Watu wa Mungu Wamsindikiza Na Kumzika Malkia Elizabeth II wa Uingereza Kwa Amani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Uingereza imetoa heshima kubwa katika mchakato mzima wa kumsindikiza Malkia Elizabeth II wa Uingereza katika usingizi wa amani. Hili limekuwa ni tukio la kipekee sana kushuhudiwa na mamilioni ya watu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao mbalimbali ya kijamii. Uingereza imeonesha ulinzi na usalama wa hali ya juu kabisa; amani na utulivu wakati wote wa kuaga, kusindikiza na hatimaye mazishi yake. Watu wa Mungu wameshuhudia ibada, uchaji na heshima kwa Malkia Elizabeth II wa Uingereza kwa kutambua mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Uingereza na Jumuiya ya Madola katika ujumla wake. Kimya kikuu kilitawala kabla ya Ibada ya Misa Takatifu, mara mlio wa kengele ulisikika mara 96, kila dakika kuashiria miaka 96 ya maisha ya Malkia Elizabeth II na hatimaye, kuagwa, Jumatatu 19 Septemba 2022 katika Kanisa la Westminster Abbey, Jijini London. Hii ni Ibada ambayo imehudhuriwa na waamini 2,000 wakiwemo wakuu wa Nchi na Serikali takribani 500 kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani, katika mahubiri yake, amesema, Malkia Elizabeth II wa Uingereza alisadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa Taifa la Uingereza na Jumuiya ya Madola katika ujumla wake, kwa kipindi cha miaka 70. Hakuwa kiongozi mwenye uchu wa madaraka, lakini akabahatika kupewa madaraka haya makubwa kunako mwaka 1953. Ni kiongozi aliyekuwa na imani, matumaini na mapendo thabiti kwa Kristo Yesu, na Mama yake Bikira Maria, daima alijitahidi kuongozwa na huduma kwa watu wa Mungu sanjari na kutekeleza majukumu yake. Ni kiongozi ambaye amejitahidi kumfuata Kristo Yesu ambaye ni: Njia, Ukweli na Uzima; Kristo Yesu aliyekuja kuhudumia na kuyatoa maisha yake, ili yawe ni fidia kwa wengi. Watu wanaopenda na kuthamini kutoa huduma kwa jirani zao ni wachache sana katika medani mbalimbali za maisha.
Watu wenye uchu wa mali na madaraka watatawala, lakini hawatakumbukwa sana, tofauti kabisa na watu wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Machungu na masikitiko makubwa kutoka ndani na nje ya Uingereza ni kielelezo makini cha sadaka ya maisha iliyomwilishwa katika huduma, Malkia Elizabeth wa II sasa anapumzika kwenye usingizi wa milele. Alikuwa ni Mama mwenye furaha, aliyejitahidi kuwa karibu na watu wake, kiasi cha kugusa maisha ya wananchi wengi Uingereza na kwenye Jumuiya ya Madola. Ibada hii, ilikuwa ni maalum kwa ajili ya kuungana na wanafamilia, ndugu, jamaa na watu wote wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za Dunia. Na imekuwa ni siku ya kuonesha mshikamano wa upendo wa kidugu na wale ambao hivi karibuni wamewapoteza wapendwa wao kutokana na kifo. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwagusa na kuwaponya na hatimaye, kuwakirimia furaha na maisha tele. Malkia Elizabeth II wa Uingereza alikuwa ni kiongozi mwenye imani, matumaini na mapendo thabiti. Kwa hakika, tutaonana naye tena katika ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele, siku ile Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa na matumaini kama alivyokuwa Malkia Elizabeth II wa Uingereza.
Fumbo la maisha na kifo liwe ni chachu ya huduma kwa watu wa Mungu. Waamini wawe na matumaini ya huduma katika maisha na kifo, kwa hakika, tutaonana tena. Amesema Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani Jeneza lililoubeba mwili wa Malkia lilipitishwa katika mitaa ya Jiji la London huku baadhi ya waombolezaji wakitupa maua kwenye msafara huo. Hatimaye mwili ulifikishwa katika Kasri la Windsor, ambako Malkia Elizabeth II aliishi kwa miaka mingi kwa ajili ya mazishi. Mamia kwa maelfu ya waombolezaji walijitokeza mitaani kutoa heshima zao za mwisho. Mwili wa Malkia Elizabeth II, umezikwa kando ya kaburi la mume wake Mwana wa Mfalme Philip katika hafla ya faragha ambayo imehudhuria na familia ya kifalme, ndugu, jamaa na marafiki wa karibu zaidi. Mfalme mpya wa Uingereza, Charles III amewapongeza wananchi wa Uingereza na Ulimwengu katika ujumla wake, akisema yeye pamoja na mke wake Camilla wameguswa kupita kifani na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa Malkia Elizabeth II wa Uingereza.