Tafuta

Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Tanzania, Dominika tarehe 4 Septemba 2022 amewekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kahama. Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Tanzania, Dominika tarehe 4 Septemba 2022 amewekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kahama. 

Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko, Kahama: Ukweli, Haki na Upendo Katika Huduma!

Ibada ya kumsimika imeongozwa na Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, akisaidiana na Askofu Ludovick J. Minde wa Jimbo Katoliki la Moshi, ambaye kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama pamoja na Askofu Joseph R. Mlola wa Jimbo Katoliki la Kigoma mahali anakotoka Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Tanzania, Dominika tarehe 4 Septemba 2022 amewekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kahama baada ya kuteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 23 Juni 2022. Katika maisha na utume wake, anaongozwa na kauli mbiu ya Kiaskofu: Ukweli na haki katika upendo na kwa lugha ya Kilatini inasomema. “Veritas et Iustitia in Amore.” Ibada ya kumsimika imeongozwa na Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, akisaidiana na Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Moshi, ambaye kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama pamoja na Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS, wa Jimbo Katoliki la Kigoma mahali anakotoka Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama. Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora katika mahubiri na wosia wake kwa Askofu mpya amerejea kwa ufupi yaliyoadhimishwa kwenye Masifu ya Jioni, Jumamosi tarehe 3 Septemba, 2022, Kumbukumbu ya Mtakatifu Gregori Mkuu. Kiri ya imani ya Kanisa ya Kanisa Katoliki, akiwa ameungana na Baba Mtakatifu Francisko na Kanisa Katoliki Tanzania. Umuhimu wa Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa pamoja na kuwapongeza wale wote waliofanikisha mchakato na hatimaye, uteuzi wa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Uaskofu ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu
Uaskofu ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu

Uaskofu ni huduma kwa ajili ya watu wa Mungu. Katika: fursa, shida, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kiaskofu, daima awe tayari kumkimbilia Kristo Yesu katika sala kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, Mtume aliyetangaza na kushuhudia upendo wake kwa Kristo hadi kuyamimina maisha yake, kichwa chini miguu juu. Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama ajitahidi kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wake, huku akiwa ameungana na Maaskofu wenzake katika urika wao. Sala ya Baba Yetu, Muhtasari wa Mafundisho ya Kristo Yesu iwe ni dira na mwongozo wa maisha. Azingatie Neno la Mung una kudumu daima katika nia njema. Awe ni shuhuda wa ukweli na haki katika upendo, daima ajitahidi kuwa mchungaji mwema kwa kusikiliza, kuongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha na kuwagawia watu wa Mungu Mafumbo ya Kanisa. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wapewe kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama katika salam zake za shukrani kwanza kabisa amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuumba, kumjalia imani, wito pamoja na kuendelea kumwongoza katika maisha na utume wake kwa Mungu na watu wake. Amewashukuru wazazi wake ambao kwa sasa wote ni marehemu kwa kukubali kuitunza Injili ya uhai na kukubali: kumzaa na kumlea katika maadili na kiutu, kiimani, kiakili na kichungaji, bila kuwasahau wadau mbalimbali waliochangia katika maisha na makuzi yake. Amewashukuru walimu na walezi wake katika hatua mbalimbali za maisha, bila kuwasahau walimu wa nje ya darasa, yaani walimu katika maisha ya kawaida. Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko, amewashukuru watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika maisha na utume wake. Amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteuwa hapo tarehe 23 Juni 2022 kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kahama na hivyo kumwaminisha utume wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Amewashukuru wale wote waliompongeza, kumtia shime, ili apate nguvu za kukubali na hatimaye, kupokea utume huu ambao unatoka kwa Mungu ambaye ataendelea kutenda kupitia katika nafsi yake na kwa njia ya wasaidizi wake. Amewashukuru wote waliomsindikiza, wakampokea na hatimaye, kushuhudia akiwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Ukweli na haki katika upendo kwa watu wa Mungu Kahama
Ukweli na haki katika upendo kwa watu wa Mungu Kahama

Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora anayo nafasi ya pekee kabisa katika maisha na utume wa Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko, kwani alimlea kama Mseminari, akamweka wakfu kuwa Padre mwaka 2001, amemwongoza kwa mafungo wakati akijiandaa kuwekwa na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama, utume ambao ameukamilika Askofu mkuu Ruzoka. Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko anakiri na kutambua uzito wa utume wa kulisha, kuchunga na kutunza wanandoo wa Mungu, lakini anaendelea kumtumaini Mungu kwa kutambua kwamba, Nira na Mzigo wa Kristo Yesu ni laini na mwepesi. Kristo Yesu atamsaidia kutenda kwa ukweli na haki katika upendo. Ameishukuru Serikali ya Tanzania katika ujumla wake na kwamba, ameahidi kuendeleza na kudumisha ushirikiano na mshikamano kati ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi.

