Tafakari Dominika ya 20 Mwaka C: Moto na Ubatizo: Utakaso na Wokovu Ili Kuwa Mashuhuda
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma
Amani na Salama! Tunaishi na kusafiri katika ulimwengu wa uimla wa maadili, ni ulimwengu ambapo uovu unaonekana ni sawa na haki kabisa, na kinyume chake wema unakosa mashiko na misingi yake. Ni ulimwengu ambao sauti ya kinabii imekuwa adimu kabisa. Manabii ni kweli ni wale wanaotukumbusha kuwa uovu ni uovu na hatuna budi kuuepuka kwani unaangamiza maisha yetu, na pia kutuhimiza kutenda yaliyo mema kwani ndio yanayotuhakikishia amani na salama yetu. Nabii Yeremia anaonya na kukaripia uovu ulioenea kwa mfalme na kwa wakazi wa mji ule wa Yerusalemu. Leo ni wajibu wetu Wabatizwa kuwa sauti ya kinabii kuanzia katika familia zetu na kwa ulimwengu mzima. Kuwa sauti inayowakumbusha watu umuhimu wa kuenenda kadiri ya mapenzi ya Mungu na si kinyume chake. Tunaweza kuwa na mifano mingi juu ya mmomonyoko wa maadili katika familia na jamii yetu kwa ujumla. Tunaishi katika jamii ambayo maadili hayana tena nafasi, kila mmoja ruksa kutenda na kufanya kadiri anavyoona yeye inampendeza, ni jamii isiyoona nafasi na umuhimu wa misingi ya maadili yetu, yaani Mungu mwenyewe. Kuenenda kama watu wenye hofu ya Mungu, tunaokiri kuwa sisi ni wana na watoto wa Mungu, hivyo njia na namna zetu hazina budi kuakisi ukweli huu.
Njia za mawasiliano leo zinatumika kinyume na maadili yetu. Ni mara ngapo mitandao ya kijamii inatumika hata na sisi Wabatizwa kueneza na kusambaza mambo yanayokuwa kinyume na maadili yetu? Mwenyeheri Carlo Acutis kijana mtakatifu alitambua hatari ya kujilinda na hivyo kuepuka matumizi mabaya au yanayokwenda kinyume na imani yetu. Hatuna budi nasi kuinjilisha kwa kuwa na matumizi chanya na yenye kutujenga kiroho kuliko kuenenda kadiri ya mitindo na mantiki ya ulimwengu huu. Kipimo chetu daima ni Yesu Kristo mwenyewe, aliye nabii wa kweli na wa milele. Yesu Kristo ni nabii wa manabii! Maisha yetu na namna zetu hazina budi kumuakisi Yesu Kristo. Ni Yesu Kristo aliye kweli, njia na uzima, hivyo hatuna budi kuyafananisha maisha yetu na kweli za Injili. Kuishi sio tena kwa mantiki na namna zetu bali kwa kuongozwa na mantiki ya Injili. Wakristo tunaalikwa kuishi maisha ya nuru, ndio maisha ya ushuhuda, ndio maisha ya kuwaonesha wengine njia, ukweli na uzima. Yesu leo anazungumzia juu ya moto na ubatizo, kwa hakika ni lugha ngumu kueleweka kirahisi kwetu. Yesu anatumia lugha ya picha, hivyo hatuna budi kuelewa vema maana ya lugha inayotumika na Yesu ili tuweze kupata ujumbe kusudiwa.
Katika Agano la Kale mara baada ya gharika kuu tunaona Mungu anaweka ahadi ya kutoangamiza tena dunia kwa maji bali kwa moto. (Mwanzo 9:11) Ni kwa moto Mungu ataleta haki ulimwenguni. (Isaya 66:16) Hata Yohane Mbatizaji katika Agano Jipya tayari anazungumzia kuwa Masiya atatubatiza katika Roho Mtakatifu na kwa moto. (Mathayo 3:11-12) Hivyo hata Yesu leo anazungumzia kuja kuleta moto ulimwenguni. Hata mitume wa Yesu, Yakobo na Yohane wana wa Zebedayo wanamuomba Yesu ashushe moto kutoka mbinguni ili kuja kuwaangamizi Wasamaria waliokataa kumkaribisha Yesu katika vijiji vyao. (Luka 9:54) Na wazo linalotujia mara moja pia ni juu ya moto utokao mbinguni na kuja kuwaangamiza wale wote wanaokwenda kinyume na Amri na maagizo yake wakati wa mwisho wa nyakati, yaani mwisho wa ulimwengu ndio wakati wa parusia. Nawaalika kutafakari vema kwani kinyume chake tunaweza kujikuta tunakuwa kinyume na Habari Njema, na Wema na Huruma ya Mungu na hivyo kuanza kuwa na sura potofu ya Mungu. Kwa hakika yafaa tuingie katika kuelewa aina ya uandishi na lugha inayotumika ili kuweza kupata ujumbe wa sehemu ya Injili ya Dominika ya leo. Moto wa Mungu hauna lengo wala shabaha ya kuangamiza na kuwaondoa wadhambi kutoka katika sura ya dunia bali ni chombo cha kututakatifuza ili kuachana na dhambi, ni chombo cha kututakasa ili kuachana na dhambi. Siyo moto wa kuja kulaani na kuangamiza watu kwani hiyo kwa hakika sio Habari Njema kwa mwanadamu na wala haileti furaha na matumaini kwa yeyote anayeisikia.
