Tafuta

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Salana kazi vinakamilishana katika maisha ya mwamini. Tafakari Neno la Mungu Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Salana kazi vinakamilishana katika maisha ya mwamini.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 16 Mwaka C wa Kanisa: Sala na Kazi Ni Mambo Yanayokamilisha Katika Utume

Sala na Kazi ni mambo yanayopaswa kumwilishwa kikamilifu katika maisha ya wafuasi wa Kristo. Yesu anamwonya Martha aliyejitaabisha mno kwa mambo ya kidunia na kwamba, alihitaji pia kusikiliza Neno la Mungu, kama alivyokuwa anafanya Maria. Wakristo wajibidishe kuwahudumia ndugu zao wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama ushuhuda wa imani tendaji! Neno!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sala na Kazi ni chanda na pete na wala hakuna msigano wa aina yoyote ile; ni mambo yanayopaswa kumwilishwa kikamilifu katika maisha ya wafuasi wa Kristo. Yesu anamwonya Martha aliyejitaabisha mno kwa mambo ya kidunia na kwamba, alihitaji pia kusikiliza Neno la Mungu, kama alivyokuwa anafanya dada yake Maria, huu ndio mwelekeo sahihi kwa mfuasi wa Kristo. Wakristo wajibidishe kuwahudumia ndugu zao wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, huku wakiendelea kujitajirisha katika maisha yao ya kiroho kwa njia ya sala. Simulizi la Martha na Mariamu ni moja kati ya masimulizi yanayotushangaza tunapolisikia kwa mara ya kwanza. Tunajiuliza, iweje Yesu haoni juhudi za ukarimu na makaribisho ya Martha dhidi ya umbu lake, yaani Mariamu aliyeketi miguuni kwa Yesu na kumsikiliza? Hata baadhi ya wataalamu wa Maandiko Matakatifu mara nyingi wanatumia sehemu hii ya Injili kujaribu kueleza aina mbili ya maisha yaani yale ya taamuli na maisha ya kisekulari. Watawa wakaa pweke au ndani kwa ajili ya maisha ya sala na tafakuri wao wamechagua fungu lililo jema. Na kinyume chake mapadre wa jimbo na wale wa maisha ya kitume wanaobaki nje na kujishughulisha na mambo mengi ya kitume na kichungaji na hata pia walei wanaojitoa kwa sadaka zao mbali mbali katika kueneza ufalme wa Mungu, kundi hili basi wamechagua fungu lisilo jema kama lile la Mariamu.

Tafsiri hiyo au hata zile zifananazo na hizo si sahihi kwa sababu nitakazojaribu kuzieleza hapa chini. Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa tulisikia mfano au simulizi lile la Msamaria, na Yesu anatualika nasi kuenenda na kutenda kama Msamaria yule. Ila kinyume chake Yesu anamsifu mwanamke aliyekuwa ameketi miguuni kwake bila kufanya lolote. Ni Yesu anajipinga katika mafundisho yake? Msamaria alitenda wema na ukarimu kwa yule mtu mmoja aliyekuwa karibu kufa njiani, lakini leo Mariamu anakaa miguuni kwa Yesu akimsikiliza wakati nduguye Martha akitumika kwa ukarimu wa kawaida wa nyumbani. Mariamu leo hatuoni akitenda jambo la ukarimu na wema isipokuwa anamsikiliza Yesu. Mwinjili Luka anatuonesha kuwa Yesu anasifu fungu alilochagua Mariamu kuwa amechagua fungo lililo jema na wala haoneshi kuwa Yesu alipinga au alikuwa kinyume na kile alichokuwa anafanya dada yake Martha. Martha alifanya akiwa na malalamiko na hivyo kupoteza umaana wa kile alichokuwa akikifanya. Na hata Martha mwenyewe hakuona umaana wa kile alichokiwa akikifanya na ndio anaenda kwa mgeni wao yaani Yesu na kumshitakia dada yake mdogo Mariamu. Kutenda hakuna budi daima kutanguliwa na sala, ni baada ya kujua na kutambua nini ni mapenzi ya Mungu katika maisha yetu.

