Tafuta

Shirika la Masista wa Maria Imakulata “Sorores Mariae Immaculatae: SMI”, tarehe 23 Julai 2022 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wao nchini Tanzania. Shirika la Masista wa Maria Imakulata “Sorores Mariae Immaculatae: SMI”, tarehe 23 Julai 2022 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wao nchini Tanzania. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Masista wa Maria Imakulata, SMI, Tanzania

Masista wa Maria Imakulata tarehe 23 Julai 2022, wameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kadiri ya karama ya Shirika. Lengo kuu la kuanzishwa kwa Shirika hili ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa, kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu na kusoma alama za nyakati.

Na Sr. Agnes Mwanajimba SMI, - Dar es Salaam, Tanzania.

Shirika la Masista wa Maria Imakulata “Sorores Mariae Immaculatae: SMI”, tarehe 23 Julai 2022 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wao nchini Tanzania. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ambaye ameshirikiana na Masista hawa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, akawataka wabaki na Kristo Yesu kikamilifu. Askofu mstaafu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi aliongoza Ibada ya Masita 6 kuweka nadhiri zao za daima na 4 kuweka nadhiri zao za kwanza. Sr. Agnes Mwanajimba Mama Mkuu wa Kanda ya Tanzania, alipokea nadhiri hizi na kuwakabidhi alama na utambulisho wa Shirika yaani: Mdali wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Sala ya Kanisa na Katiba ya Shirika, ambayo kimsingi ni Sheria Mama na Mwongozo thabiti wa maisha unaofumbatwa katika katika Mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Jubilei hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya Chikukwe, Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi na kuhudhuriwa na umati mkubwa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni mfano bora wa kuigwa katika imani.
Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni mfano bora wa kuigwa katika imani.

Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani, upendo na matumaini zaidi. Shirika la Masista wa Maria Imakulata “Sorores Mariae Immaculatae: SMI” lilianzishwa mnamo mwaka 1854 huko Wroclaw, nchini Poland, na Mtumishi wa Mungu Padre Johanne Schneider. Shirika lilisajiliwa na kupata hati ya Kipapa tarehe 22 Desemba 1897.  Lilithibitishwa na hatimaye kupewa Hati ya Sifa. Mtumishi wa Mungu Padre Yohanne Schneider, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Maria Imakulata, SMI katika wosia wake alisema “Mkitaka kunishukuru mtende matendo ya huruma kwa jina langu.’’ Masista hawa tarehe 23 Julai 2022, Parokia ya Chikukwe, Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, wameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kadiri ya karama ya Shirika. Lengo kuu la kuanzishwa kwa Shirika hili ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa, kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni Shirika linalojipambanua kwa ajili ya huduma kwa wasichana maskini, wagonjwa na wale wote wanaotelekezwa kwenye vipaumbele vya jamii.

Ni Shirika ambalo linaendelea kusoma alama za nyakati, ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo. Huu ndio utume uliotekelezwa na Mtumishi wa Mungu Padre Johanne Schneider wakati wa uhai wake. Katika kipindi cha Mapinduzi ya Viwanda Barani Ulaya, wasichana wengi walikimbilia mijini ili kutafuta fursa za ajira, ili hatimaye waweze kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji yao msingi. Ndoto hizi ziliingia “mchanga” kwani wasichana hawa walipofika mijini, walikosa hata mahitaji yao msingi, jambo ambalo lilimsukuma Askofu Henrik Forster kumwomba, Padre Johanne Schneider kuwasaidia wasichana hawa waliokuwa wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, ili kulinda, utu, heshima na haki zao msingi. Katika kukabiliana na changamoto hii, kuna baadhi ya wasichana waliojitokeza kwa ajili ya kuwasaidia wasichana wenzao waliokuwa wanaishi katika mazingira hatarishi kiutu na kimaadili na huo ukawa ni mwanzo wa Shirika la Masista wa Maria Imakulata, SMI.