Najua kuna wahubiri wengi wanapenda kutumia lugha ya kutisha na kuogofya watu na kuona Mungu basi ana hulka sawa na sisi wanadamu dhidi ya wale wanaokuwa kinyume chake. Nawasihi ni vema kuacha kuwa na Sura ya Mungu inayopotosha na kuwa kinyume na Injili: Injili ni Habari Njema yenye kuleta furaha na matumaini kwa kila inayemfikia! Moto wa Neno lake unaokuja ili sisi wadhambi tupate kuponywa na kujaliwa uzima wa milele na si kinyume chake. Ni moto wa Roho Mtakatifu uliowashukia Mitume siku ile ya Pentekoste unatushukia nasi kila mara tumuombapo ili kuweza kujua mapenzi yake na kuyashika katika maisha yetu. Ni moto unaokuja kututia joto la kuweza kushuhudia wema na huruma ya Mungu kwa watu wote, kuweza kuwa mashuhuda wa kweli zile za imani katika maisha yetu ya kila siku. (Matendo 2:3-11) Na ndio hamu ya Yesu kuona kuwa moto huo wa Mungu kuwa umewaka katika ulimwengu wetu, katika nafsi za kila mmoja wetu ili kuangamiza kila aina ya uovu na dhambi, na ndio magugu katika mioyo yetu yanaokinza ile mbegu njema ya Neno la Mungu kuweza kumea na kukua na kutoa matunda.
Ishara ya pili iliyokaribu na huo moto ndio Ubatizo. Neno Ubatizo linatokana na neno la Lugha ya Kigiriki batezo, likimaanisha zamisha. Hivyo ni hamu yake Yesu kutaka kuzama katika mateso na kifo na ufufuko wake ili kuukomboa ulimwengu, ili kutupatia uzima wa kimungu kila mmoja wetu, ili kurejesha uhusiano uliovunjika kati ya mwanadamu na muumba wake. Maji ya ubatizo wa Yesu ndio kifo chake kilichokuwa kimeandaliwa na watesi wake ili kuuzima moto wa Neno lake, wa upendo wake wa kimungu, moto wa Roho wake ya Kimungu yaani Roho Mtakatifu ila matokeo yake sisi tumepata kuponywa na ukombozi wetu. Pasaka ni uumbaji mpya, ni mwanzo wa nyakati mpya, ni mwanzo mpya kwa kila mmoja wetu kwani sasa tunatembea katika mwanga na si wana tena wa giza kwani tupo huru kama wana wa Mungu na si watumwa tena wa yule mwovu. Na ndio Yesu anatukumbusha pia wanafunzi wake kuwa kama Yeye aliye Bwana na Mwalimu amekunywa kikombe kile cha mateso na kifo basi anatuandaa nasi kukumbuka ulazima wa kupitia njia ile ile ya msalaba ya kuteswa na kukataliwa na kufanyiwa kila aina ya ubaya kama ambavyo amepitia Yeye aliye Bwana wetu.
Hakuja kuleta amani duniani bali migawanyiko, ndiyo lugha ya kutualika kila mara kutambua kuwa kwa kumfuasa Kristo tutabaguliwa na kutengwa hata na watu wetu wa karibu kama wazazi au ndugu. Ujumbe wa Injili daima ni moto kwani unakuja kututoa katika hali zetu za zamani na kuanza maisha mapya. Ni ujumbe unaokuja kuangamiza na kutetekeza kila aina ya uovu na ubaya ndani mwetu. Ni ujumbe wa kubadili vichwa na namna zetu iwe za kufikiri au za kutenda. Na kwa kuwa mashuhuda wa Injili hakika tutakutana na ukinzani na upinzani wa kila aina, kwani bado kuna wale wasiokuwa tayari kuangamiza na kuteketeza ndani mwao yao yalio ya ulimwengu huu na kuanza kufuata mantiki mpya, mantiki ya Mungu mwenyewe. Ndugu zangu, yafaa kuwa makini kwani Injili sio chuki, sio magomvi au vita kwa wale wanaokinza au kuwa kinyume nayo kwani narudia ikifikia hapo basi inakoma kuwa Habari Njema inakuwa kitu kingine. Mipasuko na migawanyiko anayozungumzia Yesu haipaswi kutokana na mapungufu yetu au hulka na tabia zetu bali ni kwa wale wasiokuwa tayari kubadili vichwa vyao, kwa maana ya kuisikiliza na kuishi kadiri ya moto wa Neno la Mungu. Hivyo si kwamba Yesu anatutuma kuwa kama wanaharakati au wapigania uhuru kutoka na kuanza kushambuliana na kila mmoja anayekuwa kinyume na Injili, la hasha hilo sio kusudi na wala sio maana ya Injili ya leo. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.