Choteni nguvu ya utume katika Neno la Mungu, Sala na Sakramenti za Kanisa
Choteni nguvu ya utume katika Neno la Mungu, Sala na Sakramenti za Kanisa

Mwinjili Luka mara kadhaa huwa anatuonesha Yesu akiwa ameketi mezani katika nyumba za watu fulani fulani, iwe ni wale wenye haki au wema na hata kati ya Mafarisayo. (Luka 7:36; 11:37; 14:1) Lakini pia alifika katika nyumba za watoza ushuru na wadhambi (Luka 5:30; 15:2; 19:6). Na leo tunamuona katika nyumba ya hawa ndugu au dada wawili, nyumbani kwa Martha na Mariamu kadiri ya Mwinjili Luka. Yesu anafika na kuingia katika nyumba na maisha ya familia, ndio kusema anataka kufanya makazi yake katika makazi ya familia ya kila mmoja wetu. Martha aliyekuwa dada mkubwa, mara moja anajituma na kufanya kitu fulani kwa ajili ya makaribisho ya ukarimu kwa mgeni wao. Ni kawaida kabisa hata katika familia zetu mgeni anapofika basi wakina mama wanajibidisha kwa ukarimu kumwandalia kitu fulani, na katika muktadha huu ni hakika Yesu alifuatana pia na wanafunzi wake, na hivyo walikuwa wageni wanaume idadi ya kutosha iliyomtaka si tu Martha peke yake, bali hata na umbu lake aungane naye katika maandalizi yale. Mariamu aliye mdogo kiumri na hapa badala ya kuona haja ya kuungana na dada yake katika maandalizi yale anabaki miguuni mwa Yesu akimsikiliza bila kufanya kitu kwa mtazamo hata wetu pia.

Mariamu alikuwa ameketi miguuni mwa Yesu. Kuketi miguuni mwa mwalimu kwa lugha ya kibiblia ina maana ya kuwa mfuasi na hivyo aliyeruhusiwa kuketi miguuni ni mwanafunzi au mfuasi aliyetaka kujifunza kutoka kwa Rabi au Mwalimu. Katika Kitabu cha Matendo ya Mitume tunaona Mtume Paulo anatuambia aliketi miguuni mwa Gamalieli, aliyekuwa mwalimu mashuhuri wa nyakati zake. (Matendo 22:3) Hivyo Mwinjili Luka kwa makusudi mazima anatueleza mkao wa Mariamu ndio kusema Mariamu alichagua kuwa mwanafunzi wa Yesu. Mariamu anatambua ni nini kilimfanya Yesu afike na kuingia katika nyumba na makazi ya familia yao. Yesu anakuja kwa nafasi ya kwanza kama Mwalimu na Bwana wetu, na hivyo hatuna budi nasi kuchukua nafasi yetu stahiki, yaani ya kuwa wanafunzi wake, kwa kukaa miguuni mwake na kumsikiliza. Labda nyakati zetu hatuoni shida kuona Mariamu anaketi miguuni na hivyo kuwa mwanafunzi wa Yesu, kwa nyakati zile kilikuwa ni kitu kigeni na kushangaza kwani hakuna Rabi wala mwalimu yeyote angekubali na kumpokea mwanamke kuwa mwanafunzi wake. Marabi walikuwa na msemo: “Ni heri kuichoma Biblia kuliko kuiweka mikononi mwa mwanamke.” Na hata wanawake wasingeruhusiwa kusali au kuombea chakula mezani na hata akienda kwenye Sinagogi basi ilibidi ajifiche na sio kukaa waziwazi.

