Tafuta

Jitahidini kupitia Njia Nyembamba inayosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; katika maadili na utu wema. Jitahidini kupitia Njia Nyembamba inayosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; katika maadili na utu wema. 

Tafakari Neno la Mungu Dominika 21 ya Mwaka C: Njia Nyembamba

Lengo na shabaha Mwinjili Luka ni kuwahimiza wakristo wa jumuiya yake kutambua wajibu wao wa kushika imani, si kwa mazoea tu bali kwa maisha halisi ya siku kwa siku, kama sehemu ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko Ni kuwaalika kubadili mtazamo na hata namna zao za kuenenda kwani wengi waliona inatosha kuwa na dini ya mazoea au wanaiita dini ya maumbile.

Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Ufuasi ni kuwa rafiki wa kweli wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa maneno na matendo yetu, na ndio hakika ya wokovu wetu! Amani na Salama! Je! Bwana, watu watakaookolewa ni wachache? Ni swali la mtu mmoja kati ya makutano ambalo linabaki na mashiko sio tu katika nyakati zile za Yesu, bali hata katika nyakati zetu leo.  Ni swali lenye mashiko kwani linaonesha wazi kuwa maisha ya mwanadamu hayaishii tu hapa duniani bali kuna maisha baada ya maisha ya sasa. Ni swali linaoonesha maisha ya mwanadamu sio ajali bali ni mpango wa milele na wa upendo wa Mungu aliye Muumbaji wetu. Ni swali lenye kuonesha maisha yetu yana maana na yana makusudi na malengo   Ni swali linaloonesha kuwa maisha yetu tungali hapa duniani hatuna budi kuyaishi kadiri ya mpango na mapenzi ya Mungu aliye muumbaji wetu. Leo kuna wasioamini katika Mungu wala dhana nzima ya uumbaji, kwani kwao maisha ni vile kila mmoja aishi kadiri anavyoona na kutaka yeye, mwanadamu aishi kana kwamba amejiumba yeye mwenyewe, kwani kwao kukiri uwepo wa Mungu ni kwenda kinyume na uhuru usio na mipaka anaojitwalia mwanadamu. Kwa wasioamini juu ya uwepo wa Mungu, kwao baada ya kifo ndio mwisho wa maisha ya mwanadamu, hivyo maisha kwao kila mmoja ajiamulie vile anavyoona inafaa na kumpendeza kufanya na kuyaishi. Kwa wasioamini mwanadamu ndiye kipimo cha maisha yake mwenyewe, ndiye mwamuzi wa mwisho kwani hakuna maisha baada ya maisha ya hapa duniani kumalizika kwa kifo.

Njia Nyembamba ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko.
Njia Nyembamba ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Mtu mmoja anayekwenda kwa Yesu na kumuuliza swali juu ya kuokoka, anaona kuwa maisha yetu ni zawadi kutoka kwa Mungu, na hivyo siku moja lazima tusimame mbele yake na kutolea mahesabu, ndio kuwajibika mbele ya Mungu aliye Baba na Muumba wetu. Swali lake ni swali la mmoja mwenye imani kwa Mungu na katika uumbaji. Ni mmoja anayeona maisha yake hapa duniani yana lengo kuu kadiri ya mpango wake Muumba wetu. Yesu hajibu moja kwa moja swali lake, kwani sio juu yetu kujua idadi ya wale watakaokooka bali anatuonesha ni kwa namna gani kila mmoja wetu anapaswa kujibidisha ili kuufikia wokovu. Yesu anatumia fursa hiyo kutuonesha jinsi ya kuusumbukia na kuushughulikia wokovu wetu katika maisha yetu tukiwa tungali hapa duniani. Haitoshi kumkiri Yesu kwa maneno matupu, kwani anatudai ushahidi wa maisha, yaani matendo yetu hayana budi kuonesha na kuakisi imani yetu. Ni kwa njia ya kuyalinganisha na kuyalandanisha maisha yetu na Neno lake, hapo hakika tunakuwa na hakika ya kualikwa nasi na kufurahi pamoja naye katika furaha ile ya milele mbinguni. Yesu anatujua sio kwa maneno yetu matupu bali kwa matendo na maisha yetu. Ni hapo tunakuwa kweli wafuasi na rafiki zake kila mara tunapojaribu kuliishi Neno lake katika maisha yetu ya siku kwa siku. Kinyume chake tunakuwa ni wafanyaji wa udhalimu, kwani maisha yetu yanakuwa kinyume na Neno lake.

