Tafuta

Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki Kahama nchini Tanzania: Kusimikwa rasmi 4 Septemba 2022 Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki Kahama nchini Tanzania: Kusimikwa rasmi 4 Septemba 2022 

Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Vipaumbele!

Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko wa Kahama maisha na utume wake unaongozwa na kauli mbiu ya Kiaskofu: Ukweli na haki katika upendo anasimikwa tarehe 4 Septemba 2022. Mapokezi yatakayofanyika kwenye Kigango cha Nyantakala, majira ya asubuhi. Jioni atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Kahama, masifu ya jioni, Kiri ya Imani pamoja na kula kiapo cha utii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Tanzania, anatarajiwa kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo la Kahama, Dominika ya 23 ya Mwaka C wa Kanisa, tarehe 4 Septemba 2022. Hili ni tukio linalotanguliwa na mapokezi makubwa ya Askofu mteule yatakayofanyika kwenye Kigango cha Nyantakala, kilichoko mpakani mwa Jimbo la Kahama na Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, majira ya saa 3:00 asubuhi. Jioni atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Kahama, yatafuatia masifu ya jioni, kiri ya Imani pamoja na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ili aweze kulichunga na kuliongoza vyema Kanisa lake, aliweka huduma mbalimbali na kuwakabidhi wafuasi wake uwezo mkatakatifu wa kuwatumikia ndugu zao ili waweze kufikia wokovu. Basi Maaskofu wamekabidhiwa huduma ya jumuiya pamoja na msaada wa Mapadre na Mashemasi wakiliongoza kundi lake kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, ambao wao ni wachungaji wake, ili kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, daima wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kudumisha mahusiano na mafungamano katika urika wao.

Kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kutatanguliwa na Masifu ya Jioni
Kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kutatanguliwa na Masifu ya Jioni

Kwa maana Maaskofu wote huwajibika kukuza na kuhifadhi umoja wa imani na nidhamu iliyo moja kwa Kanisa lote, tena huwafundisha waamini wawe na upendo kwa mwili wote wa Fumbo wa Kristo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwishoni, huwajibika kuendeleza utendaji wowote unaohusu Kanisa lote, hasa kusudi imani ipate kukua na mwanga wa ukweli kamili uwazukie watu wote, ili hatimaye, wote waweze kushiriki katika kunogesha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Rej. Lumen gentium n.18-29. Ni katika muktadha huu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Kahama, Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko anasema, kuna haja ya kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa Katoliki inayomwilishwa katika matendo. Hii ni imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili pamoja na maisha ya sala. Hili ni jukumu linalopaswa kuvaliwa njuga kwa namna ya pekee na mihimili ya uinjilishaji, huku ikisaidiana na wazazi, ili kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kikamilifu dhamana na wajibu wao kama wazazi na walezi. Huu ni wakati wa kujikita zaidi katika uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Wazazi watambue haki, wajibu na dhamana yao ili kukoleza ujenzi wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani.

Jimbo Katoliki la Kigoma linalo sababu ya kumshukuru Mungu kwa wito huu.
Jimbo Katoliki la Kigoma linalo sababu ya kumshukuru Mungu kwa wito huu.

Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo! Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko anasema anatambua fika umuhimu, uzito na changamoto za maisha na utume wa Kipadre. Kumbe kuna umuhimu kwa Mapadre kuendelea kupyaisha maisha na utume wao, kwa njia ya Neno, Sakramenti, Mafungo na Mashauri ya maisha ya kiroho, kwa kuzingatia umuhimu wa maisha ya kijumuiya, taratibu, kanuni na sheria za Kanisa. Katika maisha yake kama Padre, walijipangia kukutana walau mara moja kwa mwaka ili kushirikishana: mafanikio, changamoto na matatizo ya wito na maisha ya Kipadre.

Anasema vijana ni amana na utajiri wa Kanisa. Ni kundi linalopaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ndiyo maana Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana imejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kwa wafu! Hii ndiyo changamoto inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia; kwa kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana wa kizazi kipya. Kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Injili na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau. Vijana kwa nguvu ya Roho Mtakatifu inayotenda kazi ndani mwao, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo! Lakini si kwa vita, fujo na vurugu, bali kwa kutekeleza mpango wa Mungu kila siku ya maisha yao! Vijana wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao, kama alivyofanya Bikira Maria, kwa kukubali kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa.

Vijana wajengewe mazingira ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa
Vijana wajengewe mazingira ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa

Vijana wathubutu kuzamisha mizizi ya tamaduni zao katika maisha, huku wakiwa na matumaini kwa maisha ya mbeleni yenye msingi thabiti! Vijana wapende na kuheshimu mila, desturi na tamaduni zao njema, ili waweze kukua, kukomaa na kuchanua katika utakatifu wa maisha! Umefika wakati wa kujikita zaidi katika mchakato wa utamadunisho, kwa kuwajengea wazawa uwezo wa kushirikisha karama, mila, desturi na tamaduni zao njema sehemu ya utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Vijana wadumishe umoja na mshikamano, tayari kupambana na changamoto za maisha ya ujana! Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko anakaza kusema, ikiwa kama vijana na watoto hawatajengewa mazingira bora ya kiroho na kimwili, litania za shutuma dhidi ya vijana na watoto zinaendelea kusikika kila wakati. Vijana wanapaswa kujitambua; watangaziwe na kushuhudiwa Injili ya: Imani, Matumaini na Mapendo kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wasaidiwe kuonja uwepo na ukaribu wa Mungu katika maisha yao. Wazitambue changamoto na fursa zilizoko mbele yao tayari kuzivalia njuga na kuzigeuka kuwa ni fursa. Vijana wajifunze kutafuta haki zao msingi kwa kutimiza wajibu; wawe na nidhamu, maadili na utu wema. Vijana wajitahidi kupata malezi stahiki, ili kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha na utume wa Kanisa unaanza na kusimikwa katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, zinazomwilishwa kila siku, hatua kwa hatua hasa katika malezi na makuzi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, watoto kuendelea kuinjilisha mintarafu hali na mazingira wanayokumbana nao kwa wakati huu. Ikumbukwe kwamba, watoto wanapaswa kujifunza na hatimaye, kujenga utamaduni wa: ushirika, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Hii ni changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimisionari tangu sasa, ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na baa la umaskini linalosigina utu, heshima na haki zao msingi. Hata katika umaskini wao, watoto wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia!