Neno la Mungu liwe ni dira na mwanga katika maisha na utume wenu
Neno la Mungu liwe ni dira na mwanga katika maisha na utume wenu

Mtazamo huu ulikuwepo si tu kati ya Wayahudi bali hata katika Jumuiya za Wakristo wa mwanzo, wanawake katika mikusanyiko ya kiibada hawakupaswa kuongea chochote wala kuuliza na kama walikuwa na maswali basi walipaswa kuwauliza waume zao warejeapo nyumbani. (1Wakorintho 14:34-35) Yesu leo anavunja na kuondoa mtazamo huo uliwatenga na kuwaweka nafasi ya nyuma wanawake, na ndio anatualika hata nasi kubadili vichwa vyetu, kubadili mtazamo wetu mintarafu nafasi ya mwanamke katika familia, jamii na hata katika Kanisa. Hivyo Yesu ni mwanamapinduzi wa fikra na tamaduni za namna hiyo kwani anampokea Mariamu na kumfanya mmoja kati ya wanafunzi wake. Na ndio Yesu anatualika nasi leo kupokea mwaliko wake wa kuwa wanafunzi wake, kuketi miguuni pake na kumsikiliza na kujifunza kutoka kwake kabla ya kutoka na kwenda kufanya lolote. Ni Yesu leo anapanua uwanda wa wanafunzi wake kuwa sio tena wa kubagua jinsia au rangi au utaifa au tofauti nyingine zozote zile, kila mwanadamu anaalikwa kumpokea Yesu nyumbani kwake na kubaki miguuni mwake ili kujifunza kutoka kwake aliye Bwana na Mwalimu wetu. Mwinjili Luka pia anatuonesha kinyume na utamaduni wa nyakati zile kwani anaanza sehemu ya Injili ya leo kwa maneno kuwa; “…Mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake”.

Haikuwa inakubalika kwa mwanamke kumwalika mwanaume na kupokea mwaliko huo. Na ndio unaona Mwinjili Luka tofauti na Mwinjili Yohane hamtaji hapa kaka yao akina Martha na Mariamu yaani Lazaro. (Yohane 11 & 12:1-8) Mwinjili Luka ni mmoja kati ya waandishi wanaoonesha kinagaubaga juu ya mapinduzi ya tamaduni na fikra aliyotuletea Yesu. Mwinjili Luka anatualika hata nasi kukata na kubadili vichwa vyetu. Mwinjili Luka anaonesha waziwazi nafasi na hadhi ya mwanamke kutoka katika mafundisho ya Yesu Kristo. Yesu analeta mapinduzi makubwa ya kitamaduni na ya kifikra kwani mbele yake la muhimu ni kuwa wanafunzi wake na siyo jinsia au rangi au kabila au taifa au tofauti zetu zozote zile. Ujumbe wake ni kwa ajili ya watu wote bila ubaguzi wa aina yeyote ile. Na ndio leo Papa Fransisko anatualika kutembea na kuishi Kanisa la Kisinodi. Kanisa la Kisinodi ni lile lisilomuacha yeyote pembeni wala nyuma, lisilombagua yeyote yule kwani ujumbe wa Injili ni kwa ajili ya kila kiumbe.