Yesu leo anatumia lugha na maneno makali sio kwa nia ya kutuogofya bali hasa kutuonesha umuhimu wa kuzingatia kushughulikia wokovu wetu. Yesu anatuonesha gharama kubwa ya ufuasi wetu kama kweli tunataka kuwa rafiki na wana wa Mungu. Anayetamani wokovu ni mmoja anayetaka kuwa rafiki wa kweli wa Mungu sio tu kwa maneno bali kwa maisha yake yote. Katika Injili ya Mathayo tunakutana mara kadhaa na lugha ya kutisha na kuogofya kutoka kwa Yesu dhidi ya wadhambi na wakosefu, mathalani moto wa jehanamu, juu ya siku ya hukumu ambapo Mungu atatenganisha mbuzi na kondoo, na hata mara sita Mwinjili Mathayo anazungumzia juu ya kulia na kusaga meno kwa wale wasiotubu na kumwongokea Mungu. Lakini kwa Mwinjili Luka kinyume chake tunakutana na Sura tofauti ya Yesu, kwani ni mwenye huruma na rafiki wa wadhambi kiasi aliweza hata kula na kunywa nao walipomwalika. Hivyo, sehemu ya Injili ya Dominika ya 21 ya Mwaka C wa Kanisa Lk 13 : 22-30 inatupa sura tofauti sana na ile tunayoizoea kutoka kwa Mwinjili Luka na hapo ni vema tukatafakari kusudi na lengo lake. Yesu leo haonekani kuwa ni mganga aliyekuja ili kuwaponya walio wagonjwa, si yule anayewaacha tisini na kenda na kwenda kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea, si yule anayeamka usiku kutoka usingizini ili ampe rafiki yake mkate kwani amefikiwa na mgeni, si yule anayefanana na baba mwenye huruma aliyempokea kwa furaha na hata kufanya karamu kubwa baada ya kumpata tena mwanaye aliyepotea.

Uinjilishaji wa kweli unafumbatwa katika ushuhuda wa maisha adili na kweli
Uinjilishaji wa kweli unafumbatwa katika ushuhuda wa maisha adili na kweli

Leo anatualika kujibidisha na kupitia mlango mwembamba, na kinyume chake basi ni kutupwa nje kwenye kilio na kusaga meno. Mwinjili Luka anapoandika sehemu hii ya Injili ya leo, lengo na shabaha yake ni kuwahimiza wakristo wa jumuiya yake kutambua wajibu wao wa kushika imani, si kwa mazoea tu bali kwa maisha halisi ya siku kwa siku, kama sehemu ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko Ni kuwaalika kubadili mtazamo na hata namna zao za kuenenda kwani wengi waliona inatosha kuwa na dini ya mazoea au wengine wanaiita dini ya maumbile. Inatosha kwa kuwa nasali kila siku sala ya asubuhi, mchana na usiku, au nakwenda kanisani kila Dominika au natoa zaka na michango mbalimbali ya Kanisa na kuhudhuria jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na huku bila kuhusianisha maisha yangu na Injili ya Yesu Kristo. Imani yetu haina budi kuakisi maisha yetu ya siku kwa siku, maisha yetu hayana budi kuendana na kile tunachokiamini. Ni katika muktadha huo basi nawaalika turejee kuitafakari vema sehemu ya Injili ya leo. Mtu mmoja anaenda kwa Yesu na kumuuliza juu ya idadi ya wale watakaookoka. Yesu hamjibu swali lake kwani mtu yule alitaka kujua idadi na badala yake Yesu anatualika leo tutafakari nini tufanye kwa ajili ya kuurithi uzima wa milele. Jibidisheni, lazima kutoka jasho, lazima kufanyia kazi wokovu wetu ndio jibu la Yesu si tu kwa yule mtu bali kwa kila mmoja wetu. Kushiriki karamu ya Kristo hatuna budi kutoka jasho. Pamoja na kwamba Mwenyezi Mungu anatujalia neema zake kwa ajili ya wokovu wetu, lakini bado hatuna budi kushirikiana na neema zake kwa ajili ya kuufikia wokovu wetu.

