Askofu Mkuu Nkwande: Mapadre Katika Maisha na Utume Wenu Kwa Kanisa Zingatieni Maadili na Utu!
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli, Napoli, Italia.
Daraja Takatifu ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo Yesu kwa Mitume wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati; hivyo hii ni Sakramenti ya huduma ya Kitume nayo ina ngazi kuu tatu: yaani Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Mapadre kwa mamlaka wanayokabidhiwa na Mama Kanisa ni wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma yanayotekelezwa katika maeneo yao. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hutenda kwa nafsi ya Kristo na kutangaza Fumbo lake; huyaunganisha maombi ya waamini na Sadaka ya Kristo Yesu Msalabani inayoadhimishwa kila siku katika Ibada ya Misa Takatifu. Ni daraja linalowataka kujenga na kuimarisha umoja kati yao kama Mapadre pamoja na Askofu wao mahalia. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza: “Maneno na matamko tunayoyatoa kwa ulimi yawe na kazi ya kubariki, kutakatifuza, kuonya na kuwaelekeza watu kwenye uadilifu wa maisha. Kiongozi wa dini anayehamasisha watu kubeba bunduki na mapanga ni shetani mwingine” Askofu mkuu Renatus Nkwande katika wosia wake kwa Mapadre wapya amefafanua maana ya Sakramenti za Kanisa; wito wa Daraja Takatifu ya Upadre; umuhimu wa kukita maisha na utume wao katika maisha adili na matakatifu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Anawakumbusha Mapadre kuwa wao ni ishara ya Kristo na hivyo jamii na kanisa inawategemea wafanane na Kristo katika utendaji wao wa kitume. Anawakumbusha kuwa wanayo changamoto ya kuwa tofauti na wale wanaowafundisha na wakati huo huo wanakuwa bado ni miongoni mwao. Anasema changamoto hii siyo rahisi kuiishi na ndiyo maana kuwa mchungaji katika Kanisa la Mwenyezi Mungu ni sadaka kubwa. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande ameyakazia hayo katika mahubiri yake wakati akitoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi wawili wa Jimbo Kuu Mwanza: Alex Maya kutoka Parokia ya Ihimbili na Francis Muselemu kutoka Parokia ya Magu, upadrisho wa wote wawili uliofanyika katika Parokia ya Ihimbili, Jimbo kuu la Mwanza, tarehe 17 Septemba 2022. Upadrisho huu umefunga milango ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa mwaka 2022 ambao Jimbo Kuu Katoliki Mwanza limetunukiwa zawadi ya jumla ya Mapadre wanajimbo 12. Padre Alex Maya anaanza utume wake wa kikuhani kama Paroko msaidizi wa Parokia ya Ihago ilihali Padre Francis Muselemu anaanza utume wake kama Paroko msaidizi wa Parokia ya Sahwa.
Katika mahubiri yake Askofu mkuu Nkwande amewakumbusha Mapadre kuwa wanapaswa kujitahidi kuwa waadilifu na watakatifu ili kuwaongoza wengine kufikia uadilifu, hasa katika ulimwengu huu ambao umekumbwa na ukengeufu katika maadili na ambapo watu waadilifu wanadharauliwa na kubezwa. Askofu mkuu Nkwande amewasisitiza Mapadre wajipime wenyewe katika yale wanayohubiri. Anasisitiza pia ya kwamba maisha ya Mapadre yanapaswa yawe na rutuba nzuri na ya kwamba Neno la Mungu ambalo wanaligawa kwa watu linapaswa kuzama, kustawi, kukua na kuzaa matunda katika maisha yao wenyewe. Anasema maisha na roho za Mapadre zinapaswa kuwa udongo wenye rutuba, kama katika simulizi la mpanzi ambapo mbegu zilizoanguka kwenye udogo mzuri wenye rutuba zilizaa sana. Anawakumbusha pia kutumia ulimi wao vizuri. “Maneno na matamko tunayoyatoa kwa ulimi yawe na kazi ya kubariki, kutakatifuza, kuonya na kuwaelekeza watu kwenye uadilifu wa maisha. Kiongozi wa dini anayehamasisha watu kubeba bunduki na mapanga ni shetani mwingine” anasema Askofu mkuu Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza.
Anakaza kusema: maneno na matamko yanapaswa kuwasaidia watu wasizame katika dhambi na wala siyo kuleta migawanyiko katika jamii au kuhamasisha watu waasi au wawe watu wa ovyo katika jamii. Askofu mkuu Nkwande amewakumbusha Mapadre wapya kuwa wanapaswa kufundisha kwa jina la Kristo na wala siyo kufundisha kwa majina yao. Anakazia kusema Kristo Yesu anapaswa kuwa kitovu (centre) cha yale ambayo wanafundisha na kuhakikisha kuwa taifa la Mungu linashibishwa kwa Neno la Mungu. Katika mahubiri yake Askofu mkuu Nkwande amewaonya mapadre juu ya kuendekeza “tamaa ya kutaka kupata” na kuwakumbusha kuwa maisha ya upadre ni sadaka na hivyo wao kama manabii wanapaswa kufa kwa ajili ya wengine, wanapaswa kuwa tayari kupoteza ili wengine wapate, wanapaswa kuwa na upendo wa mshumaa ambao wenyewe unateketea ili wengine wapate mwanga. Kwa kufanya hivi watakuwa kweli ishara ya Kristo ambaye alinyenyekea hadi kufa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.