Na ndio maana Baba Mtakatif Francisko anatualika kuona ukombozi ni kwa ulimwengu mzima na ndio maana tunaalikwa hata kuitunza kwa upendo na uangalifu nyumba yetu ya pamoja, yaani ulimwengu mzima. Ukombozi wa kweli unagusa ulimwengu mzima, unagusa kila kiumbe kwani ni mpango wa Mungu tangu awali kuwa kila kiumbe kinatangaza ukuu na uweza wake, na ndio wimbo wa Laudato si’, mi’ Signore wa Mtakatifu Francisko wa Assis. Na ndio mada kuu iliyojadiliwa na mkutano mkuu wa Amecea unaomalizika leo hapa nchini kwetu Tanzania. Kumuona Mungu katika uumbaji, kwani nje ya uumbaji hatuwezi kuonja wema na ukuu wake, ni katika uumbaji tunakutana na Mungu na hata kwa wale wasiomwamini Mungu bado wanakiri ukuu na uweza wake kwa kazi yake ya uumbaji. Na vema pia kukumbuka kuwa Injili haisemi kuwa Mariamu alikuwa amezama katika sala au tafakuri, bali alikuwa akisikiliza Neno la Yesu, na sio maneno kama baadhi ya tafsiri zinavyosomeka. Maria anabaki kuwa mfano wa kusikiliza Neno la Yesu Kristo.  Hayakuwa mazungumzo ya kawaida kama yale tunayokuwa nayo tunapotembeleana majumbani bali ni juu ya Neno la Mungu. Mariamu alitambua kabla ya kutenda alipaswa kujifunza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Tunaposali haitoshi tu sisi kuongea bali yafaa kutambua pia kuwa na nafasi ya kumsikiliza Mungu, ya kukaa miguuni mwake kwa ukimya kama wa Mariamu, na hii ndio sifa ya mwanafunzi na mfuasi wa kweli, ya kuwa msikilizaji mzuri na kisha kutoka na kwenda kutenda.

Waamini choteni nguvu, neema na baraka kutoka kwenye Neno la Mungu
Waamini choteni nguvu, neema na baraka kutoka kwenye Neno la Mungu

Na moja linatutafakarisha zaidi leo ni ukimya wa Mariamu kwani Mwinjili Luka kuanzia mwanzo wa simulizi hili mpaka mwisho hatusikii hata neno moja kutoka kinywani mwa Mariamu. Ni ajabu! Ila ni fundisho kwetu tunaotaka kuwa wanafunzi wa Yesu. Ni katika nguvu ya ukimya nasi tunakutana na Mungu anaandika Kardinali Robert Sarah katika Kitabu chake “The Power of Silence”, yaani “Nguvu ya Ukimya” (Kwa tafsiri yangu siyo rasmi) Ni katika ukimya hapo tunakubali Mungu aongee nasi, atuoneshe na atufundishe mapenzi na mpango wake katika maisha yetu. Itoshe leo kutolea mfano mazungumzo ya Mtakatifu Mama Teresa wa Kalkuta na Padre kijana kabisa ambaye leo hii ndiye Kardinali Angelo Comastri, aliyekuwa Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Kardinali Angelo katika Kitabu chake anamuelezea Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta kama mwanamke wa ukimya na tafakuri, na katika ukimya huu daima aliunganika na Mungu. Kwake kusali na kubaki katika ukimya huo mkubwa ni sawa na kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa roho yote, hivyo kutenga muda wa kukaa naye na kumsikiliza. Kardinali Angelo akiwa Padre kijana alifika kumuona Mtakatifu Mama Theresa si tu kuongea naye bali hasa kuomba sala zake.

Mama Theresa akamjibu kuwa daima anasali kwa ajili ya mapadre na hapo pia akamuuliza Padre kijana Angelo Comastri kuwa anasali masaa mangapi kila siku? Pamoja na jibu ambalo labda wengi wetu tungelijibu lakini naomba hapa ninukuu sio kwa tafsiri sahihi sana maneno ya Mtakatifu Mama Theresa kwa Padre Angelo: “haitoshi mwanangu! Katika upendo tunafanya kila linalowezekana…wadhani naweza kufanya tendo lolote la upendo na huruma bila moyo wangu kujazwa na upendo wa Yesu? Waamini kuwa naweza kwenda mitaani na kuwakusanya maskini na wahitaji bila moyo wangu kuwaka na mapendo ya Yesu mwenyewe? ... Soma vizuri Injili: Yesu katika sala alitolea sadaka hata matendo ya huruma. Wajua kwa nini? Ni kwa nia ya kutufundisha kuwa bila Mungu tunakuwa maskini kiasi cha kushindwa kuwasaidia maskini! Bila Mungu sisi ni maskini na katika umaskini huo hatuwezi kutoka na kuwasaidia wengine. Hatuwezi kutoa kitu ambacho hatuna, upendo wetu lazima uangazwe na moto wa upendo wa Mungu kwanza. Kinyume chake tunabaki kama Martha wenye mahuzuniko na malalamiko katika utendaji wetu.” Sasa turejee katika Injili yetu ya leo na hasa jibu la Yesu kwa Martha ambalo mara kadhaa linatusumbua kupata ujumbe kusudiwa.

