Tafuta

2022.08.17 Askofu Kilaini, wa Jimbo katoliki la Bukoba Tanzania anapongeza vyama vya kitume kama  vile vya vijana,Wawata na Utoto Mtakatifu. 2022.08.17 Askofu Kilaini, wa Jimbo katoliki la Bukoba Tanzania anapongeza vyama vya kitume kama vile vya vijana,Wawata na Utoto Mtakatifu. 

Ask.Kilaini:Vyama vya kitume vinaimarisha Kinisa

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania amepongeza Umoja wa Wanawake wakatoliki Tanzania(WAWATA)kwa mchangomkubwa wanao utoa kwa Kanisa,lakini hata Utoto Mtakatifu,TYCS na Jumuiya Ndogondogo.Hata hivyo anahamasisha Umoja wa Wanaume Wakatoliki Tanzania(UWAKA)ili wawe na mwamko zaidi katika shughuli za kichungaji.Amesisitiza hayo akizungumza na Vatican News.

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Askofu Msaidizi wa Jimbo katoliki la Bukoba, Tanzania, Askofu Methodius Kilaini akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican hivi karibuni ameelezea juu ya shughuli za kichungaji kwa ujumla katika Jimbo lake katika fursa ya kutimiza miaka 50 tangu kupewa daraja la ukuhani mnamo 1972. Katika mahojiano hayo Askofu alilisisitizia utume hasa haja ya kuimarishwa kwa vyama vya kitume jimboni. Askofu Kilaini alisema kwamba katika vyama hivyo kuna vingine ambavyo vinatenda kwa haraka sana kama vile Umoja wa Wanawake Katoliki Tanzania (WAWATA). Kwa uzoefu wake, alibainisha jinsi ambavyo hajawahi kuona kama kuna umoja mwingine ambao unafaulu vizuri zaidi ya  umoja wa wanawake na si  tu Bukoba,  lakini pia kwa Tanzania nzima ambapo kwa ujumla  umoja huu unasaida sana kuhamasisha vyama vingine.

Miaka 50 ya Ukuhani ya Askofu Methodius Kilaini,Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania
Miaka 50 ya Ukuhani ya Askofu Methodius Kilaini,Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania

Baada ya umoja huo askofu alisema kwamba kuna vyama vingine ambavyo alivigawa katika sehemu mbili kuwa  kuna vyama vya ibada na kuna vyama vya utendaji, au jumuiya kama chama cha utoto Mtakatifu, ambacho kinapaswa kuimarishwa zaidi ili watoto wazuri wakae pamoja, wajifunze mambo kwa  pamoja, na  desturi pamoja.  Hata hivyo Chama hicho katika jimbo kinaendelea  vizuri kwa msaada wa watawa na WAWATA!

UMOJA WA WANAWAKEKATOLIKI TANZANIA(WAWATA)
UMOJA WA WANAWAKEKATOLIKI TANZANIA(WAWATA)

Kikundi kingine ni cha vijana na  ambacho Askofu Kilaini alisema ni kigumu. Kikundi cha kwanza ni kile cha Umoja wa Vijana Katoliki Tanzania(TYCS) ambacho ni rahisi sana kwa sababu wako katika mazingira ya pamoja na katika shule zote za Msingi na sekondari, kikundi hiki kipo.Tatizo linakuja pale ambapo vijana wanapomaliza shule na kurudi kijijini. Wengi wengi wao wanatawanyika, wanapotea na kuishia kuoa wakiwa vijana sana. Kwa njia hiyo mapadre wanajitahidi sana katika maparokia yao. Na zaidi kitu kinachosaidia vijana wengi ni kwaya. Hata kama wanapotea kidogo, lakini angalau wanarudi, hivyo kwaya wakati mwingine zinasaidia kurudisha vijana na Askofu amesisitiza kuwahamasisha hasa kwa kuanzisha hata shughuli ndani ya kwaya ambayo inaweza kuwasaidia kujitegemeza kidogo.

CHAMA CHA UTOTO MTAKATIFU
CHAMA CHA UTOTO MTAKATIFU

Kikundi kingine kigumu ambacho Askofu Kilaini alikitaja  ni kikundi cha akina Baba, yaani Umoja wa Wanaume Katoliki Tanzania (UWAKA). Akifafanua zaidi ametoa mfano hata wa kuwahamasisha waweze kuvaa hata sare ya nguo  ili wafanane kidogo, lakini hakuttosha  kwa maana ni kazi kubwa kuwaweka pamoja. Askofu alikiri kwamba "ingawa wapo katika uongozi lakini kuwaweka pampja, hawana muda,  wana shughuli nyingi sana; si wabaya lakini ni shughuli tu". Askofu Kilaini  akijibu swali ni kwa nini inakuwa ngumu kuwa na mwamko kama wanawake, alijibu kwamba: "Ni  kwa sababu ni wanaume". Alitoa mfano alipokuwa katibu Mkuu wa  Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) huko Dar Es Salaam   kwamba walikuwa wakijaribu kukopesha. Na iwapo wangekopesha kikundi la hakina mama, walikuwa wanafanya vitu vizuri na kwa haraka wanarudisha fedha hizo. Lakini kwa kundi la akina baba walikuwa wakizila tu bila kurudisha.

CHAMA CHA UMOJA WA WANAUME KATOLIKI TANZANIA (UWAKA)
CHAMA CHA UMOJA WA WANAUME KATOLIKI TANZANIA (UWAKA)

Suala jingine ambalo Baba Askofu Kilaini alijikita nalo kuhusu suala la kufanya kazi kwa ushirikiano na wanawake na wanaume kama wito wa Baba Mtakatifu Francisko anavyo hamasisha na yeye mwenyewe kuanzisha suala hili katika Curia Romana, alithibitisha kwamba hata hivyo Tanzania iko tayari katika suala hili kwani tayari inaonekana katika uongozi wa kuongozwa na Rais mwanamke. "Mambo mengi yanaonekana kubadilika. Wanawake wengi wanafanya kazi nzuri.  Wanawake waliachwa nje na mambo mengi yakabweteka, yakawa ya kiume kiume, lakini ambayo hayaendi. Kwa njia hiyo shukrani kwa Baba Mtakatifu ambaye kwa sasa Vatican tunao viongozi wanawake ambao wanafanya kazi pamoja na wanaume. Kristo alitengeneza mapadre kwa ajili ya Misa, lakini mambo mengine sio misa ambayo inawezekana kabisa kufanywa na wanawake na hivyo wanawake  wanaweza", alisisitiza Askofu Kilaini. Kwa kuhitimisha sehemu hii  kuhusu uongozi wa Wanawake katika kila ngazi ya kijamii na kikanisa Askofu Kilaini alisema: " Kwa maana hiyo, kwa kuongeza wanawake katika uongozi wa Kanisa utaleta ladha ya kimama na ni nzuri, shukrani kwa hili".

ASKOFU KILAINI:WAWATA,VIJANA NA UWAKA
17 August 2022, 14:32