Tafuta

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza ameitaka mihimili ya uinjilishaji kujikita zaidi katika kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu Mfufuka! Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza ameitaka mihimili ya uinjilishaji kujikita zaidi katika kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu Mfufuka! 

Askofu Mkuu Nkwande: Tangazeni Na Kushuhudia Imani ya Kanisa!

Askofu mkuu Nkwande aliwasisitiza Mapadre na Makatekista kujikita zaidi kufundisha na kushuhudia kwa kina imani katoliki. Hivyo Askofu mkuu ameitaka mihimili ya uinjilishaji kuichukua changamoto hii kwa tahadhari kubwa. Anataka imani ipandwe na kupata mizizi katika mioyo ya watoto ndani ya familia, ili wawe imara na kamwe wasiyumbishwe wakiwa watu wazima.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi “Motu Proprio” iitwayo “Antiquum Ministerium” (Huduma Kale) ya 10/05/2021 inayohusu Huduma ya Makatekista katika Kanisa anasema, “Jukumu linalotimizwa na Makatekista ni aina moja maalumu ya huduma miongoni mwa nyingine katika Jumuiya ya Kikristo. Makatekista wanaitwa kwanza kuwa wataalam katika huduma ya kichungaji ya kueneza imani inapoendelea katika hatua zake tofauti…” (rejea namba 6). Ni kutokana na kuelewa vizuri ujumbe huu wa Baba Mtakatifu pamoja na nia ya kuendelea kuwa Kanisa la Kisinodi hasa wakati huu ambao Kanisa la Ulimwengu mzima linaadhimisha Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu ili kuweza kutembea pamoja likiongozwa na kaulimbiu “Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume,” Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Mwanza limeendelea kuonesha nia yake ya kutembea pamoja na kuwatazama kwa namna ya pekee Makatekista. Makatekista ni wadau wakuu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima Barani Afrika. Wao wamekuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji wa awali Barani Afrika na wanaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwatayarisha wakatekumeni ili kupokea Sakramenti za Kanisa. Makatekista wameonesha umuhimu wa pekee katika kuzisimamia na kuziongoza Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, ukarimu na upendo kwa familia ya Mungu.

Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume
Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume

Kwa njia ya mifano bora ya Makatekista kutoka sehemu mbali mbali Barani Afrika, Kanisa Barani Afrika limeweza kuzamisha mizizi katika maisha na vipaumbele vya watu. Mchango wa Makatekista bado ni muhimu na endelevu anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume Dhamana ya Afrika, "Africae Munus." Maaskofu mahalia wanapaswa kuhakikisha kwamba Makatekista wanapewa majiundo awali na endelevu: kiakili, kimafundisho, kimaadili na kichungaji, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, katika Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria Nyegezi kwa mara nyingine Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, amewakutanisha Mapadre, Makatekista na Mafrateri ikiwa ni mwendelezo wa desturi ya kukutana kwa pamoja kama wadau wa uinjilishaji na kuzitazama kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazokwamisha ufanisi wa uinjilishaji na umuhimu wa kutembea pamoja kama Kanisa. Mkutano huu ni wa pili kufanyika ambapo mwaka 2021 Askofu mkuu, Mapadre na Makatekista walikutana katika Chuo cha Makatekista Bukumbi. Mwaka huu 2022 mkutano huu umehudhuriwa na Makatekista 339, Mapadre 59 na Mafrateri 68. Wengine hawakuweza kuhudhuria kwa sababu zisizoweza kuzuilika.

Awali ya yote Askofu mkuu Nkwande alisisitiza umuhimu wa utaratibu huu wa kukutana kila mwaka na kusisitiza kuwa unapaswa kufanyika katika ngazi zote za dekania ili kutazama kwa pamoja changamoto za uinjilishaji wa kina wanazokumbana nazo Makatekista. Aidha Askofu mkuu Nkwande aliwasisitiza Mapadre na Makatekista kujikita zaidi kufundisha kwa kina imani katoliki, hasa kipindi hiki ambapo Tanzania ina utitiri wa madhehebu na hata wengine kuwa na malengo ya makusudi ya kuua Ukristo na hasa Ukatoliki. Hivyo Askofu mkuu Nkwande ameitaka mihimili ya uinjilishaji kuichukua changamoto hii kwa tahadhari kubwa. Anataka imani ipandwe na kupata mizizi katika mioyo ya watoto ndani ya familia Watoto wakiwa imara katika imani hawataweza kuyumbishwa hata wakiwa watu wazima. Sanjari na hayo Askofu mkuu ameitaka mihimili yote ya uinjilishaji katika Jimbo Kuu la Mwanza kupinga na kukemea dhana na mawazo ya ushirikina na kurogwa ambayo yanawasulubu watu kutokana na ukosefu wa elimu. Hivyo amewataka Makatekista na Mapadre kuwahimiza watu umuhimu wa elimu na hasa kusomesha watoto maana elimu huwatoa watu katika mawazo potofu ya ushirikina na kurogwa.