Kazi ni utimilifu wa maisha ya mwanadamu, iimarishwe kwa sala.
Kazi ni utimilifu wa maisha ya mwanadamu, iimarishwe kwa sala.

Yesu hamgombezi Martha kwa kuwa anafanya kazi, la hasha, na badala yake ni ile hali yake anayokuwa nayo, ndio hasa tunaweza kusema hasira na ghadhabu yake ya kihisia kuona anatumika peke yake bila msaada wa ndugu yake. Na hii inatokana na yeye kuamua kutenda kabla ya kuketi miguuni mwa Yesu na kulisikiliza Neno la Mungu. Ni hali hiyo tunajikuta nayo hata nasi katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku na hata utume wetu tusipo mtanguliza kwanza Mungu, kupata wasaa wa kuketi miguuni mwake na kumsikiliza. Tutafakari utume wetu wa kila siku iwe maparokiani kwa wachungaji wetu au katika familia zetu kwa walei au katika jumuiya zetu kwa watawa. Ikiwa hatutaanza kwa kumsikiliza Mungu, kwa sala na tafakuri ya ndani daima mwisho wake ni uchovu na malalamiko na manung’uniko na kuishia kurusha lawama kwa wengine. Iwe ni makasisi parokiani ni vema kuchunguza majitoleo yetu chimbuko na chanzo chake ni nini? Ni bidii na nguvu na akili zetu au tunachota kwa Mungu mwenyewe? Ikiwa katika familia au jumuiya yeyote ile tujiulize na kama sio nawaalika daima turejee maneno ya Mtakatifu Mama Theresa kwa Padre Kijana ambaye leo ni Kardinali Angelo Comastri, tunachota wapi nguvu za kutenda mema kama sio kwa Kristo mwenyewe. Tukumbuke sisi bila Mungu ni maskini kiasi kwamba hatuwezi kusaidia maskini wengine!

Pamoja na kwamba Yesu hapingi bidii zetu ila anatukumbusha kabla ya yote, la kwanza ni ulazima wa kuketi miguuni mwake na kusikiliza Neno lake na ni baada ya hapo tunaweza kutoka na kwenda kutenda. Na hapo tutatenda bila lawama wala malalamiko wala kughadhibika kwani matendo yetu yataongozwa na moto wa Neno na upendo wake wa Kimungu. Tusithubutu kutenda lolote bila kwanza kuketi miguuni mwake! Ni miguuni kwa Yesu tunajifunza mapenzi na mpango wa Mungu lakini zaidi tunachota neema na nguvu ya kutumikia kadiri ya mpango huo, kinyume chake ni malalamiko na mahangaiko, ni kuona tunaonewa na kulemewa na shughuli, tunabaki watu wa kulalamika kuwa tupo busy, tunachoka kwa kazi nyingi! Mazungumzo ya Yesu na Martha na Mariamu ni kama yanakosa hitimisho kadiri ya Injili ya leo. Ila Mwinjili Luka mpaka mwisho anazidi kutuonesha ukimya wa Mariamu. Mariamu hasemi wala hatamki neno lolote iwe la kujitetea ua kujieleza kwa nini anafanya hicho anachofanya, na hivyo kuweka wazi nia yake iliyojificha ndani mwake. Ni ishara tosha kuwa ukimya wake ni baada ya kuelewa Neno la Yesu hivyo linabaki katika moyo na kuwa mwongozo wa maisha yake akibaki akilitafakari. Kila anayelisikiliza Neno la Yesu na kuongozwa naye anabaki bila maneno mengi kwani anabaki na amani na utulivu wa ndani kinyume chake ni malalamiko yasiyokuwa na mwisho na kutupia kila mtu lawama. 