Wazazi na walezi watekeleze dhamana na wajibu wao katika malezi
Wazazi na walezi watekeleze dhamana na wajibu wao katika malezi

Huu ndio mshikamano wa watoto katika huduma ya Injili ya huruma na mapendo. Hata watoto kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu, na hivyo, wanahamasishwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu katika maisha na mazingira yao. Ni katika muktadha huu wa malezi na makuzi ya watoto ndani ya familia na Kanisa anasema, Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Tanzania kwamba, watoto wanapaswa “kukunjwa wangali wabichi.” Watoto wafundishwe na kurithishwa imani, maisha adili na ya sala, kwa njia ya mifano bora kutoka kwa wazazi na walezi wao na wala si vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Kama ilivyokuwa kwa makundi mbalimbali mwanzo mwa mahubiri ya Yohane Mbatizaji, hivyo hivyo, watu wa Mungu katika ujumla wao wanapaswa kusikiliza na hatimaye kuchukua hatua stahiki kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Rej. Lk 3: 1-20.

Umoja, Ushiriki na Utume kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodini changamoto inayosimikwa katika utamaduni wa kusikiliza na kutenda kwa makini, kadiri ya uwezo ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia mja wake. Yote haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kahama. Huu ni wosia kutoka kwa Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S wa Jimbo Katoliki la Morogoro kwa Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama. Awe ni chombo cha faraja na matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Kwa matatizo na changamoto zinazoshindikana kuwa ni fursa, basi ampelekee Mwenyezi Mungu katika sala na sadaka, ili aweze kumpatia ufumbuzi. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 23 Juni 2022 alimteuwa Mheshimiwa Padre Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kigoma, kuwa ni Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kahama lililoko nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko alikuwa ni Makamu wa Askofu Jimbo Katoliki la Kigoma na Katibu mtendaji, Idara ya Kichungaji Jimbo Katoliki la Kigoma. Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko alizaliwa tarehe 25 Machi 1970 huko Kalinzi, Jimbo Katoliki la Kigoma.

Umoja, ushiriki na utume ni muhimu katika kujenga Kanisa la Kisinodi.
Umoja, ushiriki na utume ni muhimu katika kujenga Kanisa la Kisinodi.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kutoka Seminari Ndogo ya Katoke kati ya mwaka 1986 hadi mwaka 1993; Seminari Ndogo ya Ujiji kati ya Mwaka 1993 hadi mwaka 1994. Aliendelea na masomo ya Falsafa, Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kati ya Mwaka 1994 hadi mwaka 1996. Baadaye aliendelea na masomo ya Taalimungu, Seminari kuu la Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam kati ya mwaka 1996 hadi mwaka 1999. Kati ya Mwaka 1999 hadi mwaka 2000 alifanya mazoezi ya shughuli za kichungaji Seminari Ndogo ya Ujiji. Hatimaye, tarehe 5 Julai 2001 akapewa Daraja takatifu ya Upadre kwa Jimbo Katoliki la Kigoma. Baada ya Upadrisho, amewahi kuhudumu kama: Paroko-usu Parokia ya Kasulu, Jimbo Katoliki la Kigoma, Mwalimu na Mlezi, Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora. Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2008 alitumwa na Jimbo Katoliki la Kigoma, kwenda nchini Italia kujiendeleza zaidi kwa masomo na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Taalimungu Maadili. Alibahatika pia kufanya utume wake wa Kipadre katika Parokia ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, Jimbo Katoliki la Catania kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2008. Baada ya kurejea nchini Tanzania, alitumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kufundisha Seminari Kuu la Kipalapala, Jimbo Kuu la Tabora.

Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko, amewahi pia kuwa Mkurugenzi wa Utume wa Walei, Jimbo Katoliki Kigoma, Paroko wa Parokia ya Kibondo, Dekano wa Dekania ya Kibondo na Rais wa Umoja wa Mapadre Wazalendo, Jimbo Katoliki la Kigoma. Kati ya Mwaka 2015 hadi mwaka 2016 alikuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa UMAWATA, Taifa. Kati ya Mwaka 2016 hadi mwaka 2019 alikuwa Paroko wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Kigoma. Tangu mwaka 2011 aliteuliwa hadi wakati huu, amekuwa ni Mratibu waUimarishaji wa Familia Tanzania, UFATA, "Tanzania Family Strengthening" na Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa, PMS Jimbo Katoliki la Kigoma. Tangu mwaka 2016 hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Kigoma na Katibu mtendaji wa Idara ya Kichungaji Jimbo Katoliki la Kigoma. Tarehe 4 Septemba 2022 amewekwa wakfu kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Jimbo Katoliki Kahama
01 September 2022, 15:47