Amemshukuru kwa namna ya pekee kabisa Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Moshi, kwa umisionari na upendo usioganyika kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Kahama. Ni kiongozi aliyeweka akili na moyo wake wote kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Wataendeleza na kufanya yale aliyotamani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki Kahama ili yasaidie kusimika mizizi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Jiji la Mungu kwa wampendao kutoka Jimbo Katoliki Kahama. Amewakumbusha Mapadre ambao ni wasaidizi wake wa karibu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwamba, Jimbo Katoliki la Kahama ni jimbo lao. Huu ni utume unaopaswa kusimika mizizi yake katika ukweli, haki na katika upendo. Kwa kuwajibika barabara, dhamiri zao zitakuwa safi na huru mbele ya Mwenyezi Mungu kwa yale watakayoweza kuyatimiza. Amewashukuru watawa kwa kazi kubwa ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi kiroho na kimwili.

Shukrani nyingi kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma
Shukrani nyingi kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma

Wao ni sehemu ya mafanikio makubwa ya shughuli mbalimbali zinazoonekana, ni wajibu na dhamana kutunza mafanikio, kuyaendeleza pamoja na kuanzisha mapya. Wajenge umoja unaoongozwa na ukweli, haki na katika upendo, daima wakijitahidi kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa furaha. Watambue kwamba, kila mmoja wao ni mdau muhimu katika utume wa Uinjilishaji, kwani wote ni wamisionari wameitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa watu wa Jimbo Katoliki la Kahama. Amekuja kwao kama mganga ili awaponye, Mchungaji ili awaongoze; Kama Mama ilia pate kuwalisha na Baba ili awakinge na hatimaye, aweze kuwafikisha mbinguni. Jambo la msingi kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kahama ni kusikiliza na kutekeleza Mafundisho yake. Watambue kwamba, wote katika ujumla wao ni wadau muhimu sana katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, yote wayatende kwa sifa na utukufu wa Mungu huku wakiongozwa na ukweli na haki katika upendo. Na kwa njia hii, watafanikiwa kutunza, kuendeleza na kupanua huduma za kiroho na kimwili kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kahama.

Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko, amewashukuru watu wa Mungu Jimbo Katoliki Kigoma kwa malezi, ushiriki na utume. Amekazia umuhimu wa kuwarithisha watoto na vijana imani, maadili na utu wema, huku wakiendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, maisha na utume wa Kanisa. Wajitahidi kuwa wasikivu katika kutekeleza mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ambayo kwa sasa imeingia katika awamu ya pili kuanzia tarehe 15 Agosti hadi Machi 2023 kwa kunogeshwa na mambo makuu matatu: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Moshi, aliongoza Masifu ya Jioni, Dominika ya 23 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko akafungua lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Karoli Lwanga, akakiri Kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Watoto na vijana wapewe kipaumbele cha kwanza katika malezi na makuzi
Watoto na vijana wapewe kipaumbele cha kwanza katika malezi na makuzi

Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alimpongeza Askofu Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko, kwa kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama. Naye Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema wananchi wa Kahama wamepata kiongozi makini na mwenye upendo apate ushirikiano kwa wananchi wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kahama. Andengenye amesema kwamba kazi nzuri aliionesha tangu awali akiwa mkoani Jimboni Kigoma hivyo aendelee kutenda mema. Naye Mkuu wa wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga amefurahi kuona maelfu ya watu waliojitokeza kuja kumpokea Askofu Nkoronko alipowasili na hatimaye kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama, Dominika tarehe 4 Septemba 2022.

Askofu Ndizeye Kahama
05 September 2022, 15:03