Kazi iboreshwe kwa sala na Neno la Mungu
Kazi iboreshwe kwa sala na Neno la Mungu

Tujitafakari hata nasi mara nyingi tunakuwa wa maneno mengi na lawama na manung’uniko kwa kuwa hatujapata wasaa wa kuketi miguuni mwa Yesu kwanza kabla ya kutenda. Amani na utulivu wa kweli tunaipata tunapojishikamanisha kweli na Yesu, tunapodumu kubaki miguuni mwake. Sasa ni Martha anayepaswa kuketi miguuni mwa Yesu na kusikiliza Neno la Yesu ili naye apate utulivu wa ndani na amani ya ndani na hivyo kuondokana na malalamiko na lawama na hasira. Martha ni mkarimu na mchapakazi kweli kweli ila anakosea nini kianze katika maisha yake, na ndio daima tunakumbushwa na kufundishwa na Injili ya leo daima maisha yetu yaongozwe na sala na kwa kutafakari Neno la Mungu. Neno la Mungu na sala ya tafakari haina budi kupewa kipaumbele katika maisha yetu ya siku kwa siku kama kweli tunataka kuenenda na kutenda kama rafiki zake Yesu. Hatuna budi kujifunza kwa mitume ambao walitambua maisha yao yalikosa ladha na maana mpaka walipoona wamuombe Yesu; Bwana tufundishe kusali. Na kwa hakika hii inapaswa kuwa sala yetu ya kila siku kumuomba Bwana na Mwalimu wetu atufundishe jinsi na namna nzuri ya kusali. Mtakatifu Tomaso wa Akwino kadiri ya masimulizi ya msaidizi wake Reginald anasema maandiko mengi ya Mtakatifu Tomaso hayakutokana na kusoma sana bali kutafakari sana, kwani katika kujihoji maswali mengi na magumu hata kuna wakati alikuwa anafika analaza kichwa chake katika Tabernakulo ili Yesu wa Ekaristi amfunulie siri za mbinguni.  

Akili zake hazinabudi kuangaziwa na Yesu mwenyewe, hivyo Taalimungu nzuri ni ile inayotokana na Mungu mwenyewe kujifunua na kuziangaza akili zetu ziweze kumjua vema na hivyo kumpenda kweli kweli! Na ndio hata leo Wanateolijio wengi wazuri sio wale wanaotumia masaa mengi maktaba na kusoma vitabu bali hasa wanaokuwa na muda wa kukaa kimya na kutafakari Neno la Mungu. Hakika kila anayechukua wasaa wake katika siku na kusali na kutafakari Neno la Mungu huyo atatenda kwa upendo bila malalamiko na bila lawama. Nawatakia tafakari na Dominika njema na huku tukijitahidi kila mmoja wetu kutenga muda wa kutafakari Neno la Mungu, kubaki miguuni mwa Yesu ili tujifunze mapenzi na mpango wa Mungu katika maisha yetu na hapo kujichotea neema za kuweza kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Mfuasi wa kweli anapaswa kuwa na sifa ya mwanafunzi mzuri, anayesikiliza kwa makini kabla ya kutoka na kwenda kutenda na kufanya. Bila Mungu tunabaki maskini kiasi kwamba hatuwezi kutoka na kwenda kuwasaidia maskini wengine! Bila Mungu hatuwezi kuwa na ukarimu na upendo wa kweli, tunabaki wenye malalamiko na manung’uniko yasio na mwisho!

 

13 July 2022, 16:12