Watoto warithishwe imani, maadili na utu wema ili wasiyumbishwe ukubwani
Watoto warithishwe imani, maadili na utu wema ili wasiyumbishwe ukubwani

Nao Makatekista wameeleza changamoto zinazolikumba Kanisa kwa sasa. Moja ya changamoto ni waamini kutohudhuria Kanisani mara baada ya kupokea Sakramenti hasa baada ya kubatizwa. Wakichangia katika changamoto hii makatekista wenyewe wamehimizana kuwa “wawindaji” pamoja na Mapadre wao, yaani kutoka na kuwatafuta kondoo na kujua changamoto zinazowapelekea kutokufika tena kanisani na wala wasikae tu vigangoni kusubiri waamini. Kadhalika Makatekista wamesema imani ya waamini imekuwa haina mizizi kwa sababu malezi ya kiroho katika ngazi ya familia yamepuuzwa na badala yake wazazi wamejikita zaidi katika elimu dunia kwa ajili ya watoto wao. Na hivyo Makatekista wamewageukia wazazi na kuwasihi watimize wajibu msingi wa kutoa elimu na malezi ya kiroho katika ngazi ya familia. Makatekista pia wamependekeza walimu wa dini katika ngazi za Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo wapewe semina zitakazo wajengea uwezo wa kuwaandaa vyema watoto katika ngazi za Jumuiya kabla hawajaanza hatua ya kukutana na Mapadre na Makatekista kwa matayarisho ya Sakramenti mbalimbali za Kanisa. Pia changamoto ya uhitaji wa kuwainjilisha vizuri watu wenye ulemavu wa kutosikia (viziwi) imejitokeza. Katika kukabiliana na hili Askofu mkuu Renatus Nkwande ameagiza uongozi wa Chuo cha Makatekista Bukumbi kuajiri mtaalamu wa lugha za alama ili aweze kufundisha taaluma hiyo kwa Makatekista ili nao waweze kuwafikia watu wenye uhitaji huo katika uinjilishaji. Na katika kuiva vizuri Makatekista wameomba muda wa mafunzo ya ukatekista uongezwe.

Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo Kuu la Mwanza Padre Gregory Kiloma amesema watalitazama ombi hili kwa marefu na mapana. Hivi karibuni pia Askofu mkuu Nkwande aliagiza Parokia zote za Jimbo Kuu la Mwanza kupeleka walau Makatekista wawili kwa mwaka katika Chuo cha Makatekista Bukumbi ili kuongeza idadi ya Makatekista wanaopata mafunzo rasmi ya ukatekista. Wapo pia Makatekista wengi ambao wanajitolea kufundisha dini ingawa hawajapata nafasi ya kupita katika vyuo vya katekesi. Hawa pia Askofu mkuu anataka watazamwe kwa kupelekwa Chuo cha Katekesi walau hata kwa kozi maalum. Makatekista licha ya changamoto hizo walikipongeza Chuo cha Makatekista Bukumbi kwa mfumo wake wa uendeshaji ambapo kinapokea pia familia ya mume na mke. Wake wa Makatekista hupatiwa elimu ya ushonaji wakati waume zao wakipatiwa mafunzo ya ukatekista na baada ya kumalizika kwa kozi akina mama hao hupatiwa vifaa vya ushonaji kwa ajili ya kutumia ujuzi wao kumudu gharama za maisha yao ya baadaye. Mkurugenzi wa Chuo cha Makatekista Bukumbi, Padre Alex Sumbana aliwajulisha wahudhuriaji kuwa Chuo kimeanza “Refresher courses”  kozi za kujinoa za miezi mitatu mitatu. Kadhalika Padre Sumbana alieleza namna chuo cha Makatekista kinavyoendelea kuboresha miundombinu yake.

Masalia ya Mtakatifu Yohane Paulo II yamewasili tayari Mwanza. Ujenzi wa Kanisa
Masalia ya Mtakatifu Yohane Paulo II yamewasili tayari Mwanza. Ujenzi wa Kanisa

Mwaka 2021 kikundi cha “Wamissionari Wakatoliki Mtandaoni Taifa” kilifanya ziara na majitoleo yao katika Chuo cha Makatekista Bukumbi kwa lengo la kusaidia juhudi za kuboresha miundombinu ya Chuo cha Makatekista Bukumbi. Maboresho ni mengi na hivyo bado rasilimali fedha inahitajika. Kwa upande wao Mapadre, wamehimizana kuwasaidia Makatekista ili waweze kutimiza wajibu wao kwa ufanisi maana ni wasaidizi muhimu sana wa Mapadre.  Mapadre pia walitoa rai kwa Mapadre wenzao ambao Parokia zao zina uwezo na nafasi kuwawezesha Makatekista kupata ujuzi mwingine wa ziada kama vile elimu ya ufundi na kompyuta ili waweze kumudu maisha yao bila kuwa mzigo kwa waamini. Mwishoni, Askofu mkuu Renatus Nkwande aliwaomba Makatekista na Mapadre wote kuwahimiza waamini kujitokeza kwa wingi mwezi Novemba 2022 katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Kuu jipya la Kawekamo ambapo tayari shughuli ya kuliezeka imeishaanza. Askofu mkuu aliwajulisha wahudhuriaji kuwa tayari masalia ya Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye ni Mtakatifu Msimamizi wa Kanisa Kuu jipya yameshapatikana. Mwanza kumenoga!

Askofu mkuu Nkwande
07 September 2022, 11:29