Masista wa Maria Imakulata Miaka 50 ya huduma ya upendo kwa wagonjwa
Masista wa Maria Imakulata Miaka 50 ya huduma ya upendo kwa wagonjwa

Wamisionari watatu wa kwanza wa Shirika hili walifika nchini Tanzania kunako mwaka 1972, wakitokea nchini Poland na wakaweka makazi yao kwenye Parokia ya Kilimarondo. Wakaanza kutekeleza utume wao kwa kufundisha katekesi, huduma kwa wagonjwa, kufundisha maarifa ya nyumbani ili kumkomboa msichana wa Kitanzania pamoja na kuendelea kutoa elimu, malezi na makuzi kwa watoto waliokuwa wanafundishwa kwenye shule za awali. Jimbo Katoliki la Nachingwea, kunako mwaka 1984 liligawanywa na kuzaa majimbo mawili yaani: Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi na Jimbo Katoliki la Lindi, ambayo yote yako Kusini mwa Tanzania. Shirika liliendelea kufahamika ndani na nje ya Majimbo haya mawili, kutokana na mchango wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Kunako mwaka 1987, Shirika lilianza kuwapokea wasichana waliotia nia ya kuwa watawa wa Shirika hili, tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kanisa pamoja na Serikali ya Tanzania, walionesha ushirikiano na mshikamano mkubwa hasa kwa kutambua mchango wa Shirika katika ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania katika ujumla wao. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na huduma ya Uinjilishaji nchini Tanzania, Shirika linamshukuru Mwenyezi Mungu aliyewawezesha wamisionari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo nchini Tanzania. Wamisionari wakachakarika kuwalea na kuwatunza watawa wazalendo, licha ya tofauti kubwa za kimataduni zilizokuwepo kati yao. Huo ukawa ni mwanzo pia wa utamadunisho, ili kweli Injili ya Kristo iweze kuota mizizi yake katika maisha ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Shirika liliendelea kusoma alama za nyakati, ili kuhakikisha kwamba, karama ya Shirika inasaidia pia katika mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania. Shirika linawashukuru: Maaskofu wa Majimbo mbalimbali ya Kanisa la Tanzania na Wamisionari walioshirikiana nalo bega kwa bega katika kipindi cha miaka yote hii 50 katika maisha na utume wao. Kwa namna ya pekee, Shirika la Mungu Mwokozi, maarufu kama Wasalvatoriani.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu Jimbo kuu la Dar-es-salam
Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu Jimbo kuu la Dar-es-salam

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam amechangia sana kwa ustawi na maendeleo ya Shirika tangu alipokuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Nachingwea na hatimaye, Tunduru Masasi kwa kusoma alama za nyakati na kuomba, Shirika kuongeza rasilimali watu katika mchakato wa uinjilishaji. Leo hii, Shirika lina watawa 85, Wanovisi 10, Wapostulanti 7 na Watakaji 30, matendo makuu ya Mungu. Tunawashukuru viongozi wa Serikali ya Tanzania katika ngazi mbalimbali kwa ushirikiano na mshikamano wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Shirika linaendelea kuwekeza katika rasilimali watu, ili kuliwezesha kujitegemea katika huduma mbalimbali. Shirika kwa sasa linatekeleza utume wake katika Majimbo la Tunduru-Masasi, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo la Same, Jimbo la Morogoro na Jimbo kuu la Dodoma. Shirika linaendelea kujizatiti ili kujitegemea kwa rasilimali wat una vitu kama kielelezo cha ukomavu, ingawa hii ni changamoto pevu kutokana na sababu mbalimbali. Katika kipindi cha miaka 50, changamoto kubwa inayojitokeza ni uchakavu wa miundo mbinu kama vile majengo, ambayo kwa sasa mengine hayakidhi viwango vya ubora na huduma. Idadi ya watawa inazidi kuongezeka, kumbe kuna haja ya kuanza kujielekeza katika kukidhi mahitaji haya msingi. Malezi na makuzi ya awali na endelevu ni muhimu sana kwa watawa ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Kumbe, msaada wa hali na mali ni muhimu kuweza kufikia malengo haya.

Jubilei 50 SMI

 

25 July 2022, 15:54