa upo mbali nasi bali tayari ukatikati yetu ndio kusema kumpokea Masiha na kukubali kila ovu na ubaya uondoke na kutosikika katikakati yetu.

Majilio ni kipindi cha kurudi Jangwani ili kujiaminisha kwa Mungu
Majilio ni kipindi cha kurudi Jangwani ili kujiaminisha kwa Mungu

Kuandaa njia ni wajibu wetu kwani kuna vingi vinavyotukwamisha kufanya safari ya kukutana na Mungu, kila mmoja wetu aingie ndani mwake na kuangalia ni nini kinachomzuia na kumkinza katika kupiga hatua katika safari yake ya kiroho. Kila mmoja wetu anaalikwa kusawazisha milima inayomzuia kusonga na kupiga hatua, na hata kushindwa kuona hatima ya safari yetu ya kiroho. Hakika katika maisha yetu tuna mengi yanayotukinza, yanayotukwamisha katika kusafiri kumwelekea Mungu. Hivyo ni hayo tunayoalikwa leo kuyaondoa na kuyasawazisha. Mwenyeheri Jakobo Alberione alipenda kusema: “Ni kwa yule tu asiye msafiri, huyo hahitaji kuuliza njia.” Sisi Wakristo ni wasafiri na mahujaji hivyo daima hatuna budi kujua njia ya kweli na sahihi ni ipi. Na ni Yesu anayetuambia kuwa ni Yeye ndiye njia, kweli na uzima. Ni Yesu aliye kweli Odos, yaani njia ya kutufikisha mbinguni. Hivyo Majilio ni mwaliko wa kurejea kwa pamoja kama Kanisa na kusafiri kwa pamoja katika Kristo aliye kweli, njia na uzima, ndio kuwa Kanisa la Kisinodi daima. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu!

01 December 2022, 08:22