Tafuta

Askofu Michael Msonganzila anakaza kusema, mwaliko kwa watu wa Mungu Afrika Masharki na Kati ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote. Askofu Michael Msonganzila anakaza kusema, mwaliko kwa watu wa Mungu Afrika Masharki na Kati ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote. 

Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA 2022: Utunzaji Bora wa Mazingira

Tanzania ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui yake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” AMECEA ni Mzazi wa Jumuiya Ndogo Ndogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, linaloundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea, linaadhimisha mkutano wake mkuu wa 20 Jijini Dar es Salaam. Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji. Huu ni mkutano ambao hufanyika kila baada ya miaka minne. Itakumbukwa kwamba, mkutano wa 19 wa AMECEA uliadhimishwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa 20 wa AMECEA inafanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Jijini Dar es Salaam, Dominika tarehe 10 Julai 2022 kuanzia majira ya Saa 3: 30 Asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuhitimisha Mkutano wa AMECEA, itaadhimishwa Dominika tarehe 17 Julai 2022 kwenye Viwanja vya Msimbazi Centre, Jimbo kuu la Dar es Salaam mahali palipozaliwa AMECEA kunako mwaka 1961.

Tanzania ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui yake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote ndiyo mada kuu inayoongoza mkutano wa AMECEA kwa mwaka 2022. Kimsingi Waraka unazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mkutano wa 19 wa AMECEA uliadhimishwa mjini Addis Ababa Ethiopia
Mkutano wa 19 wa AMECEA uliadhimishwa mjini Addis Ababa Ethiopia

Askofu Michael Msonganzila anakaza kusema, mwaliko kwa watu wa Mungu Afrika Masharki na Kati ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza mazingira bora, unapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha mchakato wa haki, amani, maridhiano, umoja na mshikamano wa kidugu. Mazingira ni kielelezo cha siri kuu ya kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa: kuyatunza, kuyaenzi, kuhyaheshimu na kuyaendeleza kama sehemu ya maboresho ya kazi ya uumbaji. Kwa njia hii, mwanadamu anamheshimu na kumtukuza, Mungu Baba Muumbaji. Kimsingi mazingira ni muhimu sana katika kukoleza ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kumbe huu ni wajibu wa kimaadili kutunza mazingira. Familia zijenge utamaduni wa kupanda na kutunza miti, ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi na hivyo kudumisha msingi wa haki, amani na maridhiano. Familia ziwe ni vitalu vya kuotesha miti ili kuendeleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Familia wawe ni wadau wakuu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma anahitimisha sehemu ya mahojiano maalum na Radio Vatican kwa kuwataka waamini na watu wenye mapenzi mema, kujikita katika wongofu wa kiikolojia, ili kuendeleza mchakato wa utunzaji bora wa mazingora nyumba ya wote kwani uhai wa mwamadamu unategemea ia ubora wa mazingira.

Itakumbukwa kwamba, Miongozo ya Mababa waanzilishi wa AMECEA ilikuwa kuimarisha Imani Katoliki na maendeleo endelevu na fungamani ya jamii kwa kuwa na Mpango mkakati wa muda mrefu uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa AMECEA uliofanyika Julai 1961, kwenye Ukumbi wa Msimbazi Center, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Dhamira kuu ilikuwa: “Kesho ya Kanisa la Bara la Afrika.” Tangu wakati huo, AMECEA kimekuwa ni chombo madhubuti za shughuli za kichungaji katika mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu wa kibinadamu, ushirikiano na mshikamano sanjari na maboresho ya huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kumekuwepo na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwa AMECEA. Kati ya matunda haya ni pamoja na uundwaji wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Kusimama kidete katika mchakato wa kutetea haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kulea dhamiri nyofu ili watu watende kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na utekelezaji wa dhamana na wajibu wa waamini katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

AMECEA ni Mzazi wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo
AMECEA ni Mzazi wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo

Ujenzi na uimarishaji wa Jumuiya ndogo ndogo za kikristo ni changamoto ya kichungaji iliyovaliwa njuga na Mababa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki, AMECEA na Kati tangu mwaka 1973 na kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kunako mwaka 1974. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani “Koinonia.” Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia.” Lengo kuu ni kuwawesha Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kimaadili na iutu.
Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kimaadili na iutu.

Kimsingi, Jumuiya ndogo za Kikristo ni chombo makini cha uinjilishaji, zinazosaidia kujenga na kuimarisha ujirani mwema, udugu na upendo wa Kikristo. Ni mhimili wa maisha na utume wa Kikristo katika kujenga imani, maadili na utu wema. Ni sehemu ya muundo wa Kanisa Mahalia Barani Afrika, katika maisha na utume wake. Ni mahali pia pa kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

Askofu Msonganzila AMECEA
08 July 2022, 13:52