Walio ndani karamuni ndio wale waliojibidisha kwa kupitia mlango mwembamba. Katika sura ya 9 ya Injili ya Luka tunakutana na mabishano kati ya wanafunzi wa Yesu juu ya nani ni mkubwa kati yao. Yesu anawakumbusha ulazima na umuhimu wa kuwa wadogo kama watoto wadogo. Hivyo hatuwezi kuwa wafuasi wa Yesu kama hatujibidishi kuwa wadogo kwani kwa kukomaa na ukubwa wetu basi hapo itakuwa ni ngumu kupita katika mlango mwembamba. Na ndio mwaliko wa kuwa watumishi wanyenyekevu katika maisha yetu bila kujikweza na kujikuza na kusaka sifa na utukufu wetu. Mdogo ni yule anayetambua kuwa hana mastahili yeyote mbele ya Mungu, anayekiri kuwa ni mdhambi na mkosefu hivyo anaikimbilia huruma na upendo wa Mungu. Ni kwa kuwa wadogo tu hapo tunahakika ya kuweza kuingia karamuni kwa kupitia mlango mwembamba. Kundi la pili ni wale wanaobaki nje na mlango kufungwa na huko wanakuwa kwenye kilio na kusaga meno.  Hao si wapagani bali ni wale waliomjua Yesu hata kusikiliza Neno lake, na kula na kunywa naye. Ndio kutukumbusha kadi ya kushiriki karamu ile haitoshi kujua mafundisho juu ya imani yetu bali lazima kuishi Injili katika maisha yetu.  Haitoshi kushiriki Misa iwe kanisani au jumuiyani au sala kila siku bila kuiweka imani yetu katika maisha. Ni mwaliko wa kubadili mtazamo wetu kuwa maisha yetu hayana budi kuongozwa na Injili.

Waamini waboreshe maisha kwa: Neno, Sakramenti, Sala na Matendo ya huruma
Waamini waboreshe maisha kwa: Neno, Sakramenti, Sala na Matendo ya huruma

Mwinjili Luka anatuonesha tena kundi la wale walio karamuni wapo hata na watu wasio mjua Yesu. Wapo pia wapagani na watu wa mataifa kutoka kila rangi na kabila na taifa. Hivyo karamu ni kwa ajili ya watu wa ulimwengu mzima wanaokuwa tayari kuyafananisha maisha yao na kweli za Injili. Wapendwa ni mwaliko wa kuliishi Neno la Mungu ambalo kila mara tunalisikia na kulitafakari, haitoshi kulijua tu kwa akili bali tunaalikwa kuliishi katika maisha ya kila siku. Imani haina likizo, hakuna nyakati ambazo tunasamehewa na hivyo kuruhusiwa kuishi kinyume na imani yetu. Nawaalika kama tunavyosali leo katika sala baada ya Komunyo; Ee Bwana, tunakuomba dawa ya rehema yako ituponye kabisa. Ni kweli na haki kwani bila uponyaji na neema zake hatuwezi sisi wenyewe kuufikia wokovu. Uinjilishaji wa kweli na wa kina sio tu kwa maneno yetu bali haswa kwa ushahidi wa maisha yetu. Ulimwengu leo unaweza kumgeukia Mungu hasa kwa mwanga wa maisha yetu sisi tunaomwamini Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo shime tumwombe Mungu atujalie neema zake za kuwa jasiri wa kuishi imani yetu kwa maisha yetu. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

18 August 2022, 16:02